Kwa nini wanasoka Afrika hawasemi ukweli kuhusu umri wao?

Wachezaji kusema uongo kuhusu umri wao katika soka la dunia ni tatizo ambalo mamlaka imekuwa ikihangaika kulielewa kwa muda mrefu.

Katika soka, kughushi umri kunatokea pale mchezaji wa soka anapodai umri tofauti na umri wake halisi.

Gumzo la wachezaji kughushi umri limeibuka tena baada ya Cameroon kutangaza kuwa inawachunguza wanasoka 44 kwa tuhuma za kughushi umri au utambulisho wao.

Iwapo watapatikana na hatia wanakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kwa miezi sita kwenye mechi, afisa wa Fecafoot aliiambia BBC.

Shutuma za ulaghai wa umri ni za kawaida nchini Cameroon. Mnamo 2016, wachezaji 14 wa Cameroon walifungiwa kwa siku chache kabla ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya wachezaji wa chini ya miaka 17.

Umri wao wa kweli ulifichuliwa kupitia uchunguzi wa MRI, ambao hutoa picha za kina za ndani ya mwili.

Kwanini wachezaji wanasema uwongo?

Kumekuwa na nadharia tofauti kuhusu sababu za wachezaji kujifanya kuwa wadogo kuliko umri wao.

Mwandishi wa habari wa kandanda barani Afrika Oluwashina Okeleji anataja matamanio ya binafsi, shinikizo la kufaulu na urahisi wa kudanganya umri wako kama sababu za kufanya hivyo.

''Ni ngumu sana kwa wachezaji chipukizi kwenda kucheza nje ya nchi na inaweza kuchukua muda mrefu kiasi kwamba wana umri mkubwa sana wanapoonekana, hivyo lazima wapunguze umri labda kwa miaka 10,” alisema.

"Sababu nyingine ni shinikizo kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 na 20 ili kupata mafanikio. Baadhi ya makocha hawa wanalazimika kusajili wachezaji wenye umri mkubwa zaidi."

Mkurugenzi wa zamani wa vyombo vya habari katika Shirikisho la Soka Afrika (Caf) Junior Binyam, anakiri kuwa udanganyifu wa umri ni tatizo barani Afrika kwa sababu nchi hazina kanzidata ya kutegemewa kufuatilia umri.

Pia unaweza kusoma:

Alisema: "Ni rahisi katika nchi nyingi kubadili umri au 'kurekebisha' rejista hizo. Si nadra kukuta watu wenye cheti cha kuzaliwa zaidi ya kimoja.

"Katika baadhi ya matukio, mchezaji anapobadilisha utambulisho, anaweza kusajiliwa kama mchezaji mpya.

Udanganyifu wa umri huathiri programu za maendeleo ikiwa wachezaji wanaohusika katika kitengo cha umri sio wa kikundi hicho. "Kutokana na uhaba wa nyaraka za kisheria za kufafanua umri katika Afrika, Koufie anaamini mkanganyiko huo unaweza moja ya sababu ya kile kinachoitwa udanganyifu wa umri.

Alipoulizwa kuhusu ushindi wa Ghana wa Kombe la Dunia la Vijana chini ya miaka 17 mwaka 1991, alikiri baadhi ya wachezaji hawakujua umri wao halisi. Alisema: "watu wengi hawajui walizaliwa lini. Wakati mwingine wanakisia. Ni kweli tuna matatizo Afrika, ndiyo maana tuna shaka kuhusu hilo, iwe ni udanganyifu wa kweli au la."

Tatizo hili ni kubwa kaiasi gani

Sio siri kuwa baadhi ya timu za vijana za Kiafrika mara nyingi hushukiwa kuwa na wachezaji waliozidi umri, huku kashfa za umri zikikumba Nigeria, Ghana na Kenya siku za nyuma.

Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Nigeria Jonathan Akpoborie, 54, anasema udanganyifu wa umri "umekithiri" katika soka la Afrika na anaelezea kama "tatizo kubwa" ambalo linakabili mchezo huo.

Mnamo Aprili 2013, wachezaji tisa waliondolewa kwenye michuano ya Afrika ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 nchini Morocco baada ya vipimo vya kifundo cha mkono vya MRI kuonyesha kuwa wamevuka kikomo cha umri.

Congo-Brazzaville, Ivory Coast na Nigeria kila moja ilikuwa na wachezaji watatu waliopigwa marufuku.

Baadaye mwaka huo, Nigeria ilipoteza wachezaji kadhaa muhimu kushiriki Kombe la Dunia la wachezaji wa chini ya miaka 17 mwezi Oktoba kwa sababu hiyo hiyo, huku Somalia ikitimuliwa kwenye michuano ya Afrika ya U-17 ya 2013 kwa kuchezesha wachezaji waliozidi umri.

Akpoborie, ambaye sasa anafanya kazi kama wakala, anakiri kuwafahamu wachezaji wengi ambao "walidanganya" kuhusu umri wao katika soka la Afrika.

Aliambia BBC Sport: "Limekuwa tatizo kubwa na bado lipo. Baadhi yao walicheza katika kiwango cha Under-17 na kisha miaka michache baadaye kustaafu kwa sababu hawawezi kukimbia tena.

“Ukiangalia wachezaji wa Kiafrika wanaocheza chini ya umri wa miaka 17, labda mwaka mmoja au miwili baadaye wamestaafu kwa sababu hawawezi kuwasilisha stakabadhi walizotoa katika kiwango cha chini ya miaka 17 kwa sababu umri wao ni mkubwa, wachezaji wasio sahihi wanapewa. jukwaa." Si kwamba hili ni tatizo jipya.

Fifa iliifungia Nigeria kushiriki katika mechi zote za kimataifa kwa miaka miwili baada ya kubaini kuwa tarehe za kuzaliwa kwa wachezaji wake watatu katika Michezo ya Olimpiki ya 1988 zilikuwa tofauti na zile zilizotumiwa na wachezaji hao katika mashindano yaliyopita.

Mnamo 2003, timu ya taifa ya Kenya ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ilivunjwa na serikali baada ya baadhi ya wachezaji kukiri kuwa na umri mkubwa.

Je, ni nini kinafanyika kukabiliana na suala hili?

Mnamo mwaka 2009 Shirikisho la Soka Duniani Fifa, lilianzisha matumizi ya picha ya sumaku (MRI) wakati wa michuano ya Kombe la Dunia la Vijana wasiozidi umri wa miaka 17 nchini Nigeria ili kusaidia kujua iwapo wachezaji wamezidi umri au la.

Dkt Yacine Zerguini, Naibu wa Rais wa sasa wa kamati ya matibabu ya Fifa na Caf, alisema wakati huo: "Tunajua kwamba wachezaji hawafanyi hivyo kwa kudhamiria wana zaidi ya miaka 17.

"Katika baadhi ya nchi, vyeti vya kuzaliwa si sahihi au hata havipatikani, bila hiyo kuwa kosa la mchezaji au chama."

MRI hutumika kuchanganua kifundo cha mkono cha kushoto cha wachezaji ili kupata kwa usahihi umri wao halisi.

Binyam alisema kamati ya utendaji ya Caf iliiagiza kamati yake ya matibabu wakati huo kuchunguza kuendeleza matumizi yake kwenye mashindano ya vijana wa chini ya miaka 20.

Wataalamu wa Soka wanasema kuanzishwa kwa uchunguzi wa MRI kumekuwa na mafanikio na pia kusifu juhudi zinazofanywa na serikali binafsi.

Nchini Nigeria serikali kwa mfano imeweka mpango mpya ambapo kila mtoto anayesoma shule anapewa namba maalum ya utambulishoamboa unasalia shuleni.

"Bila nambari hiyo huwezi kucheza ligi za vijana, mtu kama mimi ambaye ni wakala anaweza kuchukua mchezaji ambaye ana nambari hiyo, natumai shirikisho zima litatumia mfumo huo.

"Ni tatizo ambalo utatuzi wake unahitaji ushirikiano wa washikadau wote."