Uchaguzi wa Kenya 2022: Je fomu 34A na 34B ni zipi?

Chini ya sheria ya uchaguzi, fomu 34A ndio fomu ya kwanza inayotumika kunakili matokeo ya uchaguzi wa urais
Maelezo ya picha, Chini ya sheria ya uchaguzi, fomu 34A ndio fomu ya kwanza inayotumika kunakili matokeo ya uchaguzi wa urais
    • Author, Ambia Hirsi
    • Nafasi, BBC Swahili

Ni kijitabu cha kwanza pekee cha Fomu 34-A ndicho kitatumika katika upeperushaji wa matokeo ya uchaguzi wa urais, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati amesema.

Akizungumza na wawakilishi wa wagombea wa urais hivi karibuni, Bw Chebukati alikubali kuwa maswali kadhaa yameibuliwa na wawakilishi hao kuhusu uchaguzi mkuu ujao na kuongeza kuwa tume yake itachapisha nakata ya maswali na majibu kaika magazeti nchini ili kuangazia masuala ibuka.

"Tume imechapisha vijitabu viwili vya [fomu 34A]. Sababu iliyotolewa ni kwamba [kijitabu kimoja] hakiwezi kuwa na zaidi ya nakala sita za karatasi za kaboni. Tutatumia kijitabu kimoja pekee kwa madhumuni ya kusambaza matokeo ya urais," Bw Chebukati alisema.

"Kijitabu cha pili kitafungwa na kitawekwa kwenye sanduku la kura na kufungiwa pamoja na kura baada ya kupiga kura. Kijitabu cha pili hakitatumiwa." aliongeza Chebukati.

Bw. Chebukati pia alifafanua kuwa karatasi halisi ya nakala sita za fomu 34A zitaletwa katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura, nakala nne zitapewa "wagombea wanne wa urais na na moja itawekwa ndani ya sanduku ya kupigia kura. Msimamizi wa uchaguzi atafanya mipango ya kutengeneza nakala ya nakala halisi ili kubandikwa kwenye ukuta wa kituo cha kupigia kura."

Fomu 34B, kwa upande mwingine, itashughulikiwa katika ngazi ya eneo bunge.

Je hizi ni fomu gani?

Chini ya sheria ya uchaguzi, fomu 34A ndio fomu ya kwanza inayotumika kunakili matokeo ya uchaguzi wa urais.

Fomu hiyo hujazwa na afisa wa Tume ye uchaguzi anayesimamia uchaguzi huo kwa jina la Presiding officer baada ya kuhesabiwa kwa kura katika kituo cha kupigia kura.

Fomu hiyo huwa na maelezo kuhusu kura zilizohesabiwa za kila mgombea mbali na kuwa na idadi ya wapiga kura katika kituo hicho, kura zilizoharibika, zile zilizo na utata na kura zilizokubalika.

Mgombea ama ajenti wake baadaye hutakiwa kutia saini ili kuthibitisha kwamba yaliomo ndani ya fomu hiyo ni sahihi.

Nani yuko kwenye kinyang'anyiro cha kuiongoza Kenya ?

Fahamu zaidi kuwahusu wagombea urais wa Kenya

Chagua mgombea ili kutazama wasifu wake

Raila Amollo Odinga

Muungano wa Azimio la Umoja

  • Mgombea huyo mwenye umri wa miaka 77 ni mhandisi aliyesomea Chuo Kikuu cha Ufundi cha Magdeburg (sasa kinajulikana kama Chuo Kikuu cha Otto-von-Guericke Magdeburg) nchini Ujerumani.
  • Anawania kiti cha urais kwa tikiti ya Azimio la Umoja One Kenya Coalition Party.
  • Hili litakuwa jaribio lake la tano baada ya kugombea katika: 1997, 2007, 2013 na 2017.
  • Bw Odinga alikuwa mmoja wa wapiganiaji wa demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya. Alikamatwa, akafungwa na wakati fulani akaenda uhamishoni kwa sababu ya kupigania haki hiyo
  • Aliwahi kuwa Waziri Mkuu, kuanzia 2008-2013.
  • Odinga alihusika kufanikisha miradi mikubwa iliyotekelezwa na serikali ya Kibaki, kama vile miradi ya umeme vijijini na barabara.
  • Kuafikia ukuaji wa uchumi wa tarakimu mbili kupitia uwekezaji katika biashara ndogo ndogo na sekta ya viwanda.
  • Utoaji wa huduma bora za afya kwa wote.
  • Utoaji wa vifaa vya michezo na burudani kwa ukuaji wa kimwili, kiakili, kijamii, kimaadili na maendeleo ya watu.
  • Kufuatia jaribio la mapinduzi ya Agosti 1, 1982, Raila Odinga alikamatwa na kukabiliwa na mashtaka kadhaa, yakiwemo ya uhaini ambayo alizuiliwa bila kufunguliwa mashtaka. Tume ya Ukweli ya Haki na Maridhiano iliambiwa mwaka 2011 kwamba Odinga alikuwa na mawasiliano na mpangaji mkuu wa mapinduzi hayo. Odinga amekana kuhusika kila mara. - Makavazi ya Kitaifa ya Kenya.

William Samoei Ruto

Muungano wa Kenya Kwanza

  • Mgombea huyu mwenye umri wa miaka 55 ana Shahada ya Uzamifu/PhD katika Ikolojia ya Mimea na BSc katika Botany na Zoology kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.
  • Anawania kiti cha urais kwa tikiti ya chama cha United Democratic Alliance ( chenye mafungamano na Kenya Kwanza).
  • Aliongoza Vuguvugu la vijana la Youth for Kanu '92 (YK'(92).
  • Wizara yake iliorodheshwa kama inayofanya bora zaidi serikalini alipokuwa Waziri wa Kilimo.
  • Alihudumu kama Naibu Rais wa kwanza wa Kenya chini ya katiba mpya ya 2010.
  • Alihudumu kama mbunge wa eneo bunge la Eldoret Kaskazini kuanzia 1997-2007.
  • Kutenga $424 milioni kila mwaka kwa biashara ndogo ndogo za kati.
  • Kuanzisha mfuko wa elimu wa kitaifa ili kukidhi gharama zisizo za masomo.
  • Tekeleza kikamilifu sheria ya usawa wa kijinsia ya thuluthi mbili katika uteuzi wa kisiasa na kutenga nusu ya baraza lake la mawaziri kwa wanawake.
  • Mnamo 2008, Mahakama Kuu ya Kenya iliamuru Naibu Rais William Ruto kusalimisha shamba la ekari 100 na kulipa $ 62,500 kwa Adrian Muteshi, mkulima ambaye alimshtaki kwa kuchukua mali hiyo baada ya uchaguzi wa 2007. - Kenya Law
  • Mnamo 2011, Bw Ruto alikabiliwa na kesi kwa makosa matatu dhidi ya binadamu: Mauaji, uhamisho wa watu kwa lazima na mateso ya watu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. Miaka mitano baadaye mahakama ilisitisha kesi hiyo kwa msingi kwamba - ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa dhaifu. -ICC

George Wajackoyah

Chama cha Roots

  • Profesa huyo mwenye umri wa miaka 61 ana shahada ya uzamili katika sheria kuhusu maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Warwick na shahada ya uzamili , sheria (sheria za Marekani kutoka Chuo Kikuu cha Baltimore.
  • Bw Wajackoyah anawania kiti cha urais kwa tiketi ya Chama cha Roots Party.
  • Alihudumu kama Inspekta katika idara ya usalama ya Special branch wakati wa utawala wa marehemu Rais Daniel Moi kabla ya kulazimika kutorokea ng'ambo ili kuepuka kufunguliwa mashtaka na mamlaka.
  • Yeye ni mshirika katika kampuni ya mawakili aliyoianzisha mwaka wa 2018.
  • Alifunnza somo la sheria na uchumi katika vyuo vikuu vya Marekani, Uingereza na Kenya.
  • Kuhalalisha matumizi ya kiviwanda ya bangi
  • Badilisha siku za kazi hadi Jumatatu hadi Alhamisi.
  • Huduma ya afya ya bure na msaada kwa wazee, walio hatarini na wajawazito

David Mwaure Waihiga

Chama cha Agano

  • David Mwaure anawania kiti cha urais kwa tiketi ya Chama cha Agano.
  • Ni kiongozi wa Chama cha Agano.
  • Alihitimu na shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na ana Shahada ya Uzamili katika masomo ya uongozi.
  • Yeye ni wakili mkuu na amehudumu kama mwanasheria kwa zaidi ya miongo mitatu.
  • Ana kampuni ya uwakili na amewania viti mbalimbali vya kisiasa.
  • Ilianzishwa chama cha Agano mwaka 2006.
  • Kupambana na ufisadi uliokithiri.
  • kuunda nafasi za ajira.
  • Kurejesha mali ya Kenya iliyofichwa nje ya nchi.

Pata maelezo zaidi kuhusu sera za wagombea urais hapa

Kifungu cha 39 cha uchaguzi kinasema kuwa ili kufanyika kwa uchaguzi wa urais tume ya uchaguzi itatoa matokeo hayo kielektroniki baadaye kuyasafirisha kutoka katika kituo cha kupigia kura hadi katika kituo cha kuhesabia kura cha eneo bunge na baadaye katika kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura.

Form 34A hupewa afisa anayesimamia uchaguzi katika eneo bunge ambaye hujaza fomu 34B.

Hutumika kuonyesha matokeo ya kura ya urais.

Fomu hiyo huonyesha nambari ya kituo cha kupigia kura, jina la kituo cha kupigia kura, idadi ya watu waliojisajiliwa kupiga kura katika kituo hicho, matokeo ya kila mgombea na idadi ya kura zilizokubalika.

Afisa anayesimamia shughuli ya uchaguzi katika eneo bunge kwa jina Returning officer humpelekea fomu hiyo mwenyekiti wa tume ya auchaguzi IEBC ambaye ndio afisa mkuu wa matokeo ya uchaguzi wa urais.

Uchaguzi wa Kenya 2022: Vyama vinakuahidi nini?

Chagua suala ambalo linakuvutia

Sera za kila chama

  • Azimio La Umoja One Kenya Coalition

  • Roots Party of Kenya

  • Chama cha Agano

  • Kenya Kwanza Alliance

Mwongozo huu ni muhtasari wa sera kuu zinazotolewa na kila chama.

Pata maelezo zaidi kuhusu wagombea urais wa Kenya hapa

End of Uchaguzi wa Kenya 2022: Vyama vinakuahidi nini?
th

Pia unaweza pia kusoma

th