‘Niligundua kuwa nina saratani ya shingo ya kizazi nikiwa mjamzito’

Dorothy Masasa ni mmoja wa maelfu ya wanawake wanaopatikana na saratani ya shingo ya kizazi kila mwaka nchini Malawi
Maelezo ya picha, Dorothy Masasa ni mmoja wa maelfu ya wanawake wanaopatikana na saratani ya shingo ya uzazi kila mwaka nchini Malawi
    • Author, Ashley Lime
    • Nafasi, BBC News, Thyolo
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Dorothy Masasa anatembea kwa furaha kwenye barabara ya vumbi akiwa amembeba mtoto wake mgongoni.

Miezi sita iliyopita mama huyo mwenye umri wa miaka 39 kutoka wilaya ya Thyolo kusini mwa Malawi, alikuwa nchini Kenya kwa tiba ya mionzi ya kuokoa maisha.

Hivi majuzi Malawi imepokea mashine zake za kwanza kama hizo, kwa hivyo wanawake wengine wenye saratani huenda wasilazimike tena kusafiri nje ya nchi kwa matibabu.

"Nilisajiliwa kama mgonjwa anayehitaji tiba ya dharura baada ya madaktari kugundua nilikuwa na saratani ya shingo ya kizazi nikiwa na ujauzito wa wiki 13. Waliniambia mambo haya mawili hayaendani,” mama huyo wa watoto watatu aliambia BBC.

Anasema madaktari nchini Malawi walimwambia kwamba angeweza kufanyiwa upasuaji wa kuondoa saratani hiyo lakini hii ingemaliza ujauzito, au angeweza kupata tiba ya kemikali lakini hii ingehatarisha mtoto kuzaliwa na ulemavu.

Alichagua matibabu ya kemikali hadi mtoto alipozaliwa kupitia upasuaji - bila ulemavu wowote.

Kizazi chake kilitolewa katika operesheni hiyo.

Kabla ya utambuzi huo, Bi Masasa alipata uvimbe kwenye sehemu ya chini ya fumbatio lake, akivuja damu na kutokwa na uchafu ukeni ambao mara kwa mara. Mwanzoni, madaktari walidhani ni ugonjwa wa zinaa.

Lakini licha ya matibabu ya kemikali na upasuaji, bado alihitaji matibabu zaidi kuponya saratani hiyo - matibabu ambayo yalikuwa hayapatikani nchini Malawi hadi mapema mwaka huu.

Alijiunga na kundi la wanawake 30 ambao walipelekwa katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya na shirika la misaada la Médecins Sans Frontières (MSF) kufanyiwa tiba ya mionzi ili kuua seli hizo za saratani.

Hii ilikuwa mara yake ya kwanza kusafiri kwa ndege hivyo alikuwa na wasiwasi sana na pia kusita kumwacha mtoto wake mchanga.

"Lakini kwa sababu nilikuwa nikienda huko kwa matibabu, nilijipa moyo kwamba naenda kupata matibabu na nitarudi nyumbani nikiwa mzima na mwenye furaha."

BBC ilipomtembelea hospitalini, Bi Masasa alikuwa bado mdhaifu kutokana na athari za tiba ya ionzi.

Yeye ni mmoja wa wagonjwa 77 waliosafirishwa kwa ndege kutoka Malawi hadi Kenya kwa matibabu ya saratani ya shingo ya uzazi tangu 2022.

Soma pia:

Miaka 60 baada ya kupata uhuru wake kutoka kwa Uingereza, Malawi ilikuwa na mashine yake ya kwanza ya tiba ya mionzi, katika Kituo cha Kimataifa cha Saratani cha Blantyre kinachomilikiwa na mtu binafsi, mwezi Machi mwaka huu, hatua inayoashiria hatua iliyopigwa katika mfumo wa afya wa nchi hiyo.

Mashine zaidi ziliwasili mwezi Juni na zinapaswa kuwekwa katika Kituo cha Kitaifa cha Saratani ambacho bado kinajengwa katika mji mkuu, Lilongwe.

Ingawa Malawi bado ina safari ndefu kuelekea upatikanaji wa matibabu ya kina ya saratani, iko mbele ya ikilinganishwa na nchi zingine kadhaa.

Barani Afrika katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa zaidi ya nchi 20 hazina uwezo wa kupata tiba ya mionzi, ambayo ni muhimu katika kupambana na saratani.

Hii inamaanisha wagonjwa wanalazimika kufanya safari za gharama kubwa na za kuchosha kutafuta matibabu.

Malawi imenunua machine yake ya kwanza ya tiba ya ionzi mwezi Machi
Maelezo ya picha, Malawi imenunua machine yake ya kwanza ya tiba ya ionzi mwezi Machi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Saratani ya shingo ya kizazi ni saratani ya nne inayowaathiri wanawake duniani kote, na inakadiriwa kuwa wagonjwa wapya 660,000 na vifo 350,000 viliripotiwa mnamo 2022, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Nchi zote isipokuwa moja kati ya 20 zilizo na viwango vya juu vya saratani ya shingo ya kizazi mnamo 2018 zilikuwa barani Afrika, kulingana na Shirika la Afya Duniani.

Hii inatokana na kukosekana kwa chanjo ya kuzuia virusi vya papillomavirus ya binadamu (HPV), uchunguzi na matibabu ya kutosha, ikimaanisha kuwa wanawake wengi hutibiwa wakiwa wamechelewa.

Hospitali ya Queen Elizabeth Central (QECH), kituo kikuu cha matibabu nchini Malawi na kikubwa zaidi kinachomilikiwa na serikali, hupokea idadi kubwa ya wagonjwa wa saratani ya shingo ya wa kizazi kutoka kote nchini.

Daktari wa magonjwa ya uzazi katika hospitali hiyo, Dk Samuel Meja, anasema saratani ya shingo ya kizazi ni tatizo kubwa kwa nchi nyingi za ukanda huu.

“Upatikanaji duni wa uchunguzi, na janga la VVU, ambalo limekuwa likiharibu maeneo mengi ya Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa, kumezidisha hali hiyo,” anasema.

Mnamo mwaka wa 2018, Malawi ilikuwa ya pili kwa Eswatini kusini mwa Afrika, ambayo ilikuwa na kiwango cha juu zaidi cha saratani ya mlango wa kizazi ulimwenguni.

xx

Mkurugenzi anayeondoka wa WHO kanda ya Afrika, Dk Matshidiso Moeti, anasema kuwa duniani kote mwanamke hufariki kwa saratani ya mlango wa kizazi kila baada ya dakika mbili. Afrika inachangia asilimia 23 ya vifo.

Ili kubadilisha takwimu hizi za kutisha, Afrika imeshuhudia kampeni kubwa za kuwachanja wasichana dhidi ya HPV inayosababisha saratani ya shingo ya kizazi.

Lesotho imefikia kiwango cha kipekee cha 93% baada ya kuchanja wasichana 139,000 dhidi ya HPV.

Lakini unyanyapaa unaozunguka saratani ya mlango wa kizazi katika nchi mbalimbali za Afrika umeathiri idadi ya watu wanaopata chanjo.

Nchini Zambia, kwa mfano, kuzungumza juu ya jambo lolote la uzazi halifai.

xx

Nchini Malawi, Dk Meja anasema uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi umeanzishwa.

“Huu ni mkakati rahisi sana unaowatambua wanawake walio katika hatari na unawatibu kabla ya kuwa wagonjwa wa saratani. Uwekezaji huu ndio tunaopaswa kuufanya kama taifa kabla haujatoka nje ya mkono,” anasema.

Kuhusu Bi Masasa, sasa amerejea nyumbani kwao Malawi.

Matibabu aliyopokea nchini Kenya yamempa raha mpya ya maisha. Nywele zake zimekua, anaweza kutembea na mtoto wake mgongoni, kuchunga ng'ombe wake, na kufanya kazi shambani.

Anasema kwa sasa anajua saratani ya shingo ya kizazi inaweza kutibika na chanjo hiyo inaweza kuwasaidia wanawake wengine kuepukana na ugonjwa huo hivyo hana shaka na kumchanja bintiye.

"Saratani ya shingo ya kizazi imenipitisha katika kipindi kigumu na singependa binti yangu apitie hali hiyo," anasema.

“Kuna tofauti kubwa kati ya jinsi nilivyokuwa wakati huo na jinsi nilivyo sasa. Nashkuru nimepona.”

Maelezo zaidi:

Imetafsiri na Ambia Hirsi