Uchaguzi wa Kenya 2022: Mfahamu Rachel Ruto mke wa rais mteule wa Kenya ni nani

Rachel

Chanzo cha picha, Rachel/TWITTER

    • Author, Ambia Hirsi
    • Nafasi, BBC Swahili

Ni mwanamke mtulivu na mnyenyekevu ambaye hutanguliza mapenzi yake kwa Mwenyezi Mungu katika kila hatua yake na kuwakilisha injili

Hulka hii pia inajitokeza katika mtindo wake wa mavazi na hata anavyotoa salamu.

Licha ya umaarufu wa mume wake Wakenya walipata fursa ya kutangamana naye utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ulipoingia madarakani mwaka 2013.

Kutana na Rachel Chebet Ruto, mke wa Rais Mteule wa Kenya William Ruto.

Alizaliwa tarehe 20 mwezi Novemba 1968 mjini Kakamega magharibi mwa Kenya na kupata masomo yake ya sekondari katika shule ya wasichana ya Butere hadi kidato cha sita.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta na kusomea shahada ya Elimu.

Bi Rachel pia alikamilisha shahada yake ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki mwaka 2011.

Japo hakupata nafasi ya kufanya mazoezi ya kufundisha kwa muda mrefu, aliamua kujitosa katika biashara ya utalii ambapo alikuwa akiwapeleka watu kuzuru maeneo tofauti ya ndani na nje ya Kenya.

Familia

Rachel Ruto

Chanzo cha picha, Rachel/TWITTER

Maelezo ya picha, Naibu wa Rais Wiliam Ruto na Mke wake Rachel Ruto

Bi Rachel na William Ruto walikutana mwanzoni mwa miaka ya tisini na wawili hao walianza kuchumbiana wakiwa chuo kikuu.

Rachel alikuwa akisomea Elimu na mpenzi wake wakati huo alikuwa akisomea Sayansi ya mimea (Botany).

Walifunga pingu za maisha na kuanza familia yao changa mwaka 1991.

Wanandoa hao walijaaliwa watoto sita-mabinti watatu na wavulana watatu mkubwa wao akiwa Nick Ruto.

Rachel Ruto sasa ni mama mkwe wa Mnigeria Dkt Alexander Ezenagu.

Watoto wa Ruto

Chanzo cha picha, Mitanando ya Kijamii

Maelezo ya picha, Baadhi ya watoto wa Ruto

Rachel Ruto kama mke wa mke wa rais mteule

Bi Rachel Ruto kabla ya kuwa mke wa rais mteule William Ruto alikuwa Mke rasmi wa naibu wa rais wa Kenya mwaka 2013.

Na tangu wakati huo amekuwa mstari wa mbele kupigania haki ya wanawake na harakati za kuwawezesha katika jamii.

Mpango wake kuwawezesha wanawake kupitia shirika la Joyful Women, uliangaziwa na Televisheni ya Citizen, ambapo alifichua jinsi harakati zake zilivyosaidia idadi kubwa ya wanawake.

Kupitia miradi aliyoanzisha baadhi ya wanawake wameweza kuanzisha biashara, kuweka akiba ya fedha, kununua ardhi na katika mchakato huo kuwajengea imani.

Baadhi ya miradi ya kuwawezesha wanawake ikiwa ni pamoja na:

Uwekezaji kwa wanawake: Huu ni ambao wanawake wengi wanaufahamu kama Table Banking unawawezesha wanawake walioungana 'chamaa' kuweka pesa pamoja kila mwezi au kila wiki na kutokana na fedha hizo kila mwanachama anakopa anachoweza kulipa.

Kabla ya hapo wanawake kwenye chama wamekuwa wakikutana na kuchangisha pesa pamoja na kumpatia mmoja wao kila wiki au mwezi mfumo ambao bado unaeziwa na baadhi yao.

na Ruto

Chanzo cha picha, Rachel/Twitter

Maji:Huu ulikuwa mpango wa kuwasaidia wanawake kupata maji safi ya matumizi.

Katika shughuli zake za kutangamana na wanawake katika maeneo tofauti nchini mama Rachel aligundua kuwa wanawake wamekuwa wakitembea mwendo mrefu kutafuta maji ndiposa alianzisha mradi huo kwa ushirikiano na serikali.

Kushona: Mradi huu ulianzishwa hususan kuwasaidia wafungwa wanawake: ambao wanawezeshwa kushona, vitambaa ambavyo vinawekwa kwenye fremu na kuuzwa. Pesa zinazotokana na mradi huo wanapewa watakapotoka gerezani.

Pia alianzisha mradi wa ufugaji kuku ambao unasambaza vifaranga kwa wanawake kote nchini kwa bei nafuu.

Nani yuko kwenye kinyang'anyiro cha kuiongoza Kenya ?

Fahamu zaidi kuwahusu wagombea urais wa Kenya

Chagua mgombea ili kutazama wasifu wake

Raila Amollo Odinga

Muungano wa Azimio la Umoja

  • Mgombea huyo mwenye umri wa miaka 77 ni mhandisi aliyesomea Chuo Kikuu cha Ufundi cha Magdeburg (sasa kinajulikana kama Chuo Kikuu cha Otto-von-Guericke Magdeburg) nchini Ujerumani.
  • Anawania kiti cha urais kwa tikiti ya Azimio la Umoja One Kenya Coalition Party.
  • Hili litakuwa jaribio lake la tano baada ya kugombea katika: 1997, 2007, 2013 na 2017.
  • Bw Odinga alikuwa mmoja wa wapiganiaji wa demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya. Alikamatwa, akafungwa na wakati fulani akaenda uhamishoni kwa sababu ya kupigania haki hiyo
  • Aliwahi kuwa Waziri Mkuu, kuanzia 2008-2013.
  • Odinga alihusika kufanikisha miradi mikubwa iliyotekelezwa na serikali ya Kibaki, kama vile miradi ya umeme vijijini na barabara.
  • Kuafikia ukuaji wa uchumi wa tarakimu mbili kupitia uwekezaji katika biashara ndogo ndogo na sekta ya viwanda.
  • Utoaji wa huduma bora za afya kwa wote.
  • Utoaji wa vifaa vya michezo na burudani kwa ukuaji wa kimwili, kiakili, kijamii, kimaadili na maendeleo ya watu.
  • Kufuatia jaribio la mapinduzi ya Agosti 1, 1982, Raila Odinga alikamatwa na kukabiliwa na mashtaka kadhaa, yakiwemo ya uhaini ambayo alizuiliwa bila kufunguliwa mashtaka. Tume ya Ukweli ya Haki na Maridhiano iliambiwa mwaka 2011 kwamba Odinga alikuwa na mawasiliano na mpangaji mkuu wa mapinduzi hayo. Odinga amekana kuhusika kila mara. - Makavazi ya Kitaifa ya Kenya.

William Samoei Ruto

Muungano wa Kenya Kwanza

  • Mgombea huyu mwenye umri wa miaka 55 ana Shahada ya Uzamifu/PhD katika Ikolojia ya Mimea na BSc katika Botany na Zoology kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.
  • Anawania kiti cha urais kwa tikiti ya chama cha United Democratic Alliance ( chenye mafungamano na Kenya Kwanza).
  • Aliongoza Vuguvugu la vijana la Youth for Kanu '92 (YK'(92).
  • Wizara yake iliorodheshwa kama inayofanya bora zaidi serikalini alipokuwa Waziri wa Kilimo.
  • Alihudumu kama Naibu Rais wa kwanza wa Kenya chini ya katiba mpya ya 2010.
  • Alihudumu kama mbunge wa eneo bunge la Eldoret Kaskazini kuanzia 1997-2007.
  • Kutenga $424 milioni kila mwaka kwa biashara ndogo ndogo za kati.
  • Kuanzisha mfuko wa elimu wa kitaifa ili kukidhi gharama zisizo za masomo.
  • Tekeleza kikamilifu sheria ya usawa wa kijinsia ya thuluthi mbili katika uteuzi wa kisiasa na kutenga nusu ya baraza lake la mawaziri kwa wanawake.
  • Mnamo 2008, Mahakama Kuu ya Kenya iliamuru Naibu Rais William Ruto kusalimisha shamba la ekari 100 na kulipa $ 62,500 kwa Adrian Muteshi, mkulima ambaye alimshtaki kwa kuchukua mali hiyo baada ya uchaguzi wa 2007. - Kenya Law
  • Mnamo 2011, Bw Ruto alikabiliwa na kesi kwa makosa matatu dhidi ya binadamu: Mauaji, uhamisho wa watu kwa lazima na mateso ya watu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. Miaka mitano baadaye mahakama ilisitisha kesi hiyo kwa msingi kwamba - ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa dhaifu. -ICC

George Wajackoyah

Chama cha Roots

  • Profesa huyo mwenye umri wa miaka 61 ana shahada ya uzamili katika sheria kuhusu maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Warwick na shahada ya uzamili , sheria (sheria za Marekani kutoka Chuo Kikuu cha Baltimore.
  • Bw Wajackoyah anawania kiti cha urais kwa tiketi ya Chama cha Roots Party.
  • Alihudumu kama Inspekta katika idara ya usalama ya Special branch wakati wa utawala wa marehemu Rais Daniel Moi kabla ya kulazimika kutorokea ng'ambo ili kuepuka kufunguliwa mashtaka na mamlaka.
  • Yeye ni mshirika katika kampuni ya mawakili aliyoianzisha mwaka wa 2018.
  • Alifunnza somo la sheria na uchumi katika vyuo vikuu vya Marekani, Uingereza na Kenya.
  • Kuhalalisha matumizi ya kiviwanda ya bangi
  • Badilisha siku za kazi hadi Jumatatu hadi Alhamisi.
  • Huduma ya afya ya bure na msaada kwa wazee, walio hatarini na wajawazito

David Mwaure Waihiga

Chama cha Agano

  • David Mwaure anawania kiti cha urais kwa tiketi ya Chama cha Agano.
  • Ni kiongozi wa Chama cha Agano.
  • Alihitimu na shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na ana Shahada ya Uzamili katika masomo ya uongozi.
  • Yeye ni wakili mkuu na amehudumu kama mwanasheria kwa zaidi ya miongo mitatu.
  • Ana kampuni ya uwakili na amewania viti mbalimbali vya kisiasa.
  • Ilianzishwa chama cha Agano mwaka 2006.
  • Kupambana na ufisadi uliokithiri.
  • kuunda nafasi za ajira.
  • Kurejesha mali ya Kenya iliyofichwa nje ya nchi.

Pata maelezo zaidi kuhusu sera za wagombea urais hapa

Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma

Election branding