Washambululiaji wageuka lulu Ulaya, Isak akileta vita mpya

Chanzo cha picha, BBC/getty
Liverpool tayari wameshamtambulisha Hugo Ekitike kama mshambuliaji wao mpya kutoka Eintracht Frankfurt, huku Arsenal nao wakiwa hatua chache tu kukamilisha dili la Viktor Gyokeres kutoka Sporting Lisbon kwa takriban pauni milioni 63.5.
Msweden huyo anafanyiwa vipimo vya afya Ijumaa hii London kabla ya kuungana na wachezaji wenzake wa timu mpya huko Asia
Wakati wawili hao wakikaribia kutua rasmi katika Ligi Kuu ya England, hali sokoni imekuwa ya taharuki karibu kila klabu kubwa barani Ulaya inahangaika kumvutia mshambuliaji wa daraja la juu. Kila timu anataka namba 9.
Katika dirisha hili la usajili, washambuliaji wamekuwa bidhaa adimu. Magoli sasa ni mtaji mkubwa katika soka, bila mfungaji wa kuaminika, hakuna timu inayojisikia salama.
Alexander Isak kutua Liverpool?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshambuliaji wa Newcastle, Alexander Isak, anataka kuondoka Newcastle United msimu huu wa joto baada ya kukosa ziara yao ya maandalizi ya msimu mpya Asia.
Klabu imetangaza kikosi cha wachezaji 30, bila Isak, ikisema mshambuliaji huyo wa Sweden "hajajumuishwa kutokana na jeraha dogo la paja." Inaeleweka kuwa baadhi ya vilabu vikubwa barani Ulaya vimekuwa vikifahamu kuwa Isak amekuwa akitaka kuondoka Klabuni hapo. Chanzo kimoja kimeiambia BBC Sport kuwa Liverpool bado wanavutiwa na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25, licha ya kumsajili mshambuliaji wa Eintracht Frankfurt Hugo Ekitike kwa pauni milioni 69 za awali. Wiki iliyopita meneja wa Newcastle Eddie Howe alisema Isak "kabisa" atakuwa sehemu ya kikosi kwa ajili ya mechi za Singapore na Korea Kusini.
Isak alifunga mabao 27 katika mechi 42 katika mashindano yote kwa Newcastle msimu uliopita. Newcastle walikataliwa ofa yao ya pauni milioni 70 kwa Ekitike, huku sasa wakijielekeza kwa mshambuliaji wa Brentford Yoane Wissa.
Newcastle pia tayari wameanza kumfuatilia mshambuliaji Benjamin Sesko wa RB Leipzig kama mbadala wa Isak iwapo mchezaji huyo wa Sweden ataondoka. Sesko, ambaye amesaini mkataba wa miaka mitano msimu uliopita, anagharimu hadi pauni milioni 85 kiasi kinachofanya ushindani kuwa mgumu, hasa kwa vilabu vilivyokwisha tumia fedha nyingi tayari.
Gyokeres ni suluhisho la mabao Arsenal?

Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya miezi kadhaa ya kufuatilia washambuliaji mbalimbali, Arsenal wanakaribia kumtangazwa na Viktor Gyokeres kama usajili wao mpya. Mshambuliaji huyo wa Sweden, ambaye alifunga mabao 97 katika mechi 102 akiwa Sporting, anatakiwa kuziba pengo la namba 9 ambalo limewaumiza The Gunners kwa misimu kadhaa.
Ujio wake utakuwa ishara ya mwisho ya Arsenal sokoni kwa mshambuliaji, jambo linalowaruhusu kuzingatia maeneo mengine ya kikosi kabla ya msimu kuanza.
Lakini kufuatia Isak kusema anataka kuondoka Newcastle, kunawafanya Arsenal kufikiria upya uwezekano wa kuingia sokoni tena kwa ajili ya Isak, ambaye ndiye alikuwa chaguo lao la kwanza kabisa tangu Januari, 2025.
Tatizo la fedha za uhamisho linaweza kuwakwamisha, ila kama watauza wachezaji kadhaa kutengeneza kiasi kinachofika pauni 90, wanaweza kuingia sokoni kwa ajili ya Msweden huyo mkali wa mabao.
Chelsea, Buyern, Man United, Barcelona na Tottenham hazilali

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Chelsea tayari wameshasajili Liam Delap kutoka Ipswich na Joao Pedro kutoka Brighton. Lakini macho yao sasa yako kwa Xavi Simons wa RB Leipzig. Simons mwenye umri wa miaka 22 anaonekana kuwa tayari kujiunga na The Blues huku mazungumzo yakiendelea. Bayern Munich nao wanamfuatilia, ingawa wanampa kipaumbele chao ni Luis Diaz wa Liverpool.
Baada ya kumpata Matheus Cunha na Bryan Mbeumo wa Brentford, Manchester United sasa wamehamishia macho yao kwa mshambuliaji wa England, Ollie Watkins wa Aston Villa. Vyanzo vinaeleza kuwa mazungumzo ya awali tayari yameanza, lakini Villa wameshikilia msimamo wao: Watkins hauuzwi. United wanakabiliwa na shinikizo la kumaliza usajili mapema kabla ya kuanza kwa maandalizi ya msimu mpya chini ya Amorim.
Barcelona tayari wamekamilisha usajili wa Marcus Rashford kutoka Manchester United, wakitarajia atakuwa mhimili mpya wa mashambulizi yao. Tottenham kwa upande wao, chini ya kocha mpya Thomas Frank, wanamfuatilia Yoane Wissa wa Brentford.
Dirisha la washambuliaji Ulaya?

Chanzo cha picha, Getty Images
Soka mabao. Soko la msimu huu ama dirisha la usajili la sasa limedhihirisha hilo.Kuna mabadiliko makubwa ya kimtazamo kwa sasa. Wachezaji wa ushambuliaji wanarudisha enzi zao.
Mabadiliko haya ya haraka yanadhihirisha hali halisi ya soko la sasa: washambuliaji wa hali ya juu ni wachache, mahitaji ni makubwa, na bei inapanda kila siku. Victor Osimhen, aliyekuwa akihusishwa na Arsenal, Chelsea na Manchester United, ametua Galatasaray baada ya kipindi cha mkopo. Jean-Philippe Mateta wa Crystal Palace bado anawindwa na vilabu mbalimbali, lakini klabu hiyo ya London Kusini inatarajia kumbakiza kwa mkataba mpya.
Ollie Watkins wa Villa sasa amekuwa lulu mpya sokoni baada ya mazungumzo na Manchester United kuvuja. Ingawa Villa wamesema si wa kuuzwa, presha kutoka kwa wakubwa inaweza kubadili msimamo huo kabla ya dirisha kufungwa.
Nicolas Jackson, aliyekuwa mshambuliaji wa namba moja wa Chelsea msimu uliopita, anaweza kuuzwa endapo nafasi yake itaathiriwa na ujio wa washambuliaji Delap na Joao Pedro. Dominic Calvert-Lewin, ambaye yuko huru baada ya kuondoka Everton, ni chaguo la gharama nafuu kwa klabu kama Newcastle au hata Manchester United.
Ukiwa mshambuliaji msimu huu Ulaya wewe ni Lulu.















