Moja kwa moja, Trump 'kulegeza kamba' dhidi ya wahamiaji haramu kufuatia mauaji ya Mmarekani
Hayo yanajiri huku Waziri wa masuala ya usalama Kristi Noem akikabiliwa na shinikizo la kujiuzulu kufuatia mauaji ya raia wa Marekani yaliyotokea huko Minneapolis, yaliyofanywa na Mawakala wa idara ya uhamiaji (ICE)
Seneta wa Marekani atoa wito wa kuwapa silaha waandamanaji wa Iran
Chanzo cha picha, Getty Images
Ted Cruz, Seneta wa ngazi ya juu wa chama cha Republican katika Bunge la Marekani, ametoa wito wa kukabidhiwa silaha kwa waandamanaji wa Iran, ikiwa ni majibu ya hivi punde kwa ukandamizaji wa umwagaji damu dhidi ya maandamano nchini humo.
Seneta Cruz aliandika kwenye mtandao wa X Jumanne jioni: "Sisi (Marekani) tunapaswa kuwapa silaha waandamanaji sasa, ili watu wa Iran waweze kumpindua Ayatollah - dikteta ambaye daima anapiga kelele 'Kifo kwa Marekani.' Hii itaifanya Marekani kuwa salama na utulivu zaidi.
Mazingira ya kifo cha Raila Odinga bado yaibua hisia Kenya
Chanzo cha picha, Winnie Odinga Facebook
Maelezo ya picha, Mwana wa Raila Odinga Winie Odinga
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), ambaye pia ni mtoto wa kike wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Winnie Odinga, amekataa vikali madai ya mfanyabiashara Oketch Salah kwamba alikuwa pale wakati wa kifo cha marehemu baba yake, Raila Odinga.
Winnie ameyataja madai hayo kama “uongo hatari” na kuhoji nia halisi za Salah.
Akizungumza katika mahojiano na Citizen TV siku ya Jumanne, Januari 27, Winnie alisema kuwa madai ya Salah ni ya uongo na hayafai, ikizingatiwa hali ya hisia inayozunguka kifo cha waziri mkuu huyo wa zamani.
“Nimekutana na Oketch Salah, lakini napenda kuamini hakuna anayemjua kweli. Kudai ulikuwa pale wakati wa kifo cha baba yangu wakati hakuwa pale, na kuzungumzia mambo ambayo hayajatokea, ni hatari sana na kunalazimisha kuhoji nia zake,” alisema Winnie.
Kauli yake inajiri baada ya Salah kudai hadharani kuwa alikuwa na Raila Odinga tangu mwanzo wa ugonjwa wake hadi wakati wa kifo chake.
Salah alisisitiza kuwa hakutoa taarifa hizo kwa huruma au faida ya kisiasa, bali kwa sababu ni ukweli.
Aliongeza kuwa alimuuguza kihisia Raila na kushiriki katika mazungumzo binafsi wakati wa ugonjwa wake.
Mbunge Winnie Odinga pia ametoa malalamiko makali juu ya jinsi mchakato wa uongozi ndani ya Orange Democratic Movement (ODM) ulivyoshughulikiwa baada ya kifo cha kiongozi wa muda mrefu wa chama.
“Chama hakijatimiza wajibu wake kwa uwazi. Kiongozi wetu alifariki, na chama hakujawahi kuwasiliana nasi kama wanachama kutujulisha kifo chake. Wamechagua uongozi mpya, lakini bado hatujajulishwa rasmi,” alisema.
Winnie alihoji pia msingi wa kisheria uliopewa binamu yake na kaka wa Raila, Dk. Oburu Oginga, aliposimikwa kama kiongozi wa chama, akisisitiza kuwa hatua hiyo haikuzingatia katiba.
Aliongeza kuwa msimamo wake ni kulinda maadili ya chama na uongozi wake dhidi ya hatua zisizo za kikatiba, kuhakikisha chama na viongozi wake hawadhulumiwi au kudanganywa kisheria.
Watumiaji wa Uingereza watashindwa kufikia 'Pornhub' kuanzia wiki ijayo
Chanzo cha picha, Getty Images
Ilani: Taarifa hi inahusisha mada za ngono.
Pornhub imetangaza itapunguza upatikanaji wa tovuti yake nchini Uingereza kuanzia wiki ijayo, ikilaumu ukaguzi mkali wa umri ulioanzishwa kwa tovuti zenye picha za ngono wazi.
Kuanzia tarehe 2 Februari, watu pekee waliojiunga na akaunti ya Pornhub awali ndio watakaoweza kufikia yaliyomo kwenye tovuti hiyo.
Aylo, kampuni kubwa ya Pornhub, ilisema kuwa marekebisho ya Sheria ya Usalama Mtandaoni ya Uingereza (Online Safety Act – OSA), yanayohitaji uthibitisho wa umri, hayajafanikisha lengo la kulinda watoto wadogo na yamepelekea trafiki ya watumiaji kuelekea sehemu zisizo za kawaida na zisizodhibitiwa za mtandao.
Mnamo Oktoba, Aylo ilisema kuwa mabadiliko ya sheria yalifanya idadi ya watazamaji kwenye tovuti hiyo kupungua kwa asilimia 77%.
Alex Kekesi, mkuu wa jamii na chapa (brand) katika Aylo, alisema uamuzi wa kupunguza upatikanaji wa Pornhub kwa watumiaji wa Uingereza ulikuwa uamuzi mgumu.
''Tovuti zetu, zinazotoa picha za ngono halali na zinazosimamiwa kisheria, hazitatumika tena kwa watumiaji wapya wa Uingereza, lakini maelfu ya tovuti zisizo wajibika bado zitakuwa rahisi kufikiwa'', alisema.
Vikwazo hivyo hivyo vitahusisha pia tovuti nyingine za ngono zinazomilikiwa na Aylo, zikiwemo YouPorn na Redtube.
Emma Drake, mshirika wa masuala ya usalama mtandaoni na faragha katika kampuni ya sheria ya Bird and Bird, alisema utafiti uliotajwa na Aylo unaonyesha kuwa watu wazima wanatafuta tovuti zenye hatari kubwa zaidi za ngono, pia umeonyesha kuwa matumizi ya tovuti za ngono miongoni mwa watu wazima yameshuka.
“Hali hiyo lazima iwe kweli pia kwa watoto,” alisema kwa BBC.
“Wale waliyo na azma watapata njia mbadala, kama kutumia VPN au tovuti mpya Aylo zilizotaja, lakini kuweka vizuizi kwenye tovuti maarufu zaidi bado kunaweza kulinda idadi kubwa ya watoto ambao wasingejitahidi kufanya hivyo.”
Mbunge wa Minnesota Ilhan Omar ashambuliwa kwa 'kioevu kisichojulikana' wakati akihutubia wakaazi
Chanzo cha picha, Reuters
Wakati huo huo,Mbunge wa chama cha Democratic Ilhan Omar ameshambuliwa na mwanamume mmoja wakati akihutubia katika hafla iliyokuwa ikifanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Minneapolis.
Polisi wanasema mshambuliaji huyo alimmwagia bi Omar kitu cha majimaji mwilini.
"Nilidhani ni mmoja wa wasaidizi wake aliyekwenda kumkabidhi barua au kitu," Jacquelynn Goessling alisema juu ya mtu aliyemshambulia Omar kwa kitu cha majimaji, harufu ya akridi ambayo iliteketeza sehemu ya mbele ya chumba.
Hata hivyo alichomwagia hakikumdhuru na mdemocrat huyo ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Rais Trump aliendelea na hotuba yake.
Katika taarifa yake kuhusu X, Omar alisema: "Mimi niko sawa. Mimi nimeokoka kwa hivyo mchochezi huyu mdogo hatanitisha kufanya kazi yangu. Siwaruhusu wanyanyasaji kushinda."
Maelfu ya Waethiopia watishiwa kuuawa Kenya waamriwa kuondoka
Chanzo cha picha, Getty Images
Waethiopia wanaoishi katika Kaunti ya Mandera, kaskazini-mashariki mwa Kenya, wanasema wameonywa kuwa watakabiliwa na kifo iwapo hawataondoka katika eneo hilo ifikapo tarehe 5 Februari 2026.
Wakizungumza na BBC bila kutaja majina yao, wahamiaji kadhaa walieleza hali hiyo kuwa ya kutishia maisha.
Ubalozi wa Ethiopia nchini Kenya ukiongozwa na Balozi Demeke Atnafu umethibitisha kuwa unafuatilia kwa karibu hali hiyo.
Alisisitiza kuwa ni vyombo vya serikali pekee vinavyoweza kuamua hadhi ya kisheria ya wahamiaji, akisema: “Serikali haina uhusiano na hilo. Inatoa ulinzi unaohitajika.”
Mhamiaji mmoja, baba wa watoto wawili ambaye ameishi Mandera kwa miaka minane, alisema: “Tulinunua pikipiki, tukafungua hoteli na tulikuwa tukifanya kazi. Hatufahamu sababu, lakini wao (wakazi wa eneo hilo) walianza kusema Waethiopia wote waondoke.”
Wengine waliripoti kunyanyaswa, kukamatwa na kudaiwa rushwa.
“Wanakuja kwa magari ya polisi na kutuchukua kutoka kwenye teksi hadi gerezani. Tuko matatani. Hatuna mtu wa kutusaidia,” alisema mkazi mmoja, akiongeza kuwa Waethiopia wanaoishi Mandera, wanaokadiriwa kuwa takribani watu 10,000, wamekuwa wakijihusisha na shughuli za usafiri wa pikipiki na sekta ya hoteli.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mvutano huo unatokana na malalamiko ya kiuchumi.
Wakazi wa eneo hilo wanadaiwa kuwashutumu Waethiopia kwa “kuvamia” eneo hilo na kuchukua biashara.
Wahamiaji walipotaka maelezo kutoka kwa viongozi wa serikali ya eneo hilo, waliambiwa waende kuwauliza wazee wa jamii.
Nao wazee waliwaambia: “Hatutaki kuwaona. Ondokeni katika nchi yetu.”
Mashuhuda walisema kampeni hiyo iliongezeka baada ya kuuawa kwa mhamiaji mmoja wa Ethiopia wiki moja iliyopita katika eneo linaloitwa Burabur.
Mwili wake ulizikwa hapo hapo baada ya mamlaka kukataa kurejeshwa Ethiopia.
Baada ya mazishi hayo, wakazi walianzisha kampeni ya kudai Waethiopia waondoke Mandera, wakitoa vitisho vya kupigwa mawe na kuuawa baada ya tarehe ya mwisho ya Februari.
Wahamiaji wanadai agizo hilo lilitolewa na wazee wa jamii wa kaunti na kusambazwa kupitia vipaza sauti vilivyowekwa kwenye magari.
Pia wanadai kuwa polisi wanawakamata Waethiopia na kudai hadi shilingi 20,000 ili kuwaachia huru, huku wasioweza kulipa wakifungwa gerezani.
“Hatuna chaguo jingine ila kujiandaa kuondoka,” alisema mhamiaji mmoja.
Trump asema Marekani 'haitaisaidia tena Iraq' ikiwa itamchagua Maliki kama Waziri Mkuu
Chanzo cha picha, Reuters
Rais Donald Trump ametishia kuondoa msaada wa Marekani kwa Iraq iwapo aliyekuwa Waziri mkuu wa nchi hiyo Nouri al-Mailiki atarejea madarakani.
Bwana Maliki aliye na mafungamano na Iran ameteuliwa kuwa Waziri mkuu na muungano wa vyama vya Kishia ambavyo vina wingi wa uwakilishi bungeni.
Al Maliki alikuwa waziri mkuu wa Iraq kati ya mwaka 2006 hadi 2014.Kwa mara nyingine,Rais Trump anaonekana kuingilia mchakato wa kisiasa wa taifa jingine,baada ya kufanya hivyo katika uchaguzi wa Honduras na Argentina.
Trump alisema nchi hiyo itakuwa na nafasi "sifuri" ya kufaulu bila uungwaji mkono wa Marekani baada ya kuapa "haitaisaidia tena" nchi hiyo ikiwa Maliki atachaguliwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alielezea wasiwasi wake kuhusu uhusiano wa Maliki na Iran wakati wa mazungumzo na Waziri Mkuu aliye madarakani Mohammed Shia al-Sudani siku ya Jumapili, akisisitiza "kwamba serikali inayodhibitiwa na Iran haiwezi kutanguliza maslahi ya Iraq mbele".
Seneta wa zamani wa Ufaransa apatikana na hatia ya kumlewesha mbunge dawa za kulevya
Chanzo cha picha, Getty Images
Seneta wa zamani wa Ufaransa Joel Guerriau amehukumiwa kifungo cha miaka minne jela kwa kumuwekea dawa za kulevya mbunge Sandrine Josso kwenye kinywaji chake kwa lengo la kumshambulia kingono.
Mahakama ilibaini kuwa bwana Guearriau alimuwekea bi Josso dawa aina ya ecstasy kwenye gilasi yake ya Champagne alipokuwa amemtembelea nyumbani kwake mjini Paris.
Joel Guerriau alipokea kifungo cha miaka minne jela - miezi 18 ambayo itatumikia gerezani - na, kulingana na vyombo vya habari vya ndani, aliamriwa kumlipa Sandrine Josso €5,000 (£4,348) kama fidia kwa msongo wa mawazo.
Muda mfupi baada ya uamuzi huo siku ya Jumanne, Josso alisema ilikuwa "afueni kubwa", AFP inaripoti. Wakati huo huo, mawakili wa Guerriau walisema atakata rufaa.
Zelensky alaani shambulizi baya la ndege zisizo na rubani za Urusi kwenye treni ya abiria
Chanzo cha picha, Ukraine's DSNS emergency service/Kharkiv region
Maelezo ya picha, Takriban behewa moja la treni ya abiria lilikuwa likiungua baada ya shambulio la ndege zisizo na rubani za Urusi kaskazini-mashariki mwa Ukraine
Rais wa Ukraine Volodomyr Zelensky amesema watu wanne wameuawa na wengine kadhaa hawajulikani waliko baada ya ndege ya Urusi isiyoendeshwa na rubani kushambulia treni iliyokuwa imebeba abiria kaskazini mashariki mwa Ukraine.
Rais Zelensky amelitaja shambulizi hilo kuwa la kigaidi akisema hakuna sababu yoyote ya kuwaua raia ndani ya treni iliyokuwa imewabeba zaidi ya watu mia mbili.
Urusi haijatoa maoni kufikia sasa.
Moscow katika miezi ya hivi karibuni imeongeza mashambulizi yake ya ndege zisizo na rubani na makombora yanayolenga miundombinu ya nishati na usafiri ya Ukraine huku nchi hiyo ikikabiliwa na msimu wa baridi kali zaidi kuwahi kutokea katika miaka iliyopita.
Mamilioni ya watu kote Ukraine wameachwa bila joto, umeme na maji baada ya mashambulio ya Urusi.
Rais wa Urusi Vladimir Putin alizindua uvamizi kamili mnamo Februari 2022, na Moscow kwa sasa inadhibiti karibu asilimia 20% ya eneo la Ukraine.
Iran ikivamia Israel, tutajibu kwa nguvu haijawahi kushuhudiwa - Netanyahu
Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri Mkuu wa Israel amesema kuwa iwapo Iran itajaribu kuishambulia nchi yake kwa shambulio la kushtukiza, ataijibu kwa nguvu kali.
Benjamin Netanyahu alisema katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu uwezekano wa Iran kuishambulia nchi yake mapema,
“Ikiwa Iran itafanya kosa kama hilo na kuishambulia Israel, tutajibu kwa nguvu ambayo Iran haijawahi kuona hapo awali.”
Aliongeza pia kuwa serikali ya Israel imejiandaa kwa hali yoyote kwa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya matukio, bila kujali maamuzi yatakayofanywa na Donald Trump.
Kauli za Bw. Netanyahu zilitolewa wakati mvutano ukiendelea kuongezeka kati ya Marekani na Iran, pamoja na kuwasili kwa meli ya kivita ya kubeba ndege, Abraham Lincoln, katika eneo la Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) katika Ghuba ya Uajemi.
Trump 'kulegeza kamba' dhidi ya wahamiaji haramu kufuatia mauaji ya Mmarekani
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump amesema utawala wake utapunguza operesheni yake ya kuwasaka wahamiaji haramu mjini Minneapolis baada ya maafisa wa kikosi maalum cha uhamiaji kuwaua watu wawili katika mji huo mwezi huu.
Kitendo hicho cha maafisa wa ICE kilichochea wimbi la maandamano ya umma na shutuma kali.
Hayo yanajiri huku waziri wa usalama wa ndani Kristi Noem akikabiliwa na shinikizo la kujiuzulu kufuatia mauaji hayo ya Minneapolis.
Viongozi wa Democratic bungeni wametishia kupiga kura ya kutokuwa na imani naye iwapo Rais Trump hatamfuta kazi.
Seneta wa Republican Thom Tilisi amesema bi Noem anamfanya Rais Trump kuonekana mbaya lakini Rais Trump amesema ana imani naye akiongeza kuwa amefanya vizuri tu katika wadhifa wake.
Rais pia alizungumza kwa simu Jumatatu na Gavana wa Minnesota Tim Walz na Meya wa Minneapolis Jacob Frey, ambao wote ni Wanademokratic. Frey alisema baadaye kwamba Trump alimwambia "hali iliyopo" huko Minneapolis haiwezi kuendelea.