Waethiopia wanaoishi katika Kaunti ya Mandera, kaskazini-mashariki mwa Kenya, wanasema wameonywa kuwa watakabiliwa na kifo iwapo hawataondoka katika eneo hilo ifikapo tarehe 5 Februari 2026.
Wakizungumza na BBC bila kutaja majina yao, wahamiaji kadhaa walieleza hali hiyo kuwa ya kutishia maisha.
Ubalozi wa Ethiopia nchini Kenya ukiongozwa na Balozi Demeke Atnafu umethibitisha kuwa unafuatilia kwa karibu hali hiyo.
Alisisitiza kuwa ni vyombo vya serikali pekee vinavyoweza kuamua hadhi ya kisheria ya wahamiaji, akisema: “Serikali haina uhusiano na hilo. Inatoa ulinzi unaohitajika.”
Mhamiaji mmoja, baba wa watoto wawili ambaye ameishi Mandera kwa miaka minane, alisema: “Tulinunua pikipiki, tukafungua hoteli na tulikuwa tukifanya kazi. Hatufahamu sababu, lakini wao (wakazi wa eneo hilo) walianza kusema Waethiopia wote waondoke.”
Wengine waliripoti kunyanyaswa, kukamatwa na kudaiwa rushwa.
“Wanakuja kwa magari ya polisi na kutuchukua kutoka kwenye teksi hadi gerezani. Tuko matatani. Hatuna mtu wa kutusaidia,” alisema mkazi mmoja, akiongeza kuwa Waethiopia wanaoishi Mandera, wanaokadiriwa kuwa takribani watu 10,000, wamekuwa wakijihusisha na shughuli za usafiri wa pikipiki na sekta ya hoteli.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mvutano huo unatokana na malalamiko ya kiuchumi.
Wakazi wa eneo hilo wanadaiwa kuwashutumu Waethiopia kwa “kuvamia” eneo hilo na kuchukua biashara.
Wahamiaji walipotaka maelezo kutoka kwa viongozi wa serikali ya eneo hilo, waliambiwa waende kuwauliza wazee wa jamii.
Nao wazee waliwaambia: “Hatutaki kuwaona. Ondokeni katika nchi yetu.”
Mashuhuda walisema kampeni hiyo iliongezeka baada ya kuuawa kwa mhamiaji mmoja wa Ethiopia wiki moja iliyopita katika eneo linaloitwa Burabur.
Mwili wake ulizikwa hapo hapo baada ya mamlaka kukataa kurejeshwa Ethiopia.
Baada ya mazishi hayo, wakazi walianzisha kampeni ya kudai Waethiopia waondoke Mandera, wakitoa vitisho vya kupigwa mawe na kuuawa baada ya tarehe ya mwisho ya Februari.
Wahamiaji wanadai agizo hilo lilitolewa na wazee wa jamii wa kaunti na kusambazwa kupitia vipaza sauti vilivyowekwa kwenye magari.
Pia wanadai kuwa polisi wanawakamata Waethiopia na kudai hadi shilingi 20,000 ili kuwaachia huru, huku wasioweza kulipa wakifungwa gerezani.
“Hatuna chaguo jingine ila kujiandaa kuondoka,” alisema mhamiaji mmoja.