Venezuela yawaachilia huru wafungwa kadhaa wa kisiasa

Chanzo cha picha, EPA
Kundi moja la kutetea haki za binadamu nchini Venezuela linasema takribani wafungwa 80 wa kisiasa wameachiliwa huru kutokana na shinikizo la Marekani.
Alfredo Romero, mkuu wa shirika la Foro Penal, amesema shirika lake linathibitisha utambulisho wa wale walioachiliwa siku ya Jumamosi - na kuna uwezekano wa kuachiliwa wengi zaidi.
Hilo linatokea tangu Marekani ilipomkamata Rais wa Venezuela Nicolás Maduro, na kumpeleka New York kushtakiwa kwa biashara haramu ya dawa za kulevya mapema mwezi huu.
Siku ya Ijumaa Rais wa mpito wa Venezuela Delcy Rodriguez alisema zaidi ya wafungwa 600 wameachiliwa huru - lakini Foro Penal inasema takwimu hii imetiwa chumvi.
Romero alitangaza taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii. Pia alichapisha picha ya mfanyakazi mwenzake wa Foro Penal, Kennedy Tejeda ambaye amesema alishikiliwa katika gereza la Tocorón, magharibi mwa mji mkuu wa Caracas tangu Agosti 2024.
Makundi ya haki za binadamu na wanaharakati wanaishutumu serikali kwa kuwashikilia wakosoaji. Serikali ya Venezuela imekana kuwashikilia wafungwa wa kisiasa, ikisisitiza kwamba walikamatwa kwa shughuli za uhalifu.
Wengi walikamatwa baada ya uchaguzi wa rais wa 2024, wakati Maduro alipodai ushindi licha ya upinzani na nchi nyingi kupinga matokeo hayo.
Pia unaweza kusoma:

