Marwan Barghouti: Kwanini jina lake linahusishwa na mpango wa amani wa Israel na Hamas?

Marwan Barghouti making a v-for-victory sign

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Marwan Barghouti akiweka alama ya v - kuashiria ushindi huku akisindikizwa na maafisa wa magereza
    • Author, Manar Hafez
    • Nafasi, BBC World Service
    • Akiripoti kutoka, Amman
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Mwanasiasa wa Kipalestina, Marwan Barghouti, kiongozi wa vuguvugu la Fatah ambaye kwa sasa anazuiliwa katika jela ya Israel, ni mhusika mkuu katika makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas.

Katika mpango huo wa amani, Wapalestina kadhaa waliofungwa Israel wataachiliwa huku mateka wa Israel waliopo Gaza, wakiachiliwa vilevile.

Barghouti ni nani na kwa nini kuachiliwa kwake ni muhimu lakini kuna utata?

Marwan Barghouti alianza shughuli zake za kisiasa akiwa na umri wa miaka kumi na tano katika vuguvugu la Fatah, ambalo wakati huo liliongozwa na hayati kiongozi wa Palestina Yasser Arafat.

Alihamasisha vuguvugu la Palestina na suluhisho la serikali mbili. Alipata umashuhuri kama kiongozi wa Intifadha ya pili na amekaa zaidi ya miongo miwili katika jela za Israel.

Barghouti alikamatwa katika Operesheni ya Israel mwaka 2002, wakati Israel ilipomtuhumu kuanzisha kikosi cha Al-Aqsa Martyrs, tuhuma ambayo Barghouti amezikanusha.

Kikosi hicho kilifanya msururu wa mashambulizi mabaya, ambayo yaliua wanajeshi wa Israel, walowezi na raia.

Mwaka 2004, Barghouti alihukumiwa kifungo cha maisha jela, pamoja na kifungo cha miaka 40 jela, kwa kuhusika kwake katika mashambulizi hayo.

Kiongozi huyo wa Palestina alikataa kutambua mamlaka ya mahakama ya Israel wakati wa kesi yake, na akakataa mashitaka dhidi yake.

Mkewe aitwaye Fadwa, mwanasheria wa Palestina, aliiambia BBC mwaka jana, mumewe "hakushtakiwa kwa sababu alifanya vitendo hivyo kwa mikono yake mwenyewe, lakini kwa sababu alikuwa kiongozi," lakini Barghouti alikanusha shtaka la "kuanzisha kikosi cha hicho" wakati wa upelelezi.

Kuhukumiwa kwa Barghouti kulilifanya jina lake kuwa maarufu - Wapalestina wengi wanamwona kuwa Nelson Mandela wao - na anachukuliwa kuwa mrithi wa Mahmoud Abbas kama Rais wa Mamlaka ya Palestina.

Lakini hilo linaweza kutimia tu ikiwa ataachiliwa kutoka jela ya Israel.

Uwezekano wa kuhamishwa

The late Palestinian leader Yasser Arafat holds a picture of Marwan Barghouti, with the words “Freedom for Marwan Barghouti” written on it in English, and behind him is a picture of the Dome of the Rock.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hayati kiongozi wa Palestina Yasser Arafat akiwa ameshikilia picha ya Marwan Barghouti
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baadhi ya ripoti za vyombo vya habari vya Israel zinasema Israel inaweza kumwachilia huru Barghouti - ambaye Wapalestina wengi wanamwona kama mrithi wa Mahmoud Abbas kama rais wa Palestina - kwa masharti kwamba "ataondoka kwenye ardhi ya Palestina."

Anis Al Qassem, mtaalamu wa sheria za kimataifa, anasema, ikiwa Barghouti ataondolewa katika ardhi ya Palestina, basi kinadharia hakuna kinachomzuia kutwaa urais wa serikali ya Palestina kutoka nje ya nchi. Iliwahi kuwepo serikali ya uhamishoni, wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, na sheria hazizuii hilo.

Al Qassem anasema, Israel inaweza kumfukuza Barghouti kutokana na umaarufu wake kama kiongozi wa Palestina, haswa kutoka vuguvugu la Fatah."

Kituo cha Palestina cha Utafiti wa Sera, ambacho kwa kiasi fulani kinafadhiliwa na Umoja wa Ulaya, kilichapisha kura ya maoni tarehe 13 Desemba 2023, ambayo ilionyesha kuwa Marwan Barghouti ni chaguo lipendwalo kwa urais wa Palestina.

Kura ya maoni ilionyesha ikiwa uchaguzi mpya wa rais ungefanyika wakati huo huku Barghouti wa Fatah, Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas na kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh (kabla ya kuuawa kwake Tehran Julai 2024) kama wagombea, kura hiyo ingesababisha "Barghouti kupata 47%, Haniyeh akipata 43% na Abbas akipata 7%.

Barghouti alitarajiwa kugombea katika uchaguzi wa urais wa Julai 2021, ambao ulifutwa na Abbas, ambaye alitaja sababu ni kukataa Israel kuiruhusu Jerusalem Mashariki kushiriki.

Barghouti ana misimamo gani?

Barghouti anaunga mkono amani kati ya Palestina na Israel na uwepo wa suluhisho la serikali mbili kwa kuzingatia mipaka ya kabla ya 1967.

Aliandika makala katika gazeti la Washington Post mwaka 2002 akisema, "Wakati mimi na vuguvugu la Fatah, ambalo mimi ni mwanachama, tunapinga vikali mashambulizi ya kulenga raia ndani ya Israel, jirani yetu wa baadaye, nina haki ya kujilinda, kuipinga Israel kuikalia kwa mabavu nchi yangu, na kupigania uhuru wangu."

Aliendelea kusema, "Nataka tuishi pamoja kwa amani kati ya mataifa mawili yaliyo sawa na huru Israel na Palestina, kwa msingi wa Israel kujiondoa katika maeneo ya Palestina yaliyokaliwa kwa mabavu mwaka 1967."

Barghouti, ambaye amefungwa na Israel tangu 2002, anaweza kuwa chaguo bora kuchukua mamlaka ya Palestina na kujiandaa kwa uwezekano wa taifa la Palestina.

Ingawa Waisraeli wengi wanakataa wazo la kumwachilia huru kwa sababu amepatikana na hatia katika mauaji," wengine wanaamini kuachiliwa kwake itakuwa njia ya kufikia makubaliano kati ya Wapalestina, kuunganisha pande zinazohasimiana na kutoa matumaini ya amani kwa Wapalestina.

Mwandishi wa Israel, Gershon Baskin aliandika katika gazeti la Haaretz Januari 2024, kipindi cha mpito baada ya vita vya Gaza kinahitaji "kiongozi wa Palestina mwenye uwezo wa kuimarisha umoja wa Wapalestina na kuondoa silaha katika eneo hilo. Kiongozi huyu anaweza kuwa Barghouti."

Historia ya Barghouti

A photo of Marwan Barghouti on the separation wall built by Israel in the occupied West Bank - photo taken on 24 December 2024.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Picha ya Marwan Barghouti kwenye ukuta uliojengwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi - picha iliyopigwa tarehe 24 Desemba 2024.

Barghouti alizaliwa mwaka 1958 katika kijiji cha Kobar, karibu na mji wa Ramallah. Alikuwa na umri wa miaka tisa wakati Israel ilipoteka Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki wakati wa vita vya Mashariki ya Kati vya 1967.

Akiwa na umri wa miaka 15, alijishughulisha na harakati za Fatah za marehemu Yasser Arafat. Mwaka 1978, alikamatwa na kufungwa na Israel kwa zaidi ya miaka minne kwa tuhuma za kuwa mwanachama wa kundi la Wapalestina lenye silaha.

Barghouti alimaliza elimu yake ya sekondari na kujifunza Kiebrania akiwa jela, na baada ya kuachiliwa mwaka 1983, alianza kusoma shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Birzeit.

Ilimchukua miaka mingine 11 kumaliza masomo yake, hata hivyo, alibaki shupavu kisiasa na kuwa mwanachama maarufu miongoni mwa vijana wa Fatah, wakati ambao watu mashuhuri wa vuguvugu, akiwemo Arafat na Abbas, walipokuwa uhamishoni Lebanon na Tunisia. .

Kisha, mwaka 1987, Wapalestina walianza uasi dhidi ya uvamizi wa Israel, katika kile kilichojulikana kuwa Intifadha ya kwanza. Barghouti aliibuka kama kiongozi katika Ukingo wa Magharibi, na baadaye alifukuzwa kupelekwa Jordan, na kurejea mwaka 1994 kufuatia makubaliano ya amani ya Oslo.

Aliunga mkono kwa dhati mchakato wa amani, lakini alikuwa na mashaka juu ya utayari wa Israel wa kuondoka katika ardhi ya Palestina kwa ajili ya amani.

Kufikia wakati wa Intifadha ya pili Septemba 2000, Barghouti alikuwa kiongozi wa Fatah katika Ukingo wa Magharibi na mkuu wa tawi lake la kijeshi, Tanzim.

Alinusurika katika jaribio la mauaji la Israel mwaka 2001, pale gari la mlinzi wake lilipopigwa na kombora.

Barghouti ana mtoto mmoja wa kike na watoto watatu wa kiume, na ni mume wa wakili na mwanaharakati wa kisiasa Fadwa.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah