M23: Waasi wasema wameuteka mji wa Goma huku maelfu wakikimbia DRC

Chanzo cha picha, Getty Images
Waasi wa vuguvugu la M23 wanasema wameudhibiti mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wakazi walisambaza video za waasi wa M23 wakishika doria katika mitaa mikuu ya Goma kufuatia msururu wa mashambulizi dhidi ya jeshi la Congo siku ya Jumapili na kuwashuhudia makumi ya maelfu ya watu wakikimbilia miji jirani.
Kwa upande wake serikali ya Congo inasisitiza kuwa bado inadhibiti sehemu za kimkakati za mji huo.
Imeishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kutuma wanajeshi kuvuka mpaka kusaidia M23. Kigali inakanusha hilo.
Rwanda inasema Kinshasa inaunga mkono wanamgambo wanaotaka mabadiliko ya utawala mjini Kigali.
Lakini katika mkutano wa Umoja wa Mataifa Uingereza Marekani na Ufaransa ziliilaani Rwanda kwa kuunga mkono hatua hiyo, na baraza la usalama lilitaka kuondolewa kwa vikosi vya nje.
Kenya imeitisha mkutano wa dharura wa kikanda, huku kukiwa na wasiwasi wa vita vikubwa zaidi.
Baada ya saa kadhaa za milio ya risasi na milipuko katika mitaa ya Goma, makazi ya watu zaidi ya milioni moja,sasa pako kimya, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kenya imetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, na kutangaza kuwa marais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda watahudhuria mkutano wa dharura wa kikanda katika siku mbili zijazo.
Rais wa Kenya William Ruto, mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema ni wajibu kwa viongozi wa ukanda kusaidia kuwezesha suluhu la amani kwa mzozo huo.
Kundi la M23 limechukua udhibiti wa maeneo makubwa ya mashariki mwa DR Congo yenye utajiri wa madini tangu 2021.
Katika wiki chache zilizopita kundi hilo limekuwa likisonga mbele kwa kasi katika mji wa Goma huku kukiwa na mapigano makali.
Tangu kuanza kwa 2025 zaidi ya watu 400,000 wamekimbia makazi yao kaskazini na Kivu Kusini, majimbo karibu na mpaka na Rwanda, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi.
Mwanamke mmoja aliyekimbia makazi yake, Alice Feza, alisema hajui la kufanya, kwani amekimbia kutoka Kiwanja, Rutshuru, Kibumba na sasa Goma.
Watu wanakimbia kila mahali, na hatujui pa kwenda tena, kwa sababu tulianza kukimbia zamani sana, "Bi Feza alisema na kuongeza: "Vita inatukuta hapa kati ya familia za jeshi, sasa hatuna pa kwenda. ."
Barabara kuu zinazozunguka Goma zimefungwa na uwanja wa ndege wa jiji hilo hauwezi tena kutumika kwa uokoaji na juhudi za kibinadamu, UN imesema.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameitaka Rwanda kuondoa majeshi yake katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuwataka waasi wa M23 kusitisha harakati zake.
Guterres, katika taarifa yake kupitia kwa msemaji wake, aliitaka Rwanda "ikomesha uungaji mkono kwa M23 na kujiondoa katika eneo la DRC". Pia alitoa wito kwa M23 "kukomesha mara moja vitendo vyote vya uhasama na kuondoka katika maeneo yanayokaliwa".
Haya yanajiri baada ya wanajeshi 13 waliokuwa wakihudumu kwenye vikosi vya kulinda amani kuuawa katika makabiliano na waasi hao.

Chanzo cha picha, Getty Images
Uingereza imetoa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya walinda amani, huku mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa Ufaransa, Nicolas de Rivière, akireje wito wa Guterres wa kutaka Rwanda iondoe wanajeshi wake nchini DR Congo.
Wote DR Congo na Umoja wa Mataifa wanasema kundi la M23 linaungwa mkono na Rwanda.
Rwanda haijakanusha hili, lakini viongozi wa nchi hiyo waliilaumu DR Congo kwa mzozo uliopo.
Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa Rwanda Ernest Rwamucyo alisema anasikitika kwamba jumuiya ya kimataifa ilichagua kulaani kundi la M23 badala ya jeshi la Congo, ambalo alisema limekiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.
Siku ya Jumamosi, Umoja wa Mataifa ulisema utakuwa unawaondoa wafanyakazi wake wote wasio wa muhimu kipindi hiki kutoka Goma. Operesheni muhimu zinaendelea nchini DR Congo.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












