Waasi wakaribia kuudhibiti kikamilifu mji muhimu wa Goma DRC

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Damian Zane
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Waasi wanaonekana kukaribia kuudhibiti mji muhimu wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia ripoti kwamba wameuteka uwanja wake wa ndege.
Serikali ya Congo imesisitiza kuwa bado ina udhibiti huku mapigano katika baadhi ya maeneo ya mji huo yakiendelea. Maghala yenye chakula na vifaa vya matibabu yameporwa, mashirika ya misaada yanasema.
Mapigano kati ya waasi wa M23 na jeshi na washirika wake yamesababisha hospitali kuzidiwa na majeruhi na miili iliyolala mitaani, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Kuongezeka kwa hasira kuhusu mashambulizi ya waasi kulisababisha waandamanaji kulenga balozi za kigeni katika mji mkuu, Kinshasa. Wito wa mazungumzo ya amani kukomesha mapigano unazidi kuongezeka.
Nchi jirani ya Rwanda imeshutumiwa kwa kuunga mkono kundi la M23 linaloongozwa na Watutsi huku likipiga hatua haraka katika miezi ya hivi karibuni katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Rwanda imekuwa ikikanusha hili mara kwa mara.
Mji wa Goma ulio kando ya ziwa, kwenye mpaka na Rwanda, ni kitovu muhimu cha usafiri na biashara karibu na vyanzo vikubwa vya madini ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa simu za mkononi miongoni mwa mambo mengine.
Kufuatia mkutano wa Jumanne, Umoja wa Afrika (AU) ulitoa wito kwa M23 kuweka chini silaha zake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kamishna wa amani na usalama wa AU, Bankole Adeoye, alilaani "vurugu za M23 na vikosi vingine vyote hasi, na anatoa wito wa kuheshimiwa kikamilifu uhuru wa DR Congo, umoja na uadilifu wa eneo", taarifa kutoka kwa AU kwenye X ilisema.
Wanadiplomasia walipokuwa wakijadili hali hiyo, waasi hao walionekana kupata nguvu huko Goma.
"Wamechukua udhibiti wa uwanja wa ndege, wapiganaji wa M23 wapo," chanzo cha usalama kiliambia shirika la habari la AFP.
"Zaidi ya wanajeshi 1,200 wa Congo wamejisalimisha na wamezuiliwa katika [kambi ya Umoja wa Mataifa] kwenye uwanja wa ndege."
Mapema Jumanne, Adelheid Marschang, mratibu wa dharura wa Shirika la Afya Ulimwenguni kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alisema kuwepo kwa "mamia ya watu hospitalini, wengi wamelazwa wakiwa na majeraha ya risasi".
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imesema hospitali yake mjini Goma imepokea zaidi ya majeruhi 100 katika muda wa saa 24 pekee, idadi ambayo ilipokea awali kwa muda wa mwezi mmoja.
Ilisema kuwa hali hii iliwalazimu wafanyakazi wake kugeuza maegesho ya gari ya hospitali kuwa kitengo cha kufanya tathmini ya awali ya wagonjwa au majeruhi.
Utumiaji wa silaha nzito za kivita katika maeneo yenye watu wengi husababisha majeraha makubwa, haswa miongoni mwa watoto, iliongeza.
Mjini Kinshasa, umati wa watu wenye hasira ulilenga balozi za Ufaransa, Kenya na Uganda miongoni mwa nyingine.
Walivamia barabarani, wakichoma magurudumu na kusababisha msongamano wa magari.
Pamoja na vifo vya raia, Afrika Kusini ilisema Jumanne kwamba wanajeshi wake wengine wanne, ambao wako DR Congo kama sehemu ya juhudi za kulinda amani, walikufa kutokana na mapigano na M23.
Hii inafanya jumla ya vifo vya Afrika Kusini kufikia 13. Malawi na Uruguay pia zimepoteza askari wa kulinda amani.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa siku ya Jumatatu alizungumza na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame, huku wawili hao wakikubaliana kuhusu hitaji la dharura la kusitishwa kwa mapigano na kuanzishwa tena kwa mazungumzo ya amani.
Ilikuja wakati Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alipokuwa akilaani shambulizi la M23 katika mazungumzo na Rais wa DR Congo Félix Tshisekedi.
Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kiongozi huyo wa Congo alikubaliana kuhusu haja ya kuanzisha upya mazungumzo ya amani "haraka iwezekanavyo" na Rwanda.
Rubio pia alizungumza na Rais wa Kenya William Ruto, akikubali kusukuma mbele mazungumzo ya amani. Mkutano ulioitishwa na kiongozi wa Kenya kati ya Tshisekedi na Kagame umepangwa kufanyika Jumatano.
Serikali ya Congo pia imeomba kufanyika kwa mkutano mwingine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ikitaka mara hii ichukue hatua kali dhidi ya Rwanda.
Wakati wa mkutano wa dharura wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumapili, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilidai vikwazo dhidi ya Rwanda, ikisema kuwa vikosi vyake vimevuka mpaka katika eneo lake kwa kile ambacho ni sawa na "tangazo la vita".
Kufuatia mkutano huo, Umoja wa Mataifa ulilaani maendeleo ya M23 na "kupuuzwa kwa wazi kwa uhuru na uadilifu wa eneo la DR Congo", ikiwa ni pamoja na uwepo wa "majeshi ya nje".
Rwanda siku za nyuma ilikanusha uungaji mkono wa moja kwa moja kwa M23, lakini mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix amesema hakuna shaka kuwa wanajeshi wake walikuwa wakiwaunga mkono waasi.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












