Mwanamke amshikilia mwanamke mwanzake mateka kwa miaka 25

Muda wa kusoma: Dakika 3

Raia mmoja wa Uingereza amepatikana na hatia ya kumshikilia mateka mwanamke mwenzake aliyekuwa na matatizo ya kutangamana na wengine katika jamii, na kumtumikisha kama mtumwa kwa miaka 25.

Mandy Wixon, mwenye umri wa miaka 56, mama wa watoto 10, alimlazimisha mwanamke mwenzake kusafisha nyumba yake iliyojaa vitu chungu nzima huko Tewkesbury, Gloucestershire, na kumlazimisha kula mabaki.

Mwathiriwa alimwagiwa sabuni kooni, dawa ya kuua vijidudu usoni, na kichwa chake kikanyolewa mara kwa mara kinyume cha mapenzi yake.

Katika Mahakama ya moja huko Gloucester, Jaji Ian Lawrie alisema kulikuwa na "uonevu wa kijamii" katika kesi hiyo kwani Wixon alipatikana na hatia ya kifungo cha uongo, kumtaka mtu kufanya kazi ya kulazimishwa au ya lazima, na kumshambulia mara kwa mara ambako hatimaye kulisababisha madhara katika mwili wa mwathirika.

BBC kwa sasa imeweza kutoa taarifa kamili kuhusu kesi hiyo.

Mahakama iliarifiwa kwamba mwanamke huyo - ambaye BBC inamwita K - alizaliwa katika familia maskini na alipokuwa na umri wa miaka 16 hivi mwaka 1996, alikabidhiwa Wixon, ambaye alikuwa na uhusiano mdogo na familia yake.

Sasa akiwa na umri wa miaka ya 40, K alipatikana na polisi mnamo Machi 15, 2021 baada ya mmoja wa watoto wa Wixon kuzungumzia wasiwasi wake kuhusu ustawi wa mwanamke huyo.

Mahakama ilielezwa kwamba K alipigwa mara kwa mara kwa mpini wa ufagio, na kung'olewa meno.

Wixon alimpa mwathiriwa chakula kidogo na hakumruhusu kutoka nje ya nyumba na alilazimika kuoga kwa siri usiku.

Maafisa walielezea chumba cha kulala cha K kuwa kilionekana kama "seli gerezani", huku vyumba vingine vya kulala pia vikiwa vikichafu.

Wakati mwingine, kulikuwa na angalau watu 13 wanaoishi katika nyumba hiyo.

K alikuwa amepoteza meno yake mengi kutokana na afya duni ya meno.

Alipogunduliwa na polisi, alikuwa na makovu kwenye midomo na uso wake kutokana na kunyunyiziwa dawa ya kuua vijidudu, na madoa makubwa kwenye miguu na vifundo vya miguu kutokana na kuwa kila mara alitumia mikono yake na kuinama kwa magoti akisafisha sakafu.

K aliwaambia maafisa: "Sitaki kuwa hapa. Siko salama. Mandy hunipiga kila wakati. Ninachukizwa na kitendo hicho."

Madaktari waligundua kuwa mwathiriwa alikuwa na utapiamlo, huku daktari wa meno akibainisha kwamba alikuwa katika maumivu makali kwa miaka mingi kutokana na maambukizi na majipu yasiyotibiwa.

Sajenti Mkuu Alex Pockett alisema: "Polisi walipofika, mwathiriwa alikuwa ameinamisha kichwa chake chini, ilikuwa wazi kwamba alikuwa na hofu kubwa."

Sam Jones, mwendesha mashtaka, aliambia jopo la majaji: "Kufikia mwishoni mwa miaka ya 1990 inaonekana mwanamke huyo alitoweka kwenye shimo jeusi. Hakuna hata siku moja aliwahi kwenda nje ya nyumba."

Wixon aliachiliwa kwa dhamana ya masharti na atahukumiwa tarehe 12 Machi.

Alipoondoka mahakamani aliulizwa alichokuwa anataka kumwambia mwathiriwa wake na kujibu: "Sina mengi."

Alipoulizwa kama alihisi vibaya kwa alichofanya, alisema: "Hapana. Sijawahi kufanya hivyo."

Waandishi wa habari waliuliza kama alikuwa "mnyama", aliposimama kuwasha sigara, naye akajibu: "Sema unachofikiria."

Afya ya mwathiriwa sasa 'imestawi'

Tangu alipookolewa, K sasa anaishi na familia ya kumlea, amepelekwa shule na kwenda likizo nje ya nchi.

Afisa wa polisi Emma Jackson alisema afya ya mwathiriwa "imestawi" na anaishi maisha mazuri.

Laura Burgess, mwendesha mashtaka mkuu, aliongeza: "Maendeleo aliyoyapata tangu kuondolewa katika mazingira haya ya ukandamizaji ni ushuhuda wa kupigiwa mfano."

"Tunamkumbuka katika maombi yetu anapoendelea kujenga upya maisha yake, na natumai anaweza kupata faraja katika kuona haki ikitekelezwa leo."