Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aapa vita 'vikali' vya kuwakomesha waasi wa M23
Rais wa Kongo Félix Tshisekedi ameapa kurejesha mamlaka ya serikali mashariki mwa nchi, ambako waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameuteka mji wa Goma na wanaripotiwa kuelekea kusini kuchukua maeneo zaidi.
Muhtasari
- Binti wa Rais wa zamani wa Afrika kusini akabiliwa na mashtaka ya kuchochea vurugu
- Wanajeshi wa Chad warejeshewa kambi zilizobaki zilizokuwa zikimilikiwa na Ufaransa
- Uganda yathibitisha mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika mji mkuu Kampala, huku mmoja afariki
- Mwanamume aliyechoma Quran 'auawa nchini Uswidi'
- Miili 30 imepatikana baada ya ndege na helikopta kuanguka kwenye mto Washington DC
- Mzozo wa DRC: Mamia ya wakimbizi waliokimbia Rubavu nchini Rwanda wanarejea Goma
- Kenya: Wanawake 9 hufariki kila siku kutokana na ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi
- Kenya: Gavana za zamani ahusishwa na kesi ya mauaji ya mwanafunzi
- Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aapa vita 'vikali' vya kuwakomesha waasi wa M23
- Ndege imevunjika vipande vipande huku helikopta ikisalia kuwa imara
- Wanamgambo wa Hamas na Islamic Jihad walivyokusanyika Khan Younis
- Israeli yathibitisha kuachiliwa kwa mateka mmoja
- Urusi yaondoa vifaa vya kijeshi kutoka bandari ya Syria, picha zinaonyesha
- Trump anasema Marekani itatuma wahamiaji wengine kwenda Guantanamo Bay
- Miili yapatikana mtoni; Helikopta ya kijeshi ilikuwa kwenye mafunzo - CBS
- Abiria 60 na wafanyakazi 4 walikuwa kwenye ndege iliyogongana na helikopta - CBS
- Ndege ya American Airlines yagongana na helikopta huko Washington DC
- Rwanda na Afrika Kusini zipo katika mgogoro wa kidiplomasia juu ya mzozo wa DRC
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid & Asha Juma
Binti wa Rais wa zamani wa Afrika kusini akabiliwa na mashtaka ya kuchochea vurugu

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Duduzile Zuma-Sambudla ni mwanaharakati mwenye msimamo mkali nchini Afrika Kusini Duduzile Zuma-Sambudla ambaye ni binti wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma, amefika mahakamani kwa mashtaka dhidi yake ya ugaidi akihusishwa na ghasia za 2021 zilizosababisha vifo vya watu 300.
Vurugu, ghasia, na hofu vilikumba jiji la bandari la Durban, kisha kusambaa hadi Gauteng, baada ya kifungo cha Zuma kuchochea maandamano makali zaidi ya miaka minne iliyopita.
Zuma-Sambudla, ambaye ni mwanaharakati , anashutumiwa kwa kusambaza jumbe mitandaoni zinazodaiwa kuchochea maandamano ya ghasia.
Kukamatwa kwake kumejiri baada ya ‘’uchunguzi kukamilika’’ anasema msemaji wa kikosi cha polisi cha Hawks, Brigedia Thandi Mbambo.
Zuma- Sambudla alijisalimisha katika kituo cha polisi cha Durban asubuhi ya Alhamisi kukabiliana na mashataka dhidi yake.
Zuma- Sambudla aliambia mahakama kuwa anapanga kukanusha mashtaka yake.Alisema pia hakuna Ushahidi unaoonyesha uhusiano wake na vurugu hizo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi mwezi Machi kwa ajili ya kusikilizwa katika Mahakama kuu ya Durban na yeye ameachiwa kwa dhamana.
Wafuasi wa chama cha baba yake, uMkhonto WeSizwe (MK), ambapo yeye ni kiongozi wa ngazi ya juu, walikusanyika mahakamani kumtia moyo.
Rais wa zamani wa Afrika kusini Jacob Zuma alikuwepo pia na kutoa hotuba.
“Wanakamata mtoto wangu sasa kwa sababu hawampendi, wala hawampendi baba yake, wala chama anachokiongoza. Tutakaa kimya?” alisema.
Hii siyo mara ya kwanza jina la Zuma-Sambudla kuhusishwa na vurugu za mwaka 2021, ambazo zinachukuliwa kuwa mojawapo ya matukio yenye ghasia zaidi tangu kumalizika kwa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Zuma alijiuzulu kama rais mwaka 2018 baada ya miaka tisa madarakani, akiwa na tuhuma za rushwa, ambazo alidai ni njama za kisiasa.
Alikataa kutoa ushahidi katika uchunguzi wa kisheria kuhusu tuhuma hizo na alifungwa jela kwa kudharau mahakama.
Maandamano yalianza baada ya yeye kujisalimisha kutumikia kifungo chake.
Unaweza pia kusoma:
Wanajeshi wa Chad warejeshewa kambi zilizobaki zilizokuwa zikimilikiwa na Ufaransa

Chanzo cha picha, Getty Images
Kambi tatu za kijeshi za Ufaransa zilizoko Chad zimekabidhiwa rasmi kwa jeshi la Chad, makao makuu ya jeshi la Chad yasema.
kurejeshwa kwa kambi ya kijeshi wa Sajeny Adji Kossei katika mji mkuu wa N’Djamena kunaashiria mwisho wa ushirikiano wa kijeshi wa miongo kadhaa kati ya Chad na Ufaransa, koloni lake la zamani, kwa mujibu wa taarifa za shirika la Habari la AFP.
Mwezi Novemba, Chad ilitangaza kusitisha mkataba muhimu wa ushirikiano wa ulinzi na Ufaransa, na baada ya hapo, wanajeshi 1,000 wa Ufaransa walianza kuondoka nchini humo.
Kambi hizo za kijeshi zilikuwa zikitumiwa na Wafaransa kutoa usaidizi wa kijasusi na vifaa kwa jeshi la Chad katika vita dhidi ya waasi na kulinda maslahi yake katika eneo la Sahel.
Mali, Niger, Burkina Faso, Senegal, na Ivory Coast, Chad ni miongoni mwa nchi zilizokuwa chini ya utawala wa Ufaransa katika Afrika Magharibi na Kati ambazo zimevunja mikataba ya usalama na Ufaransa na mataifa mengine ya Magharibi katika miaka ya hivi karibuni.
Baadhi ya nchi hizo zimeigeukia Urusi kwa misaada badala yake, ikiashiria kujitenga mbali na washirika wao wa jadi wa Magharibi.
Mapema mwezi Januari, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema kwamba mataifa ya Sahel “yalikosa” kuishukuru Ufaransa kwa mchango wake katika kuwasaidia kupambana na waasi wenye silaha.
Akionekana kumjibu Rais Macron, Waziri wa Mambo ya Nje wa Chad, Abderaman Koulamallah, alisema katika taarifa kwenye televisheni ya taifa kuwa maoni ya Macron yalionyesha dhihaka dhidi ya Afrika, akitaka viongozi wa Ufaransa “waheshimu na kutambua” maadili ya Kiafrika na kujitolea kwao.
Mamlaka ya Chad imeendelea kusema kwamba kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo hakutakuwa na athari kwa uhusiano wa Chad na Ufaransa katika maeneo mengine.
Pia unaweza kusoma:
Uganda yathibitisha mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika mji mkuu Kampala, mmoja afariki

Chanzo cha picha, Getty Images
Uganda imethibitisha kuzuka kwa ugonjwa wa hatari wa Ebola katika mji mkuu Kampala, huku mgonjwa wa kwanza aliyethibitishwa akifariki kutokana na ugonjwa huo siku ya Jumatano, wizara ya afya imesema Alhamisi.
Mgonjwa huyo ambaye ni muuguzi katika hospitali ya rufaa ya Mulago jijini Kampala, mwenye umri wa miaka 32 awali alikuwa akitafuta matibabu katika vituo mbalimbali ikiwemo Mulago baada ya kupata dalili za homa, maumivu ya kifua na kupata shida kupumua, kulingana na tangazo la Wizara ya afya ya Gganda
"Mgonjwa huyo alipatwa na matatizo mengi ya kiafya na akafariki dunia katika hospitali ya rufaa ya taifa ya Mulago Januari 29. Sampuli za baada ya kifo zilithibitisha 9kuwa alikuwa na aina ya ugonjwa wa Ebola ya Sudan (strain)," wizara hiyo ilisema.
Wizara ya Afya ya nchi hiyo inasema kuwa kwanza alionesha dalili za homa kali, maumivu ya kifua na ugumu wa kupumua. Baadaye alipata kuvuja damu kutoka kwa viungo vingi vya mwili kabla ya kupata kushindwa kwa aina nyingi na kusababisha kifo chake.
Maafisa wa afya wanasema timu za kukabiliana na ugonjwa huo zimetumwa kufanya ufuatiliaji wa mawasiliano na kutekeleza hatua za kudhibiti ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Huu ni mlipuko wa hivi karibuni wa Ebola nchini Uganda tangu ule uliotangazwa mnamo Septemba 20, 2022, ambao pia ulisababishwa na virusi vya Ebola vya Sudan. Mlipuko huo, uliojikita katika wilaya ya Mubende, ulikuwa mlipuko wa kwanza wa virusi vya Ebola nchini Sudan katika muongo mmoja na wa tano kurekodiwa nchini Uganda. Ilitangazwa mnamo 11 Januari 2023.
Kuna aina sita zinazojulikana za virusi vya Ebola. Nne-Zaire, Bundibugyo, Sudan, na Msitu wa Taï—zinajulikana kusababisha magonjwa kwa wanadamu. Matatizo ya Reston na Bombali kimsingi huathiri nyani wasio binadamu.
Mwanamume aliyechoma Quran ‘auawa nchini Uswidi’

Chanzo cha picha, Reuters
Mtu mmoja aliyeanzisha maandamano ya ghasia baada ya kuchoma Quran ameuawa kwa risasi nchini Uswidi, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya eneo hilo.
Salwan Momika, mwenye umri wa miaka 38, ameripotiwa kuuawa katika jumba moja huko Södertälje, Stockholm usiku wa jumatano.
Ghasia ziliibuka baada ya Momika kuchoma kitabu kitakatifu cha waumini wa kiislamu Quran nje ya msikiti wa Stockholm mwaka 2023.
Polisi mjini Stockholm wamethibitisha kuwa wamewakamata watu watano baada ya mtu mmoja aliye na umri wa makamo kuuawa kwa risasi usiku wa kuamkia leo.
Vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti kwamba Bwana Momika alikuwa akifuatilia matukio hayo kwa njia ya moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii wakati alipouawa.
Bwana Momika, raia wa Iraq aliyeishi Uswidi, alikabiliwa na mashtaka mnamo Agosti pamoja na mtu mwingine kwa “uchochezi dhidi ya kabila fulani” mara nne mwaka 2023.
Hukumu ilikuwa itolewe leo Alhamisi, lakini ilicheleweshwa baada ya “kuthibitishwa kwamba mmoja wa washtakiwa alifariki,” ilisema Mahakama ya Wilaya ya Stockholm.
Bwana Momika alifanya maandamano kadhaa dhidi ya Uislamu, na kuibua hasira katika nchi nyingi zenye idadi kubwa ya waumini wa kiislamu.
Vurugu zilizuka mara mbili kwenye ubalozi wa Uswidi mjini Baghdad, huku balozi wa Uswidi akifukuzwa mjini humo kufuatia mzozo wa kidiplomasia.
Serikali ya Uswidi ilimpa ruhusa Bwana Momika kufanya maandamano hayo ambapo alichoma kitabu kitakatifu cha Quran, akilieleze tukio hilo kuwa la sheria ya uhuru wa kujieleza.
Hata hivyo, baadaye iliahidi kuchunguza njia za kisheria za kuzuia maandamano yanayohusisha kuchoma maandiko katika hali fulani.
Pia unaweza kusoma:
Habari za hivi punde, Miili 30 imepatikana baada ya ndege na helikopta kuanguka kwenye mto Washington DC
Wahudumu wa dharura wameopoa takriban miili 30 katika eneo la ajali, mshirika wa BBC wa Marekani CBS anaripoti.
Wachezaji wa kuteleza kwenye barafu wa Marekani na Urusi walikuwa miongoni mwa abiria waliokuwa kwenye ndege hiyo.
Wanariadha "kadhaa", makocha na wanafamilia wanaohusika na Mchezo wa Skating wa Marekani walikuwa kwenye ndege, bodi inayosimamia mchezo huo ya Marekani ilisema katika taarifa.
Raia wa Urusi pia walikuwa ndani ya ndege hiyo, Kremlin ilithibitisha - baada ya vyombo vya habari vya ndani kuripoti kwamba makocha wa mchezo wa kuteleza kwenye barafu na mabingwa wa zamani wa dunia Yevgenia Shishkova na Vadim Naumov walikuwa kwenye ndege.
Inna Volyanskaya, mwanariadha wa zamani wa mchezo wa kuteleza kwenye barafu katika Umoja wa Kisovieti, pia alikuwa ndani ya ndege hiyo, kulingana na shirika la habari la serikali ya Urusi Tass.
Hatujui majina ya wanariadha wa Marekani waliokuwa kwenye ndege.
Takriban watu 15 kwenye ndege hiyo huenda ni wachezaji wa mchezo kuteleza kwenye theluji, chanzo ambacho hakikutajwa jina kiliambia shirika la habari la Reuters.
Mzozo wa DRC: Mamia ya wakimbizi waliokimbia Rubavu nchini Rwanda wanarejea Goma

Maelezo ya picha, Wakimbizi wa Congo wanajiandaa kurejea Goma Alhamisi hii kutoka kambi ya Rugerero viungani mwa mji wa Rubavu Mamia ya wakimbizi waliokimbia mji wa Goma kukimbia mapigano mapema wiki hii sasa wanarejea nyumbani, anaripoti mwandishi wa BBC Idhaa ya Kinyarwanda, Jean Claude Mwambutsa.
Wengi wa wakimbizi hao ni wale waliowekwa katika kambi ya muda ya Rugerero iliyoko viungani mwa mji wa Rubavu kaskazini-magharibi mwa Rwanda.
Wakimbizi hawa ni wa wale ambao hawakuwa na uwezo wa kukodisha nyumba katika jiji la Rubavu au kukaribisha na familia kibinafsi.
Mamlaka inasema zaidi ya 600 wamerejea nyumbani kufikia Jumatano.
Mamlaka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi linasema kuwa zaidi ya watu 500,000 wameyakimbia makazi yao mwezi huu wa Januari 2025 kutokana na mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katika kambi ya muda ya Rugerero ambako nilifika leo asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi tayari kulikuwa na watu wapatao 200 ambao walitaka kurejea nyumbani.
Tzabayo Musagara, mmoja wa wakimbizi hao aliniambia: "Niliamua kuondoka kwa sababu nilisikia kwamba amani imeanza kurejea... sina hofu ya kurudi nyumbani, hakuna tatizo."
Unaweza pia kusoma:
Kenya: Wanawake 9 hufariki kila siku kutokana na ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi

Chanzo cha picha, Science Photo Library
Kenya inapoteza wanawake 9 kila siku kutokana na ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi.
Hii ni kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa na Dkt Anne Musuva Njoroge mkurugenzi wa Kanda ya Thinkwell, Afrika Mashariki na Kusini ambazo zinaonyesha kuwa zaidi ya wanawake 3,000 hufariki kila mwaka kutokana na ugonjwa huo ambao sasa unaorodheshwa wa pili kuuwa binadamu.
Vile vile kuna visa vipya vya saratani ya shingo ya kizazi takriban 5,226 vinavyoripotiwa kila mwaka nchini kenya.
Kulingana na katibu kuu wa wizara ya afya nchini kenya Mary Muthoni amedokeza kuwa kuna mpango wa kutoa chanjo kwa wasichana walio na umri wa miaka 14 dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kama njia moja ya kukabiliana na janga hilo.
Nchi zote isipokuwa moja kati ya 20 zilizo na viwango vya juu vya saratani ya shingo ya kizazi mnamo 2018 zilikuwa barani Afrika, kulingana na Shirika la Afya Duniani.
Hii inatokana na kukosekana kwa chanjo ya kuzuia virusi vya papillomavirus ya binadamu (HPV), uchunguzi na matibabu ya kutosha, ikimaanisha kuwa wanawake wengi hutibiwa wakiwa wamechelewa.
Haya yanajiri huku ulimwengu ukiendelea kuadhimisha mwezi wa kuhamasisha kuhusu saratani ya shingo ya kizazi .
Pia unaweza kusoma:
Kenya: Gavana wa zamani ahusishwa na kesi ya mauaji ya mwanafunzi

Chanzo cha picha, SHARON OTIENO/FACEBOOK
Mahakama ya juu imempata aliyekuwa gavana wa Migori,Kenya Okoth Obado na watuhumiwa wenzake wawili wana kesi ya kujibu kufuatia mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo Sharon Otieno.
Jaji Cecilia Githua alisema ushahidi ulioletwa na upande wa mashtaka umeonesha kuwa kesi ya msingi imejengwa na kuhalalisha kuwekwa kwa watatu kujibu kesi hiyo.
Jaji alikubaliana na hoja zilizowasilishwa na utetezi kwa msingi wa kanuni ya mtoto aliyezaliwa hai, ambayo inasema kuwa ili mtoto kuwa muathirika au mtu yeyote ashtakiwe kwa mauaji, mtoto huyo lazima azaliwe hai.
Mauaji hayo yaliyotekelezwa mwezi Septemba mwaka 2018 yamekuwa yakipelelezwa na kesi kufikishwa mahakamani tangu wakati huo.
Inadaiwa Sharon aliuawa akiwa na mtoto tumboni akiwa na umri wa wiki 28.
Mwezi Novemba mwaka jana, upande wa utetezi ulidai kuwa uchunguzi ulishindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha wa kumhusisha Obado kwa uhalifu huo.
Walisisitiza kuwa mashahidi 42 waliofika mahakamani hawakuweza kumhusisha Obado moja kwa moja katika eneo la mkasa bali walidokeza Obado alikuwa tayari kumgharamia Sharon na mtoto wake.
Hata hivyo upande wa mashataka ulisema kuwa kuna msururu wa kujirudia unaomhusisha mshtakiwa katika utekaji nyara na kisha kuuawa kwa Sharon.
Pia unaweza kusoma:
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aapa vita 'vikali' vya kuwakomesha waasi wa M23

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, M23 wamekuwa wakisonga mbele hadi maeneo mengine baada ya mashambulizi yao huko Goma Rais wa Kongo Félix Tshisekedi ameapa kurejesha mamlaka ya serikali mashariki mwa nchi, ambako waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameuteka mji wa Goma na wanaripotiwa kuelekea kusini kuchukua maeneo zaidi.
Katika hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni, alisema "majibu makali yaliyoratibiwa" dhidi ya kile alichokiita "magaidi" unaendelea.
Aliikosoa jamii ya kimataifa kwa "kutochukua hatua" na kwa kutofanya juhudi za kutosha kufuatia mzozo wa usalama unaozidi kuongezeka.
Mashambulizi ya wiki moja ya waasi yameongeza tahadhari ya mzozo wa kibinadamu unaokuja na kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa kukomesha mapigano.
Wakati wa hotuba yake siku ya Jumatano usiku, Tshisekedi aliwahimiza Wacongo wote kuungana pamoja na kuunga mkono mapambano ya jeshi kutwaa tena udhibiti.
" Kuweni na uhakika wa jambo moja: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo haitajiruhusu kufedheheshwa . Tutapigana na tutashinda," alisema.
Mapigano hayo yamewalazimu takriban watu 500,000 kutoka makwao, na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu tayari, kulingana na UN.
Tangu mapigano yaanze, jiji hilo limekatiwa umeme na maji na kukabiliwa na uhaba wa chakula.
Unaweza pia kusoma:
Ndege imevunjika vipande vipande huku helikopta ikisalia kuwa imara

Chanzo cha picha, Getty Images
Ndege hiyo iliyoanguka mtoni imevunjika vipande vipande na sasa iko futi 5-8 (152-243cm) ndani ya maji, kulingana na ripoti za mshirika wa BBC wa Marekani CBS.
Timu ya wapiga mbizi sasa pia imepata kile kinachoonekana kuwa moja ya masanduku mawili meusi.
Wapiga mbizi wameweza kufikia kabati na eneo la kuwekea mizigo.
Ripoti inaeleza kuwa helikopta iko juu chini lakini inaonekana kuwa haikuvunjika.
Wachunguzi wanatarajiwa kuchunguza uzoefu wa majaribio katika anga ya Washington DC kwani helikopta zinapaswa kukaa chini ya 200ft (mita 60.9) wakati wa kuruka karibu na njia ya DC.
Wachunguzi wanatarajiwa kuchunguza uzoefu wa rubani katika anga ya Washington DC kwani helikopta zinapaswa kukaa chini ya 200ft (mita 60.9) wakati wa kuruka karibu na njia ya DC.
Soma zaidi:
Wanamgambo wa Hamas na Islamic Jihad walivyokusanyika huko Khan Younis

Chanzo cha picha, Reuters
Picha za hivi punde kutoka Khan Younis kusini mwa Gaza.
Wanamgambo wa Hamas na Islamic Jihad walivyokusanyika huko Khan Younis kabla ya kuachiliwa kwa mateka, kulingana na Reuters.

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Umati pia ulikusanyika katika eneo la tukio Soma zaidi:
Habari za hivi punde, Mateka mmoja akabidhiwa Shirika la Msalaba Mwekundu - maafisa wa Israeli

Chanzo cha picha, Reuters
Maafisa wa Israel wanasema wamepokea uthibitisho kutoka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu kwamba mateka mmoja ameachiliwa huru.
"Wako njiani kuelekea katika vikosi vya IDF na ISA katika Ukanda wa Gaza," taarifa ya pamoja kutoka kwa Jeshi la Ulinzi la Israeli na Shirika la Usalama la Israeli ilisema.
Kabla ya Agam Berger, 20, kabla ya kukabidhiwa Chama cha Msalaba Mwekundu, alipandishwa jukwaani na wanamgambo wenye silaha.

Chanzo cha picha, Reuters

Chanzo cha picha, Reuters
Pia unaweza kusoma:
Urusi yaondoa vifaa vya kijeshi kutoka bandari ya Syria, picha zinaonyesha

Chanzo cha picha, PA Media
Urusi imeongeza kasi ya uondoaji wanajeshi wake kutoka Syria, na kuondoa magari na makontena kutoka bandari yake muhimu ya Tartous kwenye pwani ya Mediterania nchini humo, uchambuzi na BBC Verify unapendekeza.
Baada ya kuanguka kwa utawala wa Assad mwezi Desemba, picha zilizothibitishwa zilionyesha safu za magari ya Urusi yakielekea kaskazini upande wa bandarini.
Picha za setilaiti baadaye zilionyesha vifaa vya kijeshi vikihifadhiwa hapo.
Lakini picha mpya zilizochapishwa Jumatano na Planet Labs zilionyesha kuwa vitu vingi sasa havipo, baada ya kuondoka kwa meli zilizohusishwa na jeshi la Urusi.
Hatua hii inawadia wakati maafisa wa Urusi wakifanya "majadiliano ya wazi" na serikali mpya huko Damascus, Reuters iliripoti Jumatano.
Kumekuwa na ripoti kwamba serikali mpya ya Syria imefuta ukodishaji wa Urusi katika bandari hiyo - lakini idara za serikali zilizowasiliana na BBC hazingethibitisha uamuzi wa mwisho uliofanywa.
Tartous imekuwa msingi muhimu kwa Urusi katika miaka ya hivi karibuni, ikiiruhusu kujaza mafuta, kusambaza na kutengeneza meli katika Bahari ya Mediterania.
Lakini meli za kivita zilizokuwa zimetia nanga kwenye bandari hiyo hazijaonekana kwenye picha za satelaiti tangu kuanguka kwa utawala wa Assad - ambao Moscow iliuunga mkono wakati wote wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria.
Ikulu ya Urusi imeashiria nia yake ya kutaka kudhibiti kambi hiyo, na ilisema mnamo mwezi Desemba kwamba ilikuwa ikizungumza na mamlaka mpya kuhusu kudumisha uwepo wake huko.
Soma zaidi:
Trump anasema Marekani itatuma wahamiaji wengine kwenda Guantanamo Bay

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump ameamuru kujengwa kwa kituo cha kizuizi cha wahamiaji katika gereza la Guantanamo Bay ambacho alisema kingehifadhi watu kama 30,000.
Alisema kituo hicho katika kituo cha Jeshi la Wanamaji la Marekani nchini Cuba, ambacho kitakuwa tofauti na jela yake ya kijeshi yenye ulinzi mkali, kitahifadhi "wahamiaji haramu wabaya zaidi wanaotishia watu wa Marekani".
Guantanamo Bay kwa muda mrefu imekuwa ikitumika kuwahifadhi wahamiaji, tabia ambayo imekuwa ikishutumiwa na baadhi ya mashirika ya kutetea haki za KIbinadamu.
Baadaye Jumatano, "mshauri wa masuala ya mpaka" wa Trump Tom Homan alisema kituo kilichopo kitapanuliwa na kuendeshwa na Idara ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha (ICE).
Alisema wahamiaji hao wanaweza kusafirishwa kwenda huko moja kwa moja baada ya kukamatwa baharini na Walinzi wa Pwani ya Marekani, na kwamba viwango vya "juu zaidi" vya kizuizini vitatumika.
Haijulikani ni kiasi gani kituo hicho kitagharimu au kingekamilika lini.
Serikali ya Cuba ililaani haraka mpango huo, ikishutumu Marekani kwa mateso na kuzuia watu kinyume cha sheria kwenye ardhi "inayokalia".
Tangazo la Trump linawadia wakati akitia saini kile kinachoitwa mswada wa Laken Riley kuwa sheria, ambayo inawataka wahamiaji wasio na vibali ambao wanakamatwa kwa wizi au uhalifu wa kutumia mabavu kuzuiliwa gerezani wakisubiri kufikishwa mahakamani.
Soma zaidi:
Miili yapatikana mtoni; Helikopta ya kijeshi ilikuwa kwenye mafunzo - CBS
Maafisa wa polisi wameiambia mshirika wa BBC wa Marekani CBS News kwamba miili 19 imepatikana na watoa huduma za dharura katika eneo la ajali, na kwamba hakuna manusura waliopatikana kufikia sasa.
Bado hakujawa na taarifa rasmi kutoka kwa mamlaka kuhusu idadi ya majeruhi, lakini tunatarajia mkutano wa habari hivi karibuni.
Helikopta ya kijeshi ilikuwa kwenye mafunzo - CBS
Mkuu wa vyombo vya habari wa Kikosi Kazi cha Pamoja, ambao ni sehemu ya Jeshi la Marekani, ameiambia CBS News, mshirika wa BBC wa Marekani, kwamba helikopta ya kijeshi ya Black Hawk iliyohusika katika ajali hiyo ilikuwa kwenye mafunzo.
Soma zaidi:
Abiria 60 na wafanyakazi 4 walikuwa kwenye ndege iliyogongana na helikopta - CBS

Chanzo cha picha, EPA
Abiria 60 na wafanyakazi wanne walikuwa kwenye ndege ya Amerika ya Airlines ambayo imegongana kwa helikopta karibu na Uwanja wa Ndege wa Kitaifa wa Reagan wa Washington, imesema CBS, mshirika wa BBC wa Marekani.
Ndege hiyo ilikuwa ikitumiwa kwa safari za kibiashara na American Airlines na ilikuwa ikielekea Washington kutoka Kansas.
Afisa wa Jeshi la Marekani amethibitisha kwa mshirika wa BBC wa Marekani, CBS kwamba ndege ya kijeshi Black Hawk imehusika katika ajali hiyo.
Soma zaidi:
Habari za hivi punde, Ndege ya American Airlines yagongana na helikopta huko Washington DC

Chanzo cha picha, Getty Images
Ndege ya shirika la ndege la American Airlines imegongana angani na helikopta huko Washington DC, Shirika la Usimamizi wa Safari za Ndege limesema.
Ajali hiyo ilitokea wakati inakaribia kwenye Barabara ya Uwanja wa Ndege wa Kitaifa wa Reagan Washington karibu saa tatu usiku kwa saa za eneo.
Mamlaka husika inachunguza chanzo cha ajali.
Ndege hiyo ilianguka katika Mto Potomac, kulingana na Idara ya zimamoto.
Idara hiyo ilisema katika ujumbe kwenye mtandao wa X kwamba boti za kuzima moto zilikuwa zimefika mtoni.
Uwanja wa Ndege wa Kitaifa wa Ronald Reagan (DCA) umesimamisha safari zote za ndege huku huduma za dharura zikishughulikia ajali hiyo.
"Safari zote za kupaa na kutua zimesitishwa katika uwanja wa ndege wa DCA," uwanja wa ndege ulisema kwenye mtandao wa X.
"Wahudumu wa dharura wako katika eneo la tukio."
Soma zaidi:
Rwanda na Afrika Kusini zipo katika mgogoro wa kidiplomasia juu ya mzozo wa DRC

Chanzo cha picha, Paul Kagame/ IG
Wasiwasi kati ya Rwanda na Afrika Kusini umeongezeka sana. Hii ni baada ya Rais wa Rwanda Paul Kagame kutoa onyo kali kwa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, akisema kwamba Rwanda imejiandaa kwa makabiliano iwapo kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.
Taarifa ya Bw Kagame ilikuwa inajibu maoni ya Bw Ramaphosa juu ya jukumu la Kikosi cha Ulinzi cha Rwanda na Kikundi cha Waasi cha M23 katika mapigano yanayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Jibu la Rais Paul Kagame kwa Cyril Ramaphosa liliashiria mzozo mbaya wa kidiplomasia kati ya Afrika Kusini na Rwanda.
Katika taarifa iliyo na maneno makali akimjibu moja kwa moja Cyril Ramaphosa kwenye mtandao wa kijamii wa X, Bwana Kagame alimshtumu Rais wa Afrika Kusini kwa kupotosha mazungumzo ya faragha juu ya hali tete mashariki mwa DRC.
Kiongozi huyo wa Rwanda pia alisema Bwana Ramaphosa alikuwa hajaonya Rwanda juu ya shughuli zake za kijeshi DRC lakini badala yake alikuwa ameomba msaada wa vifaa, pamoja na umeme, chakula, na maji kwa wanajeshi wa Afrika Kusini.
Wakati akikaribisha juhudi za Afrika Kusini za amani, Bwana Kagame alisisitiza kwamba nchi hiyo haikuwa katika nafasi ya kuwa mtafutaji amani wala mpatanishi na alionya zaidi kwamba ikiwa Afrika Kusini inataka makabiliano, Rwanda ingejibu ipasavyo.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja. Ikiwa ni tarehe 30/1/2025. Nahodha wako ni mimi Asha Juma
