Newcastle yakataa ofa ya Liverpool ya £120m kwa Isak, United yataka wawili

Chanzo cha picha, BBC/ getty image
Soko la usajili wa wachezaji limeendelea kupamba moto katika wiki hii, huku vilabu vikubwa barani Ulaya vikiwa vinatafuta njia za kuimarisha vikosi vyao kabla ya msimu mpya kuanza. Kutoka Ligi Kuu ya England, hadi Ligi Kuu ya Ujerumani na Hispania, vilabu vinafanya kila juhudi kupata vipaji vinavyoweza kuwapa taji la ubingwa.
Tetesi na mikataba iliyo karibu kufanyika imetawala vichwa vya habari, na mashabiki wanatumai kuwa usajili huu utaleta mabadiliko ya maana kwenye timu zao.
Ingawa baadhi ya vilabu vimekuwa vikifanya usajili kimya kimya, msururu wa matukio ya siku ya Ijumaa unaonyesha wazi kwamba hakuna timu iliyo tayari kubaki nyuma.
Wachezaji maarufu na wanaotarajiwa kuwa nyota wameingia kwenye orodha ya vilabu vinavyowataka, na matarajio ya kubadilisha kabisa picha ya ligi mbalimbali yanaonekana wazi. Ni msimu ambao kila uamuzi, kila makubaliano, na kila uvumi una athari kubwa kwenye mafanikio ya baadaye ya klabu, huku wachezaji wengine wakifanya maamuzi magumu kuhusu mustakabali wao.
Kwa mashabiki tunakuletea tetesi kubwa za alasiri hii, ishara ya kile kinachoendelea nyuma ya pazia, zikitoa taswira ya jinsi vilabu vinavyojipanga kwa ajili ya vita vya msimu mpya.
Alexander Isak 'asusa' mazoezi, Newcastle ikikataa £120m ya Liverpool

Chanzo cha picha, Getty Images
Liverpool leo wametoa ofa yao ya kwanza kwa thamani ya pauni £120m kwa ajili ya mshambuliaji Alexander Isak, lakini Newcastle wameikataa.
Liverpool wamekuwa wakihusishwa na mshambuliaji huyo wa Newcastle kwa miezi kadhaa sasa, na hatimaye wametoa ofa rasmi kwa ajili ya mchezaji huyo, ambaye inasemekana anataka kujiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya England.
Inaelezwa kuwa ofa hiyo kutoka kwa mabingwa hao wa Premier League iko chini ya thamani anayohitaji Newcastle, ambayo inakadiriwa kuwa karibu pauni £150 milioni.
Mshambuliaji huyo kwa sasa anafanya mazoezi peke yake katika klabu yake ya zamani ya Real Sociedad huku mustakabali wake ukiwa haujulikani.
Yoane Wissa amerudi Brentford lakini hakufanya mazoezi jana kwa sababu anataka kuondoka, huku Newcastle ikionyesha nia ya kumchukua.
Manchester United wamefanya mazungumzo ya awali na RB Leipzig kwa ajili ya Sesko, ambaye ameibuka kama mshambuliaji mkuu anayetarajiwa kusajiliwa msimu huu.
Gianluigi Donnarumma mbadala wa Onana United

Chanzo cha picha, d
Manchester United wana nia ya kumsajili kipa Gianluigi Donnarumma wa Paris Saint-Germain, lakini raia huyo wa Italia hana haraka ya kuondoka na yuko tayari kushindana na Lucas Chevalier kwa nafasi ya namba moja.
Sky Germany wanaripoti kuwa Tottenham wako katika mazungumzo ya juu ya kumsajili Palhinha kutoka Bayern Munich kwa mkopo na chaguo la kumnunua.
Chelsea wamekubali kumsajili mlinzi wa kati wa Ajax, Jorrel Hato, kwa kiasi cha pauni £35.5m za awali.
Kuuzwa kwa Joao Felix kwenda Al Nassr unatarajiwa kuharakisha uhamisho wa Chelsea wa kumsajili Xavi Simons kutoka RB Leizpig.
Arsenal huwaambii kitu kwa Eze

Chanzo cha picha, Getty Images
Arsenal bado wana nia ya kumsajili Eberechi Eze wa Crystal Palace, lakini hakujakuwa na mazungumzo kati ya vilabu hivyo kuhusu kifungu chake cha mkataba kilichokuwa kinaruhusu kuuzwa kwa pauni hadi £68m.
Everton wamekataliwa ofa yao ya pauni £27m kwa ajili ya kijana Tyler Dibling wa Southampton.
Kipa wa Southampton, Aaron Ramsdale, amewasili ili kumalizia uhamisho wake wa mkopo kwenda Newcastle.
Nottingham Forest wamemsajili Dan Ndoye kutoka Bologna kwa mpango wenye thamani ya pauni £34m.















