Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ushirikiano wa madini kati ya DRC na Marekani: Ni nani atanufaika?
Marekani imesema iko wazi kuchunguza ushirikiano wa rasilimali muhimu ya madini na serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo(DRC) , huku Congo ikitaka usaidizi wa Marekani katika vita vyake vinavyoendelea dhidi ya waasi wanaodhibiti "10% ya eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo", kulingana na Kinshasa.
Hatua hii inafuatia Kinshasa kutangaza mipango ya kuimarisha jeshi katika suala la fedha na silaha na kuiwezesha kutekeleza hilo.
DRC ambayo ina utajiri mkubwa wa kobalti, lithiamu na uranium miongoni mwa madini mengine, imekuwa ikipambana na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda ambao wameteka maeneo mengi ya ardhi yake mwaka huu.
Je, ni nani atakayenufaika katika ushirikiano huu mpya wa nchi mbili?
Ombi la uhusiano wa DRC kwa Marekani lipi?
Katika ushirikiano huu, serikali ya Kinshasa inataka kuyapa makampuni ya Marekani haki ya kuchimba na kusindika madini ya thamani, na kulipia msaada huo, serikali ya Kishasa inataka ushirikiano wa kijeshi na Marekani, ikiwa ni pamoja na mafunzo na vifaa kwa jeshi la Congo.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, serikali ya Kinshasa iliiomba Marekani kuwekeza katika "nchi yenye hifadhi ya madini ya thamaini ya dola trilioni 24 ambayo hayajatumika," madini "ni muhimu kijeshi, kiteknolojia na nishati," kulingana na barua serikali ya Kinshasa kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.
"Kuna nia ya sisi kubadilisha washirika wetu," msemaji wa serikali ya DRC, Patrick Muyaya alisema wiki iliyopita.
"Ikiwa leo wawekezaji wa Marekani wana nia ya kuja DRC, ni wazi watapata nafasi ... DRC ina akiba ambayo inapatikana na itakuwa vizuri kama mitaji ya Marekani inaweza kuwekeza hapa," alisema.
Barua ya DRC inaomba kwamba Rais Trump binafsi awepo kwenye mijadala kuhusu ushirikiano huu, na kwamba "mkutano kati ya Rais Trump na Rais Tshisekedi utakuwa muhimu" katika kufanikisha ushirikiano huu.
Akielezea kuhusu ushirikiano wa Marekani na DRC, Tina Salama, msemaji wa Rais Tshisekedi, aliandika kwenye ukurasa wa X kwamba Tshisekedi aliialika Marekani " yenye makampuni yanayonunua" vifaa vya msingi kutoka Rwanda, "vinavyoporwa nchini DRC na kuingizwa nchini Rwanda", na kwamba sasa wanaiomba Marekani inunue "kutoka kwa wamiliki wake halali".
Mamlaka za Rwanda zinasema kuwa madini ya DRC sio sababu ya mzozo wake na DRC na kwamba "wanaochimba na kufaidika nayo" ni makampuni kutoka nchi za Magharibi. Rwanda pia inakanusha kulisaidia kundi la waasi wa M23.
Marekani inasemaje?
Serikali ya Washington imetangaza kuwa iko tayari kufanya kazi na serikali ya DR Congo kuhusu madini, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani aliambia Reuters.
"Marekani iko tayari kujadili ushirikiano katika sekta hii ambao unaambatana na ajenda ya Kwanza ya Utawala wa Trump," Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema, akibainisha kuwa Congo ina "sehemu kubwa ya madini muhimu duniani yanayohitajika kwa teknolojia ya juu."
Marekani imefanya kazi "kukuza uwekezaji wa sekta binafsi ya Marekani nchini DRC ili kuendeleza rasilimali za madini kwa njia ya kuwajibika na ya uwazi," msemaji huyo aliongeza.
Je, DRC itanufaika na ushirikiano na Marekani?
Kulingana na wachambuzi waliozungumza na BBC huenda DRC ikapoteza kuliko kunufaika na uhusiano huu mpya.
Timothy J. Oloo, Profesa wa sayansi ya siasa katika vyuo vikuu nchini Kenya na Tanzania ameiambia BBC : '' Utawala wa Donald Trump nchini Marekani umeonesha kiu ya kufuatilia maslahi ya Marekani "popote wanayoweza kuyapata kwa gharama yoyote ile'', aliiambia BBC
Aliongeza: "Bila shaka kwamba DRC inaibembeleza Marekani sababu inajua kabisa kile anachokitaka Trump, na ikiwa Marekani itakuja Congo, haitakuja kama mpatanishi wa amani bali kama mtu hodari anayekuja kutafuta maslahi yake na kwa njia yoyote iwezekanayo."
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Congo Justin Hunatabu anakubaliana na Profesa Oloo kwamba uhusiano wa madini wa Marekani na DRC, hauwezi kuwa suluhu ya mzozo wa DRC.
Justin anasema hakubaliani kile anachokitaja kuwa kuonesha kuwa mzozo wa DRC unatokana na madini: '' Mimi sikubaliani kabisa na mawazo kwamba vita hivi vinatokana na madini, kwasababu madini yote ya Afrika yanaenda kwa nchi za Magharibi, Ulaya na China… Kama Marekani inaingia mikataba ya madini, ni wajibu wake tu kama mmoja tu wa vigogo wa dunia, wanaofanya biashara kwa maslahi yake lakini sio kutafuta suluhu la mzozo wa Congo.''
'Suluhisho halitatoka Washington au Paris'
Timothy Oloo ameiambia BBC kwamba juhudi za kufikia amani zinahujumiwa na vitendo vya pande zote mbili zinazoendelea kusababisha vita.
"Ukiangalia jinsi M23 inavyojijenga upya, na jinsi serikali ya Kinshasa nayo inavyozidi kupata nguvu, unaona kwamba hizi si dalili nzuri za kuelekea upatikanaji wa suluhu ya mgogoro huu ," alisema.
Madini ya thamani ya DRC yanavutia makampuni mengi kutoka nchi zilizoendelea kiteknolojia, ambayo huyatumia kutengeneza vifaa vya kisasa, kuanzia kompyuta, simu, silaha, magari hadi vyombo vya anga.
Alipoulizwa kuhusu ni kwa kiasi gani ushirikiano baina ya DRC na Marekani unaweza kuyadhibiti makundi M23 na makundi mengine yanayopigana Mashariki mwa Congo Bw Hunatabu Alisema: ''M23 sio kama makundi mengine, kwasababu makundi mengine yanakuwa hayana malengo yoyote wala uungaji mkono malengo. M23 ni muungano uliojipanga vizuri, ni watu wanaojua wanachokifanya.'', aliongeza.
Haamini kwamba Marekani kuanza ushirikiano na DRC kuhusu madini itaweza kuvunja harakati za M23, kwasababu kundi hilo limejipanga vyema.
Timothy Oloo anaamini kuwa suluhu ya mzozo nchini DR Congo itatoka Afrika.
Alisema: "Ni muhimu kwa pande zinazozozana kuelewa wazi kwamba ni juhudi za nchi na mashirika ya kikanda pekee kama vile SADC na EAC zinaweza kuleta suluhu ya kudumu. Suluhu ya tatizo hili halitatoka Washington au Paris."
Aliongeza: "Tatizo la Congo, kama matatizo kama yale ya Sudan, yanaweza kutatuliwa na sisi kama Waafrika kuaminiana na kuwasikiliza wale wanaoshiriki uzoefu hapa katika bara letu."
Hadi sasa Marekani haina makampuni yanayomilikiwa na serikali kama ilivyo kwa mshindani na hasimu wake wa kiuchumi China , na hakuna makampuni binafsi ya uchimbaji madini ya Marekani kwa sasa yanafanya kazi nchini Congo.
Iwapo itaingia nchini Congo itatakiwa kuanza mchezo mpya kwenye uwanja mpya wenye washindani wengi ambao lengo lao kuu ni madini ya kupata mgao wao raslimali muhimu za Congo. Je, serikali ya DRC itaweza kuwashinda waasi wa M23 na kumaliza makundi mengine yenye silaha na kurejesha amani na utulivu?
Imehaririwa na Lizzy Masinga