Maeneo manne ambapo vita vya Gaza vimepanuka mbali ya Israel-Hamas

vc

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Waandamanaji watiifu kwa waasi wa Houthi nchini Yemen waandamana dhidi ya Marekani kuliweka kundi hilo kuwa "kundi la kigaidi la kimataifa."

Kuna dalili kuwa mzozo kati ya Israel na Hamas unaenea Mashariki ya Kati.

Tukio la hivi karibuni la wanajeshi watatu wa Marekani kuuwawa na takribani 40 kujeruhiwa katika shambulio la ndege zisizo na rubani huko Jordan, karibu na mpaka na Syria - linatoa dalili hiyo.

Kundi linalojiita Islamic Resistance in Iraq lilidai kuhusika na shambulio hilo.

"Kumekuwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani kutoka kwa wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran dhidi ya kambi za Marekani, lakini hili ndilo baya zaidi ," anasema Frank Gardner, mwandishi wa usalama wa BBC.

Ikulu ya White House inadai Iran ndiyo inayohusika na operesheni hii na nyinginezo, tuhuma ambayo utawala wa Tehran umekanusha.

Kupanuka kwa mzozo wa Israel-Hamas kunaonyesha kuwa mkakati wa Marekani, ambao lengo lake ni kuzuia kuongezeka kwa mzozo huo, upo hatarini.

"Sasa kuna hatari ya kweli kwamba vita huko Gaza vitageuka kuwa mzozo mpana wa kikanda," anasema Profesa Fawaz Gerges, kutoka London School of Economics and Political Science.

Mzozo Unatanuka

C

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Mashambulizi ya bomu ya Israel huko Rafah, kusini mwa Gaza.

Mojawapo ya sababu inayofanya hali kuwa ngumu zaidi ni wingi wa makundi yenye silaha yaliyoenea katika nchi mbalimbali Mashariki ya Kati.

Kwa mfano, shambulio dhidi ya kambi ya Marekani ambalo lilichukua maisha ya wanajeshi watatu, lilifanywa na makundi mengi na si kundi moja.

"Kundi linalojiita Islamic Resistance la Iraq ni sehemu ya mtandao mpana wa wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran ambao wamejihami kwa silaha, wamefadhiliwa na kupewa mafunzo na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran," anaeleza Frank Gardner.

"Wanafanya kazi nchini Syria, Iraq, Lebanon na Yemen, wanapinga uwepo wa Israel na jeshi la Marekani katika eneo hilo," anaongeza.

Muda mfupi baada ya shambulio la Hamas katika eneo la Israel tarehe 7 Oktoba na baadae Israel kujibu mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Marekani ilipeleka meli za kivita kwenye Bahari ya Mediterania ili kuzionya nchi na makundi mengine kutoingilia mzozo huo. Lakini mzozo umekwenda mbali.

"Ukweli ni kwamba kuna moto unawaka katika maeneo kadhaa," anasema Lyse Doucet, mwandishi mwandamizi wa kimataifa wa BBC.

Hezbollah ya Lebanon

DC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Shambulizi la Israel huko Lebanon katikati ya mzozo na kundi la Kiislamu la Hezbollah.

Mpaka kati ya Israel na Lebanon umekuwa katika hali ya wasiwasi kwa miaka mingi tangu kumalizika kwa vita kati ya nchi hizo mbili mwaka 2006.

Katikati ya vita huko Gaza, mpaka huu umekuwa moja ya maeneo nyeti panapohusika mzozo huo.

Katika miezi ya hivi karibuni, vikosi vya Israel na kundi la Kiislamu lenye itikadi kali la Hezbollah, vuguvugu la Washia wa Lebanon linaloungwa mkono na Iran, zimekuwa zikishambuliana mara kwa mara.

Katika hali hii, Marekani inahofia kuwa Israel inaweza kushambulia au kuivamia Lebanon na imeitaka nchi hiyo kuepuka hatua hiyo.

Ikiwa hilo litatokea, eneo hilo litakuwa katika mgogoro mkubwa na kutakuwa na athari kwa Magharibi.

Houthis katika Bahari ya Shamu

DC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Waasi wa Houthi wamekuwa wakishambulia meli za mizigo zinazopita katika bahari ya Shamu

Bahari ya Shamu, wakati huo huo, imekuwa kitovu cha vurugu, baada ya Houthis, kundi la waasi linalodhibiti sehemu kubwa ya Yemen, linaloungwa mkono na Iran, kuzindua mfululizo wa mashambulizi ya makombora dhidi ya meli za mizigo.

Tangu Novemba, wanamgambo wa Yemen wameshambulia meli zinazopita kwenye Mlango wa Bab al-Mandab, njia yenye upana wa kilomita 32.

Waasi hao wanadai kulenga meli zenye uhusiano na Israel ili kulipiza kisasi vita katika Ukanda wa Gaza.

Kujibu hatua hiyo, Marekani na Uingereza zilianzisha mashambulizi dhidi ya Houthis.

Moja ya tukio la hivi punde katika eneo hilo ni la Januari 26, meli ya mizigo iliyokuwa imebeba mafuta, inayomilikiwa na kampuni ya Trafigura, mojawapo ya wafanyabiashara wakubwa wa nishati duniani, ilishambuliwa na kombora kwenye pwani ya Aden.

Mamia ya meli kubwa za makontena zinatumia njia mbadala, kwa kufanya safari ndefu yenye gharama kubwa kuzunguka Rasi ya Afrika Kusini.

Iraq na kambi za Marekani

DC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Wanajeshi William Rivers, Kennedy Sanders na Breonna Moffett waliuawa katika shambulizi huko Jordan usiku wa Januari 27-28.

Kwa upande wa Iraq, makundi yenye itikadi kali yamerusha ndege zisizo na rubani na roketi dhidi ya kambi za Marekani, kama vile kambi ya anga ya Asad magharibi mwa Iraq, shambulio lililosababisha majeraha kwa wanajeshi wawili wa Marekani.

Katika kulipiza kisasi, Marekani ilizindua mfululizo wa mashambulizi ya anga Januari 23.

Kambi za wanajeshi wa Marekani nchini Iraq na kaskazini mashariki mwa Syria zimekuwa zikishambuliwa mara kwa mara, na kusababisha Marekani kujibu mapigo.

Mashambulizi haya yanaonekana kuwa ni sehemu ya mzozo usio wa moja kwa moja wa Iran na Marekani.

Syria na uhusiano wake na Iran

C

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vimekuwa vikiendelea kwa zaidi ya miaka 12.

Ndege za Marekani zililipua bohari la silaha ambalo linaelezwa kuwa ni la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwezi Novemba.

Siku chache baadaye, walishambulia kituo cha mafunzo na nyumba ya siri ambayo inahusishwa na Iran, mashariki mwa Syria.

Mwezi Disemba, shambulio la anga la Israel katika kitongoji cha Damascus, mji mkuu wa Syria, lilimuua Jenerali wa Iran Seyed Razi Mousavi, mshauri wa zamani wa Jeshi la Wanajeshi wa Iran.

Katikati ya Januari, shambulio jingine la Israel katika mji mkuu wa Syria liliharibu jengo linalodaiwa kutumiwa na maafisa wa Iran.

Mashambulizi ya aina hii yanaendelea kujirudia. Kiwango cha mashambulizi bado kiko chini, lakini mambo yanazidi kuwa magumu.

Kutokana na hali hiyo, moja ya changamoto kubwa inayoikabili serikali ya Joe Biden ni kujibu mashambulizi na wakati huo huo, kuhakikisha mzozo haupanuki wala kuongezeka.

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla