Australia: Je, marufuku ya watoto kutumia mitandao, itawezekana?

    • Author, Hannah Ritchie
    • Nafasi, BBC News,Sydney
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

"Niliingiwa na wasiwasi mno,"anasema James ,akisimulia tukio ambalo alilitazama katika mtandao wa Snapchat uliomtatiza akili na kujiuliza iwapo yuko salama kwenda shuleni.

Kijana huyu ambaye ni raia wa Australia ,mwenye umri wa miaka 12,alikuwa amekosana na rafiki yake ,na usiku mmoja kabla ya kulala alijumuishwa kwenye kundi akiwa na matineja wengine wawili.

Dakika chache tu,mfululizo wa ujumbe wa vurugu ulianza kumiminika katika simu yake.

“Mmoja wa vijana hao alionekana kuwa ana umri wa miaka 17 ,”James aambia idhaa ya BBC. “Alinitumia video akiwa ameshikilia panga ....alikuwa akiizungusha.Kisha nikasikia sauti alizotumia kupitia arafa kuwa akinipata atanidunga.”

James-sio jina lake halisi-alijiunga na mtandao wa Snapchat akiwa na umri wa miaka 10 ,baada ya mwanafunzi mwenzake katika kundi la marafiki zake kumsihi ajiunge na apu hiyo.Lakini baada ya kuelezea wazazi wake kilichomtokea akiwa katika mtandao huo ,na tuko hilo likasuluhishwa na wasimamizi wa shule yao,James alifuta akaunti yake mara moja.

Alichokipitia James inadhihirisha kwanini serikali ya Australia inapania kupiga marafuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 16 ni muhimu ,anasema Emma ,sio jina lake halisi ,ambaye ni mama mzazi wa James.

Sheria ambazo ziliwasilishwa mbele ya bunge siku ya Alhamisi ,imetajwa na waziri mkuu Anthony Albanese kama mswada 'unaoongoza ulimwengu'

Ingawa wazazi wengi wameupigia upatu mswada huo ,baadhi ya wataalam wameibua maswali iwapo itawezekana watoto kuzuiwa kikamilifu kutumia mitandao ya kijamii,na athari gani ambazo zitatarajiwa baada ya hatua hiyo.

Je, ni kipi Australia inapendekeza?

Waziri mkuu wa Australia Antohny Albanese amesema marufuku hayo ambayo yanajumuisha mitandao kama vile X, TikTok, Facebook na Instagram ni kuwalinda watoto kutokana na madhara yanayopatikana katika mitandao ya kijamii.

"Hii ni ya akina baba na mama...kama mimi wana wasiwasi usalama wa watoto wao wakitumia mitandao ya kijamii,” anasema.

Sheria hii inatoa mfumo kazi wa marufuku hayo.Lakini hati hii ambayo ina ukurasa 17 ,inatarajiwa kuwasilishwa ,mbele ya bunge la seneti ,ingawa haina maelezeo ya kina.

Badala yake,itakuwa jukumu la mdhibiti wa kitaifa wa intaneti - kamishna wa usalama wa mitandao kuhakikisha maagizo yametekelezwa na kufuatiliwa,ambayo hayatafuatiliwa hadi mwaka mmoja baada ya kuidhinishwa kuwa sheria.

Kulingana na mswada huo ,itahusisha watoto wote walio chini ya umri wa miaka 16 na haitajalisha iwapo wameridhia kuwa kwa mitandao ama wazazi wao wamewakataza kutumia mitandao.

Kampuni za teknolojia zitaadhibiwa hadi dola milioni 32.5 iwapo hawatatekeleza sheria mpya kikamilifu,lakini kutakuwa na majukwaa mahususi ambayo yatawekwa kutoa huduma ambazo zina athari ndogo ambazo zinatajwa kuwa ni za maudhui ya watoto pekee.Hata hivyo vigezo vya jukwaa hilo bado havijabuniwa.

Huduma za arafa na majukwaa ya michezo ya mitandaoni,hazitapigwa marufuku ,hatua ambayo wataalam wameitilia shaka jinsi mdhibiti wa mitandao atajua ni majukwaa yepi ambayo watoto wanatumia haswa karne hii ambayo ina mabadiliko kila uchao.

Kikundi kinachowakilisha kampuni za teknolojia kama vile Meta, Snapchat na X nchini Australia zimepuuzilia mbali marufuku hayo wakitaja hatua hiyo imepitwa na wakati na changamoto za karne ya 21 hazitatuliwi na mawazo ya karne ya 20.

Wakidokeza kuwa sheria kama hii itasukuma watoto kujipata katika majukwaa ya mitandao ambayo ni hatari zaidi wakijificha ,kundi hilo la kampuni za kidijitali yasema -kauli ambayo pia imeungwa mkono na baadhi ya wataalam wa mitandao.

Kamishna wa Usalama wa Kielektroniki Julie Inman Grant amekubali kazi kubwa ambayo ofisi yake itakabiliana nayo wakati wa kutekeleza marufuku hiyo, ikizingatiwa "mabadiliko ya teknolojia siku zote yatapita sera zilizowekwa".

"Siku zote kutakuwa na mabadiliko, na hii ndiyo sababu wasimamizi kama eSafety wanapaswa kuwa mahiri," aliiambia BBC Radio 5 Live.

Lakini Bi Inman Grant pia ameibua wasiwasi juu ya wazo kuu ya sera ya serikali, ambayo ni kwamba kuna uhusiano wa mitandao ya kijamii na kuzorota kwa afya ya akili.

"Ningesema kwamba msingi wa ushahidi haujatatuliwa hata kidogo," alisema, akionyesha utafiti kutoka kwa ofisi yake ambayo iligundua kuwa baadhi ya vikundi vilivyo hatarini zaidi, kama vile LGBTQ+ au Vijana wa First Nations, "wanajihisi na kujieleza zaidi mtandaoni kuliko kufanya katika ulimwengu wa uhalisia."

Haya ni maoni yaliyoungwa mkono na Lucas Lane, mwenye umri wa miaka 15, ambaye anafanya biashara ya mtandaoni ya kuwauzia wavulana rangi ya kucha. "Hii marufuku ya mitandao inaharibu ... urafiki wangu na uwezo wa kufanya watu waonekane," kijana wa Perth aliambia BBC.

Bi Inman Grant anapendekeza kampuni za teknolojia zisafishe mifumo yao, pamoja na uwekezaji zaidi katika zana za elimu ili kuwasaidia vijana kuwa salama mtandaoni. Anatumia mfano wa kufundisha watoto kuogelea, badala ya kuwapiga marufuku kutoka kwa maji.

"Hatuweki uzio bahari ... lakini tunaunda mazingira ya kuogelea yaliyolindwa ambayo hutoa ulinzi na kufundisha masomo muhimu kutoka kwa umri mdogo," aliambia bunge mapema mwaka huu.

Pia unaweza kusoma:

Lakini wazazi kama Emma wana maoni tofauti.

"Je! tunapaswa kuwa tunapoteza wakati wetu kujaribu kusaidia watoto kutumia mifumo hii ngumu wakati kampuni za teknolojia zinataka tu zitumike kila wakati?" anasema.

"Au tuwaruhusu tu wawe watoto na kujifunza jinsi ya kuwa na urafiki nje na kila mmoja wao, na kisha kuanza mazungumzo haya baadaye?"

Amy Friedlander, mama wa watoto watatu kutoka vuguvugu la Wait Mate - ambalo linawahimiza wazazi kuchelewesha kuwapa watoto wao simu za mikononi - anakubali.

"Hatuwezi kupuuza manufaa yote ambayo teknolojia imeleta katika maisha yetu. Kuna mabadiliko makubwa, lakini kile ambacho hatujazingatia ni athari inayoleta kwa akili ambazo haziko tayari kwa hilo.

Sheria isiyokuwa na makali

Zaidi ya wasomi 100 wa Australia wamekosoa marufuku hiyo kama "chombo kisichokuwa na makali" na wakasema kuwa ni kinyume na ushauri wa Umoja wa Mataifa ambao unatoa wito kwa serikali kuhakikisha vijana wanapata "ufikiaji salama" wa mazingira ya kidijitali.

Pia imeshindwa kuungwa mkono na kamati ya bunge ya pande mbili ambayo imekuwa ikichunguza athari za mitandao ya kijamii kwa vijana. Badala yake, kamati ilipendekeza kwamba wakuu wa teknolojia wakabiliane na kanuni kali.

Ili kushughulikia baadhi ya maswala hayo, serikali inasema hatimaye itaanzisha sheria za "wajibu wa kidijitali wa utunzaji", ambayo itafanya kuwa wajibu wa kisheria kwa kampuni za teknolojia kuweka kipaumbele kwa usalama wa watumiaji.

Joanne Orlando, mtafiti wa tabia ya kidijitali, anasema kwamba ingawa marufuku "inaweza kuwa sehemu ya mkakati, haiwezi kuwa mkakati mzima".

Anasema "kitendawili kikubwa zaidi" kinapaswa kuelimisha watoto kufikiria kwa kina kuhusu maudhui wanayoona kwenye apu zao na jinsi wanavyotumia mitandao ya kijamii.

Serikali tayari imetumia dola milioni 6 tangu 2022 kutengeneza "zana za kusoma na kuandika dijitali" bila malipo ili kujaribu kufanya hivyo. Walakini, utafiti unapendekeza kwamba vijana wengi wa Australia hawapati masomo ya kawaida.

Bi Orlando na wataalam wengine wanaonya pia kuna vikwazo vikubwa vya kufanya teknolojia ya uthibitishaji wa umri - ambayo inahitajika kutekeleza marufuku - yenye ufanisi na salama, kutokana na "hatari kubwa" zinazohusiana na uwezekano wa kuhifadhi hati za utambulisho za kila raia wa Australia mtandaoni.

Serikali imesema inalenga kutatua changamoto hiyo kupitia majaribio ya uhakiki wa umri, na inatarajia kuwasilisha ripoti ifikapo katikati ya mwaka ujao. Imeahidi kwamba masuala ya deta za kibinafsi yatapatiwa kipau mbele , lakini imetoa maelezo kidogo juu ya aina gani ya teknolojia itakayojaribiwa.

Katika ushauri wake, Kamishna wa Usalama wa Kielektroniki ameelekeza wazo la kutumia huduma ya watu wengine kuficha kitambulisho cha mtumiaji kabla ya kutumwa kwenye tovuti zozote za uthibitishaji wa umri, ili "kuhifadhi" data zao za siri.

Hata hivyo, Bi Orlando anasalia kuwa na shaka. "Siwezi kufikiria teknolojia yoyote iliyopo wakati huu ambayo inaweza kusitisha hii," aliambia BBC.

Je, Australia itafaulu kutekeleza marufuku?

Australia ni nchi ya kwanza kujaribu kuzuia jinsi vijana wanavyofikia tovuti au majukwaa fulani mtandaoni.

Mwaka wa 2011, Korea Kusini ilipitisha "sheria yake ya kuzima" ambayo ilizuia watoto chini ya miaka 16 kucheza michezo ya mtandao kati ya saa nne na nusu hadi saa kumi na mbili asubuhi, lakini sheria - ambazo zilikosolewa vikali - baadaye zilitupiliwa mbali na kutaja haja ya "kuheshimu haki za vijana. ”.

Hivi majuzi Ufaransa ilianzisha sheria inayohitaji mitandao ya kijamii kuzuia ufikiaji wa watoto walio chini ya miaka 15 bila idhini ya mzazi. Utafiti ulionyesha karibu nusu ya watumiaji waliweza kukwepa marufuku kwa kutumia VPN rahisi.

Sheria katika jimbo la Utah la Marekani ambayo ilikuwa sawa na ya Australia ilikumbana na suala tofauti: ilizuiwa na jaji wa shirikisho ambaye aliiona kuwa ni kinyume cha katiba.

Albanese amekubali kwamba pendekezo la Australia linaweza lisiwe la udhia, na ikiwa bunge litaidhinisha , litakumbwa na changamoto nyingi si haba.

"Tunajua kwamba teknolojia inakwenda kwa kasi. Hakuna serikali itaweza kumlinda kila mtoto kutokana na kila tishio - lakini tunapaswa kufanya kila tuwezalo," alisema wakati akitangaza hatua hiyo.

Lakini kwa wazazi kama Emma na Bi Friedlander ,ambao wameunga mkono mabadiliko hayo ni ujumbe ambao marufuku hiyo itakuwa nayo ambayo ni muhimu zaidi.

"Kwa muda mrefu sana wazazi wamekuwa na chaguo hili lisilowezekana kati ya kukubali na kumpa mtoto wao kifaa kinachozoesha tabia au kuona mtoto wao akitengwa na kuhisi kutengwa kijamii," Bi Friedlander asema.

"Tumejipata katika hali ambayo hakuna mtu anataka kuwa katika hali ile."

James anasema tangu aachane na Snapchat amejikuta akitumia muda mwingi nje na marafiki.

Na anatumai kuwa sheria mpya itasaidia watoto kama yeye kutoka nje na kufanya mambo wanayopenda badala ya kuhisi kulazimishwa kuwa mtandaoni.

Soma zaidi:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid