Je, kuondolewa kwa wanajeshi wa Ufaransa kunamaanisha nini kwa Niger?
Na Yusuf Akinpelu
BBC News, Lagos

Chanzo cha picha, bbc
Ufaransa imekubali kuwaondoa wanajeshi wake 1,500 kutoka Niger baada ya miezi kadhaa ya mzozo wa kidiplomasia kati ya Paris na utawala wa kijeshi ulionyakua madaraka mwezi Julai.
Rais Emmanuel Macron alisema uamuzi huo umechukuliwa kwa sababu serikali ya Niger "haina tena nia ya kupambana na ugaidi" huku ikiendelea kumshikilia mateka Rais Mohamed Bazoum, ambaye Ufaransa inamtambua kama "rais pekee halali."
Kumekuwa na chuki kali dhidi ya Ufaransa tangu Bazoum aondolewe madarakani. Waandamanaji wameizingira kambi ya jeshi la Ufaransa na ubalozi wake katika mji mkuu wa Niamey nchini Niger.
Macron amekabiliwa na shinikizo nyumbani pia. Bunge la Ufaransa limejadili iwapo Ufaransa inahitaji kuangalia upya shughuli zake katika eneo la Sahel.
Tangu 2020, Niger ni koloni la tatu la zamani la Ufaransa katika Sahel kukumbwa na mapinduzi ya kijeshi na kuwataka wanajeshi wa Ufaransa kuondoka. Makoloni mengine mawili ni nchi jirani - Mali na Burkina Faso.
Nchini Niger, madai kwamba Rais Mohamed Bazoum alikuwa kibaraka wa maslahi ya Ufaransa yalitumiwa kuhalalisha kuondolewa kwake madarakani. Mikataba mitano ya kijeshi na Ufaransa imebatilishwa na jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdourahmane Tchiani.
"Nguvu ya utawala wa kijeshi kuikataa Ufaransa imefanya kuwa ngumu kwa wanajeshi wa Ufaransa kubaki Niger," anasema mtaalamu wa eneo la Sahel, Bram Posthumus.
Watu wengi nchini Niger wamekasirishwa na msimamo mkali wa Ufaransa dhidi ya mapinduzi ya kijeshi.
Wanasema msimamo huo unakinzana na msimamo wa Ufaransa dhidi ya mapinduzi ya Gabon na mapinduzi ya Chad ya 2021, koloni jingine la zamani la Ufaransa.
"Kukosekana kwa msimamo kumechochea chuki dhidi ya Ufaransa kote Niger," anasema mhubiri wa Kiislamu katika mji mkuu wa Niamey, Abdoulaziz Abdoulaye Amadou.
"Kwa nini Emmanuel Macron anasema hatambui mamlaka yetu? Wakati anatambua mamlaka za kijeshi katika nchi zingine kama Gabon na Chad. Hilo ndilo limetukasirisha, na tunadhani Ufaransa inatuchukulia kama wajinga,” anasema.

Chanzo cha picha, rtgfvc
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Vikosi vya Ufaransa viko nchini Niger kuongoza mapambano ya kimataifa dhidi ya waasi wa Kiislamu katika eneo la Sahel.
Licha ya ufadhili mkubwa na idadi kubwa ya wanajeshi, vikosi hivyo vinavyoongozwa na Ufaransa vimeshindwa, maeneo mengi yamesalia chini ya udhibiti wa wapiganaji wenye msimamo mkali.
"Uingiliaji wa kijeshi wa Ufaransa haujafanikiwa kupunguza mashambulizi ya wanajihadi, ila huenda umeleta utulivu katika eneo hilo," anasema Bram Posthumus.
Mwaka jana, vifo vilivyotokana na ugaidi nchini Niger vilipungua kwa asilimia 79. Ingawa haijulikani ni kwa kiasi gani uwepo wa jeshi la Ufaransa ulisaidia, waangalizi wanahofia kukosekana kwa utulivu wa kisiasa kunaweza kurudisha nyuma maendeleo haya.
Nchini Mali na Burkina Faso, tawala za kijeshi zimechukuwa madaraka na zinakabiliwa na mashambulizi na vurugu za makundi yenye silaha. Waangalizi wanahofia hali kama hiyo inaweza kutokea nchini Niger.
Niger tayari imeshuhudia ongezeko la mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi na raia kote nchini katika wiki kadhaa baada ya mapinduzi hayo, hasa katika eneo la Tillabéri ambalo liko karibu na mpaka na Burkina Faso.
"Kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa kunazua ombwe ambalo waasi na makundi mengine yenye silaha yasiyo ya serikali yana shauku ya kuliziba," anasema Posthumus.
"Ulichokiona nchini Mali ndicho utakachokiona nchini Niger kwa sababu majeshi hayana uwezo wa kulinda nchi zote hizi kubwa," anasema.
Kutoweza kutetea maeneo haya kuna uwezekano wa kuathiri shughuli za uchimbaji madini, hasa katika maeneo ya pembezoni.
Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, ni Kazakhstan pekee (27%) iliyoingiza uranium zaidi nchini Ufaransa kuliko Niger (20%). Madini hayo huwezesha nishati ya nyuklia ambayo hutumiwa kuzalisha 70% ya gridi ya umeme ya Ufaransa.

Kampuni ya mafuta ya nyuklia ya Ufaransa ya Orano, ambayo zamani ilijulikana kama Areva, inaendesha mgodi katika mji wa Airlit kaskazini magharibi mwa Niger, inasema shughuli zake zitaendelea, licha ya hali ya Niger.
"Serikali ya kijeshi inaweza kujadili upya mikataba kuhusu uchimbaji madini ya uranium," anasema Posthumus, akiongeza kuwa wanufaika wa makubaliano mapya wanaweza kuwa ni watu wenye nyadhifa za juu kisiasa badala ya raia wa kawaida.
Utajiri mkubwa katika mafuta na urani haujaleta manufaa kwa watu milioni 25 wa Niger. Zaidi ya 40% wanaishi katika umaskini na nchi iko katika nafasi ya 189 kwa umasikini kati ya nchi 191 kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa - 2022.
Wakati huo huo, tofauti na Mali na Burkina Faso ambako wanajeshi wote wa kigeni walitakiwa kuondoka, Niger haijataka kikosi cha zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Marekani kuondoka.
Hii inafanya uwezekano wa serikali ya Niger kuanzisha ushirikiano wa haraka na Urusi kuwa mdogo, ingawa imetia saini mikataba ya kijeshi na washirika wa Urusi huko Mali na Burkina Faso.
Wachambuzi wanasema kupunguza ushawishi wa Ufaransa nchini Niger, hakuwezi kuwa ni msaada wa moja kwa moja kwa utulivu wa kisiasa.
Katika miongo kadhaa ijayo, viongozi wapya wa kijeshi wanaweza kutaja hitaji la kuondoa ushawishi Urusi katika nchi zao ili kuhalalisha unyakuzi wao.












