Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Kenya 2022: Tunachojua kufikia sasa kuhusu mgogoro unaokumba tume ya Uchaguzi IEBC
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Huku Wakenya wakitarajiwa kushiriki katika uchaguzi wa kihistoria nchini Agosti tarehe 9 mwaka huu , Tume inayosimamia uchaguzi huo IEBC imejipata katika mgogoro.
Hatua hiyo inajiri baada ya maafisa wa polisi kuwakamata raia watatu wa Venezuela waliodaiwa kuingia nchini na vifaa vya uchaguzi.
Wageni hao walikamatwa katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi na kuzua hali ya swintofahamu kuhusu uchaguzi huo.
Kukamatwa kwao kunatilia shaka uadilifu na utendakazi wa tume hiyo pamoja na maandalizi yake wiki mbili kabla ya wapiga kura kufanya maamuzi yao.
Msemaji wa Polisi Bruno Shioso alinukuliwa Ijumaa iliyopita akisema kwamba, ukamataji huo na uchunguzi kuhusu vifaa vilivyopatikana na raia hao wa kigeni ulitokana na umuhimu wa vifaa hivyo vya uchaguzi.
Je ni vifaa gani vilivyopatikana na raia hao wa Venezuela?
Bwana Shioso alisema kwamba raia mmoja wa kigeni alikamatwa kwasababu stika za uchaguzi alizokuwa nazo hazikuorodheshwa katika mizigo yake kama inavyohitajika kisheria na kwamba vifaa hivyo vilibebwa katika mizigo ya kibinafsi ya wageni hao.
Msemaji huyo aliongezea kwamba maafisa wa polisi hawakuarifiwa kuhusu hatua hiyo ili kutoa usalama na kuvisindikiza vifaa hivyo kama inavyohitajika na Tume ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya IEBC.
Afisa huyo aliongeza kwamba Uchunguzi uliofanywa ulibaini kwamba stika hizo zilikuwa mali ya IEBC na miongoni mwa vifaa vya Uchaguzi.
Polisi wanasema kwamba wakati wa kukamatwa kwake raia huyo alikuwa akimiliki kipakatalishi na flash drive tano, miongoni mwa vifaa vya kompyuta pamoja na mabunda ya Stika ambayo alisema yanatoka kwa mwajiri wake.
Raia wa pili wa Venezuela alidaiwa kubeba mabunda 9 ya stika za uchaguzi huku wa tatu akibeba mabunda 8 ya stika hizo. Uchunguzi mwingine unadaiwa kufanywa katika nyumba waliokuwa wakilala ambapo maafisa wa polisi walikamata tablet moja na flash disk mbili.
Vifaa vyote vya kilektroniki vilivyokamatwa vilipelekwa katika maabara ya polisi wanaokabiliana na ugaidi ATPU kwa uchunguzi zaidi, walisema maafisa wa polisi katika taarifa iliotolewa siku ya Jumapili.
Je Tume ya Uchaguzi na Mipaka inasemaje?
Mwenyekiti wa IEBC Chebukati hatahivyo alihalalisha kuwasili kwa nyenzo za uchaguzi zilizonaswa katika uwanja wa ndege, zikiwemo stika na kutofautiana na Idara ya polisi kuhusu raia wa kigeni waliokuwa wakimiliki vifaa hivyo.
"Ili kutambua vifaa vya KIEMS kwa urahisi, Smartmatic , kampuni inayoisaidia tume hiyo ya Uchaguzi kupitia teknolojia inahitajika kutoa vibandiko ili kusaidia kuweka lebo kwa kila kifaa kwa madhumuni ya kufunga na kupeleka katika vituo vyote vya kupigia kura. Usambazaji wa vifaa vya KIEMS unaendelea kwa sasa.
"Ni muhimu kutambua kwamba vibandiko hivyo si nyenzo za uchaguzi zisizo za kimkakati. Vibandiko hivyo vilichapishwa kulingana na maelezo ya notisi ya gazeti la serikali iliyochapishwa Julai 1 2022," IEBC ilieleza.
IEBC katika taarifa yao ilisema kuwa Wavenezuela walipewa kandarasi ya kusaidia katika sekta ya ICT na usambazaji wa vifaa vya KIEMS.
Awali tume hiyo ilisema kwamba idara ya huduma za polisi inashikilia vifaa muhimu vya kielektroniki vilivyokuwa na raia hao watatu wa kigeni waliokamatwa siku ya Alhamisi wiki iliyopita.
Katika taarifa iliotolewa na mwenyekiti wake Wafula Chebukati siku ya Ijumaa, tume hiyo iliishtumu serikali ikisema hatua hiyo itaathiri maandalizi ya uchaguzi mkuu.
"I dara ya huduma ya Polisi NPS imewapokonya vitu vyote muhimu ikiwemo simu, vipakatalishi na flash disks maafisa hao , ambapo vifaa hivyo muhimu vya kielektroniki vina ujumbe muhimu sana unaohusishwa na uchaguzi ujao Pamoja na miradi mingine wanaoyofanya katika mataifa mengine.
Maafisa hao walilazimishwa kutoa nywila za simu zao na vifaa vingine hatua inayokiuka haki za faragha, Chebukati alisema katika taarifa aliotoa kwa vyombo vya habari. Aliishutumu idara ya huduma za polisi kwa kudanganya kwamba vifaa vilivyopatikana vimerejeshewa tume ya Uchaguzi.
Mwenyekiti wa Tume hiyo amedai kwamba vifaa hivyo vilevile bado vipo kwa mikono ya kitengo cha kukabiliana na ugaidi nchini ATPU.
Vilvile Mwenyekiti huyo amesema kwamba raia hao watatu kutoka Vinezuela wametakiwa kuwasili mbele ya maafisa wa polisi hii leo tarehe 26 Julai , akidai kwamba agizo hilo litaathiri utendakazi wao.
Chebukati amesema kwamba tume yake imeghadhabishwa na kitendo hicho , na kuitaka idara ya polisi nchini Kuwapatia fursa ya kutekeleza jukumu lao.
Kwanini Idara ya Jinai inakinzana na Tume ya Uchaguzi?
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti alitoa ripoti ya kina ya uchunguzi kuhusu wageni watatu waliokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta wakiwa na vifaa vya uchaguzi.
Huku akishikilia kuwa watatu hao hawakuwa maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, ripoti ya Kinoti inatoa maelezo ya kina jinsi watatu hao walivyonaswa katika uwanja wa ndege.
Anasema kwa mara ya kwanza walimkamata Jose Gregoria Camargo Castella, raia wa Venezuela ambaye wakati huo hakujitambulisha kama mfanyakazi wa IEBC lakini ambaye alikuwa na uhusiano na mfanyibiashara Abdulahi Abdi Mohammed jijini Nairobi.
Inasemekana kwamba Abdi alilipa tikiti ya ndege ya Camargo kuingia nchini na alitarajiwa kuripoti ofisini kwake atakapowasili.
Alikuwa amesafiri kutoka Panama kupitia Uturuki na aliwasili nchini Alhamisi, Julai 21.
Kinoti anasema alipofika uwanja wa ndege, alizuiliwa baada ya stakabadhi alizokuwa nazo kutiliwa shaka zikithibitishwa kuwa stika za IEBC za takribani kaunti 11 na takriban vituo 10,000 vya kupigia katika kaunti za Nairobi, Kiambu, Nakuru, Nyeri, Meru, Machakos, Murang'a. , Bomet, Tharaka Nithi, Nyandarua, Kericho na kitabu ambacho hakijachapishwa.
Akisitasita kutoa maelezo ya mzigo wake, alisema stakabadhi hizo alipewa na kampuni yake ili kumpelekea Abdi.
"Mshukiwa alikiri kwamba alipewa nyenzo hizo Panama na kampuni yake ya M/S Smartic International Holdings B.V ili kuzipeleka katika afisi ya Abdulahi Abdi Mohammed jijini Nairobi," Sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.
"Begi lake la pili lilikuwa na laptop moja, skrini moja, flash disc tano, simu moja ya mkononi na vifaa vya aina mbalimbali vya kompyuta, sio mali ya IEBC," sehemu ya taarifa hiyo ndefu ilisema .
Taarifa hiyo inazidi kubainisha kuwa wakati wakimhoji Camargo, raia wengine wawili wa kigeni ; Joel Gustavo Rodriguez na Salvador Javier Suarez walionekana kwenye uwanja wa ndege wakiuliza mahali alipo.
Kulingana na gazeti la The People Daily nchini Kenya, baada ya uchunguzi zaidi, DCI hata hivyo wanasema wawili hao hawakuwa wafanyakazi wa Smartmatic na walikuwa wamesafiri hadi nchini kwa kutumia pasi za kusafiria zilizopitwa na wakati kutoka Venezuela.
"Wakati wa kuhojiwa, Camargo aliulizwa iwapo alikuwa na mawasiliano yoyote na mtu yeyote katika Jamhuri ya Kenya na haswa IEBC -hatahivyo hakuweza kutoa mawasiliano yoyote isipokuwa mawasiliano ya nyumba aliyopangiwa."
DCI ilisema kuwa huo ulikuwa mpango uliopangwa vyema na IEBC kwani alipohojiwa na mshauri mkuu wa sheria wa tume hiyo Chrispine Owiye kuhusu namna ya utoaji wa vifaa vya uchaguzi kutoka nje ya nchi, alisema kuwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji Marjan Hussein Marjan hakutia saini kifungu chochote kuruhusu hatua hiyo.
"Mabadiliko yaliyo hapo juu yanazungumzia mwanya wa kimakusudi ulioachwa kwa makusudi kwa ajili ya kufanya ulaghai," taarifa ya DCI inadai.
Mgawanyiko ndani ya Tume ya Uchaguzi
Bwana Kinoti aliongezea kwamba Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo pamoja na mwenyekiti Wafula Chebukati walitofautiana katika kuwatambua watatu hao.
"Bw Marhan Hussein Marjan alisema kwa uwazi kuwa mshukiwa Camargo si afisa wa IEBC lakini mfanyakazi wa Smartmatic.
Tunamuona Mwenyekiti Wafula Chebukati kuwa mwongo na si mwaminifu kwa kutangaza watu ambao wamekataliwa na wafanyikazi wake kama wafanyikazi wa IEBC."
DCI Kinoti sasa amemtaka Wafula Chebukati kujitokeza wazi na kuwahakikishia Wakenya uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika 2022.
"Tunampa changamoto Chebukati kuweka mambo yake sawa na kuzungumza juu ya kutimiza maneno yake mwenyewe kuhusu uchaguzi wa haki na wa kuaminika. Anapaswa kuacha kuwatisha na kuwatusi wadau wengine wanaowajibika kwa usawa katika kutekeleza majukumu yao kwa kutumia vibaya vyombo vya habari kila mara," Taarifa hiyo inatamatisha.
Majuma mawili yaliopita makamishna katika tume ya IEBC walidaiwa kutofautiana kuhusu kuwasili kwa makaratasi ya kupigia kura tarehe 7 Julai huku baadhi ya makamishna wakidai kwamba hawakuarifiwa kuhusu hatua hiyo.