Ni nchi gani Afrika bado zina kambi za kijeshi za Ufaransa na kwanini?

fgdvcx

Chanzo cha picha, Getty Image

Wimbi la maandamano dhidi ya uwepo wa jeshi la Ufaransa limekuwa likienea barani Afrika. Maandamano haya ni matokeo ya mvutano wa kisiasa na usalama, lakini bado kuna nchi nyingi zina kambi za kijeshi za Ufaransa katika bara hilo.

Kama sehemu ya ushirikiano wa kijeshi na baadhi ya nchi ilizozikoloni na ambazo sasa ni huru, Ufaransa imeweza kuwa na kambi kadhaa za kijeshi barani Afrika.

Niger, nchi ya hivi karibuni kukabiliwa na mapinduzi ya kijeshi, iko katika mazungumzo ya kuwaondoa wanajeshi wa Ufaransa katika ardhi yake. Wanajeshi ambao wako kwa ajili ya kupambana na makundi ya kigaidi.

Asili ya kambi za kijeshi za Ufaransa Afrika

fdc

Chanzo cha picha, Getty Image

Maelezo ya picha, Kikosi cha Ufaransa huko Timbuktu, Mali - Januari 28, 2013

Tony Chafer, Profesa wa masuala ya Afrika na Ufaransa katika Kituo cha Utafiti cha Mafunzo ya Ulaya na Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Portsmouth nchini Uingereza, anatupa historia fupi ya uwepo wa jeshi la Ufaransa barani Afrika.

"Ufaransa ilitia saini mikataba ya ushirikiano wa kitamaduni, kiufundi na kijeshi na mikataba ya ulinzi na makoloni yake mengi ya zamani wakati wa uhuru miaka ya 1960."

"Washauri wa kijeshi walitumwa Afrika kufanya kazi na serikali mpya zilizokuwa huru. Mikataba ya ulinzi ilifafanua namna ambavyo uingiliaji kati wa kijeshi wa Ufaransa utafanyika wakati wa kipindi cha baada ya ukoloni."

"Mikataba hiyo iliyojumuisha ulinzi na msaada wa kijeshi. Hadi askari 10,000 waliwekwa au kushiriki katika operesheni katika miaka ya kwanza baada ya uhuru. Ufaransa imefanya takribani uingiliaji kati wa moja kwa moja wa kijeshi mara 30 barani Afrika kati ya 1964 na 1995," anaeleza Profesa Chafer.

Kambi za Ufaransa ziko nchi gani?

xz

Chanzo cha picha, Getty Image

Maelezo ya picha, Kikosi cha anga chaUfaransa huko Niamey, Mei 14, 2023.

Ikiwa na karibu wanajeshi 10,000 waliopo Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Ufaransa ina kambi za kijeshi nchini Djibouti, Ivory Coast, Senegal, Gabon, Chad na Niger.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Djibouti:

Vikosi vya Ufaransa vilivyoko Djibouti vimekuwepo uko tangu uhuru wa nchi hiyo - wakiwa na takribani wanajeshi 1,500. Wanawakilisha kikosi kikubwa zaidi cha wanajeshi wa Ufaransa barani Afrika.

Chini ya makubaliano ya Juni 1977, makubaliano mapya ya ulinzi, ambayo yalianza kutumika mwaka 2014, yanaweka masharti ya Ufaransa kusalia nchini Djibouti.

Ivory Coast:

Mwaka 2012, ukaribu wa kihistoria kati ya Ufaransa na Ivory Coast ulitia muhuri makubaliano ya ushirikiano wa ulinzi kati ya nchi hizo mbili. Januari 1, 2015, kikosi cha Ufaransa nchini Côte d'Ivoire kiliundwa ili kutekeleza operesheni barani Afrika.

Gabon:

Ufaransa ilituma vikosi vyake tangu uhuru 1960, kwa mujibu wa makubaliano ya ulinzi ya Agosti mwaka huo huo. Kulingana na tovuti ya Wizara ya Ulinzi ya Ufaransa, vikosi vya Ufaransa nchini Gabon ni pamoja na:

Kamandi kuu, kikosi cha ardhini, kikosi cha wanamaji kilicho katika kambi ya Charles De Gaulle huko Libreville na kikosi cha anga kilichopo katika kambi ya Guy Pidoux.

Senegal:

Kukiwa na takriban wanajeshi 400 - tangu 2011, wanatoa mafunzo kwa wanajeshi kutoka nchi za kikanda. Wanajeshi wa Ufaransa wako katika kambi ya Kanali Frédéric Geille huko Ouakam na kwenye kambi ya Rear Admiral Protet kwenye bandari ya kijeshi ya Dakar.

Wanajeshi wa Ufaransa nchini Senegal wana kituo cha anga katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Léopold Sédar Senghor, Dakar.

Chad:

Kikosi cha Ufaransa nchini Chad (EFT), kina karibu wanajeshi elfu moja. Misheni yao ni kulinda maslahi ya Ufaransa na raia wake wanaoishi nchini humo. Pia wanatoa msaada wa vifaa na usaidizi wa kijasusi kwa wanajeshi wa Chad, kwa mujibu wa makubaliano yaliyotiwa saini kati ya nchi hizo mbili.

Mwaka 2013, Ufaransa ilikuwa na wanajeshi 950 katika kambi mbili. Kambi ya anga huko Ndjamena na kambi ya Kapteni Croci huko Abéché, mashariki mwa Chad. Huko Faya, kaskazini mwa nchi, kuna kikosi cha zaidi ya wanajeshi 500.

Niger:

Wanajeshi kati ya 1,300 na 1,500 walitumwa nchini Niger, pamoja na ndege za kivita na ndege zisizo na rubani. Wanajeshi hawa wamepewa kambi tatu huko Niamey, Ouallam na Ayorou, kuelekea mpaka na Mali.

Niamey Air Base 101 ni kituo kisicho cha kudumu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamani Diori. Kinatumika kama uwanja wa kuondokea wa ndege zisizo na rubani za Reaper ambazo hufanya kazi za kijasusi na upelelezi katika Operesheni ya Barkhane huko Sahel.

Kufuatia mapinduzi yaliyomuingiza Jenerali Tchiani madarakani, Niger ilifanya mazungumzo ya kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa kutoka katika eneo lake.

Lengo la sasa la Ufaransa

.

Chanzo cha picha, Getty Image

Maelezo ya picha, Vikosi vya Ufaransa na Senegal wakifanya mazoezi Dakar, Novemba 18, 2019.

"Ni kweli kwamba mwanzoni mwa uhuru, uwepo wa jeshi la Ufaransa barani Afrika ilikuwa ni kulinda usalama na uimara wa tawala fulani," anasema Dkt. Bakary Sambe, mkurugenzi wa Taasisi ya Timbuktu.

Lakini leo nchini Gabon, "dhamira kuu ya kikosi cha Ufaransa ni kukamilisha mafunzo ya askari kutoka nchi washirika wa ECCAS (Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati), kabla ya kushiriki katika operesheni za ndani au nje," , tovuti ya Wizara ya Ulinzi ya Ufaransa.

Zaidi ya maslahi ya kisiasa na kimkakati, Ufaransa pia inathamini masilahi yake ya kiuchumi. Profesa Chafer anasema, "Ufaransa ina maslahi makubwa ya kiuchumi Afrika Magharibi na Afrika ya Kati; mafuta (Gabon, Jamhuri ya Kongo, Ghuba ya Guinea), uranium (Niger), biashara ya kakao na kahawa (Ivory Coast), pamoja na benki, usafiri na huduma nyingine."

"Nafasi ya Ufaransa barani Afrika inazidi kukabiliwa na changamoto na mataifa yanayoibukia kama vile Jamhuri ya Watu wa China, India, nchi za Mashariki ya Kati na Brazili."

"Katika mazingira ya ushindani wa kimataifa, Ufaransa ina nia yakudumisha uwepo wake wa kijeshi Afrika. Uwepo huu unachukuliwa kuwa njia bora zaidi ya kudumisha nafasi yake kama mhusika mkuu katika bara,” anaeleza Tony Chafer.

Afrika itaweza kusimamia usalama wake?

asd

Chanzo cha picha, Getty Image

Maelezo ya picha, Waandamanaji wakiunga mkono mapinduzi ya Niger

"Majeshi ya Ufaransa. Ondokeni..." Alpha Blondy, mwimbaji wa reggae wa Ivory Coast, alifungua maandamano ya kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa kutoka Afrika katika miaka ya 90.

Katika albamu yake Yitzhak Rabin iliyotolewa mwaka 1998, msanii huyo aliliomba jeshi la Ufaransa kuondoka. Wimbo huu uliashiria mwanzo wa enzi mpya ya uhuru.

"Kwa bahati mbaya, tuligundua kuwa lengo kuu lilikuwa ni kufanya vikundi vya kigaidi kutoweka, lakini vikundi vimeongezeka. Kwa hivyo, kuna kutofaulu kwa njia hii," anasema mwalimu-mtafiti katika Kituo cha Utafiti wa Dini (CER) katika Chuo Kikuu cha Berger cha Saint-Louis nchini Senegal.

"Sio tu wanajeshi wa Ufaransa wanaoondoka katika nchi za Sahel, bali pia MINUSMA wanaoondoka Mali. Serikali ya Mali imetoa wito kwa kundi la Wagner la Urusi kusaidia kukabiliana na mzozo wa usalama unaoongezeka nchini humo," anasema Tony Chafer. .

"Hata hivyo, kukosekana kwa wanajeshi wa Ufaransa na wa Umoja wa Mataifa nchini humo, hakuna tena udhibiti wowote juu ya kile wanachofanya wanajeshi wa Mali na washirika wao - kundi la Wagner."

"Inazidi kuwa wazi kuwa usalama wa watu umezidi kuzorota na ukiukwaji wa haki za binadamu umeongezeka tangu kuondoka kwa Barkhane na kupunguzwa kwa vikosi vya Umoja wa Mataifa," anasema Chafer.

Kulingana na yeye, "Jukumu kuu la Wagner nchini humo sio kuboresha usalama wa watu bali ni kuunga mkono utawala wa kijeshi wa Mali - kwa maneno mengine, wapo zaidi kuimarisha usalama wa serikali, na sio kuboresha usalama wa watu."

Katika hali hii mpya ya kuchanganyikiwa na ya wasiwasi, Afrika inahitaji kufikiria upya mustakabali wake. Ndivyo anavyofikiria Dkt. Bakary Sambe.

Anaamini kwamba ni wakati wa kuunganisha ujuzi na rasilimali katika ngazi ya kikanda. Pia, ni wakati wa ushirikiano wa kikanda - kutoka ECOWAS na Umoja wa Afrika kuwa na mifumo ya vikosi vya kudumu.