Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tamu na chungu ya maridhiano Tanzania
Kwa muda sasa Tanzania imejikuta katika hali ya mpito wa kisiasa unaobeba uzito mkubwa wa kihistoria. Matukio ya Oktoba 29, siku ya uchaguzi mkuu wa 2025, yameacha maswali mengi kuliko majibu.
Vifo, majeruhi, na uharibifu wa mali viliibua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa demokrasia, haki za raia, na mwelekeo wa kisiasa wa nchi.
Katika mazingira hayo, neno 'maridhiano' limeibuka tena kama suluhisho linalopendekezwa na pande tofauti lakini likiwa na tafsiri tofauti, matarajio tofauti, na masharti tofauti.
Serikali inaona maridhiano kama mchakato unaohitaji utulivu na utaratibu. Upinzani unaona kama haki iliyochelewa kutendeka. Katikati ya mitazamo hiyo miwili, Watanzania wanasalia wakijiuliza maridhiano haya ni ya nani, kwa ajili ya nani, na kwa gharama gani?
Kauli ya kiongozi wa zamani wa Chadema, Freeman Mbowe kwenye msiba wa muasisi wa chama hicho mwishoni mwa wiki, Edwin Mtei kuhusu yanayoendelea Tanzania zimerejesha upya mjadala huu midomoni mwa watu.
Tamu ya maridhiano
Kwa upande wa chama tawala na Serikali maridhiano yanatajwa kama nguzo muhimu ya kulinda amani na mshikamano wa kitaifa. Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekuwa wakisisitiza kuwa lengo kuu si kushinda hoja za kisiasa, bali kuhakikisha taifa halipasuki katika misingi ya migawanyiko ya kisiasa.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira, amekuwa mmoja wa viongozi waliotoa kauli nzito zaidi kuhusu mchakato huu. Baada ya kuchukua nafasi hiyo mwaka mmoja uliopita, Wasira alisema maridhiano hayawezi kufungwa ndani ya vyama vya siasa pekee.
"Haturidhiani na mtu mmoja. Tunaridhiana na jamii. Na jamii ina wadau wengi, kuna viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali, na hata jamii za kimataifa zinazoishi hapa nchini," alisema.
Lakini Wasira hakusimama hapo. Katika kauli iliyoonyesha mstari mwekundu wa chama tawala, aliongeza:
"Chama chetu ni cha amani. Kama chama chako kinataka vita, tutazungumza na wewe na tutakwambia sisi huko hatuendi."
Kwa wachambuzi wa siasa, kauli hii inaakisi dhamira ya CCM kujiweka kama mdhamini wa amani, chenye kuamua aina na namna ya maridhiano yatakavyokuwa. Kwa mtazamo huu, maridhiano yanakuwa matamu pale yanapodumisha mshikamano na kuleta pande mbili pamoja na kuleta umoja lakini si pale yanapotafsiriwa kama changamoto kwa mamlaka ya dola.
Chungu ya maridhiano
Hata hivyo, kwa upande wa upinzani na wanaharakati, maridhiano haya yana ladha ya uchungu. Wanalalamika kuonewa, kunyimwa haki, kukamatwa na kusekwa rumande kwa makosa wanayoyaona ni ya kusingiziwa. Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema kwa miezi 10 sasa yuko ndani kwa kesi ya uhaini, kesi ambayo wapinzani wanaitaja ni ya kusingiziwa kwa sababu ya msimamo wake kisiasa.
Wapinzani wanaona kama hakuna dhamira ya kweli ya kisiasa ya kuleta maridhiano kwa upande wa Serikali, wakigusia madai ya kukamatwa hovyo na kupotea kwa wanachama, viongozi na wafuasi wa chama hicho na wengine wanaonekana kuwa na msimamo tofauti na serikali.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche anasema: "Hatukosei chochote, lakini tunapotezwa kwa sababu tumekuwa wafuasi wa misimamo yako (akimrejea Mzee Edwin Mtei), wakati akizungumza kwenye msiba wake mwishoni mwa wiki.
Akaungwa mkono na Freeman Mbowe, kiongozi wa zamani wa chama hicho: "Hawa viongozi wangu wa chama change (Chadema) wana maumivu, magerezani wamejaa viongozi ambao wanastahili kuungana na watanzania wengine kufurahia na ndugu zao kuyaona matunda ya nchi yao" .
Mbowe akaongeza "Msitoke serikali mkasema Chadema ni wakorofi, Chadema sio wakorofi, Chadema wameonewa, na wanapoonewa ni lazima wasimame".
Chanzo kikubwa cha hali hiyo ni matakwa ya kisiasa ya muda mrefu kuhusu mifumo ya uchaguzi, katiba mpya, haki na demokrasia. Kuchelewa kwa maridhiano kukachagiza matukio ya Oktoba 29, ambayo bado mpaka leo hayajapata majibu yanayoridhisha kwa wahanga na familia zao.
Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume ya uchunguzi kuchunguza yaliyojiri, hatua iliyopokelewa kwa tahadhari kubwa na vyama vya upinzani. Wengine walisema tume hiyo haina uhalali, wakidai baadhi ya wajumbe wake wanahusishwa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na mifumo ya dola inayotuhumiwa katika matukio hayo.
Mashaka yaliongezeka zaidi baada ya waandishi wa habari kuzuiwa kuripoti ushuhuda wa baadhi ya waathiriwa. Hatua hiyo ilizua maswali mazito: Kama maridhiano yanajengwa juu ya ukweli, basi ukweli huo unafichwa kwa nini?
"Bila uwazi wamepanga kuwawekea maneno wahanga na kuficha ukweli", anaandika kwenye mitandao yake mwanaharakati Maria Sarungi.
Lakini Jaji mstaafu Profesa Ibrahim Juma, mjumbe wa tume, alisema uamuzi huo ulilenga kulinda faragha ya mashahidi. Lakini kwa wakosoaji, hiyo haikutosha kuondoa hofu ya kuanza kufunikwa kwa ukweli.
Lakini kama pia Tume itatoa ripoti tofauti na matarajio ya wengi, huenda ikaongeza ugumu zaidi wa maridhiano.
Maridhiano yatafanikiwa? Nini ugumu na urahisi wake?
Historia ya karibuni inaonyesha kuwa maridhiano si jambo geni nchini Tanzania. Mara tu Rais Samia alipoingia madarakani, kulikuwa na hatua za awali za kufungua anga la kisiasa. Lakini mchakato huo ulikwama baada ya Chadema kujitoa, wakidai ahadi hazitekelezwi kwa vitendo.
Kwa upinzani, maridhiano hayawezi kuwa mazungumzo ya heshima tu bila kugusa mizizi ya migogoro ikiwemo haki za kisiasa, uhuru wa mikutano, na matumizi ya vyombo vya dola. Swali linaloulizwa ni je, maridhiano ni njia ya kutafuta suluhu, au ni mbinu ya kudhibiti taharuki ya kisiasa?
Katika msiba wa muasisi wa Chadema, Edwin Mtei, aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kimya cha muda mrefu. "Njia bora kabisa ya kuleta maendeleo ni kurejesha uhuru wa watu, furaha ya watu na haki za watu, na kukiri ukweli pale ambapo serikali imekosea," alisema.
Kauli hiyo ilionekana kama muhtasari wa msimamo wa upinzani: Maridhiano hayawezi kufanikiwa bila kukiri makosa na bila hatua za wazi za kurejesha haki. Lakini je serikali itakiri kama wanavyotaka wapinzani? na kama isipokiri nini hatma ya taifa hilo kisiasa?
Ugumu wa safari hii kwa mujibu wa wachambuzi ni utayari wa pande zote ambazo kila leo wanaotunishiana misuli. Lakini urahisi uliopo angalau kila pande inakiri kuna tatizo, taifa halipo pamoja na njia inayotajwa na wote ni maridhiano. Sasa kama yatafanikiwa ama hayatafanikiwa ni suala la muda tu.