Marekani yapeleka meli kubwa ya kivita mashariki ya kati kuna nini?

    • Author, Ghoncheh Habibi-Azad
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Maandamano nchini Iran na mauaji ya waandamanaji, yamefanya mvutano kati ya Iran na Marekani kuongezeka, na uwezekano wa shambulio la Marekani dhidi ya Iran umeongezeka.

Mapema wiki hii, Rais wa Marekani Donald Trump alisema "manowari kubwa inaelekea Iran." Hata hivyo, alisema, “sio lazima itumike.”

Kwa sababu hiyo, BBC Persian imekuwa ikifuatilia mienendo ya manowari za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati kwa wiki chache zilizopita.

Mojawapo ya manowari zilizogonga vichwa vya habari katika wiki za hivi karibuni ni manowari ya kubeba ndege za kivita ya USS Abraham Lincoln.

Manowari hii inayoendeshwa kwa nishati ya nyuklia imekuwa ikifanya kazi na Jeshi la Wanamaji la Marekani tangu 1989 na inachukuliwa kuwa mojawapo ya manowari kubwa na za kisasa zaidi za kubeba ndege za Marekani.

Ingawa manowari hiyo imezima mfumo wake wa ufuatiliwaji, lakini bado inaweza kufuatiliwa kwa kutumia mbinu mbalimbali. Kimsingi, hata kama meli izime mfumo wake wa ufuatiliaji, haitatoweka kabisa kutokana na uchunguzi wa wataalamu wa ufuatiliaji wa meli.

Katika kisa hiki, tuliweza kufuatilia helikopta za kijeshi za Marekani zikiruka juu ya manowari hiyo kupitia tovuti ya ufuatiliaji wa ndege, FlightRadar24, na kukadiria eneo ilipo.

Helikopta hizi, ambazo kwa kawaida huruka pamoja na manowari kama hizo kwa ajili ya misheni mbalimbali kama vile doria, usafiri wa wanajeshi, au usaidizi wa vifaa, wakati mwingine hutumia mifumo ambayo inaweza kufuatiliwa katika data za ndege.

Lincoln ilianza safari kutoka Bahari ya Kusini ya China kuelekea Mashariki ya Kati Januari 14, na mahali ilipokuwa Januari 26, ni karibu na pwani ya Oman.

CENTCOM, kamanda ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani, pia ilithibitisha katika chapisho kwenye X kwamba manowari ya kubeba ndege za kivita ya Abraham Lincoln imeingia Bahari ya Hindi. CENTCOM imesema meli hiyo imetumwa Mashariki ya Kati ili "kukuza usalama na utulivu wa kikanda."

CENTCOM ni mojawapo ya kamandi sita za Wizara ya Ulinzi ya Marekani zinazoshughulikia Mashariki ya Kati, ambayo inajumuisha Iran.

Misri na Asia ya Kati pia ziko chini ya CENTCOM. Iraq, Afghanistan, na Syria zilikuwa chini ya operesheni za CENTCOM baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001 dhidi ya Marekani.

Manowari ya USS Abraham Lincoln

Manowari ya kubeba ndege ya USS Abraham Lincoln, iliyopewa jina la Rais wa 16 wa Marekani, Novemba 11, 1989.

Meli hiyo ni sehemu ya kikosi kazi cha Jeshi la Wanamaji la Marekani, pia ina makombora ya aina tatu: USS Frank E. Peterson Jr., USS Spruance, na USS Michael Murphy.

Lincoln inabeba ndege za kivita za F/A-18E/F Super Hornet, ndege za AA-18G Growler, ndege za kivita za F-35C, na helikopta za MH-60R/S.

Manowari hii imeainishwa kama meli ya kubeba ndege ya daraja la V Nimitz na ina uwezo wa kubeba takriban wafanyakazi elfu sita.

Ina urefu wa mita 333 na upana wa takriban mita 77 katika sehemu yake pana zaidi. Abraham Lincoln, ina uzito wa tani 100,000, inaweza kusafiri kwa kasi ya kilomita 56 kwa saa.

Meli hiyo hapo awali imetumwa kwenye Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman mara kadhaa. Ilitumwa kwenye eneo hilo kwa misheni za upelelezi wakati wa operesheni iliyozinduliwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 ili kuiondoa Iraq kutoka Kuwait.

Mwaka 1995, 1998, na 2000, manowari ya Abraham Lincoln ilikwenda Ghuba ya Uajemi kushiriki katika operesheni ya doria ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani inayoitwa "Southern Watch."

Manowari hiyo ilikwenda tena katika eneo hilo mwishoni mwa mwaka wa 2002, usiku wa kuamkia uvamizi wa Marekani na washirika wake nchini Iraq, uvamizi ulioanza Machi 2003.

Wakati huo, Iran ilikuwa ikikabiliwa na vikwazo vya mafuta kutoka Marekani na Ulaya kutokana na mpango wake wa nyuklia, na wakati huo huo, mvutano kati ya Iran na Marekani ulikuwa ukiongezeka juu ya Mlango wa Bahari wa Hormuz.