Kombe la Dunia 2026: Sera za Trump zitaathiri mashindano hayo?

Muda wa kusoma: Dakika 7

Kundi la wabunge wa vyama mbalimbali wameitaka Fifa kuiondoa Marekani kwenye Kombe la Dunia hadi nchi hiyo itakapo kubali "kufuata sheria za kimataifa na kuheshimu uhuru wa mataifa mengine."

Ni baada ya kukamatwa kwa kiongozi wa Venezuela Nicolas Maduro na vikosi vya Marekani katika shambulio dhidi ya mji mkuu Caracas mwezi huu, pamoja na maonyo ambayo rais wa Marekani Donald Trump ametoa hivi karibuni kwa nchi nyingine nyingi.

Marekani inatarajiwa kuandaa Kombe la Dunia na Olimpiki katika kipindi cha miaka miwili na nusu ijayo.

Mwezi Desemba, Fifa ilimpa Trump 'Tuzo ya Amani' katika sherehe ya kupanga makundi ya Kombe la Dunia la 2026 huko Washington, ikisema "alikuwa na jukumu muhimu" katika kuanzisha usitishaji mapigano na kukuza amani kati ya Israel na Palestina, na amejitahidi kukomesha migogoro mingine.

Katika wiki chache zilizopita, Marekani imechukua hatua za kijeshi nchini Venezuela na Nigeria na imedokeza uwezekano wa operesheni huko Greenland, pia dhidi ya mwenyeji mwenzake wa Kombe la Dunia Mexico, na washiriki wengine wawili katika mashindano hayo - Colombia na Iran.

Wanasiasa 25 kutoka chama cha Labour, chama cha Lib Dems, chama cha Green Party na Plaid Cymru wamesaini hoja bungeni, wakitoa wito kwa mashirika ya michezo ya kimataifa kuiondoa Marekani katika mashindano makubwa ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Kombe la Dunia.

Wanasema matukio ya michezo "hayapaswi kutumiwa kuhalalisha ukiukwaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na mataifa yenye nguvu."

Wabunge wanaelezea wasiwasi wao kuhusu "vitendo vya Marekani dhidi ya Venezuela," ikiwa ni pamoja na "kutekwa nyara kwa Rais Nicolas Maduro," wakidai ni sawa na "kuingilia moja kwa moja masuala ya ndani ya taifa huru."

Hoja yao pia inabainisha "vitisho vilivyojificha na vya wazi vinavyotolewa na maafisa wakuu wa Marekani," dhidi ya Denmark, Colombia na Cuba," na kusema "vinadhoofisha utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria."

Marekani imefanya nini?

Ikulu ya White House bado haijatoa jibu kwa BBC kuhusu hoja ya wabunge hao, lakini katika siku za nyuma ilidai kukamatwa kwa Maduro ni operesheni ya kutekeleza sheria dhidi ya kiongozi haramu anayehusika na biashara haramu ya dawa za kulevya na ugaidi. Trump alisema Marekani sasa itaidhibiti Venezuela na uzalishaji wake wa mafuta.

Maduro anasisitiza kwamba yeye ni mfungwa wa vita, na Trump alikabiliwa na ukosoaji mkali katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema "ana wasiwasi mkubwa kwamba sheria za kimataifa hazijaheshimiwa" wakati wa operesheni hiyo ya Marekani.

Wakati huo huo, Trump pia ameiambia Cuba "kuingia kwenye makubaliano" kuhusu kununua mafuta ya Venezuela "kabla haijachelewa," na akasema operesheni ya kijeshi dhidi ya Colombia "ni kitu kizuri."

Kama ilivyo kwa Venezuela, Trump ameishutumu Colombia kwa kutofanya vya kutosha kukabiliana na biashara haramu ya dawa za kulevya. Rais wa Colombia Gustavo Petro ameiambia BBC anaamini kuna "tishio la wazi" la hatua za kijeshi kutoka Marekani dhidi ya nchi yake.

Trump pia amedai dawa za kulevya "zinamiminika" kupitia Mexico hadi Marekani, na kusema "itabidi tufanye jambo," huku kukiwa na ripoti kwamba ameanza kupanga misheni ya kutuma wanajeshi wa Marekani kwenda Mexico.

Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum amekataa pendekezo lolote la hatua za kijeshi kutoka Marekani katika ardhi ya Mexico.

Trump pia amesisitiza nchi yake inataka kuichukua Greenland kwa sababu za usalama wa taifa na hajakataa uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi. Ametangaza ataweka ushuru mpya kwa washirika wanane wa Ulaya wanaopinga pendekezo lake la kuichukua Greenland.

Kisiwa hicho cha Aktiki chenye utajiri wa madini kinadhibitiwa na Denmark, mwanachama mwenzake wa Nato, na pengine pia itashiriki Kombe la Dunia ikiwa timu hiyo itafuzu katika mechi za mchujo.

Utawala wa Trump pia unakabiliwa na maswali kuhusu uhalali wa mashambulizi ya anga dhidi ya boti zinazodaiwa kuwa za dawa za kulevya kimagendo katika Bahari ya Karibi na Pasifiki Mashariki.

Fifa itachukua hatua?

Fifa imekataa kutoa maoni kuhusu hoja ya wabunge hao, na hakuna muelekeo kwamba itafikiria upya kuhusu tuzo yake ya amani.

Ni wachache wanaoamini itachukua hatua yoyote dhidi ya nchi ambayo inaandaa mechi zake nyingi kwenye Kombe la Dunia, hasa kutokana na uhusiano wa karibu ambao rais wa shirikisho hilo Gianni Infantino anao na Trump.

Uhusiano kama huo umesababisha shutuma kwamba Fifa imejiingiza katika siasa, ingawa inasisitiza kwamba kama mratibu wa matukio ya mpira wa miguu ina wajibu wa kisheria kutoegemea upande wowote.

Hii si mara ya kwanza kwa Fifa kukumbwa na shinikizo kutokana na vitendo vya mwenyeji wa Kombe la Dunia.

Mwaka 2018, mashindano hayo yalifanyika nchini Urusi licha ya nchi hiyo kuinyakua Crimea miaka minne iliyopita. Urusi pia ilikosolewa kwa mashambulizi ya mtandaoni, kuingilia chaguzi za nchi za magharibi na kutekeleza shambulio la sumu ya Novichok huko Salisbury, Uingereza.

Hata hivyo Fifa imeipiga marufuku Urusi baada ya uvamizi wake nchini Ukraine mwaka 2022, adhabu ambayo bado ipo.

Baadhi ya maafisa wa Fifa wanaeleza faraghani kwamba Shirikisho la Soka la Urusi bado ni mwachama na marufuku dhidi ya Urusi kutocheza michezo ya kimataifa ilitokana zaidi na timu kukataa kucheza dhidi ya Urusi na wasiwasi wa usalama, na sio kutokana na msimamo wa kimaadili wa Fifa.

Mwezi Oktoba, rais Infantino alisema, Fifa "haiwezi kutatua matatizo ya kijiografia na kisiasa" wakati huo kulikuwa na shinikizo la kuiwekea vikwazo Israel baada ya tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhitimisha kwamba imefanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Wizara ya mambo ya nje ya Israel iliikataa ripoti hiyo na kuilaani kuwa "inapotosha na ni ya uwongo."

Vipi kuhusu Olimpiki?

Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) pia imepiga marufuku timu za Urusi, huku wana michezo kutoka Urusi wakiruhusiwa kushindana kama wana michezo huru, madam tu wako chini ya mashirikisho ya michezo yanayotambulika.

Hata hivyo, Kamati hiyo imeondoa uwezekano wa mwanamichezo yeyote wa Marekani kupigwa marufuku kwenye Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Februari huko Milan na Cortina nchini Italia.

Katika taarifa iliyotolewa kwa BBC Sport, imesema: "Uwezo wa kuwaleta wanariadha pamoja, bila kujali wanatoka wapi, ni muhimu kwa mustakabali wa michezo ya kimataifa."

"Kwa sababu hii, IOC haiwezi kujihusisha moja kwa moja na masuala ya kisiasa au migogoro kati ya nchi, kwani haya yanaangukia nje ya mamlaka yetu. Huo ni ulimwengu wa siasa."

Mwaka jana, IOC ilikataa wito wa kuizuia Israel kutokana na vita vya Gaza, ikisema kamati ya kitaifa ya Olimpiki ya nchi hiyo imefuata Mkataba wa Olimpiki.

Vyanzo ndani ya IOC vimeiambia BBC Sport, Urusi ilipochukua udhibiti wa eneo la Ukraine, iliwaweka wana michezo wa eneo hilo chini ya udhibiti wa Kamati ya Olimpiki ya Urusi, jambo ambalo ni kinyume na Mkataba wa Olimpiki.

Los Angeles, Marekani inaandaa Michezo ya Olimpiki mwaka 2028.

Hatari inayojongea

Baadhi wanaamini, hatua za Trump, zinaweza kuifanya hali kuwa ngumu kwa mashirika ya michezo.

"Fifa na IOC huenda zikaingia kwenye tatizo moja kubwa," kulingana na John Zerafa, mshauri mkongwe katika kuandaa matukio makubwa ya michezo.

"Mikataba ya mashirika yote mawili inasisitiza amani, kuheshimu mipaka, na kutobaguana.

"Katika kesi ya Urusi, hilo lilisababisha marufuku na vikwazo kwa wanariadha na timu. Ikiwa Marekani itatumia nguvu dhidi ya Greenland – Je, kanuni hizo hizo zitatumika?

Ikiwa Denmark itafuzu kuingia kombe la Dunia: Je, itasusia Kombe la Dunia? Je, viongozi wa Ulaya au Nato watakataa kuhudhuria matukio yanayoandaliwa na Marekani?

"Hizi si siasa za kijiografia tu. Ni mtihani unaokuja kwa taasisi za michezo zinazojivunia kutoegemea upande wowote, lakini mara kwa mara hujikuta wakilazimika kuchukua misimamo ya kisiasa wakati sheria na migogoro ya kimataifa inapogongana na ushindani wa kimataifa."

Sera kali za uhamiaji za Trump zinaweza pia kuwa na athari kwenye Kombe la Dunia, litakaloanza tarehe 11 Juni.

Fifa na Marekani zimeahidi mashindano hayo yatakaribisha watu wote na kuwaunganisha, lakini kuna nchi nne - Iran, Haiti, Senegal na Ivory Coast - ambazo mashabiki wake wanakabiliwa na marufuku ya kutoingia Marekani, huku Ikulu ya White House ikitaja hitaji la kudhibiti usalama.

Hata hivyo, Kikosi Kazi cha Ikulu cha Kombe la Dunia hakijakataa uwezekano wa uvamizi wa Maafisa wa Uhamiaji na Forodha (ICE) kuwalenga wahamiaji wasio na vibali katika viwanja vya Kombe la Dunia.

Wakati huo huo, mvutano wa ndani nchini Marekani umeongezeka baada ya Renee Good, mwenye umri wa miaka 37, kupigwa risasi na afisa wa uhamiaji huko Minneapolis wiki iliyopita, na kusababisha maandamano makubwa jijini humo.

Chama cha Democratic cha Ulaya (EDP) kinasema kinaweza kuyaomba mashirikisho ya soka ya kitaifa kufikiria kujiondoa kwenye mashindano hayo ikiwa hakutokuwa na dhamana ya usalama kutoka Marekani.

Huku mashindano makubwa zaidi kuwahi kutokea ya Fifa yakikaribia, ni jambo la kusubiri na kuona kama sera za Marekani ndani na nje ya nchi zitakuwa na athari kwenye mauzo ya tiketi, ushirikiano kati ya waandaaji wenza, na ikiwa mashirika ya michezo yanahitaji kufanya zaidi katika mazingira magumu ya kisiasa na kijiografia.