'Kupewa dawa za kulevya, kuibiwa, kuuawa': Jiji linalonasa watalii wa Marekani katika mtego wa programu za kuchumbiana

Msururu wa vifo vya kutatanisha vilivyohusisha wanaume wa Marekani nchini Colombia vimehusishwa na programu za uchumba. Jamaa za waliouawa sasa wanatafuta majibu, anasimulia Austin Landis akiwa Medellin.
Tou Ger Xiong alipenda kurudi Colombia.
"Alizungumza juu ya watu wenye uchangamfu ... waliofurahia tu maisha," kaka yake, Eh Xiong, aliiambia BBC News. "Hata alijifunza Kihispania."
"Haijawahi hata kuingia akilini mwake kwamba angeishia kwenye tukio la kutisha namna hii."
Tou Ger, 50, alikuwa mwanaharakati wa jamii ya Hmong-American na mcheshi kutoka Minnesota. Kabla ya safari yake ya hivi majuzi zaidi huko Medellin, alikuwa akizungumza na mwanamke mtandaoni.
Wiki chache katika ziara yake ya miezi miwili, katikati ya Desemba, alimpigia simu kaka yake na kumwomba $2,000 lakini hakusema ilikuwa ya nini au kwamba kulikuwa na kitu kibaya. Eh alisema atamtumia pesa. Hakuwahi kusikia kutoka kwa kaka yake tena.
Siku iliyofuata, polisi walipata mwili wa Tou Ger katika eneo la mbali, lenye miti ya jiji. Rafiki mmoja huko Medellin alimweleza Eh kwamba kaka yake alikuwa ametekwa nyara na kushikiliwa akiwa amenyooshewa bunduki kwa ajili ya fidia ya $2,000.
"Sikutaka kuamini. Sikujua kama ilikuwa inafanyika kweli," Eh alisema. "Moyo wangu ulizama tu."
Eh alihangaika kuwasiliana na ubalozi wa Marekani, ambao ulithibitisha kuwa ulikuwa mwili wa kaka yake. Polisi wa Colombia wiki hii walimkamata mwanamke mmoja na wanaume wawili wanaohusishwa na kifo chake, wakiwafungulia mashtaka ya utekaji nyara na mauaji.
Haijabainika iwapo alikutana na mwanamke huyo kwa mara ya kwanza kupitia programu ya kuchumbiana au kupitia marafiki. Lakini kifo chake ni kimoja kati ya wanane huko Medellin ambacho kilisababisha onyo kutoka kwa ubalozi wa Marekani kuhusu hatari za kutumia programu za kuchumbiana. Waathiriwa wote wanane walikuwa Wamarekani ambao walikufa katika hali ya kutiliwa shaka mnamo Novemba na Desemba.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema inafahamu kuhusu genge katika jiji hilo ambalo hapo awali lilitumia programu za uchumba kuwatenga waathiriwa kabla ya kuwateka nyara na kuwaua. Lakini haijulikani ikiwa genge lilikuwa likihusika na vifo vya Wamarekani.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika miezi 10 ya kwanza ya 2023, kituo cha uangalizi wa utalii cha Medellin kilikuwa tayari kimerekodi mauaji ya kikatili 32 ya wageni katika jiji hilo - ikiwa ni pamoja na takriban Wamarekani 12 na watatu kutoka Uingereza - ongezeko la 40% kutoka mwaka uliopita.
Jeff Hewett alipatikana "akiwa amekufa kwenye dimbwi la damu" katika chumba chake cha hoteli cha Medellin, marafiki zake waliandika mtandaoni, wakimtaja kama "mwenye roho nzuri , mkarimu" na mwathirika wa "wizi uliotibuka".
Johny Jerome aliuawa katika siku yake ya kuzaliwa akitimiza miaka 45. Phillip Mullins alilewa na kufariki kutokana na matumizi ya kupita kiasi, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.
Ubalozi huo unasema baadhi ya visa hivi vilianza na programu ya kuchumbiana inayotumiwa kuwarubuni waathiriwa, ikiwa ni sehemu ya ongezeko la watu ambao huishia "kunywa dawa za kulevya, kuibiwa, na hata kuuawa wakikutana na wasichana wa Colombia". Hakuna kati ya Tinder wala Bumble, zote maarufu katika jiji, zilizoweza kutoa maoni.
Carlos Calle, mkurugenzi wa zamani wa kituo cha uchunguzi wa utalii cha jiji hilo, alisema ni kawaida kwa wahalifu kuwalevya watalii kutumia dawa iitwayo scopolamine, isiyo na harufu inayojulikana kama "Pumzi ya Shetani". Ubalozi wa Marekani pia ulionya kuhusu dawa hiyo, ambayo huwatuliza waathiriwa kwa hadi saa 24.
"Kuna wasifu mbaya wa mtalii katika jiji ambao hutafuta aina fulani ya fursa," Calle alisema katika mahojiano. Kawaida inahusiana na kazi ya ngono, alisema.
Msemaji wa kitengo cha uchunguzi wa utalii alithibitisha kuwa "wengi" wa waathiriwa mwaka jana walikuwa wanaume, lakini akaongeza kuwa kesi nyingi bado zinaendelea kuchunguzwa.
Ukahaba ni halali nchini Kolombia na umeenea katika maeneo yenye utalii kama vile miji ya Medellin na Cartagena. Lakini hakuna kitu kinachoonyesha kuwa wanaume waliouawa walikuwa wakitumia makahaba.
Alok Shah, 36, anadhani scopolamine ndiyo iliyosababisha uwezo wake wa kuona vizuri 'kupotea' alipokuja na mwanamke kwenye chumba chake cha hoteli mwishoni mwa 2022. Ilikuwa kana kwamba kumbukumbu yake ya muda mfupi ilikuwa ikitoweka, alisema.
Mkazi huyo wa Texas alikuwa amepatana na mwanamke wa Colombia mwenye umri wa miaka 20 hivi kwenye Tinder. Walitoka kwanza kunywa kahawa, lakini baadaye Shah aliamua kununua bia na kumleta hotelini kwake.
Anasema hakujisikia salama wakati wa ziara zake za mara kwa mara huko Medellin, au kama ukahaba ulikuwa umeenea alipokuja kwa mara ya kwanza mwaka wa 2017. Lakini alijua wanawake walikuwa kivutio cha jiji hilo. "Ikiwa wewe ni mvulana bila mchumba wanawake ni wazuri sana hapa," rafiki yake alimwambia.
Kabla ya saa yake, koti na pesa taslimu $200 kutoweka usiku huo, anakumbuka mwanamke huyo akipaka 'unga' kwenye shingo yake. Lakini alikaa na fahamu kiasi cha kutambua kwamba kuna kitu kibaya kilikuwa kikifanyika na kutishia kuwaita polisi na kumfukuza.
"Kwa ujumla sitangamani na wenyeji huko sasa," alisema. "Kuna hatari nyingi sana, kuna hatari nyingi sana."
Notisi mpya ya ubalozi wa Marekani inapendekeza raia wake waepuke kupeleka wanawake wanaofanya nao urafiki katika maeneo ya faragha kama vile hoteli, pamoja na kuwafahamisha marafiki, familia au wafanyakazi wa majengo kuhusu walio nao. Na usijaribu kuzuia wizi kwa sababu hiyo inaweza kugeuka na kuwa janga.

Chanzo cha picha, Getty Images
Polisi wa jiji la Medellin hawakutoa maoni yoyote juu ya ongezeko la hivi majuzi la vifo vya kikatili na walielekeza BBC News kwa ofisi ya meya.
"Tunataka wageni zaidi na zaidi kuja mjini," alisema Meya Federico Gutierrez, lakini akaongeza kuwa watalii wanaokuja kwa ajili ya ngono na dawa za kulevya hawakaribishwi. Alisema amewaelekeza polisi kukabiliana na kile anachosema ni suala la msingi linalohusiana - biashara ya ngono ya watoto.
Polisi wameagizwa kuanza "uchunguzi maalum" katika vitongoji ambako utalii ni maarufu zaidi, msemaji wa meya aliambia BBC News, ikiwa ni pamoja na eneo maarufu la burudani ya usiku liitwalo El Poblado.
Zaidi ya wageni milioni 1.4 walitembelea jiji hili kama watalii mnamo 2022, rekodi mpya zaidi ya miaka iliyopita, na zaidi ya robo walikuwa Wamarekani, kulingana na takwimu zilizotolewa na ofisi ya meya. Takwimu za 2023 zinatarajiwa kuwa kubwa zaidi, kwa sababu Medellin imekuwa mahali pa juu kwa wafanyikazi wa mbali.
Wiki iliyopita, Eh Xiong alikuja Medellin mwenyewe kwa mara ya kwanza, kutekeleza mila ya Hmong kwa kuita roho ya kaka yake irudi nyumbani.
"Hatuna hasira na watu wa Colombia," alisema. "Ninaamini kweli kwamba angewasamehe watu waliomfanyia hivyo."
Aliongeza: "[Tou Ger alikuwa] na akili hii ya haraka, kutoogopa, ambayo inaamini katika wema wa watu wote."
Austin Landis ni mwandishi wa habari aliyeko Medellin, anayeangazia uhamiaji na habari kutoka Colombia. Hapo awali aliandika kuhusu Ikulu ya White huko Washington akifanyia kazi shirika la Spectrum News
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












