Mamlaka ya Kongo imezuia ufikiaji wa uwanja wa ndege wa Goma
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa dharura baadaye leo kujadili mzozo unaoongezeka mashariki mwa Kongo.
Muhtasari
- Katibu Mkuu wa UN aihimiza Rwanda kuondoa wanajeshi wake DRC
- Mamlaka ya Kongo imezuia ufikiaji wa uwanja wa ndege wa Goma
- M23 inasema imefunga anga ya Goma
- Kuna uwezekano chanzo cha mlipuko wa Covid kilitoka kwenye maabara
- Tarehe ya mwisho ya kujiondoa kwa Israeli kutoka Lebanon yapita
- Kurejea kwa Wagaza kwasitishwa
- SADC yalaani mauaji ya vikosi vyake yaliyotekelezwa na M23
- Waasi wawaua wanajeshi 13 wa kigeni wa kulinda amani DR Congo
- DRC yaamuru Rwanda kukomesha shughuli za kidiplomasia Kinshasa
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Katibu Mkuu wa UN aihimiza Rwanda kuondoa wanajeshi wake DRC

Chanzo cha picha, AP
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amewahimiza Rwanda kuondoa wanajeshi wake kutoka DRC na kukomesha msaada kwa waasi wa M23 ambao wanafanya mashambulizi ya kutwaa mji wa Goma Mashariki mwa Kongo.
Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake leo, Bwana Guterres alionyesha wasiwasi mkubwa juu ya vurugu zinazoongezeka huko DRC.
"Ameendelea kulaani vikali Kikundi cha M23 kinachoendeleza mashambulia huku kikielekea Goma kaskazini mwa Kivu kwa msaada wa Kikosi cha Ulinzi cha Rwanda," alisema msemaji wa Katibu Mkuu Stephane Dujarric.
Katibu Mkuu alitaka M23 kumaliza mashambulizi yake, kujiondoa katika maeneo yote yaliyochukuliwa, na kuomba kuheshimiwa kwa mikataba ya kusitisha vita.
"Anatoa wito kwa vikosi vya ulinzi vya Rwanda kukomesha msaada kwa M23 na kujiondoa katika eneo la DRC," Dujarric alisema.
Kufuatia mauaji ya walinda amani watatu wa Umoja wa Mataifa na M23, Bw. Guterres alitoa wito wa uchunguzi wa tukio hilo, akionya kwamba mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuwa uhalifu wa kivita.
Kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kinaendelea, huku hali ya usalama nchini DRC ikiwa kwenye ajenda.
Mamlaka ya Kongo imezuia ufikiaji wa uwanja wa ndege wa Goma

Chanzo cha picha, AFP
Mamlaka ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo imezuia ufikiaji wa uwanja wa ndege katika mji wa mashariki wa Goma na kufuta safari zote za ndege, huku waasi walioungwa mkono na Rwandan wakiendelea kufikia jiji.
Awali, waasi wa M23 walitoa taarifa wakisema walikuwa wamefunga uwanja wa ndege wa Goma.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa dharura baadaye leo kujadili mzozo unaoongezeka mashariki mwa Kongo.
Wanajeshi 13 wa kigeni wanaohudumu na vikosi vya kulinda amani ni miongoni mwa mamia ya watu waliouawa katika siku za hivi karibuni.
Jiji la Goma linashuhudia hali ya wasiwasi sana - milio ya risasi na makombora inakaribia.
Ikiwa waasi wa M23 watajaribu kuuteka mji huu, raia watakuwa katika hatari kubwa. Watu ambao tayari wamekimbia makazi yao kutokana na vita vya miaka mingi wamekuwa wakitoka kambi nje ya jiji kuelekea katikati mwa jiji.
Soma zaidi:
Trump anasema anataka Misri na Jordan kuchukua Wapalestina kutoka Gaza

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump amesema anataka Misri na Jordan kuwachukua Wapalestina kutoka Gaza, eneo ambalo alilitaja kuwa "mahali palipo haribiwa".
Katika simu wikendi hii, Bw Trump alisema alimwambia Mfalme Abdullah wa Jordan: "Ningependa uchukue hatua zaidi, kwa sababu ninatazama Ukanda wote wa Gaza hivi sasa na umeharibiwa kabisa." Alisema alipanga kutoa ombi sawa kwa rais wa Misri siku ya Jumapili.
Hatua hiyo "inaweza kuwa ya muda" au "inaweza kuwa ya muda mrefu", alisema.
Hamas imeapa kupinga hatua yoyote kama hiyo, na maoni hayo huenda yakawakasirisha Wapalestina huko Gaza, ambao ni makazi yao.
"Watu wetu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza walivumilia kifo na uharibifu kwa muda wa miezi 15 ... bila kuondoka katika ardhi yao. Kwa hiyo, hawatakubali mapendekezo yoyote au suluhisho, hata kama inaonekana kuwa nia nzuri chini ya jina la ujenzi upya, kama ilivyotangazwa na Marekani katika mapendekezo ya Rais Trump," Bassem Naim, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, aliiambia BBC.
"Watu wetu, kama vile wamezuia mipango yote ya kuhama na makazi mbadala kwa miongo kadhaa, pia watazuia miradi kama hii," aliongeza.
Wengi wa wakazi milioni mbili wa Gaza wamekimbia makazi yao katika miezi 15 ya vita na Israel, ambayo imeboresha miundombinu mingi ya Gaza.
Umoja wa Mataifa hapo awali ulikadiria kuwa 60% ya miundo kote Gaza imeharibiwa na inaweza kuchukua miongo kadhaa kujengwa upya.
M23 inasema imefunga anga ya Goma

Chanzo cha picha, AFP
Kundi la waasi la M23 mashariki mwa DRC linasema kuwa limefunga anga ya Goma, huku likiendelea na mashambulizi yake ya kuuteka mji huo.
Katika taarifa yake siku ya Jumapili, ilisema vikosi vinavyoshirikiana na serikali ya Kongo "vinatumia uwanja wa ndege wa Goma kupakia mabomu ambayo yanaua raia."
Jeshi la Kongo bado halijasema lolote kuhusiana na hilo, huku wasiwasi ukiendelea kuongezeka katika pande zote mbili.
Msemaji wa jeshi alisema Jumamosi kuwa limewarejesha nyuma waasi kuingia Goma.
Lakini bado haijafahamika hali halisi ilivyo sasa, huku kukiwa na ripoti kwamba Rwanda imetuma wanajeshi kuvuka mpaka kusaidia M23 kuuteka mji huo wenye takriban watu milioni mbili.
DRC tayari imekata uhusiano wa kidiplomasia na Rwanda kutokana na kile inachokiona kuwa Rwanda kuunga mkono M23.
Mapigano ya kuuteka mji wa Goma yamekuwa makali katika siku za hivi karibuni, na wanajeshi 13 wa kulinda amani wa kigeni wameuawa katika mapigano na waasi wa M23.
Mratibu wa usimamizi wa UN huko DRC Bruno Lemarquis alisema mashambulizi ya M23 kwa sasa yametatiza shughuli za kibinadamu, akihimiza pande zote kuacha "kuongezeka jeshi."
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kufanya kikao cha dharura kuhusu hali nchini DRC hii leo.
CIA inasema kuna uwezekano chanzo cha mlipuko wa Covid kilitoka kwenye maabara

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) limetoa tathmini mpya juu ya mlipuko wa Covid, likisema kuna "uwezekano mkubwa" chanzo cha ugonjwa wa corona ni maabara ya Uchina kuliko wanyama.
Lakini shirika hilo la ujasusi lilionya kuwa lina "Imani kidogo" katika hili.
Msemaji alisema kwamba kuna uwezekano mkubwa wa "chanzo kuwa utafiti" kuliko asili kulingana na ripoti iliyopo".
Uamuzi wa kutoa tathmini hiyo ni moja ya tathmini ya kwanza kufanywa na mkurugenzi mpya wa CIA John Ratcliffe, aliyeteuliwa na Donald Trump, ambaye alichukua uongozi wa shirika hilo siku ya Alhamisi.
Ratcliffe, ambaye aliwahi kuwa mkurugenzi wa ujasusi wa kitaifa wakati wa muhula wa kwanza wa Rais Trump, kwa muda mrefu amependelea nadharia ya virusi kutoka kwenye maabara, akidai uwezekano mkubwa wa Covid ulitokana na kuvuja kwa virusi kutoka katika Taasisi ya Wuhan.
Taasisi hiyo ni mwendo wa dakika 40 kutoka soko la Huanan ambapo kundi la kwanza la maambukizo liliibuka.
Lakini maafisa waliviambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba tathmini hiyo mpya haikuegemezwa kwenye ujasusi mpya na ulitoka kabla ya utawala wa Trump kuanza kazi.
Utafiti huo uliotolewa siku ya Jumamosi bado sio wa "kuaminika", hiyo ina maana kwamba taarifa yenye kuelezea hilo sio ya kutosha, inazua maswali mengi au inaleta utata.
Hakuna makubaliano juu ya chanzo cha janga la Covid.
Wengine wanaunga mkono nadharia ya "chanzo cha asili", ambayo inasema kwamba virusi huenea kwa asili kutoka kwa wanyama, bila ushiriki wa wanasayansi au maabara yoyote.
Dhana ya kuwa virusi vinavuja kutoka kwenye maabara imepingwa vikali na wanasayansi, wakiwemo wengi wanaosema hakuna ushahidi kamili wa kuunga mkono.
Na China hapo awali ilitupilia mbali madai ya maabara kama "yenye kuingizwa kisiasa" na Washington.
Pia unaweza kusoma:
Tarehe ya mwisho ya kujiondoa kwa Israeli kutoka Lebanon yapita, huku wanajeshi wakiendelea kuwepo

Chanzo cha picha, Reuters
Wanajeshi wa Israel bado wapo katika maeneo ya kusini mwa Lebanon licha ya kupita kwa siku ya makataa ya kuondoka ambayo ni Jumapili baada ya kusema makubaliano ya kusitisha mapigano na Hezbollah hayajatekelezwa kikamilifu.
Makubaliano hayo ya siku 60, ambayo yalisimamiwa na Marekani na Ufaransa na kukomesha mgogoro wa miezi 14, yalitaja kuondolewa kwa wanajeshi wa Israel kutoka kusini mwa Lebanon na kuondolewa kwa wapiganaji wa Hezbollah na silaha kutoka eneo hilo.
Wakati huo huo, maelfu ya wanajeshi wa Lebanon wanatazamiwa kupelekwa katika eneo ambalo, kwa miongo kadhaa, Hezbollah imekuwa jeshi kubwa.
Haijabainika ni wanajeshi wangapi wa Israel waliosalia Lebanon kufikia Jumapili na ni muda gani wananuia kusalia huko.
Huku siku ya mwisho ikiwa imepita, baadhi ya wakaazi wanajaribu kurejea majumbani mwao, licha ya onyo la majeshi ya Lebanon na Israel, wizara ya afya ya Lebanon ilisema watu watatu waliuawa na 44 kujeruhiwa na jeshi la Israel.
Huu ni mtihani wa kwanza mkubwa kwa rais mpya wa Lebanon, mkuu wa jeshi Joseph Aoun, ambaye ana nia ya kuleta utulivu katika nchi iliyochoshwa na migogoro mingi. Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, alisema "uhuru na uadilifu wa eneo la Lebanon ni jambo lisiloweza kujadiliwa", akiongeza kuwa "anafuatilia suala hili katika viwango vya juu".
Mzozo huo uliongezeka Septemba iliyopita, na kusababisha operesheni kali ya anga ya Israel kote Lebanon, mauaji ya viongozi wakuu wa Hezbollah na uvamizi wa ardhini kusini mwa Lebanon.
Mashambulizi hayo yaliua takriban watu 4,000 nchini Lebanon - ikiwa ni pamoja na raia wengi - na kusababisha zaidi ya wakaazi milioni 1.2 kuyahama makazi yao.
Soma zaidi:
Kurejea kwa Wagaza kwasitishwa huku Israel ikiishutumu Hamas kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano

Chanzo cha picha, EPA
Maelfu ya Wapalestina waliokimbia makazi yao bado wanazuiwa kurejea makwao kaskazini mwa Gaza baada ya Israel kuishutumu Hamas kwa kukiuka masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Siku ya Jumamosi, Hamas iliwaachia huru wanajeshi wanne wa kike wa Israel iliyokuwa imewashikilia tangu tarehe 7 Oktoba 2023, ikiwa ni malipo ya wafungwa 200 wa Kipalestina.
Hata hivyo, mzozo ulizuka wakati raia wa Israel Arbel Yehud hakujumuishwa katika mabadilishano hayo, ingawa Hamas ilipanga kuwaachilia mateka zaidi wasio wanajeshi.
Wakati Hamas ikisisitiza kuwa Bi Yehud yu hai na ataachiliwa wiki ijayo, Israel ilijibu kwa kuchelewesha mpango wa kuondoka kwa baadhi ya wanajeshi kutoka Gaza, ambayo ingewaruhusu Wapalestina kurejea makwao kaskazini mwa Gaza.
Soma zaidi:
SADC yalaani mauaji ya vikosi vyake yaliyotekelezwa na M23

Chanzo cha picha, SADC
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) inalaani mauaji ya vikosi vyake yaliyotekelezwa na M23 mashariki mwa DRC, na kutaja mashambulizi hayo kama "kitendo cha uchokozi."
"Kutafuta upanuzi wa eneo kwa M23 kunafanya hali ya kibinadamu na usalama kuwa mbaya zaidi huko Mashariki mwa DRC," SADC ilisema katika taarifa yake Jumamosi.
Ingawa haikutoa takwimu ya idadi ya wapiganaji wa SAMIDRC waliouawa au kujeruhiwa, nchi wanachama zimethibitisha kifo cha raia wao katika shambulio la M23 wiki hii.
Afrika Kusini ilisema wanajeshi wake tisa waliuawa, wakati Malawi pia alitangaza mauaji ya raia wake watatu. Mbali na Waafrika, mwanajeshi wa Uruguay anayehudumu na ujumbe wa kulinda amani wa UN pia alipoteza maisha katika shambulio la M23, wakati raia wengine wanne walijeruhiwa, serikali yao ilitangaza.
Katika mkutano na waandishi wa habari Jumamosi, msemaji wa jeshi la DRC Jenerali Sylvain Ekenge alisema: "Rwanda imedhamiria kuuteka mji wa Goma," akimaanisha mashambulizi ya hivi karibuni ya M23 katika eneo hilo.
Mamlaka ya Kongo na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi, lakini Kigali imekanusha mara kwa mara madai hayo.
Mapema Jumamosi, EU ililaani kwa nguvu uwepo wa kijeshi wa Rwanda huko DRC, na kuiita "ukiukaji wazi wa sheria za kimataifa, makubaliano ya UN na uadilifu wa eneo la DRC."
"Rwanda lazima iache kusaidia M23 na kujiondoa," Mkuu wa sera ya kigeni ya EU Kaja Kallas alisema.
SADC pia iliwasihi pande zote katika mzozo huo kufuata sheria na masharti ya makubaliano ya amani yaliyopo na kupendelea mazungumzo.
Mkutano wa dharura wa UN wa kujadili hali ya sasa ya Mashariki ya DRC awali ulikuwa umepangwa kufanyika Jumatatu, lakini ukasongezwa hadi Jumapili kutokana na kuongezeka kwa mapigano, AFP ilinukuu vyanzo vya kidiplomasia.
Soma zaidi:
Waasi wawaua wanajeshi 13 wa kigeni wa kulinda amani DR Congo

Chanzo cha picha, Reuters
Wanajeshi 13 wanaohudumu na vikosi vya kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameuawa katika makabiliano na waasi wa kundi la M23.
Jeshi la Afrika Kusini lilisema wanajeshi wake tisa wameuawa wakisaidia kuwarudisha nyuma waasi katika mji wa Goma, mashariki mwa DR Congo, huku raia watatu wa Malawi na Uruguay pia wakiuawa.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema amezungumza na viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Rwanda huku kukiwa na wito wa kimataifa wa kutaka ghasia hizo zisitishwe.
Umoja wa Mataifa unawaondoa wafanyakazi wote wasio wa lazima kutoka Goma - jiji lenye zaidi ya watu milioni moja - wakati mapigano yanapozidi.
DRC yaamuru Rwanda kukomesha shughuli za kidiplomasia Kinshasa

Chanzo cha picha, Getty Images
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imeamuru Rwanda kukomesha shughuli zake zote za kidiplomasia na za kibalozi nchini humo ndani ya saa 48, katika hatua ambayo inaweza kuonekana kama kuongezeka kwa mvutano kati ya nchi hizo mbili.
Hatua hiyo inawadia wakati kikundi cha waasi cha Tutsi kinachoongozwa na M23 kinaendelea na mashambulizi huko Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini.
Mamlaka ya Congo na wataalam wa UN wanaishtumu Rwanda kwa kuwasaidia waasi, ingawa Kigali imekanusha mashtaka hayo mara kwa mara.
"Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imejitolea kuheshimu taratibu zote za kidiplomasia na kuhakikisha mabadiliko ya utaratibu ya uamuzi," Wizara ya Mambo ya Nje ya DRC ilisema katika taarifa.
Taarifa hiyo pia iliongeza kuwa DRC imewaita tena wanadiplomasia wa Kongo mjini Kigali "mara moja."
Rwanda bado haijajibu hatua ya hivi karibuni zaidi ya DRC.
Kuzorota zaidi kwa uhusiano ambao tayari umeharibika kati ya nchi hizo mbili kunafuatia kuuawa kwa Gavana wa kijeshi wa Kivu Kaskazini siku ya Alhamisi na waasi wa M23.
Katika mashambulizi yao dhidi ya mji wa Goma, pia waliwaua wapiganaji wasiopungua 12 wa kigeni katika siku za hivi karibuni.
Wakati huo huo, Uturuki ilijitolea kuwa mpatanishi katika mzozo kati ya DRC na Rwanda, lakini viongozi wa Kongo walikataa ombi hilo, wakisema: "Suluhisho za Kiafrika lazima zipatikane na Waafrika."
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 26/01/2025
