Moja kwa moja, Trump atishiwa kuuawa kwa 'mafumbo' kupitia Televisheni ya Iran

Pande zote mbili zimekuwa zikionya mara kwa mara kuhusu madhara ya shambulio lolote.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Ufaransa yaidhinisha mswada wa kupiga marufuku mitandao ya kijamii kwa watoto chini ya miaka 15

    Chini ya pendekezo hilo, orodha ya mitandao ya kijamii inayoonekana kuwa na madhara itapigwa marufuku kwa watoto wa chini ya miaka 15.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Chini ya pendekezo hilo, orodha ya mitandao ya kijamii inayoonekana kuwa na madhara itapigwa marufuku kwa watoto wa chini ya miaka 15.

    Wabunge wa Ufaransa wamepitisha mswada ambao utawapiga marufuku vijana wa chini ya umri wa miaka 15 nchini humo kuwa katika mitandao ya kijamii.

    Mswada huo uliopitishwa katika Bunge la kitaifa sasa utapelekwa kwa Baraza la Seneti ili kupitishwa kuwa sheria.

    Rais Emmanuel Macron ameitaja kuwa hatua muhimu kuelekea kuwalinda watoto wa Ufaransa.

    Maafisa wa Serikali wanatumai kuwa mswada huo utaidhinishwa haraka kuwa sheria ili ianze kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka mpya wa masomo nchini humo unaoanza mwezi Septemba.

    Sheria hiyo ikipitishwa,itapiga pia marufuku wanafunzi kwenda shuleni na simu za mkononi.

    Mwezi uliopita,Australia ilikuwa nchi ya kwanza kupiga marufuku mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 16.

    Soma pia:

  2. Marekani yaonesha picha za ndani ya meli ya kivita Abraham Lincoln inayoelekea Iran

    f

    Chanzo cha picha, US Central Command

    Kamandi kuu ya jeshi la Marekani ya Kati (CENTCOM) imetoa picha mpya zilizopigwa ndani ya meli ya kivita ya ndege, USS Abraham Lincoln (CVN-72).

    Picha hizo zinaonesha wanajeshi wakiwa ndani ya meli, wakifanya kazi za matengenezo ya kawaida huku meli ikiwa safarini katika Bahari ya Hindi, Januari 26.

    Tamko hilo liliendelea kufafanua kwamba kundi la mashambulio la meli ya Abraham Lincoln limepelekwa Mashariki ya Kati ili kuimarisha usalama na utulivu katika eneo hilo.

    Hapo awali, afisa mmoja wa serikali ya Marekani alithibitisha katika mahojiano na CBS kwamba kundi la mashambulio limeingia eneo la amri la CENTCOM Mashariki ya Kati, likiwemo Iran.

    Meli hiyo iliondoka katika eneo la Pasifiki la Asia Mashariki takriban wiki mbili zilizopita, ikiwa inaelekea Bahari ya Hindi na Bahari ya Oman, kufuatia ongezeko la mvutano kati ya Iran na Marekani.

    F

    Chanzo cha picha, US Central Command

    Soma pia:

  3. Hezbollah yatoa tamko dhidi ya Marekani

    Naim Qasim

    Chanzo cha picha, IRIB

    Maelezo ya picha, Naim Qasim

    Naim Qasim, Katibu Mkuu wa shirika la Hezbollah la Lebanon, aliwaambia wafuasi wake katika hotuba ya televisheni na mkutano wa umma wa kuunga mkono Iran: “Kama Marekani na Israel zitaanza vita na Iran, hatutakaa kimya.”

    Kiongozi wa Hezbollah wa Lebanon alisema: “Tunaona tishio la Marekani dhidi ya Iran kama tishio kwetu, na tuna nguvu kamili kuchukua hatua yoyote tunayoyaona inafaa kukabiliana nalo.”

    Hotuba ya Naim Qasim ilipeperushwa moja kwa moja kwenye Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

    Aliongeza: “Sisi hatutaunga mkono upande wowote katika suala la Iran, na tutatangaza hatua zetu wakati unaofaa,” akionya kuwa vita vipya na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinaweza “kuzuka tena katika eneo lote.”

    Miezi ya hivi karibuni, kumekuwa na mvutano wa maneno kati ya maafisa wa Iran na serikali ya Lebanon kuhusu usalimishaji wa silaha wa kundi hilo.

    Soma pia:

  4. UN yasisitiza utekelezaji kamili wa makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza

    Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wanakabiliwa na "ubaguzi wa kimfumo" na mamlaka ya Israel

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wanakabiliwa na "ubaguzi wa kimfumo" na mamlaka ya Israel

    Umoja wa Mataifa umesema ni muhimu sana kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yakatekelezwa kikamilifu baada ya mwili wa mateka wa mwisho wa Israeli kupatikana jana Jumatatu.

    Wanamgambo wa Hamas wamesema walisaidia katika kupatikana kwa mwili wa Ran Gvili kama sehemu ya kuonesha wamejitolea kuzingatia makubaliano kati yao na Israel.

    Umoja wa Mataifa umesema idadi kubwa inayovunja rekodi ya Wapalestina waliaachwa bila ya makazi katika Ukingo wa Magharibi mwaka jana.

    Zaidi ya watu elfu thelathini na saba walilazimika kuyahama makazi yao kwa kiasi kikubwa wakikimbia mashambulizi makali ya Israeli yaliyolenga kambi za wakimbizi kaskazini mwa Gaza.

    Soma zaidi:

  5. Afisa mkuu wa uhamiaji aondoka Minneapolis, Trump apeleka 'Tsar' wa mipaka Tom Homan eneo la tukio

    Gregory

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Meya wa mji wa Minneapolis, Marekani, Jacob Frey amesema amefanya mazungumzo ya tija na Rais Donald Trump na kumuomba akomeshe operesheni ya kuwasaka wahamiaji haramu inayoendeshwa na kikosi maalum cha maafisa wa uhamiaji, operesheni ambayo imesababisha kamata kamata kubwa na mauaji ya raia wawili.

    Msemaji wa Ikulu ya Rais Karoline Leavit amesema Rais Trump anataka uchunguzi kuendeshwa kikamilifu kuhusu matukio yaliyojiri Minneapolis.

    Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa uhamiaji nchini Marekani anatarajiwa kuondoka mjini Minneapolis, hatua inayotafsiriwa kama dalili ya mabadiliko ya msimamo wa Ikulu ya Marekani kufuatia kuuawa kwa raia wa pili wa Marekani kwa kupigwa risasi na maafisa wa ICE mwishoni mwa wiki.

    Wakati Kamanda wa Doria ya Mpakani Gregory Bovino na baadhi ya maajenti wa uhamiaji wakiondoka, “msimamizi wa mipaka” Tom Homan anatarajiwa kuongoza moja kwa moja shughuli za utekelezaji wa sheria eneo la Minnesota. Hatua hii inakuja baada ya tukio la Jumamosi lililosababisha kifo cha Alex Pretti na kuongeza mvutano.

    Uamuzi huo wa Rais Donald Trump unaonekana kuashiria nia ya utawala wake kupunguza au kurekebisha matumizi ya hatua kali za shirikisho katika operesheni yake ya kitaifa ya kudhibiti uhamiaji.

    Hata hivyo, licha ya mabadiliko hayo ya kiuongozi, ufuatiliaji wa shughuli za mtandaoni unaonyesha kuwa operesheni za ukaguzi na misako ya uhamiaji bado zinaendelea katika maeneo mbalimbali.

    Soma zaidi:

  6. Trump aongeza ushuru wa bidhaa zinazoagizwa Marekani kutoka Korea Kusini hadi 25%

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuwa ataongeza ushuru wa bidhaa zinazoingizwa kutoka Korea Kusini hadi kufikia asilimia 25.

    Hatua hiyo imekuja baada ya kumshutumu Seoul kwa “kutotekeleza ipasavyo” makubaliano ya biashara yaliyofikiwa mwaka jana.

    Kupitia ujumbe aliouandika kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema ataongeza ushuru huo kutoka asilimia 15 kwa bidhaa mbalimbali zikiwemo magari, mbao, dawa, na “ushuru mwingine wote wa kulipizana (reciprocal tariffs)”.

    Trump alisema kuwa wabunge wa Korea Kusini wamekuwa wakichelewa kuidhinisha makubaliano hayo, ilhali Marekani “imechukua hatua haraka kupunguza ushuru wake kulingana na makubaliano yaliyofikiwa”.

    Kwa upande wake, Korea Kusini imesema haijapewa taarifa rasmi kuhusu uamuzi wa kuongeza ushuru kwa baadhi ya bidhaa zake, na imeomba mazungumzo ya haraka na serikali ya Marekani juu ya suala hilo.

    Ushuru hulipwa na makampuni yanayoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi.

    Katika hali hii, makampuni ya Marekani yatalipa kodi ya asilimia 25 kwa bidhaa wanazonunua kutoka Korea Kusini.

    Trump amekuwa akitumia mara kwa mara ushuru kama njia ya kushinikiza au kutekeleza sera zake za kigeni katika muhula wake wa pili Ikulu.

    Jumamosi iliyopita, alitishia kuiwekea Canada ushuru wa asilimia 100 endapo ingeingia makubaliano ya biashara na China.

    Siku ya Jumatatu, maafisa wa China walisema kuwa makubaliano yao ya “ushirikiano wa kimkakati” na Canada hayalengi kudhoofisha au kuathiri nchi nyingine.

    Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, alisema nchi yake haifuatilii makubaliano ya biashara huria na China, na kwamba “haijawahi” kufikiria kufanya hivyo.

    Awali, Trump alisema angeweka ushuru wa kuagiza bidhaa kutoka nchi nane, zikiwemo Uingereza, ambazo zilipinga mpango wa Marekani wa kuichukua Greenland, eneo linalojitawala chini ya Ufalme wa Denmark, ambayo ni mwanachama wa NATO.

    Baadaye, Trump aliondoa tishio hilo la ushuru kuhusu Greenland, akisema kumekuwa na maendeleo kuelekea “makubaliano ya baadaye” juu ya kisiwa hicho.

    Hata hivyo, tukio hilo liliharibu uhusiano wa Marekani na Denmark pamoja na washirika wengine wa NATO.

  7. Trump atishiwa kuuawa kwa 'mafumbo' kupitia Televisheni ya Iran

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Baada ya meli ya kivita ya kubeba ndege Abraham Lincoln kuingia katika eneo la operesheni la CENTCOM Mashariki ya Kati, mvutano kati ya Tehran na Washington umeongezeka tena.

    Pande zote mbili zimekuwa zikionya mara kwa mara kuhusu madhara ya shambulio lolote.

    Shirika la Habari la Fars, ambalo liko karibu na Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, lilitoa video kadhaa siku ya Jumatatu za mahojiano yaliyofanywa kwenye kituo cha Ofogh cha Shirika la Utangazaji la Iran.

    Katika mahojiano hayo, Mostafa Khoshcheshem, mhadhiri wa chuo kikuu na mgeni kwenye kipindi hicho, anaelezea hali ya usalama nchini Iran baada ya kuuawa kwa waandamanaji kwa wingi.

    Pia anazungumzia kwa njia ya mafumbo suala la “kuuawa” kwa Rais wa Marekani Donald Trump, akilitaja kama “mshale usioonekana” na “msaada wa Mungu.”

    Donald Trump alisema katika mahojiano ya televisheni wiki iliyopita kwamba “ataifuta Iran kabisa kwenye uso wa dunia” endapo kutakuwa na jaribio lolote la kumuua.

    Soma Pia:

  8. Hujambo, na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja ya tarehe 27/01/2026.