Rekodi ya Guiness yamtambua Truphena Muthoni kwa kuukumbatia mti kwa saa 72
Mwanamazingira kutoka Kenya, Truphena Muthoni, amepokea uthibitisho rasmi kutoka rekodi ya dunia ya Guinness (GWR) kwa kukumbatia mti kwa saa 72, zaidi ya mwezi mmoja baada ya kufanikisha rekodi hiyo.
Truphena mwenye umri wa miaka 22 alishiriki rekodi hiyo kuanzia Jumatatu, Desemba 8, hadi Alhamisi, Desemba 11, 2025, nje ya ofisi ya gavana wa Nyeri, nchini Kenya, Mutahi Kahiga, akitumia jitihada hiyo kulalamika dhidi ya ukataji miti na kushirikisha utunzaji wa mazingira.
Hii ilikuwa jitihada yake ya pili ya kuvunja rekodi, baada ya hapo awali kuweka rekodi ya saa 48 mnamo 2025.
Katika chapisho la Facebook lililosomwa na BBC Swahili, Guinness ilieleza kuwa lengo la Truphena lilikuwa kukuza utunzaji wa miti na kuheshimu hekima za jadi za mazingira.
"Shindano refu zaidi ya kukumbatia mti — saa 72 na @truphena_muthoni. Lengo la Truphena katika jitihada hii ya rekodi lilikuwa kuinua na kutetea ulinzi wa miti ya kienyeji na kuheshimu hekima za watu wa asili. Aliivunja rekodi yake mwenyewe ya saa 48, iliyowekwa awali mnamo 2025," ilisema taarifa hiyo, ikifuatana na video yake akiukumbatia mti.