Zijue nchi tano zilizoathirika zaidi na ushuru mpya wa Trump

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais Donald Trump wa Marekani, aliahidi kuzitoza ushuru nchi anazoamini zinaitendea Marekani isivyo sawa katika biashara, iwe kupitia ushuru wa juu au vikwazo visivyo vya ushuru. Na hilo amelitekeleza kwa kuweka ushuru mpya, ambao anadai utaunda nafasi za kazi na kukuza viwanda vya ndani vya Marekani.

Kutoza ushuru wa juu kwa mataifa mengine, kuna uwezekano wa kuzifanya bidhaa nyingi za matumizi kuwa ghali zaidi, wakati huu ambapo Wamarekani wengi wana hofu inayoongezeka juu ya kushuka uchumi wa nchi hiyo.

Kwa ahadi za kupunguza deni la taifa na kusawazisha biashara ya kimataifa, Trump tayari amepitisha ushuru mkubwa dhidi ya washirika wakuu wa biashara na sekta muhimu - sera hiyo tayari inakabiliwa na vitisho vya kulipiza kisasi kutoka kwa washirika hao.

Ifuatayo ni orodha ya mataifa matano ambayo yamewekewa ushuru mkubwa zaidi kuliko mataifa mengine. Mengi ya mataifa hayo ni kutoka bara la Asia na Afrika.

Pia unaweza kusoma

Lesotho ushuru wa 50%

Miongoni nchi zilizowekewa ushuru mkubwa ni ule wa asilimia 50 dhidi ya Lesotho. Nchi ndogo Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa na moja ya nchi maskini duniani, iliyozungukwa na Afrika Kusini.

Walesotho ama Wamarekani wanaoleta bidhaa kutoka nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Afrika watalazimika kulipa ushuru wa ziada wa 50%.

Kwa mujubu wa shirika la Biashara la Marekani, linaloshughulikia sera na Biashara za nje za Marekani, biashara kati ya nchi hizo mbili inahusisha hasa nguo, madini, na chuma.

Ushuru wa asilimia 50 kwa Lesotho, nchini ambayo pato la taifa lilikuwa takribani dola bilioni 2 mwaka 2024, ni miongoni mwa viwango vya juu zaidi kwenye orodha hiyo mpya ya utawala wa Trump.

Waziri wa Biashara wa Lesotho Mokhethi Shelile alisema serikali yake itatuma wajumbe Washington kupinga hatua hiyo mpya ya kibiashara.

"Wasiwasi wangu mkubwa ulikuwa kufungwa mara moja kwa viwanda na kupoteza kazi," shirika la habari la AFP linamnukuu akiwaambia waandishi wa habari siku ya Alhamisi.

Moja ya malengo ya Trump na tangazo lake la ushuru ni kupunguza nakisi ya biashara ya nchi yake na ulimwengu wote.

Na hii inatoa picha ya kwa nini Lesotho imewekewa kiwango hicho kikubwa sana.

Kulingana na takwimu za Ikulu ya Marekani, mwaka 2024 wakati Marekani ilisafirisha bidhaa zenye thamani ya $2.8m (£2.1m) tu kwa Lesotho, yenyewe iliagiza kutoka nchi hiyo ya kusini mwa Afrika bidhaa za thamani ya $237.3m.

Katika hesabu zao, maafisa wa Marekani walitumia tofauti kati ya thamani ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na mauzo ya nje katika kuweka viwango vya ushuru kwa nchi mbalimbali.

Saint Pierre na Miquelon ushuru wa 50%

Hivi ni visiwa vya Ufaransa kusini mwa kisiwa cha Canada cha Newfoundland. Hadi kufikia Januari 2022 kisiwa hiki kilikuwa na idadi ya watu 5,819 kwa mujibu wa sensa ya mwaka huo.

Saint Pierre na Miquelon, eneo lililowekewa ushuru wa 50% na Trump, ni maarufu kwa historia yake kama kituo cha uvuvi, na milki ya mwisho ya Ufaransa ya Amerika Kaskazini, na ina utamaduni wake wa kipekee ulioathiriwa na mila za ki-faransa na watu wa jamii ya Basque.

Visiwa hivyo huitegemea Ufaransa kwa ruzuku na Canada kwa bidhaa na njia ya usafiri. Utalii unazidi kuwa muhimu. Ingawa sekta ya uvuvi imekabiliwa na changamoto katika miaka ya hivi karibuni, bado ni sehemu muhimu ya uchumi wa ndani.

Visiwa hivi huagiza bidhaa mbalimbali kutoka Marekani, vitoweo kutoka viwandani kama kaa, kamba na uduvi. Bidhaa nyingine ni zana za mikono, makontena, na chupa za glasi, miongoni mwa vitu vingine.

Cambodia ushuru wa 49%

Cambodia, nchi inyaoendelea ambapo 17.8% ya watu wake wanaishi chini ya mstari wa umaskini kulingana na Benki ya Maendeleo ya Asia (ADB), ni nchi iliyoathirika zaidi katika kanda ya Asia kwa kuwekewa kiwango cha ushuru cha 49%. Zaidi ya nusu ya viwanda nchini humo vinaripotiwa kumilikiwa na Wachina.

Kwa mujubu wa shirika la Biashara la Marekani, mwaka 2023, Cambodia ilisafirisha bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 12.2 kwenda Marekani, na mauzo hayo yakiwemo vifaa vya semikonda, mabegi, makasha, na masweta, na Marekani ndilo soko kubwa zaidi la kuuza nje la Cambodia.

Katika kipindi cha miaka 5 iliyopita, mauzo ya Cambodia kwenda Marekani yameongezeka kwa kiwango cha kila mwaka cha 24.3%, kutoka dola biloni 4.12 mwaka 2018 hadi dola bilioni 12.2 mwaka 2023.

Laos ushuru wa 48%

Taifa la Kusini-mashariki mwa Asia la Laos ambalo halina bandari, nchi iliyoshambuliwa kwa bomu na Marekani wakati wa vita baridi, imewekwa ushuru wa asilimia 48%. Kulingana na ADB, Laos ina kiwango cha umaskini cha 18.3%.

Kwa mujubu wa shirika la Biashara la Marekani, 2023, Laos ilisafirisha bidhaa za dola milioni 306 milioni kwenda Marekani, zikiwemo nyaya, masweta na viatu, wakati Marekani iliuza bidhaa za dola milioni 40.4 kwenda Laos.

Mauzo ya Laos kwenda Marekani yameongezeka kwa kiwango cha kila mwaka cha 15.6% katika miaka mitano iliyopita, kutoka dola milioni 148 mwaka 2018 hadi dola milioni 306 mwaka 2023.

Marekani husafirishaji kwenda Laos, bidhaa kama vile ndege, dawa, mbao, magari, bidhaa za kilimo, na vyombo vya macho na matibabu.

Madagascar ushuru wa 47%

Kwa mujubu wa shirika la Biashara la Marekani, Madagascar husafirisha bidhaa nyingi zaidi kuliko inazoagiza kutoka Marekani, hasa vanila, nguo, na bidhaa zingine kama karafuu na mafuta muhimu.

Vilevile, Madagascar husafirisha kwenda Marekani, suti za wanaume, madini ya titani, na vitu vingine vya nguo. Mwaka 2023, Madagascar ilisafirisha bidhaa zenye thamani ya dola milioni 669 kwenda Marekani.

Madagascar, ama Jamhuri ya Madagascar, ni nchi ya visiwa inayojumuisha kisiwa cha Madagascar na visiwa vingi vidogo vya pembezoni. Madagascar iko nje ya pwani ya kusini-mashariki mwa Afrika, ni kisiwa cha nne kwa ukubwa duniani, imewekewa ushuru wa 47 na Marekani.

Ushuru huu mpya ambao umepiga hadi nchi ambazo ziko katika vita kama Myanmar kwa 44% na visiwa visivyo ishi watu vya Heard and McDonald karibu na Antarctica, umekoseloewa pakubwa na viongozi wa dunia.

Huku ikisubiriwa nchi hizi zitatii ushuru huu au zitalipiza kisasi, mhariri wa masuala ya kiuchumi wa BBC, Faisal Islam anaamini vita vibaya vya kibishara duniani huenda visikwepeke.

Nchi zingine za Afrika

Nchi nyingine za Kiafrika zilizoathiriwa na ushuru wa ziada ukiacha 47% kwa Madagascar, ushuru wa 40% umewekwa kwa Mauritius, 37% kwa Botswana na 30% kwa Afrika Kusini.

Mauzo ya nje ya Nigeria yataathiriwa pia - kwa kiwango cha 14%.

Kenya, Ghana, Ethiopia, Tanzania, Uganda, Senegal na Liberia ni miongoni mwa nchi ambazo mauzo yake yatatozwa ushuru wa awali wa 10%. Marekani haiendeshi nakisi ya kibiashara na nchi hizi.