Kwanini Waeritrea wanataka Isak asalie Newcastle?

gg

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Tesfalem Araia & Teklemariam Bekit
    • Nafasi, BBC Tigrinya, Newcastle
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Alexander Isak amekuwa kiungo muhimu katika ufanisi wa klabu ya Newcastle United tangu ajiunge na kikosi cha Eddie Hwe.

Hata hivyo mashiko yake yametanua zaidi hadi katika jamii.

Haswa wanachama wa raia wa Eritrea wanaoishi ughaibuni, wanajivunia kumuona kijana ambaye ana mizizi katika taifa lao anatikisa nyavu katika mojawapo ya klabu kubwa Uingereza.

Katika bustani na viwanja vya mazoezi kote kaskazini mashariki mwa Uingereza, mabadiliko ya kimya yanaendelea.

Vijana wa asili ya Eritrea, wakihamasishwa na simulizi ya mafanikio ya mshambuliaji huyo, wanavaa viatu vyao vya michezo wakiwa na matumaini mapya.

"Ninapenda soka sasa kwa sababu ya Alexander," alisema kijana mwenye umri wa miaka 13 wa asili ya Eritrea anayeongea lugha ya Tigrinya aambia BBC.

"Kumuona akicheza hapa kunanipa fahari kubwa. Yeye ni kama mimi."

Eritrean.mabadiliko ya utulivu yanaendelea, huku vijana wa Eritrea wakichochewa na hadithi ya mshambuliaji huyo kuweka buti zao kwa nia mpya.

"Ninapenda soka sasa kwa sababu ya Alexander," mvulana mwenye umri wa miaka 13 mwenye asili ya Eritrea, Tigrinya, aliiambia BBC. "Kumuona akicheza hapa kunanifanya nijivunie. Yeye ni kama mimi."

Yacob Akale, baba wa watoto watatu, alizungumzia jinsi mmoja wa watoto wake wa kiume anavyovutiwa na mshambuliaji huyo, ambaye anaiwakilisha Sweden lakini wazazi wake ni Waeritrea.

Isak, ambaye amefunga mabao 62 katika mechi 109 tangu ajiunge na Newcastle mnamo Agosti 2022, huenda tayari amecheza mechi yake ya mwisho akiwa katika jezi ya Magpies.

Taarifa hizi zimezua hisia mseto miongoni mwa mashabiki.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amekuwa lengo la Liverpool, ambao walitoa ofa mapema mwezi huu, huku Isak akiwa anafanya mazoezi kando na kikosi.

Kocha Eddie Howe amekiri kuwa "kila kitu kiko kwenye mizani," huku ripoti zikionyesha kuwa Isak mwenyewe ana nia ya kuondoka.

Uvumi unapunguza matumaini

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati Newcastle walipofuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwezi Mei, shangwe ya mashabiki wakiwemo Weritrea ilikuwa ya dhati na ya kugusa moyo.

Hata hivyo, ndoto ya kushindania kombe la kifahari zaidi barani Ulaya imewekwa kando kwa sasa, licha ya Newcastle kuweka thamani ya Isak kuwa pauni milioni 150 (takribani dola milioni 201), ili kuwazuia mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Liverpool.

Ingawa Liverpool wameanza kuangalia wachezaji wengine kama Hugo Ekitike wa Eintracht Frankfurt, bado hawajaacha kummezea mate Isak.

Tayari ofa ya pauni milioni 110 (dola milioni 147.5) imetupiliwa mbali na Newcastle, huku Liverpool wakiongeza uwezo wao wa kifedha kwa kumuuza Darwin Núñez.

Inaaminika kuwa nia yao ilichochewa na bao la ushindi alilofunga Isak katika fainali ya Carabao Cup msimu uliopita bao lililowapatia Magpies taji lao la kwanza baada ya kipindi cha miaka 70.

Katika siku ile ile aliyokosa kuingia kwenye msafara wa maandalizi ya msimu mpya huko Asia, mwishoni mwa Julai, Isak alithibitisha kuwa alikuwa akitafakari kuondoka Newcastle.

Weritrea wanaoishi eneo la Tyneside, hata hivyo, wangependa abaki.

Balozi" wa Eritrea kwenye spoti

Mashabiki wa Newcastle waliinua bendera ya Eritrea kwa ajili ya kumuenzi Isak kabla ya mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza Novemba mwaka jana.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mashabiki wa Newcastle waliinua bendera ya Eritrea kwa ajili ya kumuenzi Isak kabla ya mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza Novemba mwaka jana.

Isak alizaliwa Stockholm, mji mkuu wa Uswidi, lakini mara kadhaa ameelezea kwa fahari asili yake ya Eritrea.

"Ingawa nililelewa Uswidi, niliishi katika mazingira ya jamii kubwa ya Kieritrea. Nilizungukwa na kulelewa katika utamaduni huo," alisema wakati wa mahojiano na gwiji wa soka Alan Shearer.

Akiwa mchezaji wa kwanza mwenye asili ya Eritrea kuwahi kung'ara katika soka ya kimataifa, Isak anachukuliwa kama balozi wa taifa hilo dogo la Pembe ya Afrika si tu na Waeritrea walioko nyumbani, bali pia na wale walioko ughaibuni.

"Ni heshima kubwa kumuona mtu wa hadhi ya Alexander akifika hapa," alisema Mehari Estifanos, mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya vijana ya Eritrea, ambaye sasa anaishi Newcastle aiambia BBC.

"Hapo awali, watu wengi katika eneo hili hawakuwa na ufahamu kuhusu Eritrea. Lakini tangu Isak ajiunge na Newcastle, wengi sasa wanajua ilipo na wanafahamu utamaduni wetu."

Kwa mujibu wa Estifanos, mafanikio ya Isak yamewahamasisha vijana wengi walioko ughaibuni kujitosa katika soka.

Baadhi yao tayari wamejiunga na akademia mbalimbali nchini Uingereza na barani Ulaya.

Maendeleo haya ni ya maana sana, hasa ikizingatiwa kuwa hali ya soka nchini Eritrea imezorota kiasi cha FIFA kuiondoa timu ya taifa katika viwango vyake mwaka uliopita.

Katika miaka ya hivi karibuni, visa vya wachezaji wa Eritrea kukimbilia uhamishoni walipokuwa kwenye majukumu ya kimataifa ndivyo vimekuwa vikiangaziwa.

Waeritrea waishio Tyneside wanahisi kuwa ni jukumu lao kumuunga mkono Isak, na mara kwa mara huonekana wakiwa wamebeba bendera ya Eritrea yenye rangi nyekundu, kijani na buluu kila Newcastle wanaposhuka dimbani.

"Alexander ni balozi wa Eritrea, kama walivyo wapanda baiskeli maarufu Biniam Girmay na Daniel Teklehaimanot," alisema Akale.

"Tunajivunia kuwa naye. Hata kwenye buti zake, ameweka bendera ya Uswidi pamoja na ile ya Eritrea."

Utambuzi wa utamaduni wa Eritrea

Mehari Estifanos anasema vijana wa Eritrea wanaingia kwenye soka kutokana na Alexander Isak
Maelezo ya picha, Mehari Estifanos anasema vijana wa Eritrea wanaingia kwenye soka kutokana na Alexander Isak

Mbali na mchango wake mkubwa ndani ya uwanja, Isak pia ameibua shauku ya kipekee miongoni mwa mashabiki wa Newcastle kuhusu tamaduni na urithi wake wa Kiafrika.

Bereket Kiflu, mmiliki mwenza wa mgahawa maarufu wa vyakula vya Eritrea na Ethiopia karibu na uwanja wa St James' Park, anasema biashara imeongezeka sana hasa baada ya Isak kupiga picha ya mgahawa huo wakati wa gwaride la ushindi wa Carabao Cup na kuiweka kwenye mitandao ya kijamii.

Wakazi wengi wa eneo hilo wameanza kufurika mgahawani hapo kuonja vyakula vya kigeni kama anjera, mkate wa chachu unaotumiwa sana katika kanda ya Pembe ya Afrika.

"Nimesikia kuwa Isak alikuwa anawaleta baadhi ya wachezaji pale," alisema mchekeshaji na mtangazaji wa podikasti Anth Young kupitia BBC Tigrinya.

"Sijawahi kula chakula cha Kieritrea, lakini sasa nitajaribu."

"Niliona picha hizo kwenye Instagram vyakula vinaonekana kuwa vya kuvutia sana."

Mashabiki wa Newcastle wanatamani Isak abaki, wakimuona kama mchezaji ambaye anaweza kuwa gwiji wa klabu hiyo.

"Siku moja atahesabiwa kama Bobby Robson au Alan Shearer," alisema shabiki mmoja wa mtaa huo.

Wakati dunia ikisubiri hatima ya mshambuliaji huyo, thamani ya Isak kwenye soko huenda ikawa kubwa mno kwa vilabu vingi.

Lakini kwa vijana wa Eritrea, mafanikio yake hayawezi kupimwa kwa kipimo cha pesa.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid