Tunachojua kuhusu ajali ya ndege ya Azerbaijan Airlines

Chanzo cha picha, EPA
Tarehe 25 Disemba, watu 38 walifariki wakati ndege ya Shirika la Ndege la Azerbaijan, ambayo ilikuwa ikitua nchini Urusi, ilipotua Kazakhstan.
Mazingira karibu na ajali hiyo bado hayaulikani, lakini ushahidi mdogo hadi sasa unaonyesha kuwa inaweza kuwa imeharibiwa na makombora yaliyorushwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa Urusi ilipojaribu kutua Chechnya.
Haya ndiyo tunayojua kuhusu Flight J2-8243.
Ndege ilipaa kutoka wapi?
Asubuhi na mapema Siku ya Krismasi, Ndege ya J2-8243 ilipaa kutoka uwanja wa ndege wa Baku, mji mkuu wa Azerbaijan. Ilitarajiwa kutua huko Grozny, mji mkuu wa mkoa wa Urusi wa Chechnya.
Ndani ya ndege hiyo kulikuwa na abiria 67, wengi wao wakiwa raia wa Azerbaijan, pamoja na wale kutoka Urusi, Kazakhstan na Kyrgyzstan.
Ndege hiyo ilikuwa aina ya Embraer 190, inayoendeshwa na Azerbaijan Airlines.
Ilipokaribia Grozny
Ndege ilipokaribia Grozny, iliipitia ukungu mzito, abiria walionusurika wanasema.
Wanaelezea jinsi rubani alivyojaribu kutua ndege mara mbili katika hali hizi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ilikuwa ni katika jaribio la tatu, walionusurika wanasema, ambapo walihisi mfululizo wa milipuko kugonga ndege.
"Mara ya tatu, kitu kililipuka ... baadhi ya ngozi ya ndege ilikuwa imepeperuka," mmoja aliiambia TV ya Kirusi.
Mhudumu wa ndege kwenye ndege hiyo, Zulfuqar Asadov, aliambia vyombo vya habari vya ndani athari za shambulio hilo "zilisababisha hofu ndani".
"Tulijaribu kuwatuliza [abiria], ili kuwaondoa wasiwasi. Wakati huo, kulikuwa na shambulio jingine , na mkono wangu ulijeruhiwa," alisema.
Video iliyorekodiwa katika ndege na abiria ilionyesha barakoa za oksijeni zikining'inia kutoka kwenye dari.
Waziri wa uchukuzi wa Azerbaijan Rashad Nabiyev alisema: "Wote [walionusurika] walisema walisikia sauti tatu za mlipuko wakati ndege ilipokuwa juu ya anga ya Grozny."
Alisema ndege hiyo iliathiriwa "nje" na kuharibika ndani na nje ilipokuwa ikijaribu kutua.
Katika wiki za hivi karibuni, Ukraine imekuwa ikilenga Chechnya na maeneo mengine ya Caucasus ya Urusi kwa mashambulizi ya drone.
Baada ya ajali hiyo, mamlaka huko Moscow ilisema mashambulizi kama hayo yalisababisha itifaki ya kufunga anga ya juu ya Grozny.
Kulingana na maafisa wa eneo hilo, ndege isiyo na rubani ilidunguliwa na walinzi wa anga juu ya duka kubwa huko Vladikavkaz, karibu na Ossetia Kaskazini, asubuhi hiyo.
Haijabainika iwapo itifaki ya angailiofungwa - inayojulikana kama "mpango wa zulia" - ilipitishwa kabla au wakati Flight J2-8243 ilipokuwa katika anga ya Urusi.
Kubadilisha njia kwenda Kazarkhstan

Baada ya tukio hilo huko Grozny, ndege ilielekezwa kwa takriban kilomita 450 (maili 280) mashariki hadi uwanja wa ndege wa Aktau huko Kazakhstan.
Bado haijulikani kwa nini ilielekezwa kwenye Bahari ya Caspian - safari ndefu zaidi kuliko chaguzi zingine kadhaa.
Mamlaka ya anga ya Urusi imedai marubani wa ndege hiyo "walipewa viwanja vingine vya ndege", lakini wakachagua Aktau.
Data iliyotolewa na tovuti ya ufuatiliaji wa safari za ndege ya Flight Radar inaonyesha ndege hiyo ikiyumba-yumba juu na chini ilipokaribia Aktau, kabla ya kugeuka na kutua kilomita chache kutoka uwanja wa ndege.
Ilianguka wakati ikitua
Video kutoka karibu na eneo la tukio inaonyesha ndege hiyo ikishuka kwa kasi angani kabla ya kuanguka ardhini na kuserereka kwa mita mia kadhaa kwenye ikiwa inawaka moto.
Watu 38 waliuawa na 29 walinusurika, wengine wakiwa na majeraha mabaya. Ajabu ni kwamba baadhi ya walionusurika walionekana wakitembea na kutambaa kutoka kwenye mabaki ya ndege hiyo.
Marubani wa ndege hiyo wanasifiwa kwa kuokoa maisha kwa kufanikiwa kutua sehemu ya ndege hiyo, licha ya wao kuuawa kwenye ajali hiyo.
Inaaminika wengi wa walionusurika walikuwa wameketi nyuma yake.
Je! ilishambuliwa na ulinzi wa anga wa Urusi?
Ripoti za awali kutoka vyombo vya habari vya Urusi zilidokeza kuwa ndege hiyo iligongana na kundi la ndege.
Hata hivyo, wataalam wa masuala ya usafiri wa anga na watu wengine nchini Azerbaijan wanaamini kuwa mifumo ya GPS ya ndege hiyo iliathiriwa na msongamano wa kielektroniki na kisha kuharibiwa na vipande vya milipuko ya makombora ya ulinzi wa anga ya Urusi.
Siku ya Ijumaa msemaji wa usalama wa taifa wa White House John Kirby aliwaambia waandishi wa habari kwamba Marekani ilikuwa na "dalili za mapema" kwamba Urusi ilihusika, lakini alikataa kutoa maoni zaidi.
Kufikia sasa, serikali ya Azerbaijan imeepuka kuishutumu Urusi moja kwa moja - lakini vyanzo vya serikali ya Azerbaijan vililiambia shirika la habari la Reuters kwamba uchunguzi tayari umegundua silaha iliyofyatuliwa kwenye ndege hiyo kuwa ni mfumo wa kuzuia ndege wa Pantsir-S wa Urusi.
Ikulu ya Kremlin hadi sasa imekataa kuzungumzia taarifa za ndege hiyo kupigwa na silaha za Urusi.
"Uchunguzi... unaendelea na hadi mahitimisho yatakapofanywa kutokana na uchunguzi huo, hatuoni kuwa tuna haki ya kutoa tathmini yoyote," alisema msemaji Dmitry Peskov.
Uchunguzi
Vinasa sauti vya ndege hiyo ambavyo vina data za kusaidia kubaini chanzo cha ajali hiyo vimepatikana.
Ripoti huko Baku zinaonyesha Urusi na Kazakhstan zimependekeza kuwa na kamati kutoka Jumuiya ya Madola Huru (CIS) - shirika la kikanda linalotawaliwa na Urusi - kuchunguza ajali hiyo, lakini Azerbaijan badala yake imedai uchunguzi wa kimataifa.
Mashirika ya ndege ya Azerbaijan na mashirika mengine kadhaa ya ndege yamesitisha safari za ndege kuelekea katika baadhi ya miji ya Urusi kufuatia ajali hiyo.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla













