Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi wa Kenya 2022: Je fomu 34A na 34B ni zipi?
- Author, Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili
Ni kijitabu cha kwanza pekee cha Fomu 34-A ndicho kitatumika katika upeperushaji wa matokeo ya uchaguzi wa urais, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati amesema.
Akizungumza na wawakilishi wa wagombea wa urais hivi karibuni, Bw Chebukati alikubali kuwa maswali kadhaa yameibuliwa na wawakilishi hao kuhusu uchaguzi mkuu ujao na kuongeza kuwa tume yake itachapisha nakata ya maswali na majibu kaika magazeti nchini ili kuangazia masuala ibuka.
"Tume imechapisha vijitabu viwili vya [fomu 34A]. Sababu iliyotolewa ni kwamba [kijitabu kimoja] hakiwezi kuwa na zaidi ya nakala sita za karatasi za kaboni. Tutatumia kijitabu kimoja pekee kwa madhumuni ya kusambaza matokeo ya urais," Bw Chebukati alisema.
"Kijitabu cha pili kitafungwa na kitawekwa kwenye sanduku la kura na kufungiwa pamoja na kura baada ya kupiga kura. Kijitabu cha pili hakitatumiwa." aliongeza Chebukati.
Bw. Chebukati pia alifafanua kuwa karatasi halisi ya nakala sita za fomu 34A zitaletwa katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura, nakala nne zitapewa "wagombea wanne wa urais na na moja itawekwa ndani ya sanduku ya kupigia kura. Msimamizi wa uchaguzi atafanya mipango ya kutengeneza nakala ya nakala halisi ili kubandikwa kwenye ukuta wa kituo cha kupigia kura."
Fomu 34B, kwa upande mwingine, itashughulikiwa katika ngazi ya eneo bunge.
Je hizi ni fomu gani?
Chini ya sheria ya uchaguzi, fomu 34A ndio fomu ya kwanza inayotumika kunakili matokeo ya uchaguzi wa urais.
Fomu hiyo hujazwa na afisa wa Tume ye uchaguzi anayesimamia uchaguzi huo kwa jina la Presiding officer baada ya kuhesabiwa kwa kura katika kituo cha kupigia kura.
Fomu hiyo huwa na maelezo kuhusu kura zilizohesabiwa za kila mgombea mbali na kuwa na idadi ya wapiga kura katika kituo hicho, kura zilizoharibika, zile zilizo na utata na kura zilizokubalika.
Mgombea ama ajenti wake baadaye hutakiwa kutia saini ili kuthibitisha kwamba yaliomo ndani ya fomu hiyo ni sahihi.
Kifungu cha 39 cha uchaguzi kinasema kuwa ili kufanyika kwa uchaguzi wa urais tume ya uchaguzi itatoa matokeo hayo kielektroniki baadaye kuyasafirisha kutoka katika kituo cha kupigia kura hadi katika kituo cha kuhesabia kura cha eneo bunge na baadaye katika kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura.
Form 34A hupewa afisa anayesimamia uchaguzi katika eneo bunge ambaye hujaza fomu 34B.
Hutumika kuonyesha matokeo ya kura ya urais.
Fomu hiyo huonyesha nambari ya kituo cha kupigia kura, jina la kituo cha kupigia kura, idadi ya watu waliojisajiliwa kupiga kura katika kituo hicho, matokeo ya kila mgombea na idadi ya kura zilizokubalika.
Afisa anayesimamia shughuli ya uchaguzi katika eneo bunge kwa jina Returning officer humpelekea fomu hiyo mwenyekiti wa tume ya auchaguzi IEBC ambaye ndio afisa mkuu wa matokeo ya uchaguzi wa urais.
Pia unaweza pia kusoma