Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Baraza la amani la Trump tishio jipya kwa Umoja wa Mataifa?
- Author, Lyse Doucet
- Nafasi, Chief International Correspondent, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 8
"Kwa pamoja, tuna fursa ya [...] kukomesha miongo kadhaa ya mateso, kukomesha vizazi vya chuki na umwagaji damu, na kujenga amani nzuri, ya kudumu na tukufu kwa eneo hilo na kwa ulimwengu wote."
Hii ilikuwa ahadi kabambe iliyotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump wiki hii alipokuwa akizindua Baraza jipya la Amani wakati wa Kongamano la Kiuchumi la Dunia huko Davos, Uswizi.
Lakini kwa waangalizi wengi na mamlaka duniani kote, huu ni uthibitisho zaidi wa nia ya Trump kufuta utaratibu wa kimataifa wa baada ya Vita vya Pili vya Dunia na badala yake kuweka taasisi mpya zinazotawaliwa naye.
"Hatutaruhusu mtu yeyote atudanganye," Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk alionya kwa ufupi kwenye mitandao ya kijamii.
Lakini pendekezo hilo lilipata sifa za kutosha kutoka kwa mfuasi mkuu wa Trump barani Ulaya - Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orbán: "Ikiwa ni Trump, basi kutakuwa na amani."
Baraza hili litafanya nini hasa, Trump mwenyewe akiwa rais wake wa maisha? Je, kweli hili linaweza kuwa pendekezo la kujenga UN ndogo.
Uwezo wa Mwenyekiti wa Bodi
Wazo hilo liliibuka mwaka jana wakati wa majaribio yaliyoongozwa na Marekani ya kumaliza vita katika Ukanda wa Gaza, iliyoidhinishwa na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Sasa, Baraza la Amani lina matarajio makubwa zaidi ya kimataifa, makubwa zaidi. Na inahusu rais wa Marekani.
Maelezo yaliyovuja kutoka kwa rasimu ya sheria zake yanaonyesha kuwa Trump ndiye mwenyekiti wa Baraza hilo kwa maisha yake yote, hata baada ya kuacha wadhifa wa Rais wa Marekani.
Kwa mujibu wa sheria, nguvu zake zitakuwa kubwa: mamlaka ya kualika au kutokualika nchi wanachama; kuunda au kufuta mashirika tanzu; na mamlaka ya kuteua mrithi wake anapoamua kuondoka madarakani au kukosa uwezo wa kuendelea.
Iwapo nchi nyingine yoyote inataka kuwa mwanachama wa kudumu, bei ni kubwa mno: Dola za Marekani bilioni 1 (takriban R$5.3 bilioni).
Bomu hili la hivi punde linawasili katika mwezi ambao tayari ulikuwa wa kichaa.
Katika wiki chache tu, tuliona kukamatwa kwa Nicolás Maduro na Marekani, vitisho vya Trump, na maandalizi ya hatua za kijeshi dhidi ya Iran mbali na mahitaji yake ya kuinunua Greenland, hatua ambayo ilileta mshtuko kote Ulaya na kwingineko.
Nchi kumi na tisa zilihudhuria uzinduzi wa Baraza la Amani huko Davos. Walikuja kutoka pande zote za dunia—kutoka Argentina hadi Azabajani, kutoka jamhuri za zamani za Sovieti hadi falme za Ghuba. Na neno moja ni kwamba wengine wengi tayari "wamekubali kuwa sehemu yake."
"Ninapenda kila mmoja wao katika kundi hili," Trump alisema, akitabasamu, huku akiwatazama viongozi na maafisa ambao majina yao sasa yako kwenye Baraza au vyombo vyake vya utendaji vilivyo chini yake.
Washiriki wengine wengi walikataa mwaliko huo.
"Huu ni mkataba ambao unaibua masuala mapana zaidi, na pia tuna wasiwasi kuhusu ushiriki wa Rais Putin katika jambo ambalo linazungumzia amani," alieleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Yvette Cooper.
Serikali ya Brazil bado haijatoa tamko rasmi kuhusu suala hilo.
Wanadiplomasia wanaofahamu suala hilo walithibitisha kwa BBC News Brazil kwamba serikali ilipokea mwaliko huo na kwamba nchi hiyo inafanya mashauriano ya ndani na washirika wake kuhusu iwapo itakubali au kutokubali mwaliko wa Rais Trump, lakini bado hakuna muda wa mwisho wa Brazil kufanya uamuzi kuhusu suala hilo.
Trump anadai Urusi itakuwa mshirika wake, lakini ujumbe wa Moscow unaonyesha bado "wanashauriana na washirika."
"Kwa maandishi ya sasa ," hatutajiunga, Sweden ilijibu.
"Pendekezo hilo linazua maswali ambayo hayajajibiwa ambayo yanahitaji mazungumzo zaidi na Washington," lilikuwa jibu la kidiplomasia la Norway.
Hata kundi la nchi saba zenye Waislamu wengi, ikiwemo mataifa sita ya Kiarabu, pamoja na Uturuki na Indonesia, walisema wazi kwamba wanajiunga na Baraza kwa ajili ya "amani ya haki na ya kudumu huko Gaza," ikiwa ni pamoja na ujenzi wa eneo lililoharibiwa.
Lakini maelezo yaliyovuja ya sheria ya Baraza hilo hayataji chochote kuhusu Ukanda wa Gaza.
Baadhi ya wakosoaji, zikiwemo baadhi ya nchi zinazositasita kujiunga na Baraza hilo, wanahoji kuwa huu ni mradi ulioundwa kwa ajili ya majivuno ya rais ambaye hafichi tamaa yake ya kushinda tuzo ya juu zaidi - Tuzo ya Amani ya Nobel, ambayo Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama alishinda mwaka 2009, mwanzoni mwa muhula wake wa kwanza katika Ikulu ya White House.
Viongozi wa dunia wanajua kunaweza kuwa na gharama ya kutojiunga na klabu hii mpya.
"Nitamwekea ushuru wa 200% kwa mvinyo na shampeni zake na ataingia, lakini sio lazima aingie," ilikuwa ni karipio la Trump kwa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, akitishia kutumia silaha yake ya ushuru wa juu.
Ni Slovenia pekee ambayo imezungumza kwa sauti ambayo wengine wamenyamaza kuyahusu. Waziri Mkuu wake, Robert Golob, aliweka wazi wasiwasi wake, akisema kuwa Baraza la Amani "linaingilia kwa hatari utaratibu wa kimataifa kwa ujumla."
Trump alijibu swali hili kwa majivuno.
"Baraza hili litakapoundwa kikamilifu, kimsingi tunaweza kufanya chochote tunachotaka, na tutafanya kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa," alielezea ukumbi uliojaa, akizingatia kwa makini kila neno.
Lakini anapenda kuweka ulimwengu katika hali ya wasiwasi.
Siku moja kabla, alipoulizwa na mwandishi wa habari kutoka mtandao wa TV wa Marekani Fox iwapo Baraza lake litachukua nafasi ya Umoja wa Mataifa, Trump alijibu: "Sawa, labda. Umoja wa Mataifa haujasaidia sana."
Kisha akaongeza: "Mimi napenda sana uwezo wa Umoja wa Mataifa, lakini haijawahi kutumia uwezo wake wote. Umoja wa Mataifa ulipaswa kukomesha kila moja ya vita ambavyo nimesitisha."
Mgombea mpya wa nafasi ya mlinda amani mkuu?
Ikiwa na wanachama wake 193, Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu umepoteza jukumu lake kama "mleta amani mkuu".
Mnamo mwaka wa 2016, nilimhoji Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, siku ya kwanza ya muhula wake wa kwanza, saa chache baada ya kuidhinishwa kwa kauli moja na Baraza la Usalama.
Aliahidi "kuongezeka kwa diplomasia kwa ajili ya amani".
Katika muongo mmoja uliopita, juhudi za Umoja wa Mataifa zimetatizwa na Baraza la Usalama lililopooza, idadi inayoongezeka ya mashirika na majimbo yanayoendeleza vita kote ulimwenguni, na kuzorota mara kwa mara kwa msimamo wake ukilinganisha na nchi zenye nguvu zaidi ulimwenguni, ikiwemo Marekani.
"Sote tunahitaji kupongeza mipango ya Trump kumaliza vita," alitangaza Martin Griffiths, mkongwe wa Umoja wa Mataifa. Anaamini kuwa jaribio hili jipya ni "dhahiri ni taswira ya kushindwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Mataifa kwa ujumla."
Griffiths alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura. Anaonya kwamba "kile tulichojifunza katika miaka 80 iliyopita, pamoja na kushindwa na kutokuwa na uwezo, ni thamani ya ushirikishwaji, wa kuwakilisha jumuiya ya kimataifa, sio tu marafiki wa Trump."
Guterres mwenyewe hivi majuzi alilalamika kwamba kuna "watu wanaoamini kwamba utawala wa sheria unapaswa kubadilishwa na sheria ya nguvu."
Alipoulizwa katika mahojiano na kipindi cha Leo cha BBC kuhusu madai ya mara kwa mara ya Trump ya kumaliza vita vinane, alijibu kivitendo sana: "Ni usitishaji mapigano."
Na baadhi ya makubaliano tayari yamevunjwa.
Makubaliano ya muda ya amani kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yalivunjwa mara baada ya hapo. Cambodia na Thailand zilianza kubadilishana shutuma na mengi zaidi juu ya mipaka yao. Na India inapinga jukumu kuu la Trump katika kumaliza mzozo wake na Pakistan.
Lakini upatanishi madhubuti wa Trump pekee unaweza kuwa ulimaliza vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel.
Ushiriki wake binafsi pia hatimaye ulifanikisha kusitishwa kwa mapigano Oktoba iliyopita katika mzozo wa Ukanda wa Gaza, na kupunguza mateso ya Wapalestina na uchungu wa mateka wa Israel.
Uamuzi wake wa kuangazia kabisa maafa haya, ikiwa ni kujibu maombi ya washirika wake wa karibu wa Kiarabu na familia zinazoomboleza za Israeli, ulimpelekea kushinikiza Hamas na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kufikia makubaliano.
Lakini hata mtihani wa kwanza kwa Baraza la Amani (kupiga hatua kutoka kwa awamu ya kwanza ya makubaliano ya kumaliza vita huko Gaza) ni wa kutisha.
Hata hivi sasa, linapoanza kujitokeza taratibu, Baraza hilo jipya linamjumuisha Netanyahu, ambaye ameahidi kuzuia kuanzishwa kwa taifa la Palestina, na viongozi wa nchi za Kiarabu ambao wanasisitiza kuwa njia pekee ya amani endelevu lazima ielekezwe kwa Wapalestina kujitawala na kukomesha uvamizi wa Israel.
Na vita vingine vikuu katika ajenda ya Ulaya na Marekani ni Ukraine. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesita kuketi meza moja na Urusi na Belarus.
Vyombo vitatu vimejipanga chini ya Baraza hilo, viwili vikiwa vimejitolea mahsusi kwa Ukanda wa Gaza: Halmashauri Kuu, Halmashauri Kuu ya Gaza, na Kamati ya Kitaifa ya Serikali ya Gaza.
Wanaleta pamoja mchanganyiko wa maafisa wa ngazi za juu wa Marekani, mabilionea, na wanasiasa wa zamani wanaoheshimika na wajumbe wa Umoja wa Mataifa wanalolifahamu vyema eneo hilo. Kando yao ni mawaziri wa Kiarabu na wakuu wa kijasusi, pamoja na wanateknolojia wa Palestina.
Hata wakosoaji wengine wanampa Rais Trump sifa kwa kuleta mbele vita vya zamani na tofauti: hitaji la kudumu la marekebisho ya usanifu wa Umoja wa Mataifa baada ya vita, ikiwa ni pamoja na Baraza lake la Usalama, ambalo kwa sasa linahusishwa vibaya na ramani ya kisiasa ya mataifa makubwa katika kila eneo la dunia.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halitoshi kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
"Pengine matokeo chanya yasiyotarajiwa ya hatua za Trump ni kwamba masuala haya yataletwa juu ya ajenda ya kimataifa," alionyesha Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Mark Malloch Brown.
Kulingana naye, "tunatoka katika kipindi cha uongozi dhaifu sana katika Umoja wa Mataifa, na nadhani huu unaweza kuwa wito wa kuchukua hatua."
Jambo la kushangaza ni kwamba, pendekezo la Trump la kuuongoza ulimwengu kuelekea katika amani linakuja huku mijadala ikishika kasi katika nchi nyingi kuhusu kuchukua nafasi ya Guterres, ambaye muhula wake wa pili unamalizika mwishoni mwa mwaka huu.
Rais wa Marekani, ambaye aliwahi kutangaza kuwa anaweza kumaliza vita nchini Ukraine kwa siku moja, alijifunza katika mwaka wake wa mwisho madarakani kwamba ujenzi wa amani ni mchakato wa muda mrefu na hatari.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuharirwa na Ambia Hirsi