Israel yawaachilia huru wafungwa 200 wa Kipalestina baada ya mateka wake walioachiliwa kuungana na familia zao
Wafungwa hao wameachiliwa baada ya mateka wanne wa kike wa Israel kuachiliwa huru na Hamas na kurejea nyumbani Israel kufuatia makubaliano ya usitishaji wa mapigano.
Muhtasari
- DRC: AU yatoa wito wa usitishaji mapigano, huku M23 wakitoa muda wa saa 48 kwa jeshi kuweka silaha chini
- Marekani imeagiza kusitishwa mara moja kwa misaada ya kigeni, taarifa iliyovuja yasema
- Wapalestina washerehekea kurejea nyumbani kwa wafungwa walioachiliwa huru na Israel
- Ukraine yadai ndege droni zake zimekipiga kiwana cha kusafisha mafuta cha Urusi
- Wafungwa wote 200 wa Kipalestina waachiliwa - Jeshi la Magereza la Israeli latangaza
- Rais wa Afrika Kusini atia saini sheria yenye utata ya kunyakua ardhi
- Tazama: Mateka wanne wa Israel wakiachiliwa na Hamas
- Mateka wanne wa Israel waachiliwa na Hamas na kurejeshwa nyumbani
- Ufaransa, Marekani, na Uingereza zawataka raia kuondoka Goma nchini huku vita vya M23 vikiendelea
- Pete Hegseth aidhinishwa kuwa waziri wa ulinzi wa Marekani baada ya kuhojiwa kuhusu tabia zake.
- Hamas yawataja mateka wengine wa Israel wanaotarajiwa kuachiliwa
Moja kwa moja
Na Dinah Gahamanyi
DRC: AU yatoa wito wa usitishaji mapigano, huku M23 wakitoa muda wa saa 48 kwa jeshi kuweka silaha chini

Chanzo cha picha, AU
Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika Moussa Faki Mohammat amezitaka pande husika na mzozo wa mashariki mwa jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuheshimu mikataba ya usitishaji mapigano na kumaliza uhasama baina yao.
Haya yanajiri huku huku M23 wanaopigana na jeshi la DRC kwa la kuuteka mji wa Goma wakitoa muda wa saa 48 kwa jeshi kuweka silaha chini.
Moussa Faki Mohammat amesema ametambua kuzorota kwa hali ya usalama na ya kibinadamu Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katika taarifa yake kuhusu mzozo huo mkuu huyo wa AU amesema anahofia kuwa hali inayoendelea mashariki inatishia juhudi kubwa zilizofanyika za kurejesha amani, husan mchakato wa upatanishi uliosimamiwa na Rais wa Angola Joao Lourenço.
Bw Mohammat amesisitiza kuwa anaunga mkono juhudi za aina hiyo ambazo amesema ndio njia pekee yakukomesha uhasama baina ya DRC na Rwanda na DRC na wapiganaji wa M23.
Katika taarifa yao M23 – wapiganaji wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda na ambao wameyateka maeneo ya Kivu Kusini na Kaskazini wanalaani ‘’vitendo vya hivi karibuni vya kigaidi vinavyofanywa dhidi ya raia wa Congo, hasa wakazi wa Goma’’.
‘’Tunatoa wito kwa taasisi, mashirika na mashirika yote yanayohusika na utoaji wa huduma ya maji na umeme jijini humo kuchukua hatua za haraka ili kurejesha huduma za msingi za kijamii kwa manufaa ya wananchi’’.
AFC/M23 inatoa wito kwa wanajeshi na washirika wote wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) waliopo Goma na viunga vyake kuweka chini silaha zao ndani ya saa 48.
‘’Pia tunatoa wito kwa MONUSCO kusitisha mara moja ushirikiano wake na vikosi vya FARDC na genocidal ambavyo vinarusha mabomu katika maeneo yenye watu wengi na kushambulia maeneo yetu’’, imeeleza taarifa hiyo.
Unaweza pia kusoma:
Marekani imeagiza kusitishwa mara moja kwa misaada ya kigeni, taarifa iliyovuja yasema

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Hapo awali Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio alisema Marekani inapaswa kutumia pesa nje ya nchi iwapo tu itaifanya Marekani kuwa yenye "nguvu", "salama" au "kustawi zaidi" Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesitisha karibu misaada yote ya kigeni iliyopo na kusitisha msaada mpya, kulingana na taarifa ya ndani iliyotumwa kwa maafisa na balozi za Marekani nje ya nchi.
Agizo hilo lililovuja linafuatia agizo kuu la Rais Trump alilolitoa siku ya Jumatatu la kusitisha kwa siku 90 usaidizi wa maendeleo ya kigeni ikisubiri kuhakikiwa kwa ufanisi na uthabiti wa sera yake ya kigeni.
Marekani ndiyo mfadhili mkubwa zaidi wa kimataifa wa misaada duniani ikitumia $68bn mwaka 2023 kulingana na takwimu za serikali
Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje inaonekana kuathiri kila kitu kuanzia usaidizi wa maendeleo hadi usaidizi wa kijeshi.
Misaada hiyo inasitishwa isipokuwa msaada wa dharura wa chakula na ufadhili wa kijeshi kwa Israeli na Misri. Maudhui ya taarifa hiyo yaliyovuja yamethibitishwa na BBC.
Unaweza pia kusoma:
Wapalestina washerehekea kurejea nyumbani kwa wafungwa walioachiliwa huru na Israel
Jeshi la Magereza la Israel limesema kuwa wafungwa wote 200 wa Kipalestina wanaotakiwa kuachiliwa leo wameachiliwa huru.
Takriban nusu yao wataruhusiwa kurejea makwao katika Ukingo wa Magharibi. Wafungwa 70 ambao wamehukumiwa kwa makosa makubwa zaidi wasindikizwa kupitia Misri hadi nchi jirani kama Qatar na Uturuki, na idadi ndogo itapelekwa Gaza.
Takriban Wapalestina 121 walioachiliwa huru wiki hii walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha jela.
Zifuatazo ni picha za wafungwa hao wakijumuika na familia zao.

Chanzo cha picha, Reuters

Chanzo cha picha, Reuters

Chanzo cha picha, Reuters

Chanzo cha picha, Reuters
Unaweza pia kusoma:
Ukraine yadai droni zake zimekipiga kiwanda cha kusafisha mafuta cha Urusi

Chanzo cha picha, reuters
Maelezo ya picha, Moshi ulionekana ukifuka kutoka kwa jengo la makazi linaloungua huko Hlevakha, mkoa wa Kyiv, ambalo maafisa wa Ukraine wanasema liligongwa na ndege isiyo na rubani ya Urusi. Ukraine inaripotiwa kukipiga kiwanda cha kusafisha mafuta cha Urusi na kuilenga Moscow wakati wa shambulio lililohusisha wimbi la ndege zisizo na rubani zisizopungua 121, mojawapo ya operesheni kubwa zaidi za aina yake wakati wa vita.
Picha za video zilizothibitishwa na BBC zinaonyesha moto ukilipuka juu ya kituo cha kusafishia mafuta na kumwaga maji katika eneo la Ryazan, kusini mashariki mwa Moscow, ambalo maafisa wa Ukraine walisema kuwa walililenga.
Urusi ilisema imetungua ndege 121 ambazo zilikuwa zimelenga mikoa 13, ikiwa ni pamoja na Ryazan na Moscow, lakini iliripoti kuwa hakuna uharibifu wowote.
Kwingineko, mamlaka ya Ukraine ilisema watu watatu waliuawa na mmoja kujeruhiwa wakati ndege isiyo na rubani ya Urusi ilipogonga jengo la makazi katika mkoa wa Kyiv.
Unaweza pia kusoma zaidi:
KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
Habari za hivi punde, Wafungwa wote 200 wa Kipalestina waachiliwa - Jeshi la Magereza la Israeli latangaza
Ripoti kutoka kwa Jeshi la Magereza la Israel ikisema wafungwa wote 200 wa Kipalestina wanaopaswa kuachiliwa leo wameachiliwa.
"Baada ya kukamilika kwa shughuli muhimu katika magereza na idhini ya mamlaka ya kisiasa, magaidi wote waliachiliwa kutoka magereza ya Ofer na Ktziot," taarifa hiyo, iliyotajwa na AFP na Reuters, inasema.
Rais wa Afrika Kusini atia saini sheria yenye utata ya kunyakua ardhi

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Sheria ya unyakuzi inaonekana itaongeza mageuzi ya ardhi nchini Afrika Kusini Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, ametia saini sheria inayoruhusu serikali kunyakua ardhi kutoka kwa wazungu bila kutoa fidia, hatua ambayo imezua mzozo mkali ndani ya serikali yake.
Zaidi ya miaka 30 baada ya kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi, waafrika kusini weusi wanamiliki sehemu ndogo tu ya ardhi ya kilimo nchini mwao, huku sehemu kubwa ikibaki mikononi mwa walowezi wachache wazungu.
Serikali imesema sheria hiyo "inafafanua jinsi kupokonywa ardhi kunaweza kufanyika na kwa misingi gani."
Sheria mpya inachukua nafasi ya sheria ya awali ya Upokonyaji wa mashamba ya mwaka 1975, iliyokuwa ikiilazimisha serikali kulipa fidia wamiliki wa ardhi waliokuwa tayari kuuza mali zao kwa mfumo wa "muuzaji na mnunuzi aliyeridhia." Mfumo huo umeleta hasira na kufadhaika kutokana na kasi ndogo ya mabadiliko katika umiliki wa ardhi.
Chama cha ANC cha Ramaphosa kimepongeza sheria hiyo kama hatua muhimu katika mageuzi ya nchi, lakini baadhi ya wanachama wa serikali ya muungano wametishia kuipinga mahakamani. Sheria mpya inaruhusu serikali kuchukua ardhi bila fidiaikiwa itakuwa "ya haki na sawa" na kwa maslahi ya umma.
Msemaji wa Rais, Vincent Magwenya, alisema kuwa chini ya sheria hiyo, "serikali haiwezi kunyakua mali ya watu kiholela au kwa sababu nyingine yoyote isipokuwa kwa maslahi ya umma."
"Kunyang'anywa mali hakuwezi kufanyika isipokuwa mamlaka husika itajaribu bila mafanikio kufikia makubaliano na mmiliki," aliongeza.
Sheria hii imetangazwa baada ya mchakato wa mashauriano wa miaka mitano pamoja na mapendekezo ya kamati maalum ya rais iliyoundwa kuchunguza suala hili.
Tazama: Mateka wanne wa Israel wakiachiliwa na Hamas
Maelezo ya video, Tazama: Mateka wa Israel wakiachiliwa na Hamas Video kutoka mji wa Gaza inaonyesha mateka wanne wa Israel wakikabidhiwa na watu wenye silaha wa Hamas katika tukio lililoandaliwa na kupelekwa katika magari ya shirika la msalaba mwekundu.
Wanajeshi Karina Ariev, Daniella Gilboa, Naama Levy - wote watatu wenye umri wa miaka 20 - na Liri Albag, 19 walichukuliwa kutoka kambi ya kijeshi katika mpaka wa Israel na Gaza wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7. Hii ni sehemu ya pili ya kuachiliwa kwa mateka wa Israel na kubadilishana wafungwa wa Kipalestina tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yalipofikiwa mapema mwezi huu.
Unaweza pia kusoma:
Mateka wanne wa Israel waachiliwa na Hamas na kurejeshwa nyumbani

Chanzo cha picha, Reuters
Tofauti na makabidhiano ya mwishoni mwa wiki iliyopita ya mateka huko Gaza, matukio ya leo yamechochewa sana na Hamas.
Wasichana hao wanne waliibuka kutoka kwenye magari yaliyolindwa na watu wenye silaha waliojifunika nyuso zao na kuwekwa kwenye eneo lililoandaliwa, ambapo muda mfupi kabla ya hapo afisa wa shirika la msalaba mwekundu alitia saini nyaraka na mpiganaji wa Hamas.
Watekaji hao walionekana wakiwa wamevalia mavazi yanayofanana huku shingoni mwao wakiwa wameshikilia beji za kitambulisho – huku watu wenye silaha waliojifunika nyuso zao wakiwa wamesimama karibu nao, kila mmoja akiwa na aina yake ya kibali kwa ajili ya tukio hilo.
Karibu na jukwaa na dawati lake, viti na bendera kulikuwa na bunduki aina ya machinegun.
Huku mamia ya wapiganaji wa Hamas na raia wa Palestina wakiwatazama, wanawake hao wanne wa Israel walionekana wakitabasamu, wakishikana mikono na kusalimiana. Nani anayejua ni nini walikuwa wanafikiria baada ya hisia za maumivu yao ya miezi 15 hatimaye kufikia mwisho.
Hamas - ambayo ilikuwa imewapa kila mmoja wa wanawake nyaraka na mikoba ya kubebea vitu vyao, ina matumaini kuwa picha hii itaonyesha umoja na nguvu.
Ujumbe huo bila shaka uliwalenga Wapalestina wanaotarajia kuiendesha Gaza siku moja, na Waziri Mkuu Netanyahu, ambaye amekuwa na uzoefu wa kudanganya ili kuliangamiza kundi hilo baada ya mashambulizi ya Oktoba 7.
Kwa Israel, kuna afueni kubwa kwamba mateka wengine wanne wako salama. Wiki iliyopita, wengi walihisi hasira kwamba wanawake watatu wa kwanza walioachiwa huru waliondolewa bila utaratibu maalumu.
Leo, pamoja na matukio ya tofauti sana, kutakuwa na hasira - lakini wakati huu katika kuhusu kuonyeshwa kwa wanawake hao kwa umma katika nyakati zao za mwisho kabla ya kupewa uhuru wao.
Unaweza pia kusoma:
Ufaransa, Marekani, na Uingereza zawataka raia kuondoka Goma nchini huku vita vya M23 vikiendelea

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Waasi wa M23 wameyateka maeneo mengi ya Kivu Kusini na Kaskazini Wakati waasi wa M23 wakisonga mbele kuelekea Goma, mji mkubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Marekani, Uingereza na Ufaransa siku ya Ijumaa zilitoa wito kwa raia wao kuondoka eneo hilo.
Mapigano kati ya jeshi la Congo na waasi yamezusha mzozo wa kibinadamu huku juhudi za kidiplomasia kupatanisha mazungumzo kati ya viongozi wa Congo na Rwanda zimeshindwa.
DRC na Umoja wa Mataifa zinaishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuchochea uasi wa miaka mitatu wa M23 kwa kutumia wanajeshi wake na silaha. Rwanda inakanusha hili.
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na M23 walipambana nje ya Goma Ijumaa huku Uingereza, Marekani na Ufaransa zikiwataka raia kuondoka katika mji huo ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zikionya hali inaweza kuwa mbaya zaidi.
Tangu mazungumzo ya amani kushindikana, wapiganaji wa M23 wanaoungwa mkono na wanajeshi wa Rwanda wametateka maeneo mengi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika wiki za hivi karibuni, na kusababisha mgogoro wa kibinadamu kuukumba mji mkuu wa jimbo hilo, ambao ni makazi ya watu wapatao milioni mbili.
Marekani, Uingereza na Ufaransa zilitoa wito kwa raia kuondoka Goma wakati viwanja vya ndege na mipaka bado viko wazi, kwa taarifa za mtandaoni au kwa ujumbe unaotumwa moja kwa moja kwa barua pepe au SMS.
Umoja wa Mataifa umeonya kwamba mzozo unaoendelea katika jimbo la Kivu Kaskazini umesababisha zaidi ya watu 400,000 kuyahama makazi mwaka huu na huenda ukazua vita vya kikanda.
Unaweza pia kusoma:
Pete Hegseth aidhinishwa kuwa waziri wa ulinzi wa Marekani baada ya kuhojiwa kuhusu tabia zake.

Maelezo ya picha, Pete Hegseth ana uzoefu mdogo wa kisiasa baada ya kugombea na kushindwa kiti cha Useneti Pete Hegseth, ambaye aliteuliwa na Donald Trump kuwa waziri wa ulinzi wa Marekani, amethibitishwa na Baraza la Seneti usiku wa kuamkia leo, baada ya kukabiliwa na madai ya utovu wa nidhamu ambayo yalikaribia kuvuruga uthibitisho wake.
Makamu wa Rais JD Vance alipiga kura ya marudiano iliyomuunga mkono Hegseth, baada ya maseneta watatu wa chama cha Republican, akiwemo aliyekuwa kiongozi wa wengi katika Seneti Mitch McConnell, kupiga kura dhidi yake.
Wakati wa kusikilizwa kwa uthibitisho wa Hegseth, alikabiliwa na maswali mengi kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono, ambayo ameyakanusha, pamoja na kutokuwa mwaminifu kwa mkewe na ulevi.
Mwanajeshi huyo wa zamani aliyepigana vita ambapi pia wakati mmoja aliwahi kuwa mtangazaji wa wa televisheni ya Fox News ataongoza wizara ya ulinzi yenye wafanyikazi milioni tatu na atasimamia bajeti ya dola bilioni $849 (£695bn).
Unaweza pia kusoma:
Hamas yawataja mateka wengine wa Israel wanaotarajiwa kuachiliwa

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Kutoka juu kushoto: Karina Ariev, Naama Levy, Daniella Gilboa na Liri Albag Hamas imewataja mateka wanne watakaoachiliwa siku ya Jumamosi chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza.
Inasema ni askari Karina Ariev, Daniella Gilboa, Naama Levy na Liri Albag. Wataachiliwa kwa kubadilishana na wafungwa 180 wa Kipalestina wanaoshikiliwa nchini Israel.
Hii itakuwa ni mara ya pili mazungumzo hayo kufanyika tangu usitishaji mapigano uanze kutekelezwa Jumapili iliyopita.
Mateka watatu na wafungwa 90 waliachiliwa katika mabadilishano ya kwanza ya wafungwa.
Usitishaji huo wa mapigano ulisimamisha vita vilivyoanza wakati Hamas iliposhambulia Israel tarehe 7 Oktoba 2023. Takriban watu 1,200 waliuawa na 251 kurudishwa Gaza kama mateka.
Zaidi ya Wapalestina 47,200, ambao ni raia wengi zaidi, wameuawa katika mashambulizi ya Israel, wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas inasema.
Hapo awali ilifikiriwa kuwa raia wa kike wa Israel, Arbel Yehud, angejumuishwa katika orodha ya wale watakaotolewa Jumamosi.
Haijulikani ni kwa nini jina lake halimo kwenye orodha hiyo, ingawa vyombo vya habari vya Israel viliripoti kwamba Palestina Islamic Jihad (PIJ), kundi tofauti, linamshikilia.
Hamas inatarajiwa kutoa taarifa kuhusu mateka 26 waliosalia kutokana na kuachiliwa kwa muda wa wiki tano zijazo.
Unaweza pia kusoma:
Habari na wikendi...Karibu katika matangazo haya ya mubashara ya Jumamosi tarehe 25.01.2025 tukikuletea habari za kikanda na kimataifa.

