Je, historia ya Iraq, Libya na Palestina inajirudia Iran?

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC, Nairobi
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Wakati ambapo vita kati ya Iran na Israel vinaendelea, Marekani imeonyesha ubabe wake kwa kushambulia maeneo ya Iran kwa makombora ya B-2.
Hatua hii imethibitishwa na Rais Trump mwenyewe kwa kuonyesha kusherehekea kushambulia maeneo ya nyuklia ya Iran na kueleza kuwa amesababisha uharibifu mkubwa.
Licha ya kwamba wachambuzi wengi wamezungumzia hili kama hatari ya kuwezesha kutanuka kwa vita katika Mashariki ya Kati, siku ya Jumapili kwenye jukwaa lake la mawasiliano la Truth Social, aliandika juu ya mustakabali wa serikali inayotawala Iran mjini Tehran, na kusema "Kwa nini kusiwe na mabadiliko ya utawala?"
"Si sahihi kisiasa kutumia neno 'mabadiliko ya utawala' lakini ikiwa serikali ya sasa ya Iran haiwezi kuifanya Iran kuwa bora tena, kwa nini kusiwe na mabadiliko ya utawala", Trump aliandika.
Wafuasi wake kwa kiasi kikubwa na washirika wameonekana kujitenga na kauli hiyo.
Ila nikurudishe nyuma kidogo, alilotaja Trump sio jambo geni kwa ulimwengu. Nchi kama Iraq, Libya na Palestina zimewahi kuwa mashahidi wa hali hii.
Je, Iran kufuata mkondo huo?
Iraq

Chanzo cha picha, Getty Images
Utawala wa Saddam Hussein ulipinduliwa mwaka 2003 kwa kisingizio cha kuwa na silaha za maangamizi ya halaiki, ambazo baadaye hazikupatikana.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio nambari 687 la kuiamuru Iraq kuharibu silaha zake zote za maangamizi makubwa (WMDs) - neno linalotumiwa kuelezea silaha za nyuklia, za kibayolojia na kemikali, na makombora ya masafa marefu.
Mnamo mwaka 1998, Iraq ilisitisha ushirikiano na wakaguzi wa silaha wa Umoja wa Mataifa, na Marekani na Uingereza zilijibu kwa mashambulizi ya anga.
Baada ya mashambulizi ya al-Qaeda ya Septemba 11, 2001 kwenye Kituo cha Biashara huko New York na Pentagon huko Washington, utawala wa Rais George W Bush ulianza kupanga mipango ya kuivamia Iraq.
Rais Bush alidai Saddam alikuwa akiendelea kuhifadhi na kutengeneza slaha za nyuklia na kwamba Iraq ilikuwa sehemu ya "mhimili wa uovu" wa kimataifa pamoja na Iran na Korea Kaskazini.
Mnamo Oktoba 2002, Bunge la Marekani liliidhinisha matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya Iraq.
Hata hivyo, hakulishawishi Baraza. Wengi wa wanachama wake walitaka wakaguzi wa silaha kutoka Umoja wa Mataifa na Mamlaka ya Nishati ya Kimataifa - ambao walikuwa wamekwenda Iraq mwaka 2002 - kufanya uchunguzi zaidi huko kutafuta ushahidi wa uwepo wa silaha hizo.
Hata hivyo, Marekani ilisema haitasubiri wakaguzi kuripoti, na ikakusanya "muungano wa walio tayari" dhidi ya Iraq.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Colin Powell aliiambia Umoja wa Mataifa mwaka 2003 kwamba Iraq ina "maabara maalum" kwa ajili ya kutengeneza silaha za kibaolojia.
Hata hivyo, alikubali mwaka 2004 kwamba ushahidi huo "unaonekana si ... wa uhakika".
Kwa upande wake, serikali ya Uingereza iliweka hadharani ripoti ya kijasusi ikidai kuwa makombora ya Iraq yanaweza kutayarishwa ndani ya dakika 45 kulenga shabaha za Uingereza mashariki mwa Mediterania.
Nchi hizo mbili zilitegemea sana madai ya waasi wawili wa Iraq - mhandisi wa kemikali kwa jina Rafid Ahmed Alwan al-Janabi na afisa wa ujasusi anayeitwa Maj Muhammad Harith - ambao walisema walikuwa na ujuzi wa moja kwa moja wa mpango wa WMD wa Iraq.
Wanaume hao wawili baadaye walisema walikuwa wametunga ushahidi wao kwa sababu walitaka washirika hao wavamie na kumfurusha Saddam.
Libya

Chanzo cha picha, Getty Images
Utawala wa Muammar Gaddafi uliangushwa mwaka 2011 kwa madai ya kuwa wa kidikteta, kwa msaada wa mashambulizi ya NATO.
Muammar Gaddafi alizaliwa mwaka wa 1942. Hakupata elimu ya kisasa ila madrassa pamoja na shule ya kijeshi.
Mwaka wa 1969 kanali Muammar Gaddafi aliongoza mapinduzi wakati huo akiwa afisa katika jeshi. Baada ya mapinduzi, Gaddafi aliahidi kuleta mageuzi ya kiuchumi, na kuwaondoa wageni aliosema wamethibiti taifa hilo.
Kanali Gaddafi akiwa kiongozi mpya alitaka kandarasi zote kubatilishwa na kutolea chini ya masharti mapya.
Sheria mpya ilifanya Libya kuwa taifa la kwanza masikini kuthibiti biashara ya mafuta, hatua iliyofanya nchi zingine za kiarabu kushinikiza umiliki wa mafuta yao. Miaka ya 70 kukawa na msisimuko wa kiuchumi katika mataifa ya kiarabu yaliyozalisha mafuta.
Kanali Gaddafi alijitangaza kama kiongozi wa waarabu, mfalme wa Afrika, Imam wa Waisilamu na mtetezi wa uhuru wa wanyonge.
Hata hivyo, uhusiano wa Libya na Marekani ulikuwa unaendelea kudorora na hamu ya Marekani ya kumuondoa Muammar Gaddafi ilitokana na mchanganyiko wa mambo ikiwa ni pamoja na msaada wa Gaddafi kwa ugaidi.
Gaddafi ilitajwa na Marekani kuwa "kiongozi wa nchi anayefadhili ugaidi" kutokana na kuhusika kwake katika mashambulizi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na bomu la 1986 la klabu ya usiku ya Berlin ambayo ilitembelewa na wanajeshi wa Marekani na bomu la Lockerbie, Scotland mnamo Desemba 21, 1988.
Vile vile, utawala wa Gaddafi ulikosolewa kwa rekodi yake ya haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kukandamiza upinzani, kufungwa jela kwa wanasiasa waliompinga na mauaji ya kiholela na upinzani wake dhidi ya sera ya kigeni ya Marekani katika eneo hilo.
Gaddafi alipinga waziwazi ushawishi wa Marekani katika Mashariki ya Kati na Afrika na kuunga mkono harakati za zilizopinga nchi za Magharibi na sera ya kigeni ya Marekani katika eneo hilo.
Vile vile, vuguvugu la ghafla katika nchi za Uarabuni ambazo pia zilikumba Libya mwaka 2011, ilisababisha Libya kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe huku NATO na mshirika wake Marekani, zikianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya majeshi ya Gaddafi, na hatimaye kuchangia kuuawa kwa Gaddafi na kuanguka kwa utawala wake.
Hata hivyo, mashirika ya haki za binadamu yalitilia shaka madai hayo baada ya kupata ukosefu wa ushahidi.
Palestina

Chanzo cha picha, Getty Images
Israel ilianzisha kampeni ya kijeshi huko Gaza kujibu shambulio la kuvuka mpaka lililoongozwa na Hamas tarehe 7 Oktoba 2023 ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka. Vita hivyo bado vinaendelea hadi sasa.
Marekani kwa muda mrefu imekuwa ikitafuta suluhisho la mzozo kati ya mataifa hayo mawili ambão umekuwepo tangu jadi, lakini utawala wa Trump ulichukua sera ambazo zilitofautiana na lengo la awali na moja kwa moja Marekani ikaonekana kuunga mkono Israel kwa hoja ya kupambana na mamlaka za kigaidi au kuziangamiza kabisa makundi hayo kama vile Hamas.
Lakini watetezi wa Palestina na Hamas wanaona kuwa uungwaji huu mkono wa Israel na taifa la Marekani ndio unaolipa nguvu taifa hilo hata wakati mwengine kukiuka maagizo ya Umoja wa Mataifa.
Kwa kifupi, nikufahamishe yaliyofanywa Marekani kuonyesha kuunga mkono Palestina.
Waisrael na Wapalestina wamekuwa wakigombana tangu enzi na enzi juu ya madai ya ardhi Takatifu ikiwa ni pamoja na migogoro juu ya mipaka, Yerusalemu, usalama, na wakimbizi wa Kipalestina mzozo ambao umekuwa moja ya mgogoro mgumu zaidi ulimwenguni.
Marekani iliitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Wayahudi chini ya utawala wa kwanza wa rais wa Marekani Donald Trump. Hili ni jambo ambalo liliwakera sana Wapalestina waliochukulia hatua hiyo kama ushahidi wa wazi kuhusu msimamo wa Marekani kwa Israel.
Chini ya utawala wa Trump, Marekani ilisitisha fedha zote kwa shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Palestina, UNRWA.
Hilo likitokea zaidi ya nchi 10, ziliunga mkono Marekani na kusitisha ufadhili wake kufuatia madai ya kijasusi ya Israel kwamba wanachama wasiopungua 12 wa UNRWA walihusika katika shambulio la Hamas dhidi ya Israel.
Hata hivyo, Sweden na Canada baadaye, zilitangaza tena malipo ya kufadhili UNRWA, shirika lililopo kwa ajili ya kusaidia Wapalestina.
Israel imekuwa ikipewa misaada ya kifedha na Marekani kwa muda mrefu na hilo limekuwa likifanyika tangu vita vya pili vya dunia. Kwa mfano mnamo mwaka wa 2016 rais wa Marekani wakati huo Barack Obama alisaini mkataba wa ulinzi wa Dola bilioni 386 kuisaidia Israel pamoja na ufadhili wa miaka 10 wa mfumo wao wa ulinzi.
Vile vile, Donald Trump alishtua dunia kwa kupendekeza kwamba Marekani inaweza "kuchukua" na "kumiliki" Gaza.
Trump alidokeza kuwa chini ya mpango wake, Gaza itakabidhiwa kwa Marekani na Israel na wakazi wake watahamishwa mahali pengine bila kuwa na haki ya kurudi.
Trump aliamini kwamba Wagaza wakiondoka, "ataweza kujenga eneo la kitalii la Mashariki ya Kati" na kutoa fursa za kazi kwa maelfu ya watu, fursa za uwekezaji, na, mwishowe, mahali pa "watu wa ulimwengu kuishi".
Hata hivyo, mpango huo ulipingwa vikali na nchi za Uarabuni.

Chanzo cha picha, Reuters
Hali ikiwa sio tofauti sana na ilivyotokea katika nchi nilizoziangazia, Juni 13, 2025 Israel ilianza kuyashambulia maeneo ya kurutubisha madini ya Urani, na kuua makamanda na wanasayansi kadhaa wa nyuklia wa Iran.
Ripoti ya robo mwaka ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) ilionyesha kuwa Iran imefanikiwa kurutubisha urani hadi asilimia 60 lakini lilisitisha uchunguzi wake wa hivi karibuni baada ya kuanza kwa vita huku Netanyahu akisisitiza kuwa Iran ingeweza kutengeneza silaha za nyuklia "ndani ya mwaka mmoja au miezi michache" kama hali halisi isingebatilishwa.
Lakini madai kwamba Iran iko karibu kutengeneza vifaa vinavyoweza kutumika kutengeneza silaha za nyuklia si mapya na yamekuwa yakitolewa mara kadhaa.
Ikiwa Iran kufuata mkondo wa Iraq, Libya na Palestina ni suala la kusubiri kwa muda tu huku Marekani ikiwa tayari imeshachukua hatua ya kushambulia maeneo ya nyuklia ya nchi hiyo.















