Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Unatumia WhatsApp bure: Je, mtandao huo unapataje pesa?
Katika saa 24 zilizopita nimeandika zaidi ya meseji 100 za WhatsApp. Zinazohusu mipango na familia yangu, kujadili kazi na wafanyakazi wenzangu, na tukapeana habari na tukapiga porojo na marafiki kadhaa.
Hata jumbe zangu za kuchosha nimezituma na kufika kwa walengwa na nimetumia seva za kompyuta zenye nguvu za WhatsApp, zilizowekwa katika vituo mbalimbali vya data duniani kote.
Si kazi ya bei nafuu, lakini si mimi wala watu ambao nilikuwa nikipiga gumzo nao jana, ambao tumelipa pesa yoyote ili kutumia. Jukwaa hilo lina karibu watumiaji bilioni tatu ulimwenguni.
WhatsApp - au zapzap, kama inavyoitwa kwa jina la utani huko Brazili - inapataje pesa?
WhatsApp inapataje pesa?
WhatsApp ni mtandao mkubwa nyuma ya kampuni ya Meta, ambayo inamiliki Facebook na Instagram pia.
Akaunti binafsi za WhatsApp kama yangu ni za bure kwa sababu WhatsApp hutengeneza pesa kutoka kwa wauzaji wanaotaka kuwasiliana na watumiaji kama mimi.
Tangu mwaka jana mtandao huo umeweka chaneli ya bila malipo kwenye WhatsApp, ili wauzaji na watengeneza maudhui wengine waweze kutuma ujumbe na usomwe na wote wanaochagua kujiunga na chaneli hiyo.
Chaneli hizo hulipia ikiwa tu zinataka kuwa na mwingiliano na wateja kupitia programu, kwa mazungumzo na biashara.
Katika jiji la India la Bangalore, sasa unaweza kununua tiketi ya basi, na kuchagua kiti chako, kupitia WhatsApp.
“Maono yetu ni kwamba, ikiwa unataka kukata tiketi, unataka kurudisha pesa, ikiwa unataka kufanya malipo, uwe na uwezo wa kufanya hivyo. Na kisha urudi moja kwa moja kwenye mazungumzo yako ya kawaida," anasema Nikila Srinivasan, makamu wa rais wa biashara ya ujumbe katika Meta.
Sasa pia mtu anaweza kulipia moja kwa moja kwa WhatsApp kupitia (kiunganishi) linki ya tangazo la bidhaa mtandaoni kwenye Facebook au Instagram.
Bi Srinivasan ananiambia njia hii kwa sasa inazalisha "mabilioni ya dola" kwa kampuni hiyo kubwa ya teknolojia.
Lakini mitandao mengine kama Signal, jukwaa maarufu na salama kutuma ujumbe, ni mtandao usiozalisha faida. Inasema haijawahi kuchukua pesa kutoka kwa wawekezaji (tofauti na mtandao kama Telegram, ambao unategemea wawekezaji).
Badala yake Signal, inategemea michango - ambayo ni pamoja kiasi cha dola za kimarekani milioni 50 kutoka kwa Brian Acton, moja ya waanzilishi wa WhatsApp, mwaka 2018.
"Lengo letu ni kuungwa mkono kwa asilimia zote na wafadhili wadogo wadogo, na kutegemea michango kutoka kwa idadi kubwa ya watumiaji wanaojali huduma za Signal," aliandika rais wake Meredith Whittaker mwaka jana.
Discord, programu ya kutuma ujumbe inayotumiwa kwa kiasi kikubwa na wachezaji wa gemu, ni bure kujisajili, lakini kupata huduma za ziada, ikiwa ni pamoja na kupata michezo ya gemu, ni lazima ulipie. Pia hutoa huduma nyingine iitwayo Nitro, ambayo huonyesha video katika ubora wa hali ya juu na emoji maalumu, kwa usajili wa kila mwezi wa dola 9.99.
Snap, mtandao unaomilikiwa na Snapchat. Unakuwa na matangazo, na ina watumiaji milioni 11 wanaolipa (hilo limeanza Agosti 2024) na pia inauza miwani za Snapchat Spectacles.
Kwa mujibu wa Forbes, kati ya 2016-2023 kampuni hiyo ilipata karibu dola milioni 300 kutokana na riba tu. Lakini chanzo kikuu cha mapato ya Snap ni kutoka katika matangazo, ambayo huleta zaidi ya dola bilioni 4 kwa mwaka.
Kampuni yenye umri wa miaka 10 ya Element yenye makao yake nchini Uingereza huzitoza pesa serikali na mashirika makubwa ili kutumia mfumo wake salama wa kutuma ujumbe. Wateja wake hutumia teknolojia yake lakini wanaiendesha wenyewe, kwenye seva zao za binafsi.
Mifumo mingi ya mitandao huuza matangazo kwa kufuatilia kile ambacho watu hufanya, wanazungumza na nani, na kisha huwalenga kwa matangazo kulingana na uhitaji wao.
"Kauli ya muda mrefu ipo - ikiwa wewe mtumiaji, hulipi chochote, basi kuna uwezekano kuwa wewe ndiye bidhaa," anasema mwanzilishi wa Element, Matthew Hodgson.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla