Tanzania, Uganda kama tumewakosea kwa namna yoyote tunaomba radhi- Rais Ruto

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Rais wa Kenya William Ruto, ameyaomba radhi mataifa jirani ya Uganda na Tanzania katika hatua ambayo inaonekana kama juhudi za kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo ya Afrika Mashariki.
Baadhi ya Wakenya katika mitandao ya kijamii wamekuwa wakimlenga Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufuatia hatua ya hivi majuzi ya kufurushwa kwa wanaharakati mashuhuri wa Afrika Mashariki.
Wabunge wa Tanzania waliokuwa na ghadhabu siku ya Jumatatu waliwalaumu Wakenya kwa kuwanyanyasa na kuwakosea heshima Watanzania na ''kuingilia masuala ya ndani'' ya taifa hilo.
Akizungumza wakati wa dhifa ya ibada ya kitaifa jijini Nairobi leo Jumatano, Rais Ruto alitoa wito wa kuboreshwa kwa uhusiano, akibainisha kuwa Kenya iko harakati ya "kujijenga upya".
"Jirani zetu wa Tanzania kama tumewakosea kwa namna yoyote tunaomba radhi, wenzetu wa Uganda ikiwa kuna jambo ambalo Wakenya wamefanya ambayo sio sahihi tunawaomba radhi," alisema Rais Ruto.
Kauli ya Ruto inakuja wakati ambapo mvutano umeibuka kufuatia hatua ya Tanzania kuwatimua wanaharakati wa Kenya waliokuwa wamesafari hadi nchini humo kushuhudia kusikilizwa kwa kesi kiongozi wa upinzani Tundu Lissu.
Miongoni mwa waliofurushwa nchini Tanzania ni pamoja na mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi na mwenzake wa Uganda Agather Atuhaire ambao walizuiliwa kwa siku kadhaa kabla ya kuachiliwa huru.
Wawili hao walidai kuwa waliteswa, kabla ya kuachwa mpakani na vikosi vya usalama vya Tanzania, jambo lilikosolewa vikali na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu katika eleo hilo.
Tanzania bado haijatoa tamko lolote kuhusu madai hayo ya mateso lakini awali Rais Samia alikuwa ameonya kwamba hatawaruhusu wanaharakati kutoka nchi jirani "kuingilia" masuala ya nchi yake na kusababisha "machafuko".
Kauli ya Rais Samia imeibua majibizano makali kati ya raia nchi hizo mbili za Afrika Mashariki huku watumiaji wa mtandao wakiwa katika mzozo wa muda mrefu kuhusu siasa za kikanda na uanaharakati.
Wengine waliofukuzwa ni wakili mwandamizi wa Kenya na aliyekuwa wakati mmoja Waziri wa Haki na Sheria Martha Karua na wezake wawili walioambatana naye.
Karua ni wakili anayeheshimika kwa haki za kibinadamu na mkosoaji mkuu wa kile anchokiita kurudi nyuma kwa demokrasia Afrika Mashariki.
Amekuwa akiwakilisha kiongozi wa upinzani Uganda Kizza Besigye ambaye alikuwa ametekwa nchini Kenya mwaka uliopita na kurudishwa nchini mwao kuhudhuria mashtaka ya uhaini yanayomkabili. Kama Lissu, amekanusha mashtaka akisema yameshinikizwa kisiasa
Jaji Mkuu wa zamani wa Kenya Willy Mutunga na mawakili - wapiganiaji wa haki za kibinadamu walizuiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere kwa saa kadhaa kabla ya kurudishwa nyumbani.
Majibizano mitandaoni

Chanzo cha picha, Getty Images/AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Madai ya dhulma dhidi ya wanaharakati hao yaulizua makabiliano makali mtandaoni, huku watumiaji wa mitandao ya kijamii kutoka Kenya na Tanzania wakizozana kuhusu madai hayo.
Katika mjadala mkali siku ya Jumatatu, wabunge wa Tanzania walionyesha kughadhabishwa kwao na vijana wa Kenya wanaomlenga Rais Samia.
Wabunge hao walisema Samia ana kila haki ya kutetea maslahi ya taifa la Tanzania.
Matamshi ya wabunge hao yawalikasirisha baadhi ya Wakenya ambao waliwajibu kwa kuweka mitandaoni nambari za simu za wabunge hao na kwataka wenzao wawasiliane nao ili kuwaeleza kuwwa hawakuridhishwa na hatua yao.
Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu alisema kuwa alipokea ujumbe mwingi kwa njia ya WhatsApp na hivyo kumlazimu kuzima simu yake kwa muda.
Msambatavangu, hata hivyo, alikaribisha hatua hiyo, akiwahimiza Wakenya kwenye mitandao ya kijamii "kukabiliana na kwa hoja".
Aliwaomba vijana wa Kenya kuunda kikundi cha WhatsApp kwa ajili ya mawasiliano zaidi na akaahidi kuwashirikisha katika kipindi cha moja kwa moja siku ya Jumamosi.
"Wakenya ni majirani zetu, ndugu zetu, na hatuwezi kuwapuuza," aliongeza.















