Tetesi za Soka Ulaya: Liverpool kuvunja rekodi ya uhamisho kwa Isak?

Chanzo cha picha, Getty Images
Liverpool wako tayari kutoa ofa itakayovunja rekodi ya uhamisho Uingereza kwa mshambuliaji wa Newcastle na Sweden Alexander Isak, 25 (Mail+).
Lakini klabu ya Saudi Al-Hilal pia wanajiandaa kutoa ofa, inayodhaniwa kuwa zaidi ya pauni milioni 130, kwa Isak baada ya kuondolewa kwake kwenye kikosi cha Newcastle kilichoko kwenye ziara yao ya maandalizi ya msimu mpya huko Singapore (Talksport).
Chelsea na Manchester United hawana uwezekano wa kumsajili Isak, huku United wakiwa tayari wametumia fedha nyingi kuwasajili mshambuliaji wa Brazil Matheus Cunha, 26, na mchezaji wa kimataifa wa Cameroon Bryan Mbeumo, 25 (Mail).
Newcastle wameelekeza mawazo yao kwa mchezaji wa kimataifa wa Slovenia Benjamin Sesko huku mshambuliaji huyo wa RB Leipzig mwenye umri wa miaka 22 akiwa mbadala iwapo Isak ataondoka (ipaper).
Aston Villa wameiambia Manchester United kuwa mshambuliaji Ollie Watkins hauzwi, licha ya klabu hiyo ya Old Trafford kumtaka sana mchezaji huyo wa Kiingereza mwenye umri wa miaka 29 (Telegraph).

Chanzo cha picha, Getty Images
Leeds United waliopanda daraja msimu huu wamekubaliana na Lyon kumsajili kipa Lucas Perri kwa thamani ya pauni milioni 15.6, huku mchezaji huyo wa Brazil mwenye umri wa miaka 27 akitarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya kwenye kambi ya mazoezi ya Whites nchini Ujerumani (Mail).
Bayern Munich wako tayari kutoa ofa nyingine tena kwa winga wa Liverpool na Colombia Luis Diaz. Klabu hiyo ya Merseyside inafahamu nia ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 kuondoka na mazungumzo yataendelea (Fabrizio Romano).
Liverpool wamempa beki wa Ufaransa Ibrahima Konate, 26, mkataba mpya ili kumzuia asiende Real Madrid, ambao wanataka kumsajili msimu huu wa joto au msimu ujao (Footmercato).
Mchezaji wa kimataifa wa Brazil Douglas Luiz, 27, alishindwa kuripoti katika siku ya kwanza ya mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya Juventus Alhamisi huku West Ham, Everton na Liverpool zote zikionyesha nia kwa kiungo huyo (Gazetta dello Sport).

Chanzo cha picha, Getty Images
Winga wa Chelsea na England Raheem Sterling, 30, ameibuka kama mmoja wa walchezaji kadhaa wa washambuliaji wanaosakwa na mabingwa wa Italia Napoli (Calciomercarto).
Mshambuliaji wa Liverpool Harvey Elliott yuko tayari kuondoka klabu hiyo ya Anfield. Mchezaji huyo wa kimataifa wa vijana wa England mwenye umri wa miaka 22 anasakwa na West Ham (Metro).
Spurs wanaifanyia kazi ofa ya pauni milioni 15 kutoka LAFC kwa ajili ya nahodha wake Son Heung-min huku mchezaji huyo wa Korea Kusini mwenye umri wa miaka 33 akifikiria mustakabali wake (Sun).
Real Madrid wako tayari kumtoa kwa mkopo mshambuliaji Endrick, 19, kwenda timu nyingine ili kuboresha kiwango chake, lakini mchezaji huyo wa Brazil angependelea kupigania nafasi yake Bernabeu (ESPN).















