DRC: Tunachokifahamu kuhusu utekaji wa M23 wa maeneo ya Kivu Kusini na Kaskazini

h

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Vikosi vya serikali vinapambana na waasi wa M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wametangaza kwamba wamerejesha udhibiti kusini mwa eneo la Lubero, katika milima ya Sake na Nyiragongo, kwa kuwarudisha nyuma waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.

Vikosi vya jeshi la DRC, ambavyo vilisema kuwa "vita dhidi ya uchokozi wa Rwanda vinaendelea katika pande zote", hata hivyo vilisisitiza kuwa "adui amefapata mafanikio katika eneo la Bweremana katika Kivu ya Kaskazini na Minova katika Kivu Kusini".

Hatua ya M23 kuteka mji wa Minova, ambao ni muhimu wa kibiashara mashariki mwa DRC, kunawaweka waasi wa M23 chini ya kilomita 40 kutoka mji mkuu wa jimbo wa Goma, uliopo karibu na mpaka na Rwanda.

"Minova iko mikononi mwetu," Corneille Nangaa, kiongozi wa Congo River Alliance, - muungano unaojumuisha kundi la M23, aliliambia shirika la habari la Reuters.

Duru kutoka mjini Goma zimeiambia BBC kuwa Minova ameangukia mikononi mwa waasi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, ambalo linawanukuu maafisa wa shirika la Msalaba Mwekundu, waasi hao wamewajeruhi watu kadhaa ambao wamelazwa hospitalini katika mji mkuu wa jimbo hilo.

Kulingana na Mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu katika mkoa wa Kivu Kaskazini, Myriam Favier, aliyezungumza na shirika la habari la AFP, wagonjwa 100 walitibiwa katika hospitali hiyo kati ya tarehe 1 Disemba 1 na 21, na wagonjwa 211 kati ya Januari 1 na 20.

Kwa mujibu wa taarifa ya FARDC, "kila mahali, adui anakabiliwa vikali." Siku chache zilizopita, vikosi vya serikali vilikomboa tena eneo la Masisi mashariki mwa nchi kutoka kwa waasi wa M23.

"Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo linawataka watu kuwa watulivu na kuwaomba wasijitoroke kwa kuzingatia taarifa za uongo zinazosambazwa na adui kwenye mitandao ya kijamii," alisema Meja Jenerali Ekenge Bomusa Efomi Sylvain, msemaji wa FARDC, ambaye aliahidi kurejesha hali ya amani katika eneo la mashariki mwa nchi.

Unaweza pia kusoma:
g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, M23 inasema kuwa inawalinda Wacongo wenye asili ya Kitutsi Watutsi dhidi ya mateso wanayofanyiwa na jeshi na wapiganaji wa zamani wa Rwanda FDLR.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Jeshi la Congo na washirika wake, wamechukua udhibiti wa mji wa Ngungu katika eneo la Masisi, mji muhimu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kufuatia mapigano makali na waasi wa M23, tovuti ya Radio Okapi inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa iliripoti Juma Tano.

"Jeshi la Congo na washirika wake wanadhibiti vijiji kadhaa karibu na Ngungu. Vijiji hivyo ni pamoja na Kataandwa, Ruzirantaka na maeneo ya jirani," Radio Okapi alisema.

Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Msemaji wa Jeshi la Congo Guillaume Ndjike alitangaza kuwa kikosi cha kupambana na FARDC kimeruhusu maeneo kadhaa kukamatwa tena.

Uasi wa M23, kundi lenye silaha linaloungwa mkono na Rwanda liliuteka mji wa Masisi siku ya Jumamosi. Rwanda imekanusha kuliunga mkono kundilo.

Masisi iko karibu kilomita 80 kaskazini mwa Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, kwenye barabara inayoelekea maeneoa kati ya nchi.

Kwa mujibu wa Aimé Von Businga, Mhariri Mkuu wa gazeti la mtandaoni la Kinshasa Times Online, "idadi kubwa ya watu wanatafuta hifadhi katika vijiji jirani karibu na mji wa Goma, ambao tayari imefurika watu wapatao milioni nne waliokimbia makazi yao." Alisema hali bado ni tete.

Mkuu wa shirika la kimataifa linalofanya kazi Masisi ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wafanyakazi wamekuwa katika hali ya mshtuko na hawawezi kuendelea na shughuli zao kwasababu biashara zimefungwa, na imekuwa vigumu kupata vifaa.

"Hawajui jinsi ya kuondoka katika mji huo kwasababu tunahofia kwamba vikosi vya Congo vitaanzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi," ana wasiwasi.

Mkazi mmoja ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kundi la M23 liliandaa mkutano na wakazi wa mji huo, akisema "limekuja kuikomboa nchi".

Kusema ukweli, kila wakati M23 inapouteka mji, inajionyesha kama yenye nguvu na ambayo itasimamia vyema jiji.

Aimé Von Businga anasema kwamba "katika miji yote iliyochukuliwa na M23, siku za kwanza, watu walikimbia, kisha mikutano ya M23 ilipangwa kuwaambia watu waendelee na maisha yao ya kawaida na wasiogope kulipiza kisasi."

Baadhi ya watu watarudi lakini wengi hawatarudi.

Siku ya Ijumaa, kundi la M23 liliuteka mji wa karibu wa Katale.

Serikali ya Congo bado haijatoa tamko lolote kuhusu kupotea kwa miji hiyo.

Lakini Alexis Bahunga, naibu wa mkoa, alisema kuwa "Serikali itachukua hatua za kurejesha mamlaka ya Serikali juu ya eneo lote."

MONUSCO yalaani

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umewashutumu waasi wa M23 kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa na DRC na Rwanda mwezi Julai mwaka jana.

Mkuu wa ujumbe huo Bintou Keita alielezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa mashambulizi na kuelezea kukamatwa kwa mji wa mashariki wa Masisi kama hatua ya kutisha.

Wiki iliyopita, ghasia zilizoongezeka zilisababisha vifo vya watu saba na maelfu ya wengine kuyakimbia makazi yao katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Kuongezeka kwa mashambulizi ya M23

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, M23, ambayo iliibuka kutoka kwa kundi lingine la waasi, ilianza kufanya kazi mwaka 2012

Tangu Novemba 2021, waasi wa kundi la M23 wameteka maeneo makubwa ya mashariki mwa DRC, yenye utajiri wa maliasili na kusambaratishwa na vita kwa miaka 30.

Mwishoni mwa mwezi wa Desemba, waasi wameendelea kuyateka maeneo katika sehemu ya kaskazini ya Kivu ya Kaskazini.

Walifika kilomita hamsini kutoka Lubero, mji mkuu wa eneo hilo, na takriban kilomita mia moja kutoka mji wa Butembo.

Mwezi Julai, Rwanda haikukanusha ripoti ya Umoja wa Mataifa kwamba ilikuwa na wanajeshi 4,000 wanaopigana pamoja na kundi la M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hata hivyo, ameishutumu serikali ya Congo kwa kushindwa kuzuia harakati za wapiganaji waasi wa Rwanda, FDLR ambao Rwanda inawatuhumu kuchochea miongo kadhaa ya mizozo mashariki mwa nchi hiyo.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Afrika (AU) ulioteuliwa kuwa mpatanishi katika mgogoro huu haukufanyika.

Kusonga mbele na kuendelea kwa mapigano kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano kunadhoofisha zaidi juhudi za kumaliza mzozo.

Mwezi Desemba, Rais wa Congo Félix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame walitarajiwa kukutana kwa ajili ya mkutano wa kilele ulioandaliwa mjini Luanda na Rais wa Angola Joao Lourenço.

Hata hivyo mkutano huo ulioandaliwa na mpatanishi aliyeteuliwa wa Umoja wa Afrika (AU) katika mgogoro huu haukufanyika.

Makubaliano ya kurejesha amani na utulivu mashariki mwa DR Congo yalikuwa yajadiliwe lakini pande hizo mbili zilishindwa kukubaliana juu ya masharti hayo.

Hii ilisababisha kufutwa kwa mkutano huo dakika za mwisho.

Lakini mwezi mmoja uliopita, mamlaka mjini Kinshasa zilitangaza kuwa zitaendelea na harakati za kijeshi.

Serikali ya DRC inaonekana kuchukua kuchukua hatua za kijeshi. Lakini, Aimé Von Businga anaamini kwamba utekaji huu mpya wa miji na M23 "ungeweza kuilazimisha DRC kurudi kwenye meza ya mazungumzo".

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Ambia Hirsi