'Msitupeleke hospitalini': Waandamanaji wa Iran wanaotibiwa kwa siri wakikwepa kukamatwa

Muda wa kusoma: Dakika 5

"Watu walitusaidia na tukaingia kwenye gari... Nikasema, 'Msitupeleke hospitalini.'"

Tara na rafiki yake walikuwa wakishiriki maandamano katika jiji la Isfahan katikati mwa Iran wakati vikosi vya usalama vilipofika kwa pikipiki na kuanza kupiga kelele kwa umati.

"Rafiki yangu alimwambia afisa wa usalama mwenye silaha, ''Msitupige risasi tu,'' na mara moja akatufyatulia risasi kadhaa. Tulianguka chini. Nguo zetu zote zilikuwa zimejaa damu," alisema.

Waliwekwa kwenye gari la mtu wasiyemfahamu, lakini Tara alisema walikuwa na hofu sana kupelekwa hospitalini kwa sababu ya hatari ya kukamatwa. "Vichochoro vyote vilikuwa vimejaa vikosi vya usalama, kwa hivyo niliwaomba wanandoa waliokuwa wamesimama mlangoni mwao waturuhusu kuingia."

Walikaa nyumbani kwa wanandoa hao hadi karibu alfajiri na kisha wakafanikiwa kupata daktari waliyemjua, ambaye alisafisha majeraha ya risasi kwenye miguu yao, kulingana na Tara.

Alisema daktari bingwa wa upasuaji baadaye aliweza kuondoa baadhi ya risasi za ndege nyumbani lakini akawaonya: "Haziwezi kuondolewa zote na zitabaki kwenye miili yenu."

Majina yote katika makala haya yamebadilishwa kwa usalama wao.

Kiwango kamili cha umwagaji damu uliotokana na ukandamizaji wa vikosi vya usalama dhidi ya maandamano ya kupinga serikali yaliyokumba Iran mwezi huu bado hakijajulikana kutokana na kufungwa kwa mtandao na marufuku ya kuripoti kwa mashirika mengi ya habari ya kimataifa.

Lakini Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Binadamu (HRANA) lenye makao yake Marekani limesema limethibitisha mauaji ya watu 6,301, wakiwemo waandamanaji 5,925, watoto 112, watu 50 waliokuwa wamesimama na 214 walioshirikiana na serikali. Pia linachunguza ripoti za vifo zaidi ya 17,091.

Takribani waandamanaji wengine 11,000 walijeruhiwa vibaya, kulingana na HRANA.

Baadhi yao wameiambia BBC kwamba wameepuka kutafuta matibabu ya majeraha yao hospitalini kwa sababu wanaogopa kukamatwa.

Hilo limewaacha wakiwategemea madaktari, wauguzi na watu wengine wa kujitolea walio tayari kuhatarisha usalama wao kwa kuwatibu kwa siri nyumbani kwao.

Wafanyakazi wa afya pia wameiambia BBC kwamba vikosi vya usalama vipo hospitalini na kwamba vinafuatilia rekodi za matibabu za wagonjwa kila mara ili kutambua waandamanaji waliojeruhiwa.

Nima, daktari bingwa wa upasuaji huko Tehran, alisema alishuhudia vijana wengi wakijeruhiwa mitaani akiwa njiani kuelekea kazini mnamo Januari 8, wakati mamlaka zilipodhibiti maandamano yaliyoongezeka kwa nguvu kali.

"Nilimtia mmoja wa waliojeruhiwa kwenye buti ya gari langu ili kumpeleka hospitalini, kwani nilikuwa na wasiwasi kwamba tungepata shida tukisimamishwa na polisi," aliiambia BBC.

Nima alisema maafisa wenye silaha walimzuia lakini wakamruhusu aende baada ya kuona kitambulisho chake cha hospitali.

"Kwa karibu saa 96 mfululizo, bila usumbufu, bila usingizi, bila hata kufunga macho yetu kwa muda, tulikuwa tukifanya upasuaji. Tulikuwa tukilia na kufanya upasuaji. Hakuna mtu aliyelalamika."

"Nguo zetu zote na gauni za hospitali zilikuwa zimejaa damu, nguo zetu za nje, nguo zetu za ndani, kila kitu kilikuwa kimelowa kwenye damu ya vijana hawa."

Nima alielezea upasuaji kwa mtu mmoja ambaye alikuwa amepigwa risasi mguuni na usoni wakati wa maandamano.

"Risasi ilikuwa imeingia kupitia kidevu chake, ikachanika mdomoni na kutoka kupitia taya yake ya juu," alikumbuka.

Nima pia alisema vijana wengi waliotibiwa katika hospitali yake walipata majeraha ya risasi kwenye viungo na miguu yao ambayo yalihitaji kukatwa viungo na kuwaacha na ulemavu wa kudumu.

Mamlaka ya Iran imesema zaidi ya watu 3,100 wameuawa wakati wa machafuko hayo, lakini wengi wao walikuwa wafanyakazi wa usalama au watu waliosimama karibu na "waandamanaji".

Msemaji wa wizara ya afya Hossein Shokri pia alinukuliwa na shirika la habari la Tasnim ambalo si rasmi akisema kwamba karibu operesheni 13,000 zimefanywa wakati wa machafuko hayo.

"Kwa bahati nzuri, watu wanaiamini wizara ya afya na hospitali, na imani kwamba watu wote waliojeruhiwa hutendewa bila upendeleo katika vituo vya matibabu imesababisha watu wapatao 3,000 ambao walikuwa wakijitibu nyumbani kwa siku sita zilizopita kutafuta huduma hospitalini," aliongeza.

Mkuu wa Hospitali ya Macho ya Farabi huko Tehran, Dkt. Qasem Fakhrai, aliiambia Isna, shirika jingine la habari ambalo si rasmi, kwamba lilikuwa limewatibu jumla ya wagonjwa 700 wenye majeraha makubwa ya macho yanayohitaji upasuaji wa dharura kufikia tarehe 10 Januari, na kuwaelekeza karibu 200 katika hospitali nyingine. Alisema karibu wagonjwa wote walilazwa baada ya tarehe 8 Januari.

Saeed aliiambia BBC kwamba macho ya rafiki yake yalipigwa na risasi za ndege zilizopigwa na vikosi vya usalama wakati wa maandamano katika jiji kuu la Arak.

Madaktari wa eneo hilo walimwambia aende katika hospitali maalum ya macho huko Tehran, alisema.

Walipofika, wauguzi waliwapeleka waandamanaji wenye majeraha ya macho kwenye vyumba vya upasuaji kupitia lifti za wafanyakazi.

Kulingana na rafiki wa Saeed, karibu watu 200 wenye majeraha ya macho kutoka miji tofauti walikuwa wakipatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

"Alifanya upasuaji mara mbili, lakini daktari wa upasuaji hakumshtaki," Saeed alisema.

Mfanyakazi wa afya huko Tehran pia alisema kwamba madaktari walikuwa wakijaribu kuepuka kutaja majeraha ya risasi katika rekodi za matibabu kwa sababu yalikuwa yakifuatiliwa kila mara na vikosi vya usalama.

Sina alimpeleka kaka yake hospitalini baada ya kupigwa risasi miguuni wakati wa maandamano huko Tehran.

"Ilikuwa kama hospitali ya uwanja wa vita, kulikuwa na majeruhi wengi sana kiasi kwamba hakukuwa na blanketi au vifaa vya matibabu," Sina aliiambia BBC.

"Nilipomuomba muuguzi blanketi kwa ajili ya kaka yangu, aliniambia nilete moja kutoka nyumbani kwa sababu kulikuwa na majeruhi wengi sana na vifaa vya kutosha havikuwapo."

Sina alisema hawakuwa na chaguo ila kutoa nambari yao halisi ya kitambulisho ili kutumia bima yao ya afya. "Wakati wowote, vikosi vya usalama vinaweza kuvamia nyumba yetu," aliongeza.

Katika miji midogo, hali inaaminika kuwa mbaya zaidi.

Ripoti zilizopokelewa na BBC zilisema vikosi vya usalama vilikuwa vimewateka nyara wagonjwa kutoka hospitalini na kwamba hawakuwa wameonekana tena.

Makundi ya haki za binadamu pia yamesema kwamba madaktari na wengine ambao wamewatibu waandamanaji waliojeruhiwa sasa wenyewe wanalengwa na vikosi vya usalama.

IHR ilisema wiki iliyopita vyanzo vyake vilivyoko Iran viliripoti kukamatwa kwa madaktari wasiopungua watano na mtu mmoja wa kujitolea.

"Mashirika ya usalama yanaonekana kulenga kuusha umma na kuzuia matibabu kwa waandamanaji waliojeruhiwa kwa kuwakamata madaktari na kuvamia makazi ya muda ya matibabu," shirika hilo lenye makao yake Norway lilionya.

Na wiki hii, vyanzo vilivyo karibu na Dkt. Alireza Golchini, daktari wa upasuaji kutoka mji wa kaskazini wa Qazvin, vilisema alipigwa nyumbani kwake na vikosi vya usalama walipomkamata kwa kuwatibu waandamanaji waliojeruhiwa.

Waliongeza kwamba alikuwa ameshtakiwa kwa "moharebeh" (uadui dhidi ya Mungu) - kosa ambalo linaweza kubeba adhabu ya kifo chini ya sheria ya Iran.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi