Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uganda yafungua tena majukwaa ya mitandao ya kijamii
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda (CDF), Jenerali Muhoozi Kainerubaga awasifu Waganda kama watu bora zaidi duniani.
Muhtasari
- China yaonya raia wake kutosafiri Japan
- Israel yasema imerejesha mabaki ya mateka wa mwisho wa Gaza
- Wahouthi waonya kushambulia meli katika bahari ya shamu
- KNCHR yashutumu mashambulizi dhidi ya waumini kanisani, Kenya
- Maseneta wa Republican waunga mkono wito wa uchunguzi wa mauaji ya Minneapolis mauaji ya Minneapolis
- Polisi Kenya yahakikishia raia usalama kufuatia shambulio eneo la Garissa
- Taiwan inafuatilia mabadiliko ya uongozi wa kijeshi wa China 'yasiyo ya kawaida'
- Uganda yafungua tena majukwaa ya mitandao ya kijamii
- Sudan Kusini yawaamuru wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na raia kuondoka Jimbo la Jonglei
- Watu wenye silaha waua watu 11 katika uwanja wa mpira Mexico
- Watu saba wamefariki kutokana na dhoruba ya theluji Marekani
- Dhahabu yapanda thamani kutokana na mivutano ya kisiasa
- Watu 15 wafariki baada ya feri kuzama Ufilipino
- Umeme wakatika na vifo vyatangazwa kutokana na dhoruba ya theluji Marekani
- Venezuela yawaachilia huru wafungwa kadhaa wa kisiasa
- Waandamanaji wakusanyika Marekani baada ya afisa wa uhamiaji kutekeleza mauji
Moja kwa moja
Rashid Abdallah & Asha Juma
China yaonya raia wake kutosafiri Japan
China imetoa onyo kwa raia wake kutosafiri nchini Japan msimu wa sherehe za mwaka mpya wa China, maarufu Lunar Year.
Hii imetokana na China kukasirishwa na matamshi ya Waziri Mkuu wa Japan Sanae Takaichi, aliyoyatoa mwezi Novemba 2025, kuhusu kuunga mkono eneo linalojitawala la Taiwan.
“Kuna uhalifu ambao umeongezeka dhidi ya raia wa China, matetemeko ya ardhi na tishio la usalama kwa Wachina nchini Japan.” Wizara ya mambo ya kigeni ya China ilisema
Beijing imetoa onyo dhidi ya semi za Takaichi baada ya kusema kuwa iwapo China itaishambulia Taiwan, Japan itajibu kwa njia ya kijeshi.
Semi hizo zilikasirisha utawala wa Beijing, ambayo ilijibu kwa kusitisha kuuza baadhi ya bidhaa zake nchini Japan, safari za ndege na kutoa maoni makali ya kuilenga Japan.
Wizara ya ulinzi ya Beijing ilionya Tokyo kuwa watawashinda kivita iwapo watahitajika kutumia nguvu kuitawala Taiwan.
Mashirika ya ndege ya China ya Air China, China Eastern na China Southern airlines, Jumatatu yamewaruhusu wateja wake kubatilisha tiketi zao za ndege hadi mwezi Oktoba.
Idadi ya raia wa China wanaozuru Japan, imepungua kwa asilimia arubaini na tano mwezi Disemba, ila kwa ujumla idadi ya watalii wanaozuru Japan iliongezeka kulingana na wizara ya utalii ya Japan.
Ingawa Takaichi hajafuta kauli yake ya mwezi Novemba, alisisitiza nafasi ya Japan ya kuunga mkono umoja wa China, na kusema kuwa jinsi China ilitafsiri kauli yake, haiambatani na ukweli.
Soma zaidi:
Israel yasema imerejesha mabaki ya mateka wa mwisho wa Gaza
Jeshi la Israel linasema limefanikiwa kupata mwili wa mateka wa mwisho aliyesalia huko Gaza.
Ilikuwa ikimtafuta Sajenti Mkuu Ran Gvili tangu makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas yalipoanza Oktoba.
Hamas ilikusudiwa kuwarudisha mateka wote, walio hai na waliokufa, ndani ya saa 72 baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza.
Mateka ishirini wa Israeli walio hai na miili ya mateka 27 wa Israeli na wageni waliokufa ilikabidhiwa lakini kwa wiki chache zilizopita Hamas ilisema bado haijaweza kumpata Gvili.
Siku ya Jumapili, Israeli ilisema itafungua tena kivuko muhimu cha mpaka wa Gaza na Misri mara tu operesheni ya kumtafuta na kumrudisha Gvili itakapokamilika.
Kupatikana kwa mwili wa Gvili kunafungua njia kwa Israel na Hamas kusonga mbele kwa awamu ya pili ya mpango wa amani wa Donald Trump.
Awamu ya pili inalenga kuhusisha ujenzi mpya na kuondoa wanajeshi kabisa katika eneo la Gaza, ikiwa ni pamoja na kupokonya silaha Hamas na makundi mengine ya Wapalestina.
Israeli ilikuwa imekataa kusonga mbele hadi Gvili atakapopatikana.
Soma zaidi:
Wahouthi waonya kushambulia meli katika bahari ya shamu
Kundi la wanamgambo wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Yemen, wametishia kufanya mshambulizi dhidi ya meli zinazopitia bahari ya shamu katika jaribio la kuunga mkono Iran, baada ya rais wa Marekani Donald Trump kutishia kuichukulia hatua ya kijeshi Iran kutokana na maandamano yanayoshuhudiwa nchini humo.
Katika video moja iliyochapishwa na wa Houthi, ilionyesha picha za meli moja ikiwa inawaka moto na kuandikia kua “itatokea hivi karibuni”.
Wanamgambo hao hawakutoa maelezo zaidi ila wameshambulia zaidi ya meli mia moja zinazotumia bahari ya shamu, hii ikiwa moja ya kampeni walizotumia kuishinikiza Israel dhidi ya vita vyake eneo la Gaza.
Kundi hilo lilisitisha mashambulizi yake baada ya makubaliano ya amani kuafikiwa eneo la Gaza, na wameonya kuwa wako tayari kurejelea mashambulizi yao iwapo itawalazimu kufanya hivyo.
Kundi hilo pia limerusha mamia ya makombora nchini Isreal katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Vitisho vya wa Houthi, vinakuja wakati ndege ya Marekani ya USS Abraham Lincoln, ambayo imeambatana na meli za kivita za kudungua makombora zimeonekana zikielekea eneo hilo.
Trump amesema meli hiyo inaelekea eneo hilo, katika utayari wa kufanya shambulizi iwapo atahitajika kuichukulia Iran hatua.
Trump amesema anaweza kuishambulia Iran kwasababu ya kuwaua waandamanaji, na kuwanyonga wale waliokamatwa wakiandamana.
Pia unaweza kusoma:
KNCHR yashutumu mashambulizi dhidi ya waumini kanisani, Kenya
Tume ya Kutetea Haki za Binadamu Kenya (KNCHR) imesema imepokea kwa mshutuko na kushutumu vikali taarifa kutoka kwa vyombo vya habari za mashambulizi dhidi ya waumini wa dini ya Kikiristo waliokuwa wamehudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa la St. Peter’s ACK kaunti ya Nyeri nchini Kenya.
Taarifa ya KNCHR imesema kuwa siku ya Jumapili, 25/01/2026, maafisa wa polisi ambao baadhi yao walikuwa wamejifunika vichwa, inadaiwa walifyatua mabomu ya machozi wakati wa ibada iliyokuwa imehudhuriwa na watoto wa wazee bila mamlaka ya kisheria au sababu ya msingi.
"Utumiaji wa nguvu ulikuwa wa kupita kiasi, usiofaa, na wa kibaguzi hasa katika hali hii ambayo watu walikuwa wamekusanyika na wengine walio katika hatari," taarifa ilisema.
Shirika hilo lilisema utumiaji wa mabomu ya machozi Kanisani au eneo lolote la kuabudu ni kitendo kisichokubalika kwa namna yoyote ile na maafisa waliohusika walikiuka sheria ya haki kama inavyolindwa kikatiba.
KNCHR pia ilizungumzia matukio ya mashambulizi yalioongezeka katika maeneo ya kuabudu ambayo chimbuko lake ni ushindani wa kisiasa.
"Ghasia zinazotekelezwa kupitia makundi ya kihuni yanaongeza hatari ya kutokea kwa vurugu hasa wakati ambapo nchi inaelekea kipindi cha uchaguzi," shirika la KNCHR lilisema.
Aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua ni miongoni mwa waliokuwa katika kanisa hilo na aliandika kupitia mtandao wa X kuwa yeye na wafuasi wake walikwama ndani ya kanisa baada ya polisi kurusha mabomu ya machozi, akidai kuwa lilikuwa jaribio la mauaji.
Mamlaka ya Kenya ilisema uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen alisema, "Vurugu popote pale, na hasa katika sehemu ya ibada, haikubaliki...nimezungumza na Inspekta Jenerali wa Polisi, Bw Douglas Kanja, ambaye amenihakikishia kuwa uchunguzi unaendelea na kwamba wahusika watafikishwa mahakamani."
Pia unaweza kusoma:
Maseneta wa Republican waunga mkono wito wa uchunguzi wa mauaji ya Minneapolis
Rais Donald Trump anakabiliwa na wito wa kuanzisha uchunguzi kamili kufuatia mauaji ya muuguzi mwenye umri wa miaka 37, na raia wa Marekani, Alex Pretti, yaliyofanywa na maafisa wa serikali.
Kifo cha Pretti kinakuja chini ya wiki tatu baada ya Renee Good kupigwa risasi na afisa wa uhamiaji huko Minneapolis.
Gavana wa Minnesota Tim Walz amerudia kudai utawala wa Trump kuwaondoa maafisa wa shirikisho kutoka jimboni humo, akisema Marekani iko katika "kipindi cha mabadiliko".
Katika mahojiano na Wall Street Journal siku ya Jumapili, Trump alisema utawala wake "unapitia kila kitu" na pia alionyesha kwamba hatimaye anaweza kuwaondoa maafisa wa Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha (ICE) kutoka jijini - lakini hakutoa muda muafaka.
Maafisa wa serikali kuu na jimbo wamekuwa wakitoa maelezo tofauti kabisa kuhusu matukio kabla ya kifo cha Pretti huku maafisa katika utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumapili wakitetea kupigwa risasi na kuuawa kwa Prettihuko Minneapolis, ushahidi wa video ukienda kinyume na taarifa yao.
Wakazi walitembelea eneo la tukio na kuweka mashada ya maua na mishumaa licha ya hali ya hewa ya baridi kali na theluji kuadhimisha kupigwa risasi kwa Alex Pretti siku ya Jumamosi.
Maafisa wa utawala wa Trump walisema kwamba Pretti aliwashambulia maafisa, na kuwachochea kufyatua risasi ili kujilinda.
Soma zaidi:
Polisi Kenya yahakikishia raia usalama kufuatia shambulio eneo la Garissa
Idara ya polisi nchini Kenya imethibitisha kutokea kwa shambulio lililosababisha kifo cha chifu na mwalimu mmoja katika eneo la Hulugho kaunti ya Garissa.
Idara ya polisi imesema kuwa imechukua hatua na kuhakikisha kuwa maafisa wa usalama wako kwenye eneo la tukio kutafuta waliotekeleza kitendo hicho cha kioga.
Polisi ilisema imeimarisha ushikaji doria katika eneo husika na viunga vyake.
"Usalama umeimarishwa na operesheni inaendelea kuwakamata waliotekeleza kitendo hicho na kuhakikisha wanakabiliwa na sheria kikamilifu," Idara ya polisi imesema.
Polisi imetoa wito kwa raia kusalia watulivu na waangalifu na kushirikiana na maafisa wa usalama huku ikitoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za tukio hilo zinazoweza kusaidia katika uchunguzi kuwasiliana na kituo cha polisi kilicho karibu.
Inasemekana kuwa wavamizi hao walianza na kituo cha polisi cha eneo kabla ya kuelekea nyumbani kwa chifu, kisha wakaelekea nyumbani kwa mwalimu na kumpiga risasi.
Soma zaidi:
Taiwan inafuatilia mabadiliko ya uongozi wa kijeshi wa China 'yasiyo ya kawaida'
Taiwan inafuatilia kile ilichokiita mabadiliko "yasiyo ya kawaida" katika uongozi wa kijeshi wa China baada ya jenerali wake mkuu kuanza kuchunguzwa, na kusema kuwa itaendeleza ulinzi wake kwani kiwango cha tishio bado kiko juu, waziri wa ulinzi amesema.
China ilitangaza Jumamosi kwamba Zhang Youxia, naibu mkuu chini ya Rais Xi Jinping ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa Tume Kuu ya Jeshi, na afisa mwingine mwandamizi, Liu Zhenli, kuwa wanachunguzwa kwa tuhuma za ukiukaji mkubwa wa nidhamu na sheria.
"Tutaendelea kufuatilia kwa karibu mabadiliko yasiyo ya kawaida katika ngazi ya juu ya chama cha China, serikali, na uongozi wa kijeshi wa China.
Msimamo wa jeshi unatokana na kuwa China haijawahi kuondoa uwezekano wa kutumia nguvu dhidi ya Taiwan," Waziri wa Ulinzi wa Taiwan Wellington Koo aliwaambia waandishi wa habari bungeni.
Zhang ameonekana kwa muda mrefu kama mshirika wa karibu wa kijeshi wa Xi, na ni mmoja wa maafisa wakuu wachache wa China wenye uzoefu wa mapigano, baada ya kushiriki katika mzozo wa mpaka na Vietnam wa 1979.
China, ambayo inaiona Taiwan inayojitawala kidemokrasia kama eneo lake na hutuma ndege na meli za kivita angani na majini kuzunguka kisiwa hicho karibu kila siku, katika kile ambacho Taipei inakiona kama kampeni ya unyanyasaji ili kuishawishi serikali kukubali madai ya China.
Soma zaidi:
Uganda yafungua tena majukwaa ya mitandao ya kijamii
Serikali ya Uganda imetangaza kufunguliwa tena kwa mitandao ya kijamii baada ya kuminywa kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika mapema mwezi Januari.
Siku ya Jumatatu, Januari 26, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda (CDF), Jenerali Muhoozi Kainerubaga, alitangaza kuondolewa kwa marufuku ya kuminya majukwaa ya mitandao ya kijamii, akiwashukuru Waganda kwa ushirikiano wao katika kipindi chote cha uchaguzi.
Katika taarifa hiyo, Muhoozi aliwasifu Waganda kama watu bora zaidi duniani. Pia alibainisha kuwa uungwaji mkono alioupata kutoka kwa Waganda ulimpa yeye na timu yake ujasiri wa kutumikia, na kuombea baraka nchi na raia wake.
"Tunaachilia mitandao yote ya kijamii leo. Ninawashukuru raia wote wa Uganda kwa ushirikiano wao katika msimu huu wote wa uchaguzi," Muhoozi alisema.
"Ninyi ni watu bora zaidi duniani, na mnatupa ujasiri wa kutumikia. Mungu awabariki nyote," aliongeza.
Kabla ya uchaguzi, serikali ya Uganda ilitangaza kufungwa kwa intaneti kote nchini ambako kuliathiri huduma zote za simu na setilaiti, ikitaja hitaji la kupunguza ukiukwaji wa sheria za uchaguzi na kulinda utulivu wa umma wakati wa kipindi cha uchaguzi.
Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC), mnamo Januari 18, iliondoa marufuku ya mtandao lakini ikaagiza kwamba mitandao ya kijamii na programu za ziada (OTT) ziendelee kuzuiwa hadi itakapotangazwa tena.
Kulingana na tume hiyo, majukwaa kadhaa ya mitandao ya kijamii yalisalia kuwekewa vikwazo. Programu hizo ni pamoja na WhatsApp, TikTok, X (zamani Twitter), Instagram, Telegram na app stores, huku Facebook ikiendelea kusimamishwa tangu 2021.
Soma zaidi:
Sudan Kusini yawaamuru wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na raia kuondoka Jimbo la Jonglei
Jeshi la Sudan Kusini limewaamuru raia wote na wafanyakazi kutoka Umoja wa Mataifa na mashirika mengine yote ya kutoa misaada kuondoka katika kaunti tatu katika Jimbo la Jonglei kabla ya operesheni dhidi ya vikosi vya upinzani kuanza.
Mapigano ambayo Umoja wa Mataifa unasema yanatokea kwa kiwango ambacho hakijawahi onekana tangu 2017 yamekuwa yakiikumba Sudan Kusini, nchi changa zaidi barani Afrika, kwa miezi kadhaa.
Baadhi ya mapigano makali zaidi yametokea huko Jonglei, iliyoko mashariki mwa nchi hiyo kwenye mpaka na Ethiopia, ambapo Kikosi cha Ulinzi cha Wananchi wa Sudan Kusini (SSPDF) kinataka kuzuia mashambulizi ya wapiganaji wanaotii Jeshi la Ukombozi wa Wananchi wa Sudan (SPLA-IO).
Operesheni iliyopewa jina la "operesheni ya kudumisha amani" "imekaribia," SSPDF ilisema katika taarifa siku ya Jumapili.
Jeshi lilisema raia wote wanaoishi katika kaunti za Nyirol, Uror na Akobo huko Jonglei "wameagizwa kuhama mara moja kwa ajili ya usalama wao kwenda katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali haraka iwezekanavyo."
Wafanyakazi wote kutoka Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) na wale wanaofanya kazi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali pia waliamriwa kuhama kaunti hizo tatu ndani ya saa 48.
Wiki iliyopita SPLA-IO ilitoa wito kwa vikosi vyake kwenda mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, na kuashiria ongezeko la mapigano.
Mapema mwezi huu vikosi vya SPLA-IO viliuteka mji wa Pajut katika mapigano makali kaskazini mwa Jonglei na kutekwa kwa mji huo kulionekana kama kuuweka mji mkuu wa jimbo la Bor hatarini.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, UNMISS ilisema watu 180,000 katika jimbo hilo tayari wameyakimbia makazi yao kutokana na mzozo huo na kuwasihi viongozi wa Sudan Kusini "kutanguliza maslahi ya watu wao kwa kusimamisha mapigano."
Shirika la hisani la madaktari Médecins Sans Frontières (MSF) lilisema katika taarifa Jumapili kwamba limewahamisha wafanyakazi muhimu kutoka kaunti ya Akobo baada ya "maagizo kutoka serikalini na, na kutokana na hali mbaya ya usalama katika eneo hilo."
Vikosi vya SPLA-IO vikiongozwa na makamu wa rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, vilipambana na jeshi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2013-18, ambavyo vilipiganwa kwa misingi ya kikabila na kuua watu wapatao 400,000.
Mkataba wa amani mwaka 2018 ulituliza mzozo huo, ingawa mapigano ya ndani yameendelea.
Pia unaweza kusoma:
Watu wenye silaha waua watu 11 katika uwanja wa mpira Mexico
Kundi la washambuliaji wenye silaha limewaua watu 11 na kuwajeruhi 12 katika uwanja wa soka baada ya mechi katika jiji la Salamanca huko Mexico, amesema meya Cesar Prieto, kwenye Facebook siku ya Jumapili.
Prieto aliongeza kuwa mwanamke na mtoto ni miongoni mwa waliojeruhiwa katika shambulio la "kusikitisha" dhidi ya jamii ya Loma de Flores.
Uchunguzi umeanzishwa kuhusu shambulio hilo, imesema ofisi ya mwanasheria mkuu katika jimbo la Guanajuato.
"Wale waliohusika watapatikana," Prieto aliongeza katika maelezo yake ya Facebook.
Bado haijafahamika sababu ya shambulio hilo lakini Guanajuato ni mojawapo ya majimbo hatari zaidi nchini Mexico.
Pia unaweza kusoma:
Watu saba wamefariki kutokana na dhoruba ya theluji Marekani
Dhoruba hatari ya majira ya baridi imeikumba Marekani, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua saba na kukata umeme kwa maelfu ya nyumba.
Shule na barabara kote nchini zimefungwa na safari za ndege zimefutwa huku theluti mbaya ikienea kutoka Texas hadi New England, kulingana na Mamlaka ya Kitaifa ya Hali ya Hewa (NWS).
Watu wawili wamefariki kutokana na baridi kali huko Louisiana, na vifo vingine vinavyohusishwa na dhoruba hiyo vimeripotiwa huko Texas, Tennessee na Kansas.
Kufikia Jumapili alasiri, zaidi ya kaya 800,000 zimepoteza umeme, kulingana na poweroutage.us. Wakati huo huo, zaidi ya safari za ndege 11,000 zimefutwa, imeripoti FlightAware.
Theluji nzito inaweza kuathiri takribani Wamarekani milioni 180 - zaidi ya nusu ya idadi ya watu.
"Theluji na barafu zitayeyuka polepole sana na hazitatoweka hivi karibuni," Allison Santorelli, mtaalamu wa hali ya hewa katika Mamlaka ya Kitaifa ya Hali ya Hewa, ameiambia CBS News.
Idara ya Afya ya Louisiana imethibitisha Jumapili kwamba wanaume wawili wamefariki kutokana na baridi kali.
Meya wa Austin, Texas, amesema mtu mmoja amefariki kutokana na baridi.
Maafisa huko Kansas wamesema mwanamke, ambaye mwili wake ulipatikana Jumapili alasiri ukiwa umefunikwa na theluji, "huenda alikufa kutokana na baridi."
Vifo vya watu watatu vinavyohusiana na hali ya hewa pia vimeripotiwa huko Tennessee.
Meya wa Jiji la New York Zohran Mamdani aliandika katika chapisho kwenye X kwamba watu watano katika jiji hilo walifariki Jumamosi lakini akaongeza kuwa chanzo cha vifo vyao bado hakijabainika.
Marekani inakumbwa na moja ya dhoruba kubwa zaidi za theluji katika zaidi muongo mmoja
Wataalamu wa hali ya hewa wameonya kwamba moja ya hatari kubwa za dhoruba hiyo ni barafu, ambayo ina uwezo wa kuharibu miti, kuangusha nyaya za umeme na kufanya barabara kuwa hatari.
Huko Virginia na Kentucky, kumetokea mamia ya ajali barabarani.
Wacanada pia wamekumbwa na theluji kubwa na mamia ya safari za ndege zilizofutwa.
Maafisa wanakadiria kwamba kutakuwa na theluji ya sentimita 15-30 (inchi 5-11) katika jimbo la Ontario.
Dhahabu yapanda thamani kutokana na mivutano ya kisiasa na kiuchumi
Bei ya dhahabu imepanda kwa zaidi ya dola za kimarekani 5,000 (£3,659) kwa gramu 28.35 kwa mara ya kwanza, ni ongezeko la thamani kwa zaidi ya 60% mwaka 2025.
Hii inakuja huku mvutano kati ya Marekani na NATO kuhusu Greenland ukiongeza wasiwasi kuhusu fedha na siasa.
Sera za biashara za Rais wa Marekani Donald Trump pia zimetia wasiwasi masoko. Siku ya Jumamosi alitishia kuitoza Canada ushuru wa asilimia 100 ikiwa itaingia makubaliano ya kibiashara na China.
Dhahabu na madini mengine ya thamani huonekana kama mali salama ambapo wawekezaji hununua wakati wa wasiwasi katika biashara.
Mahitaji ya madini ya yamechochewa na mambo mengine mbalimbali ikiwa ni pamoja na mfumuko wa bei, dola dhaifu ya Marekani, manunuzi ya benki kuu kote ulimwenguni na huku Hifadhi ya Shirikisho ya Marekani ikitarajiwa kupunguza viwango vya riba tena mwaka huu.
Vita nchini Ukraine na Gaza, pamoja na Washington kumkamata Rais wa Venezuela Nicolás Maduro, pia vimesaidia kuongeza bei ya dhahabu.
Pia unaweza kusema:
Watu 15 wafariki baada ya feri kuzama Ufilipino
Watu wasiopungua 15 wamefariki baada ya feri iliyokuwa imebeba abiria zaidi ya 350 na wafanyakazi wake kuzama kwenye maji ya pwani ya kusini mwa Ufilipino.
Wafanyakazi wa uokoaji wamewaokoa watu 316 waliokuwa ndani ya meli ya MV Trisha Kerstin 3, lakini watu 28 bado hawajulikani walipo.
Meli hiyo, ambayo ilikuwa ya mizigo na abiria, ilikuwa njiani kutoka kusini mwa nchi, Mindanao, kwenda kisiwa cha Jolo kusini-magharibi siku ya Jumatatu.
Serikali inasema wanachunguza chanzo cha kuzama.
Ufilipino - taifa la visiwa 7,100 - lina historia ndefu ya majanga ya baharini yanayohusisha feri.
Mei 2023, watu 28 walifariki baada ya kivuko cha abiria kushika moto. Waliofariki ni pamoja na watoto watatu, miongoni mwao mtoto wa miezi sita.
PIa unaweza kusoma:
Umeme wakatika na vifo vyatangazwa kutokana na dhoruba ya theluji Marekani
Dhoruba ya theluji imeikumbuka Marekani, na kusababisha vifo vya watu watatu na kukosa umeme kwa maelfu ya nyumba.
Shule na barabara kote nchini zimefungwa na safari za ndege zimefutwa huku hali "inayohatarisha maisha" ikienea kutoka Texas hadi New England, kulingana na Mamlaka ya Kitaifa ya Hali ya Hewa (NWS).
Watu wawili wamefariki kutokana na baridi kali huko Louisiana, huku maafisa wa afya wa jimbo wakihusisha vifo vyao na dhoruba hiyo, na kifo kingine kimeripotiwa huko Texas.
Kufikia Jumapili alasiri, takriban kaya 900,000 zilikuwa zimepoteza umeme, kulingana na poweroutage.us. Wakati huo huo, zaidi ya safari 10,000 za ndege zimefutwa, FlightAware iliripoti.
"Theluji na barafu zitayeyuka polepole sana na hazitatoweka hivi karibuni," amesema Allison Santorelli, mtaalamu wa hali ya hewa katika Mamlaka ya Kitaifa ya Hali ya Hewa, ameiambia CBS News.
Pia unaweza kusoma:
Venezuela yawaachilia huru wafungwa kadhaa wa kisiasa
Kundi moja la kutetea haki za binadamu nchini Venezuela linasema takribani wafungwa 80 wa kisiasa wameachiliwa huru kutokana na shinikizo la Marekani.
Alfredo Romero, mkuu wa shirika la Foro Penal, amesema shirika lake linathibitisha utambulisho wa wale walioachiliwa siku ya Jumamosi - na kuna uwezekano wa kuachiliwa wengi zaidi.
Hilo linatokea tangu Marekani ilipomkamata Rais wa Venezuela Nicolás Maduro, na kumpeleka New York kushtakiwa kwa biashara haramu ya dawa za kulevya mapema mwezi huu.
Siku ya Ijumaa Rais wa mpito wa Venezuela Delcy Rodriguez alisema zaidi ya wafungwa 600 wameachiliwa huru - lakini Foro Penal inasema takwimu hii imetiwa chumvi.
Romero alitangaza taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii. Pia alichapisha picha ya mfanyakazi mwenzake wa Foro Penal, Kennedy Tejeda ambaye amesema alishikiliwa katika gereza la Tocorón, magharibi mwa mji mkuu wa Caracas tangu Agosti 2024.
Makundi ya haki za binadamu na wanaharakati wanaishutumu serikali kwa kuwashikilia wakosoaji. Serikali ya Venezuela imekana kuwashikilia wafungwa wa kisiasa, ikisisitiza kwamba walikamatwa kwa shughuli za uhalifu.
Wengi walikamatwa baada ya uchaguzi wa rais wa 2024, wakati Maduro alipodai ushindi licha ya upinzani na nchi nyingi kupinga matokeo hayo.
Pia unaweza kusoma:
Waandamanaji wakusanyika Marekani baada ya afisa wa uhamiaji kutekeleza mauaji
Umati wa watu umekusanyika Minneapolis, Marekani kupinga uwepo wa maafisa wa uhamiaji wa shirikisho katika jimbo hilo, baada ya kupigwa risasi na kuuawa Alex Pretti mwenye umri wa miaka 37.
Gavana wa Minnesota Tim Walz ametoa wito kwa Rais wa Marekani, Donald Trump kuwaondoa maafisa hao wa shirikisho katika jimbo lake, akisema: "Huu ni wakati wa mabadiliko."
Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social, Rais wa Marekani Donald Trump amesema Walz na Meya wa Minneapolis Jacob Frey wanapaswa kuwasalimisha "wahamiaji wote haramu wahalifu" waliofungwa katika magereza ya serikali kwa ajili ya kuwafukuza nchini.
Maafisa wa jimbo na shirikisho wametoa maelezo yanayokinzana kuhusu tukio la kifo cha Pretti siku ya Jumamosi.
Alipoulizwa kuhusu video zilizoibuka zikionyesha tukio hilo la mauaji, Kamanda wa Doria ya Mpakani Greg Bovino anasema kuna haja ya kuwepo kwa uchunguzi ili kubaini ukweli.
Pia unaweza kusoma:
Hujambo na karibu
Nikukaribishe katika taarifa zetu za moja kwa moja, leo Jumatatu ya tarehe 26, Januari 2026