Viongozi wa Chad na Ufaransa wakubaliana kuimarisha uhusiano wao.
Mataifa ya Chad na Ufaransa yamekubaliana kuimarisha ushurikiano wao kwa kuheshimu maslahi ya kila mmoja, hii ikiashiria mwamko mpya wa uhusiano wao.
Uamuzi huo unafuatia kile wachambuzi wanakitaja kuwa '‘uhusiano baridi’' kati ya mataifa hayo mawili, baada ya Chad kujiondoa kwenye mkataba wa kiusalama kati yake na Ufaransa mwaka wa 2024.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alimualika kiongozi wa Chad Mahamat Deby, katika ziara ya kikazi na baadaye kufanya mazungumzo naye mjini Paris siku ya Alhamisi.
Katika taarifa ya pamoja, viongozi hao wawili walisema wamezungumzia maswala tofauti na wamekubaliana kuimarisha uhusiano wao haswa kiuchumi.
'‘Mazungumzo kati ya Ufaransa na Chad yataendelea, kuhakikisha tunatekeleza yale tuliokubaliana na kila upande unatimiza ahadi zake”
Wawili hao pia waliakubaliana kuhusu njia muafaka ya kufufua uhusiano wao wa awali, wakikuwa na matumaini na mkakati huu mpya.
Lakini bado haijabainika jinsi viongozi hao wawili watatatua kuvunjika kwa mkataba wao wa muda mrefu wa kiusalama, kwani swala la usalama halikuangaziwa katika taarifa ya pamoja walioitoa.
Viongozi hao wawili aidha walizungumzia kuhusu vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini Sudan, wakitoa wito kwa pande mbili zinazozozana kusitisha vita hivyo.
Awali baada ya Chad kuvunja mkataba wa kiusalama waliokuwa nao na Ufaransa, wanajeshi wa Ufaransa waliokuwa nchini humo walitakiwa kuondoka mara moja, na kuzua wasiwasi kuhusu uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.