Auawa na kundi la watu kwa kuchoma Quran

Mtu mmoja ameuawa na kundi la watu kwa madai ya kuchoma kurasa za Koran katikati mwa Pakistan, Khanewal, polisi wanasema, katika tukio la hivi karibuni la vurugu zinazohusiana na kukufuru ama kukashifu dini nchini humo.

Moja kwa moja

  1. Mpaka hapa tumefika mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja ya ukurasa wetu wa BBC Swahili, tukutane tena kesho...Asante!

  2. 'Sijaja na malori kuwahamisha wakazi wa Ngorongoro' asema Waziri Mkuu Tanzania

    ngoro

    Waziri mkuu wa nchini Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaangalia utaratibu utakaofaa kuhusu suala la uhifadhi katika eneo la Loliondo lililopo kwenye wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.

    Mkutano wa waziri mkuu na viongozi wa Ngorongoro na wadau wa hifadhi umekuja baada ya jamii ya kimaasai kulalamikia hatua ya serikali kudaiwa kutaka kuwaondoa ndani ya hifadhi hiyo ambayo wamekuwa wakiishi kwa miaka mingi bila kuwa na madhara kwa wanyama waliomo humo.

    "Katika mjadala wetu wa leo, mmetoa maoni nasi tumeyapokea. Bado Serikali inayaangalia maslahi mapana ya umma. Tutawashirikisha pia ni lipi lina maslahi mapana kwa Watanzania,"Waziri mkuu amesema.

    Aidha aliongeza kusema "Sikuja na malori kuwachukua sijui muende wapi huko, naomba sana kwenye mijadala ya namna hii muwe makini maana kuna watu wananufaika kwa kuwa kila mmoja ana mfumo wake wa kuishi, wanaweza kutumia mijadala hii kutuchonganisha tu ila nnawahakikishia kuwa serikali yenu iko makini na rais yuko makini, na tumehaidi kuwatumikia" waziri mkuu alisema.

    Pia bwana Majaliwa amesema alichoenda kufanya leo ni utekelezaji wa ushauri uliotolewa na wabunge kwa Serikali kupitia Mwenyekiti wa Kamati wa Maliasili na Utalii iliyoielekeza Serikali iende katika maeneo ya Loliondo, Ngorongoro na Sale na kuzungumza na wananchi.

    Waziri Mkuu amesema wote tunatambua kuwa idadi ya watu na mifugo imeongezeka ndani ya hifadhi ambapo tusipotafuta suluhisho la kudumu hifadhi zetu zitaathirika. “Sisi sote tunatambua eneo hili ni la utalii, lazima tufike mahali tuamue kama tunataka utalii au la," amesema.

    Vilevile Waziri Mkuu amesema amefarijika kusikia kwamba wachangiaji wote waliozungumza hakuna aliyesema ardhi ni yao. "Kati ya mambo yamenifariji, sijasikia mtu akisema ardhi yetu, ardhi yetu. Sote tunatambua kuwa ardhi iliyo ndani ya mipaka ya nchi hii ni ya umma lakini tumeikasimu kwa Rais kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."

  3. Halima Mdee na wabunge wengine 18 wa Chadema wasubiri mchakato wa chama chao kusalia bungeni

    m

    Siku chache baada ya Spika mpya wa Bunge la Tanzania kuanza kazi, Dk Tulia Ackson ametolea ufafanuzi juu ya uhalali wa wabunge 19 wa viti Maalum wa chama cha upinzani cha Chadema ambao waliondolewa katika chama chao.

    Dk.Tulia ametoa ufafanuzi juu ya hilo leo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma.

    Amesema uhalali wa mbunge nchini Tanzania unafuata sheria, ili mtu uwe mbunge lazima uwe umetoka katika chama fulani.

    Hivyo kwa upande wa wabunge hao ni sahihi kuwepo bungeni kwa sasa mpaka michakato halali ndani ya chama chao ikithibitisha basi uamuzi utatekelezwa kulingana na katiba.

    Mwishoni mwa mwa mwaka jana, wabunge hao 19 viti maalum waliovuliwa uanachama wa chama chao, na walisema wataendelea kuwa 'wanachama wa hiari' wa chama hicho huku wakipanga kukata rufaa juu ya adhabu walopewa.

    • Halima Mdee: Hatuondoki Chadema, tunakata rufaa
    • Athari za kuwafukuza wanachama 19 wa Chadema
  4. Mwalimu akamatwa kwa madai ya kumpiga mtoto viboko hadi kufa

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwalimu wa shule amekamatwa nchini Nigeria kwa madai ya kumpiga mwanafunzi wa miezi 19 hadi kufa, polisi wanasema.

    Mwalimu huyo katika shule ya msingi ya Asaba, jimbo la Delta, alidaiwa kuacha alama nyingi kwenye mwili wa mtoto huyo baada ya kumchapa viboko Jumatatu iliyopita.

    Mshukiwa huyo anayedhaniwa kuwa mtoto wa mmiliki wa shule hiyo ya kibinafsi, anadaiwa kuanza kumpiga mwanafunzi huyo baada ya kumshika akicheza na maji.

    Hajaripotiwa kuzungumzia tukio hilo.

    Mwanafunzi huyo alisemekana kuugua baada ya tukio hilo na alipelekwa katika Kituo cha Afya cha Shirikisho (FMC) huko Asaba ambapo hatimaye alifariki.

    Msemaji wa polisi DSP Dafe Bright aliambia BBC Pidgin kwamba mshukiwa atashtakiwa kwa mauaji bila kukusudia.

  5. Wanajeshi wa Mali wauawa na wapiganaji wa jihadi

    Mali imekuwa ikijitahidi kuzuia waasi wa jihadi

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Mali imekuwa ikijitahidi kuzuia waasi wa jihadi

    Wanajeshi wawili wa Mali wameuawa katika shambulizi linalodaiwa kufanywa na wapiganaji wa jihadi.

    Shambulio hilo limetokea kwenye kituo cha Niafunké katikati mwa Mali Jumapili asubuhi.

    Watano kati ya wanamgambo hao wameuawa wakati wa shambulio hilo.

    Jeshi la Mali, ambalo limekuwa likihangaika kuwadhibiti waasi wa kijihadi, limekuwa likiendesha operesheni ya kuharibu kambi za wanajihadi.

    Rais wa zamani Ibrahim Boubacar Keita alitimuliwa na jeshi mnamo mwaka 2020 baada ya kushutumiwa kwa kushindwa katika vita dhidi ya uasi.

  6. Msumbiji yaondoa kitabu cha kusoma chenye mada za ngono

    Kitabu hiki cha sayansi kimepewa jina la ‘The Secret of Life’
    Maelezo ya picha, Kitabu hiki cha sayansi kimepewa jina la ‘The Secret of Life’

    Msumbiji inaondoa katika mtaala wake wa elimu kitabu kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la saba wenye umri wa miaka 12 chenye baadhi ya masomo yenye utata kuhusu ngono.

    Kitabu hicho cha sayansi kinazungumzia masuala kama vile kupiga punyeto na mvuto wa hisia za mapenzi.

    Wizara ya elimu inasema kitabu hicho kimekuwa kikitumika tangu mwaka 2004 lakini mada hizi "zinazozua utata katika jamii" hazitafundishwa tena.

    Kufundisha masuala ya kujamiiana kwa vijana katika baadhi ya jamii nchini Msumbiji huchukuliwa kuwa ni mwiko.

    Wengine pia wanaamini kuwa elimu ya ngono kwa watoto katika kundi hili inaweza kuendeleza ndoa za mapema na mimba za utotoni.

    Kitabu hicho kitabadilishwa mwaka ujao lakini wizara ya elimu imezitaka shule "kutozungumzia masuala haya".

    "Tulizungumza na mchapishaji ili kuondoa ukurasa huo", alisema Ismael Nheze, mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Maendeleo ya Elimu.

    Wizara ya elimu imemtaka mchapishaji kuondoa ukurasa huu
    Maelezo ya picha, Wizara ya elimu imemtaka mchapishaji kuondoa ukurasa huu
  7. Kenya yakumbwa na uhaba mkubwa wa kondomu

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kuna uhaba mkubwa wa upatikanaji wa kondomu nchini Kenya, hivyo kuwaweka wananchi katika hatari ya kuambukizwa VVU/UKIMWI, mimba zisizotarajiwa na magonjwa mengine ya zinaa.

    Baraza la Taifa la Kudhibiti Ukimwi (NACC) limesema mahitaji ya kondomu nchini yanafikia milioni 480 kila mwaka huku akiba ya sasa ikiwa ni milioni 79 pekee.

    Akizungumza wakati wa kuadhimisha Siku ya Kondomu Duniani katika Chuo Kikuu cha Kenya Coast Polytechnic mjini Mombasa jana, Mratibu wa NACC Kanda ya Pwani Omar Mwanjama alisema nchi inakabiliwa na upungufu wa kondomu milioni 401, hatua ambayo imeathiri ugavi wa bure wa bidhaa hiyo kwa watu wanaolengwa.

    “Nchi inajitahidi katika kushughulikia upatikanaji wa chini ikilinganishwa na mahitaji.”

    Uhaba huo ni wa kweli na unahitaji kutatuliwa kwani unaweza kupunguza kasi ya mafanikio katika mapambano dhidi ya Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa,” alisema Mwanjama.

    Uhaba huo umeilazimu NACC kuzingatia tu wale wanaohitaji sana bidhaa hiyo inayotolewa bure na serikali.

    “Hali imetulazimisha kuzingatia wale tu wenye uhitaji mkubwa, jambo ambalo limezua malalamiko.

    Mahitaji yanaonyesha kuwa idadi kubwa ya watu inategemea kondomu za serikali,” aliongeza Mwanjama.

  8. Hoteli ya kwanza ya wapenzi wa jinsia moja yafunguliwa Cuba

    Wacheza densi hutumbuiza na bendera za upinde wa mvua katika Hoteli inayofafanuliwa kuwa ya kwanza ya Cuba ya LGBTQ

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Wacheza densi hutumbuiza na bendera za upinde wa mvua katika Hoteli inayofafanuliwa kuwa ya kwanza ya Cuba ya LGBTQ

    Waandishi wa habari walipowasili kwa ziara iliyoandaliwa na serikali katika hoteli ya kifahari katika eneo la mapumziko la Cuba la Cayo Guillermo, walilakiwa na kikundi cha densi kilichovalia nguo za kubana umbo la samaki na viatu virefu.

    Juu ya mlango huo, bendera ya upinde wa mvua, ishara ya kimataifa ya wapenzi wa jinsia moja, ilipepea upepo mwanana wa Caribbean.

    Hoteli ya Rainbow, iliyofafanuliwa kuwa hoteli ya kwanza ya LGBTQ ya Cuba, ilifunguliwa tena mnamo Desemba.

    Wakati wageni walifurahia huduma ya nyota tano karibu na bwawa au kutembea kwenye mchanga safi, Cuba haijakuwa ikikaribisha watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.

    Katika utawala wa awali wa kiongozi wa kikomunisti Fidel Castro, wanaume na wanawake wa jinsia moja walipelekwa kwenye kambi za kazi kwa ajili ya " elimu upya."

    Serikali ya Cuba na kampuni iliyo nyuma ya Hoteli hiyo, wanasema inaonesha mabadiliko.

    Ubia kati ya Muthu Hotels na Gaviota, kampuni ya utalii inayoendeshwa na jeshi la Cuba, Hoteli hiyo iliwekwa kwenye orodha ya serikali ya Marekani ya mashirika yaliyowekewa vikwazo nchini Cuba hata kabla ya kuzinduliwa mnamo 2019.

  9. Sadio Mane: Uwanja wapewa jina la nyota wa Liverpool Senegal

    Sadio Mane
    Maelezo ya picha, Sadio Mane akiwa na Kombe la Mataifa ya Afrika

    Uwanja umepewa jina la Sadio Mane katika mji wa kusini-magharibi wa Sedhiou baada ya kuisaidia Senegal kupata mafanikio yao ya kwanza.

    Mshambulizi huyo wa Liverpool alifunga penalti ya ushindi wakati Simba ya Teranga ilipoishinda Misri kwa mikwaju 4-2 ya penalti na kutwaa ushindi wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza, baada ya mchezo kumalizika bila bao kufuatia muda wa ziada.

    Mabao yake matatu na pasi mbili murua kwa taifa hilo la Afrika Magharibi yalimpa tuzo ya Mchezaji bora na sasa meya wa Sedhiou, Adboulaye Diop, anasema uwanja wa soka wa eneo hilo utapewa jina la mtoto wao kipenzi.

    "Ningependa, kupitia uamuzi huu wa kutoa jina la Sadio Mané kwa uwanja wa Sédhiou, kuelezea utambuzi wa watoto wote wa mkoa huo, kwa mtu anayejulikana kwa utu wake kwa ujumla, Bambali na mji mkuu wake wa kikanda, ambao ni Sédhiou," Diop, ambaye ni waziri wa utamaduni na mawasiliano wa Senegal, alinukuliwa

    "Sadio Mané anastahili heshima hii."

    "Mane anapendwa na mamilioni ya watu kufuatia misaada anayotoa katika mji wake wa nyumbani kwa kuahidi pesa za kujenga hospitali na shule, kuchangia ujenzi wa misikiti na kutoa pesa kusaidia mapambano dhidi ya Covid-19.

    Kabla ya fainali ya Ligi ya Mabingwa mnamo Mei 2018, aliwazawadia jezi ya Liverpool, wenyeji wa mji aliozaliwa wa Bambali ili waweze kuzivaa wakati wa mchezo.

    “Kijijini wapo 2,000, nilinunua jezi 300 za Liverpool ili niwapelekee wananchi wa kijijini, ili mashabiki wavae kuangalia fainali,” alisema Mane.

    Bambali ni mahali ambapo Mane alitazama urejeo wa umaarufu wa Liverpool dhidi ya AC Milan na kushinda fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2005 - akiwa na umri wa miaka 13.

    Na nyumbani anapotokea hakujawahi kuwa mbali na mawazo yake.

    Kutoka kwa klabu ya Metz ya Ufaransa hadi Liverpool kupitia RB Salzburg ya Austria na Southampton, Mane ametoka mbali hadi kutambuliwa kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani.

    Na baada ya mafanikio ya timu yake nchini Cameroon, Mane alisema kushinda Senegal Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza ni jambo kuu katika maisha yake ya soka.

    Soma zaidi:

  10. Aliyekuwa mjumbe wa baraza tawala la Sudan akamatwa

    Mohamed al-Faki Suleiman

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Mohamed al-Faki Suleiman alichukuliwa karibu na nyumbani, Jamaa wanasema

    Mwanasiasa wa Sudan ambaye alikuwa mwanachama wa serikali iliyovunjwa ya kiraia na kijeshi amekamatwa.

    Jamaa wanasema Mohamed al-Faki Suleiman alichukuliwa karibu na nyumbani kwake katika mji mkuu Khartoum.

    Hii inafuatia kukamatwa kwa wanasiasa wengine wawili wiki jana.

    Walikuwa sehemu ya kikosi kazi kinachojaribu kusambaratisha mtandao ulioanzishwa na rais wa zamani Omar al-Bashir.

    Pia ilikuwa ikijaribu kurejesha pesa na mali zilizoporwa wakati wa utawala wake wa miongo mitatu.

    Sudan iko katikati ya mzozo wa kisiasa na kiuchumi kufuatia mapinduzi ya Oktoba ambayo yalitupilia mbali ratiba ya uchaguzi.

    Tangu mapinduzi kumekuwa na maandamano makubwa dhidi ya jeshi.

    Vikosi vya usalama vimewaua takriban waandamanaji 80.

  11. Auawa na kundi la watu kwa kuchoma Quran

    Jamaa na wenyeji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa mtu kwa ajili ya mazishi yake huko Khanewal siku ya Jumapili.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Jamaa na wenyeji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa mtu kwa ajili ya mazishi yake huko Khanewal siku ya Jumapili.

    Mtu mmoja ameuawa na kundi la watu kwa madai ya kuchoma kurasa za Koran katikati mwa Pakistan, Khanewal, polisi wanasema, katika tukio la hivi karibuni la vurugu zinazohusiana na kukufuru ama kukashifu dini nchini humo.

    Polisi wanasema zaidi ya watu 80 wamekamatwa kuhusiana na mauaji hayo siku ya Jumamosi katika wilaya ya Khanewal katika mkoa wa Punjab.

    Ripoti zinasema kuwa mtu huyo alikuwa chini ya ulinzi wa polisi kabla ya umati wa watu kumteka na kumuua kwa kipigo.

    Mwili wake ulikabidhiwa kwa familia yake na mazishi yaliyofanyika siku ya Jumapili.

    Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan amesema suala hilo "litashughulikiwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria" na kuomba ripoti juu ya maafisa wa polisi wanaotuhumiwa kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kumwokoa mtu huyo.

    Munawar Gujjar, mkuu wa kituo cha polisi mjini Tulamba, ambako tukio hilo lilitokea, aliliambia shirika la habari la AP kwamba mwathiriwa huyo "alikuwa na matatizo ya akili kwa miaka 15 iliyopita".