'Walilenga kuua' - BBC yawatambua waliowapiga risasi vijana Kenya

.
Muda wa kusoma: Dakika 8

Maafisa wa polisi wa Kenya waliowaua waandamanaji waaliokuwa wakipinga mswada nyongeza ya ushuru uliokuwa ukijadiliwa katika Bunge la nchi hiyo mwezi Juni mwaka jana wametambuliwa na BBC.

Uchunguzi wa picha zaidi ya 5,000 uliofanywa na BBC pia unaonyesha kuwa waliouawa katika eneo hilo hawakuwa na silaha na pia, hawakuwa tishio kwa usalama.

Katiba ya taifa hilo la Afrika Mashariki inaruhusu kufanyika kwa maandamano ya amani, na vifo hivyo vilisababisha malalamiko ya umma.

Licha ya kamati ya bunge kuagiza Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi nchini Kenya (IPOA) kuchunguza vifo vilivyotokea katika mitaa ya mji mkuu, Nairobi - na kuweka hadharani matokeo yake - hakuna ripoti kuhusu mauaji yaliyotokea bungeni ambayo yametolewa na hakuna aliyewajibishwa kwa mauaji hayo.

BBC ilichambua video na picha zilizopigwa na waandamanaji na waandishi wa habari siku hiyo. Tulibaini kila mmoja kwa kutumia metadata ya kamera, muda halisi wa tukio na saa za umma zinazoonekana kwenye picha.

Tuliweka matukio ya mauaji matatu katika mfumo wa 3D yaliyokea katika bunge la Kenya, na kutuwezesha kufuatilia mauaji ya risasi ya bunduki za afisa wa polisi na mwanajeshi.

Kinachofuata ni ratiba ya kina ya matukio ya BBC Africa Eye wakati wabunge wa Kenya walipoingia bungeni kwa ajili ya kupiga kura ya mwisho kuhusu mswada wa fedha wa serikali wenye utata, huku waandamanaji wakikusanyika barabarani siku ya Jumanne tarehe 25 Juni 2024.

Onyo: Makala hii ina picha za maiti

Vijana, waliofahamika kama waandamanaji wa Gen Z ambao walikuwa wamehamasishana kwenye mitandao ya kijamii, walianza kumiminika katikati mwa Nairobi mapema asubuhi - katika yale ambayo yangekuwa maandamano makubwa ya tatu katika mji mkuu huo tangu mswada wa fedha kuwasilishwa tarehe 9 Mei.

"Kilikuwa kitu kizuri," anasema mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu Boniface Mwangi, ambaye alikuwepo.

"Vijana walitoka na spika za Bluetooth na maji yao. Ilikuwa sherehe."

Soma zaidi:
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Maandamano ya mwanzoni mwa wiki tayari yalikuwa yamesababisha wabunge kuongeza ushuru wa mkate, mafuta ya kupikia, huduma ya pesa ya simu na magari, pamoja na ushuru wa bidhaa zenye uhusiano na mazingira ungepandisha gharama ya bidhaa kama vile nepi na sodo.

Lakini pia hatua zingine za kuongeza $2.7bn (£2bn), serikali ilisema ilihitaji kupunguza utegemezi wake wa kukopa kutoka nje, kama vile ushuru wa juu wa bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi huku mwingine kwa hospitali maalum, ukisalia ulivyo.

"Kwa mara ya kwanza ilikuwa ni raia wa Kenya – tabaka la wanaofanya kazi, la kati na la chini – dhidi ya tabaka linalotawala," anasema Mwangi.

Waandamanaji walikuwa na lengo moja – kufika bunge ambapo kura ya mwisho ilikuwa inafanyika.

Ilipofika saa 09:30 kwa saa za eneo, wabunge wa mwisho walifika bungeni.

Nje, maelfu walielekea kwenye Barabara ya Bunge kutoka mashariki, kaskazini na magharibi mwa jiji.

"Kwangu mimi, ilikuwa siku ya kawaida," anasema mwanafunzi ambaye anasomea uanahabari Ademba Allans mwenye umri wa miaka 26.

Watu walikuwa wakipeperusha kinachoendelea moja kwa moja kwenye akaunti zao za TikTok na Instagram, huku matukio yakitangazwa moja kwa moja kwenye TV ya taifa, anaongeza.

Awali, waandamanaji walizuiliwa kwenye vizuizi vya barabarani kwa vitoa machozi na virungu, kisha polisi wakaanza kutumia maji ya kuwasha na risasi za mpira.

Kufikia 13:00, zaidi ya watu 100,000 walikuwa mitaani.

"Idadi ikaanza kuongezeka na watu wakaanza kukamatwa," anasema Allans. "Polisi wako kila mahali. Wanajaribu kuwarudisha watu nyuma. Watu walipanda hata juu ya magari yenye maji ya kuwasha."

Licha ya machafuko yaliyokuwa yakiongezeka nje, wabunge walikuwa ndani ya ukumbi na upigaji kura ukaanza.

Kufikia saa 14:00, waandamanaji walikuwa wamewasukuma polisi hadi kwenye upande wa kaskazini-mashariki mwa bunge.

.

Chanzo cha picha, EPA

Kufikia saa 14:14, Mswada wa Fedha wa 2024 ulipigiwa kura na matokeo yakawa ni: 195 waliunga mkono, 106 walipinga.

Wabunge wa upinzani walitoka nje bunge na maneno yakawafikia watu waliokuwa wameandamana.

"Hapa ndipo kila mtu alisema: 'Liwalo na liwe, tutaingia bungeni na kuwaonyesha wabunge kwamba tunaamini katika kile tunachopigania," anasema Allans.

Saa 14:20, waandamanaji hatimaye walivuka kizuizi cha polisi na kufika kwenye barabara inayoingia bunge.

Lori la polisi lililotelekezwa lililokuwa nje ya lango lilichomwa moto. Uzio ulibomolewa na waandamanaji wakaingia maeneo ya bunge. Uvamizi huo ulikuwa wa muda mfupi. Vikosi vya usalama vya bunge viliwaondoa waandamanaji haraka sana.

Wakati huo huo, maafisa wa polisi wakarejea Barabara ya Bunge kwa nguvu ili kutawanya waandamanaji.

Wakati haya yakifanyika, waandishi wa habari walikuwa wakirekodi, wakitoa picha za kila dakika kutoka pembe zote.

Moja ya video hizo ilinasa afisa wa polisi aliyevalia nguo za kawaida akipaza sauti "uaa!". Sekunde chache baadaye, afisa wa polisi alipiga magoti, milio ya risasi ilisikika na waandamanaji katika umati wakaanguka - saba kwa jumla.

David Chege, mhandisi wa programu na mwalimu wa kufundisha watoto elimu ya dini ya Kikiristo, mwenye umri wa miaka 39, na Ericsson Mutisya, muuza nyama mwenye umri wa miaka 25, walipigwa risasi na kufa. Wanaume wengine watano walijeruhiwa, mmoja wao akiwa amepooza kuanzia kiunoni kwenda chini.

Mwandishi tarajali Ademba Allans akijaribu kumfikia David Chege na mtu mwingine aliyejeruhiwa abaye amelala chini baada ya kupigwa risasi - Juni 25 2024
Maelezo ya picha, Mwandishi tarajali Ademba Allans akijaribu kumfikia David Chege na mtu mwingine aliyejeruhiwa ambaye amelala chini baada ya kupigwa risasi

Picha zinamuonyesha Allans, mwanahabari tarajali, akiinua bendera ya Kenya alipokuwa akijaribu kumfikia Chege na majeruhi mwingine akitokwa na damu baada ya milio ya risasi.

Lakini ni nani aliyefyatua risasi hizo?

Katika video hiyo ya afisa huyo akipiga kelele, "uaa!", mgongo wa mpiga risasi ulikuwa kwenye kamera. Lakini BBC ililinganisha silaha zake za mwili, ngao ya kutuliza ghasia na vazi la kichwani na kila afisa wa polisi katika eneo la tukio.

Katika kisa chake, alikuwa na mlinzi aliyegeuza shingo yake. Tulilinganisha sare yake ya kipekee na afisa katika video iliyorekodiwa sekunde chache baadaye. Lakini, alihakikisha ameficha uso wake kabla ya kufyatua risasi kwenye umati. Hatujui jina lake.

Hata baada ya matukio ya risasi, afisa huyo aliyekuwa amevalia mavazi ya kiraia alisikika akiwahimiza wenzake "kuua". Hakuwa mwangalifu sana kuhusu kuficha utambulisho wake: jina lake ni John Kaboi.

Vyanzo vingi vimeiambia BBC kwamba anahudumu katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nairobi.

BBC iliwasilisha madai yake kwa mamlaka ya polisi ya Kenya (IPOA), ambayo ilisema polisi haiwezi kujichunguza, na kuongeza kuwa IPOA ndiyo iliyohusika na kuchunguza madai ya utovu wa nidhamu.

Kaboi ametafutwa ili atoe maoni yake na hajajibiwa.

Hakuna aliyewajibishwa kwa vifo vya Chege au Mutisya. BBC iligundua kuwa hakuna hata mmoja wao aliyekuwa na silaha.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Ambia Hirsi