Je, mabomu ya kutoa machozi ni nini?

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Mabomu ya kutoa machozi au vitoa machozi ni mkusanyiko wa kemikali ambazo hukera neva na tezi za macho na kuanza kutoa machozi.
Ni kemikali ambayo husababisha macho, pua na koo kuwasha na kuvimba.
Mabomu ya kutoa machozi kwa kawaida hutumika yakiwa kwenye kopo ambalo hurushwa na kusababisha ukungu au vumbi jembamba hewani.
Wakati mtu anavuta pumzi, kemikali hiyo husababisha hisia inayowasha machoni na kwenye koo, na kufanya kupumua kuwa vigumu.
Mara nyingi, hutumiwa na polisi kutawanya umati mkubwa wa watu, kuvunja maandamano au kutuliza ghasia.
Hilo limeweza kushuhudiwa katika maandamano ambayo yamekuwa yakiendelea nchini Kenya dhidi ya serikjali ya rais William Ruto..
Licha ya jina hilo, mabomu ya kutoa machozi sio kwamba ni mabomu, bali ni poda iliyoshinikizwa ambayo hutengeneza ukungu inarushwa.
Bomu la kutoa machozi liligundulika kwa mara ya kwanza na wanasayansi wa Marekani mwaka 1928.
Aina ya mabomu ya kutoa machozi
Kuna aina tatu pekee za mabomu ya kutoa machozi zenye uwezo wa kutumiwa:
(i) 1-chloroacetophenone (CN)
(ii) 2-chlorobenzylidene malononitrile (CS)
(iii) Dibenz[b,f]-1,4-oxazepine (CR)
1-chloroacetophenone (CN)

Chanzo cha picha, AFP
Aina hii ya bomu la kutoa machozi husababisha muwasho wa macho, koo na ngozi.
Punde mwanadamu anapovuta pumzi huhisi macho kana kwamba yanachomwa, kutoweza kuona vizuri, uwezekano wa kuharibika kwa konea, kuwashwa na kuchomeka kwa pua, koo, na ngozi, kuhisi kuchomeka kifuani na ugumu wa kupumua.
Majaribio ya kemikali hiyo kali kwa wanyama kama panya, sungura na nguruwe yameonyesha kuwa na sumu kali hasa ikiingia mdomoni.
2-chlorobenzylidene malononitrile (CS)

Chanzo cha picha, AFP
Kemikali hiyo ilitumika kudhibiti umati mapema miaka ya 1950, lakini hadi katikati ya miaka ya 1960 ndipo ilipoanza kutumika katika nchi kadhaa.
Nchini Uingereza kumekuwa na wasiwasi unaoendelea kuhusu matumizi ya gesi ya CS huku mamlaka ya polisi ikilaumiwa kwa matumizi yake na makala moja kwenye jarida la matibabu la Lancet likitaka kusitishwa kwa matumizi ya gesi ya machozi ya CS.
Jicho ndio kiungo nyeti zaidi wakati wa kudhibiti ghasia kwa kutumia kitoa machozi kwa sababu hufanya macho kutoka machozi mengi, yanafumba na kufumbua pamoja na mienendo mingine isiyo ya kawaida ya kope, kama vile kutekenya, ambayo huwezi kudhibiti, hisia ya macho kuwaka moto na matatizo ya kuona.
Pia husababisha kikohozi, kuongezeka kwa kamasi, maumivu makali ya kichwa, kizunguzungu, kubanwa kwa kifua, kupumua kwa shida, athiri ya ngozi na kuwa na mate mengi mdomoni.
Dibenz[b,f]-1,4-oxazepine (CR)
Imefanyiwa utafiti kutokana na athari zake za sumu wakati wa matumizi yake wakati wa kudhibiti ghasia.
Uchunguzi katika mamalia mbalimbali umeonyesha CR kuwa na sumu kidogo ikilinganishwa na kemikali zingine zinazotumiwa kudhibiti ghasia kama vile gesi ya CS lakini iwapo itakupata kwa kiwango cha juu hali yako inaweza kuwa mbaya.
CR ni kemikali inayokera macho na kusababisha kutoa machozi.
Maji ya pilipili

Chanzo cha picha, Reuters
Pia kuna, maji ya pilipili ambayo ni tofauti na CN, CS na CR.
Kemikali hiyo yenye pilipili hutengenezwa kutokana na capsaicin, kiungo muhimu kwenye utengenezaji wa pilipili kali.
Maji ya pilipili hukera macho na kusababisha hisia za kuchomwa na maumivu, pamoja na kutoona kwa muda.
Upofu huu wa muda huruhusu maafisa kuwazuia watu kuendelea kusababisha ghasia.
Pia husababisha kukera wa muda na kuchomeka kwa mapafu na kupelekea matatizo ya kupumua.
Mabomu ya kutoa machozi hufanya kazi vipi?
Mabomu ya kutoa machozi husababisha dalili mbalimbali za kimwili kwa kuchochea vipokezi vya maumivu ya mwili.
Mara nyingi mtu anapojikuta kwenye mazingira yenye mabomu ya kutoa machozi, macho huwaka moto na kutoa machozi, kukohoa, kupiga chafya, na kupumua kwa shida.
Vilevile, kemikali hiyo inaweza kufanya ngozi kuwasha na hata kutapika.
Lengo la utumiaji wa mabomu ya kutoa machozi ni kusababisha usumbufu na maumivu makali, hivyo kufanya iwe vigumu kwa watu kukaa katika eneo ambalo kemikali hiyo imetumiwa.
Namna ya kukabiliana na mabomu ya kutoa machozi

Chanzo cha picha, Reuters
Wakati unapojikuta umerushiwa mabomu ya kutoa machozi bila shaka utakuwa unapitia madhara ya kemikali hiyo. Lakini unaweza kufanya yafatayo kupunguza nguvu ya athari yake.
- Songea sehemu yenye hewa safi haraka iwezekanavyo
- Osha uso wako kwa kutumia maji ya baridi. Pia, unaweza kutumia mchanganyiko wa salini
- Mabomu ya kutoa machozi yanaweza kushika kwenye nguo, kwa hiyo, pindi unapofika nyumbani, toa nguo ulizokuwa umevaa na kuziosha peke yake.
- Aidha, kuna wale ambao wanasema kuosha uso kwa maziwa na maji inaweza kusaidia kupunguza hisia za kuchomeka.
- Hata hivyo, unashauriwa kunywa maji mengi kusaidia kuondoa chembe zozote za mabomu ya kutoa machozi zilizosalia kwenye mfumo wako.
- Ikiwa dalili zako ni kali au una shida ya kupumua, ni vyema kutafuta matibabu hospitalini.
Kwa ujumla athari za mabomu ya kutoa machozi zinaweza kutofautiana kulingana na umri, afya ya mtu na ikiwa pengine tayari ana maradhi mengine au yuko katika hatari ya kupatwa na magonjwa.
Athari ya muda mrefu ya mabomu ya kutoa machozi inaweza kusababisha matatizo makubwa zaidi kiafya, kama vile kuungua kwa kemikali kwenye ngozi na macho, upofu wa kudumu na uharibifu wa mapafu.
Katika matukio nadra, imeweza kuhusishwa na kifo.















