Mzozo wa DRC: Ushahidi unaoonesha Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23

Five men in Kinshasa tear apart a Rwandan flag as they shout in protest about the M23's attack of Goma in DR Congo - 28 January 2025

Chanzo cha picha, EPA

    • Author, Ian Wafula
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Waandamanaji mjini Kinshasa, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wamekuwa wakichoma picha za rais wa Rwanda na kurarua bendera za Rwanda huku waasi wa M23 wakidhibiti sehemu kubwa ya mji wa Goma mashariki mwa nchi hiyo.

Hasira zao zinaelekezwa kwa Rais wa Rwanda Paul Kagame, ambaye wanamtuhumu kuwaunga mkono waasi - shutuhuma zilizotolewa kwa muda mrefu na Umoja wa Mataifa.

Wataalam wa Umoja wa Mataifa wanashikilia kuwa jeshi la Rwanda "linaongoza operesheni za M23", wakielezea jinsi makurutu wa M23 wanavyopewa mafunzo chini ya usimamizi wa Rwanda na kupewa silaha za hali ya juu za Rwanda.

Mji wa Goma uko karibu na Ziwa Kivu kwenye mpaka na Rwanda. Huu ni mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini lenye utajiri wa madini - na ni kitovu muhimu cha biashara, kituo cha kutoa hudoma ya kibinadamu na kituo cha ujumbe mkubwa zaidi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Jiji hilo pia lilikuwa kimbilio la wale wanaokimbia mzozo kati ya wapiganaji wa M23 na jeshi ambao ulizuka tena mwishoni mwa 2021 - na idadi ya watu ikiongezeka hadi karibu milioni mbili.

Wakazi wa jiji hilo wanakabiliwa na hatari zaidi baada ya mapigano kuzuka tena Jumapili usiku. Makabiliano makali yaliyoshuhudiwa yamesababisha maafa yaliyoacha miili ya watu ikiwa imetapakaa mitaani. Hali halisi ya kinachoendelea haijulikani kwasababu mawasiliano ya simu, huduma za umeme na usambazaji wa maji pia imekatizwa. Lakini M23 wanasadikiwa kuteka sehemu kubwa ya jiji hilo.

"Suala la iwapo wanajeshi wa Rwanda kuunga mkono wapiganaji wa M23 ndani ya Goma halina mjadala ," alisema mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix, japo aliongeza kuwa ilikuwa vigumu kutaja idadi kamili katika eneo la Goma.

Wapiganaji wa M23 - Picha ilipigwa 2023

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, M23 inasema ni kundi la waasi waCongo wanaotoa ulinzi kwa jamii ya Watutsi wenye asili ya DR Congo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Jumatatu wiki hii baadhi ya wanajeshi wa jeshi la Congo waliokuwa Goma walijisalimisha kwa kuvuka mpaka na kuingia Rwanda.

Tangu mzozo huo uanze, Rais Kagame mara kwa mara amekanusha kuhusika kwa namna yoyote katika kusaidia waasi wa M23, ambao wana vifaa vya kutosha, silaha za kutosha na mafunzo ya kutosha.

Hata hivyo, msimamo huo umebadilika sana huku shutuma zikiendelea kuongezeka huku "uwezo mkubwa" wa kundi hilo la waasi ukioonyesha uungaji mkono wa Rwanda, kulingana na Richard Moncrief, mkurugenzi wa mradi wa International Crisis Group kwa Maziwa Makuu.

"Msimamo umebadilika hadi wakaishia kuhalalisha hatua za kujilinda," aliiambia BBC. "Imekuwa vigumu kutenganisha msaada wa Rwanda kwa M23."

Siku ya Jumapili, Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda ilisema katika taarifa yake: "Mapigano yanayoendelea karibu na mpaka wa Rwanda ni tishio kwa usalama wa Rwanda, na hivyo basi Rwanda haina budi kujilinda."

Ilisema inasikitishwa na kauli za "kupotosha na za kijanja" zisizo na msingi zinazotolewa kuhusu mzozo huo.

Kwa Kagame, muktadha wa yote haya unatokana na mauaji ya halaiki ya Rwanda ambayo yalifanyika kwa siku 100 mwaka 1994.

Wanamgambo wa kabila la Wahutu waliohusika na mauaji ya hadi watu 800,000 - wengi wao kutoka jamii ya Watutsi - walikimbilia eneo ambalo sasa ni DR Congo, wengine wakijiunga na Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR).

Kundi hili la waasi bado linafanya kazi katika eneo la mashariki mwa DR Congo ambalo halijatulia - na bado linajumuisha baadhi ya wale waliohusika na mauaji ya halaiki.

Kagame, ambaye aliongoza kikosi cha waasi cha Watutsi ambacho kilimaliza mauaji zaidi ya miongo mitatu iliyopita, anawachukulia "wanamgambo hao wa mauaji ya halaiki" kama tishio lililopo.

Soma pia:
Mwezi huu pekee watu 400,000 wamekimbia makwao kutokana na mapigano

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mwezi huu pekee watu 400,000 wamekimbia makwao kutokana na mapigano

Serikali ya Kagame imevamia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mara mbili, ikisema inataka kuzuia vikundi vya waasi wa Kihutu kufanya mashambulizi ya kuvuka mpaka.

Mapema Mwezi huu, alimshutumu rais wa DR Congo, Félix Tshisekedi, kwa kushindwa kushughulikia FDLR na kuzungumza na M23, akisema kuwa hili linazidi kuzidisha mgogoro.

Bwana Moncrief anaamini kuwa shambulizi la Goma linahusiana zaidi na kutoa ujumbe wa kisiasa, akisema kuwa M23 halihitaji jiji hilo kimkakati kwani tayari "linadhibiti maeneo mengi yenye faida zaidi."

"Ni njia ya Rais Kagame kuonyesha nguvu yake juu ya nani anayeongoza Kivu Kaskazini," alisema mtaalamu wa Maziwa Makuu.

Rwanda ilimlaumu gavana wa kijeshi wa Kivu Kaskazini, ambaye aliuawa katika mapigano wiki iliyopita, kwa kushirikiana na FDLR.

Wataalamu wanakubaliana kuwa kugundulika kwa ushirikiano wa kiwango cha juu kama huu, ingekuwa kama changamoto kuu kwa Rwanda.

A Rwandan policeman and Rwandan army soldiers escort a group of Congolese soldiers into Gisenyi after they surrendered

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Rwanda waliwasaidia wanajeshi wa Congo waliojisalimisha kuvuvuka mpaka na kuingia Rwanda siku ya Jumatatu.

Asili ya M23 inahusishwa na mivutano hii – ni kundi la waasi ambalo linasema linapigania maslahi ya jamii ya Watutsi walio wachache mashariki mwa DR Congo.

Uasi wake wa kwanza wa zaidi ya muongo mmoja uliopita ulimalizika kwa makubaliano ya amani - wapiganaji wake walipokonywa silaha na wengi wao wakahamia katika kambi nchini Uganda.

Lakini miaka mitatu iliyopita, walianza kuondoka kambini wakisema mpango wa amani haukuheshimiwa na ndani ya miezi michache wakaanza kuteka maeneo.

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa - uliotumwa mara ya kwanza mwaka 1999 - hauna mamlaka ya kufanya mashambulizi. Vikosi viwili vya kikanda - kimoja cha Afrika Mashariki kikifuatiwa na cha kusini mwa Afrika - vilitumwa miaka michache iliyopita kwa ombi la Tshisekedi, lakini vimeshindwa kuwadhibiti M23.

Hilo linatoa mwanga juu ya uwezo mkubwa wa M23.

Kulingana na kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa, uwezo wao unajumuisha mafunzo ya miezi mitano katika kambi kuu ya M23 huko Tchanzu, eneo lenye milima, si mbali na mpaka wa Rwanda. Mafunzo hayo yanajumuisha kozi za nadharia na itikadi na kisha vitendo ikiwa ni pamoja na "mbinu za vita," "sheria za mapambano'' na "mbinu za msituni."

Inaelezwa kuwa maafisa wa Rwanda mara nyingi walikuwepo kwenye kambi hiyo, ambapo waajiriwa, wakiwemo watoto, waliletwa - wengine wakijiunga kwa hiari, wengine walilazimishwa kujiunga kupitia operesheni maalumu ambapo machifu wanalazimika kutoa wapiganaji.

Wataalamu hao walisema Sultani Makenga, aliyepigana upande wa Kagame mwanzoni mwa miaka ya 1990 nchini Rwanda na sasa ni mkuu wa waasi wa M23, alihudhuria baadhi ya sherehe za waliofariki dunia kati ya Septemba 25 na 31 Oktoba 2024 zilizohusisha wapiganaji 3,000.

Msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo hakujibu swali la iwapo maafisa wa Rwanda walikuwa katika kambi ya M23 au la, lakini alikanusha tuhuma kuhusu askari watoto, aliiambia BBC mwaka jana: "Madai ya kuandikishwa watoto katika kambi ni ya upuuzi, ni vita vya wazi vya taarifa dhidi ya Rwanda."

Hata hivyo wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaeleza jinsi nguvu za M23 zilivyoongezeka tangu mwezi Mei, wakati huo ilipokuwa na wapiganaji karibu 3,000.

Wataalamu hao wanakadiria kuwa kati ya wanajeshi 3,000 na 4,000 wa jeshi la Rwanda wako ardhini nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo - wakisema idadi hiyo inatokana na uthibitisho wa picha, picha za ndege zisizo na rubani, rekodi za video, ushuhuda na ujasusi.

Wapiganaji waliokamatwa wa M23 walisema kuwa Wanyarwanda wanajulikana kuwa ni "friendly force" (vikosi rafiki,) na ripoti ya wataalamu ya mwezi Disemba inasema neno hilo la Kiingereza "lilitumiwa na wote" hata wakati ambao waliohojiwa walipokuwa wakizungumza kwa lugha zingine.

A black and white screenshot of a short-range air defence system - a weapon that resembles a tank.

Chanzo cha picha, UN

Maelezo ya picha, Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanajumuisha picha za mfumo wa ulinzi wa anga wa masafa mafupi katika ripoti yao ya hivi karibuni, wakisema mifumo mitatu ilionekana katika maeneo ya M23 (Kibumba, Kitchanga na Karuba) mwezi Novemba, ikiendeshwa na askari kwa kutumia silaha sawa na za jeshi la Rwanda.

Walisema vikosi hivi maalumu vya Rwanda vilikuwepo huko kutoa mafunzo na kuwasaidia waasi, na hawakuingiliana na wapiganaji wa kawaida wa M23.

Mshirika wa Rwanda, Uganda, ambaye anapambana na kundi jingine la waasi nchini DR Congo ambalo linatishia usalama wake, pia inashutumiwa kuwasaidia M23 - huku maafisa wake pia wakionekana Tchanzu.

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wanasema Uganda pia imesambaza silaha, kuwakaribisha viongozi wa waasi na kuruhusu shughuli za kuvuka mpaka za wapiganaji wa M23 - shutuma ambazo Kampala inazikanusha.

Hivi karibuni Kagame alieleza kusikitishwa kwake, kwamba baada ya Tshisekedi kuingia madarakani mwaka 2019, pendekezo la Rwanda la kushirikiana na jeshi la Congo kukabiliana na FDLR lilikataliwa. Ni tofauti na mashambulizi ya pamoja ya DR Congo na Uganda dhidi ya waasi wa Islamic Allied Democratic Forces (ADF).

Hilo linaweza kuelezea sababu ya kuibuka upya kwa M23 mwaka 2021 - huku ushahidi unaonyesha uungaji mkono wa Rwanda kwa kundi hilo unaendelea kukua.

Clémentine de Montjoye, mtafiti mwandamizi katika idara ya masuala ya Afrika katika shirika la Human Rights Watch, ameiambia BBC, picha za kijiografia zilionyesha wanajeshi wa Rwanda huko Sake, mji ulio nje kidogo ya Goma wiki iliyopita.

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wanasema uamuzi wa M23 wa kuteka mji wenye madini wa Rubaya, ulioangukia mikononi mwa vikosi vyake mwezi Mei, "ulichochewa na hitaji la kimkakati la kuhodhi" biashara yenye faida kubwa ya madini ya coltan, ambayo yanatumika kutengenezea betri za magari ya umeme na simu.

Ripoti ya mwezi Disemba inasema kundi hilo sasa linakusanya takribani dola za kimarekani 800,000 (£643,000) kwa mwezi kutokana na ushuru wa coltan huko Rubaya - na kuhakikisha kwamba karibu tani 120 za madini hayo yanapelekwa moja kwa moja nchini Rwanda kila baada ya wiki nne.

Ripoti hiyo inajumuisha picha za satelaiti zinazoonyesha jinsi barabara ilivyopanuliwa kufikia mwezi Septemba katika upande wa Congo wa kivuko cha mpaka wa Kibumba, ili kuruhusu malori makubwa ambayo hapo awali hayakuweza kutumia njia hii ya kuingia Rwanda.

Kundi la M23 na jeshi la Rwanda wanatuhumiwa kutatiza mawimbi ya GPS, na hivyo kufanya iwe vigumu kuendesha ndege zisizo na rubani na ndege nyingine.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kundi la M23 na jeshi la Rwanda wanatuhumiwa kutatiza mawimbi ya GPS, na hivyo kufanya iwe vigumu kuendesha ndege zisizo na rubani na ndege nyingine.

Bi De Montjoye alielezea kuhusu silaha zenye uwezo mkubwa zinazotumiwa na M23, ambazo hazipatikani katika vikundi vingine vyenye silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

"Mapema mwaka jana, tulirekodi jinsi majeshi ya Rwanda, na M23 walivyorusha makombora ya 122mm, na kupiga kambi za watu waliokimbia makazi yao," aliiambia BBC.

"Kwa hakika, aina ya usaidizi wa kijeshi ambao M23 wameupokea, ndio wameweza kusonga mbele namna hiyo [huko Goma]."

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wametoa mifano mingi kama hii, ikiwa ni pamoja na utumiaji wa makombora ya kushambulia vifaru yaliyotengenezwa Israel.

Bw Moncrief alisema M23 pia ilikuwa ikitumia teknolojia kutatiza mfumo wa Global Positioning System (GPS), ambao umelizuia jeshi la Congo kurusha ndege zisizo na rubani walizonunua kutoka China.

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wanasema "udukuzi na kuvuruga GPS" karibu na maeneo yanayodhibitiwa na M23 na jeshi la Rwanda pia umetatiza ndege nyingine.

Rais Kagame amepuuzilia mbali ripoti hizi za Umoja wa Mataifa, akitoa dharau kwa "utaalamu" wao na kusema wanapuuza maovu mengi yanayofanywa nchini DR Congo kwa kutazama tu "matatizo ya kufikirika" yaliyoundwa na M23.

Jumuiya ya Afrika Mashariki - ambayo kwa sasa inaongozwa na rais wa Kenya - sasa inajaribu kupatanisha, ingawa Tshisekedi amesema hatahudhuria mkutano wa dharura ulioandaliwa haraka.

Waangalizi wa mambo wanasema rais wa Rwanda atamwambia mpatanishi yeyote kwamba FDLR ndiyo pekee inayotakiwa kujadiliwa kwani anasisitiza kuwepo kwao kunaifanya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuwa jirani asiye salama - jambo ambalo alilieleza katika mkutano na waandishi wa habari mapema mwezi huu.

"Kusema kweli, kwa miaka 30 iliyopita kama mtu anataka kuelewa matatizo ya [Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo] na ni masuluhisho gani yanapaswa kufanywa, huhitaji hata kuwa mtaalamu," alisema Kagame.

Ramani

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na Rashid Abdalla