Gen Z ni kizazi gani?
Na Asha Juma,
BBC Swahili, Nairobi

Chanzo cha picha, SHUTTERSTOCK
Kenya imeshuhudia maandamano siku za hivi karibuni yaliyokuwa yakishinikiza kuondolewa kwa Muswada wa Fedha 2024, uliopendekeza ushuru zaidi ili kufadhili bajeti ya mwaka mpya wa kifedha.
Licha ya kuwa sio maandamano ya kwanza nchini humo, yalivutia kiasi kikubwa cha vijana wa kizazi cha Z maarufu kama Gen Z, waliojitokeza barabarani katika maeneo tofauti tofauti na kutumia zaidi teknolojia kupaza sauti zao.
Kuna sintofahamu kuhusu ni lini kizazi cha Gen Z kinaanza na kumalizika lakini kinaundwa na watu waliozaliwa kati ya miaka ya 1990 na katikati ya miaka ya 2000.
Gen Z wametumia sana intaneti tangu umri mdogo, ikiwa sio maisha yao yote, na inafurahia teknolojia na mitandao ya kijamii.
Kwa hakika, kizazi hiki kilizaliwa kabisa ndani ya enzi ya kiteknolojia na kinafahamu vyema ulimwengu wa teknolojia na utandawazi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hayo yamejidhihirishwa wakati wa maandano ya nchini Kenya, walipoonekana kutumia mitandao kujipanga na kutekeleza walichotaka kifahamike na jamii kwa ujumla.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Calvin Muga anasema kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii na intaneti yalikuwa chombo muhimu sana cha kupashana habari kabla, wakati wa maandamano hayo.
‘Wengi wao wana uzoefu na ni watumizi wakubwa wa mitandao ya kijamii na hili lilirahisisha sana wao kuwasiliana na kupanga maandamano yaliyofanyika,’ anasema Muga.
Kwa hivyo, kizazi cha Gen Z kina nia iliyo wazi zaidi kuliko vizazi vilivyotangulia na ifahamike kuwa mitindo na mawasiliano yao yanashirikishwa kote ulimwenguni.
BBC Swahili imezungumza na Patience Mwende Muia, mmoja wa vijana aliyezaliwa ndani ya kizazi cha Gen Z kufahamu zaidi jinsi kinavyotaka kuchukuliwa katika jamii.
Bi. Muia anakiri kuwa kizazi hiki kina sifa nzuri na mbaya.
"Kizazi hiki...ni watu ambao wanaelewa, wameona na hawapuuzi vitu. Pia ni kizazi ambacho kinapenda vitu kulingana na teknolojia na ubunifu. Kile ambacho watu wanasema ni kibaya kwetu, ni kwamba tuna msimamo...hatutingishiki"

Chanzo cha picha, Reuters
Gen Z wanasemekana kuwa na maoni ya nguvu zaidi kutokana na jinsi wanavyojielewa na kujitambua. Labda pia hili limechangiwa na mabadiliko ya kiutamaduni.
Zamani, wakati wa majadiliano ilikuwa mwiko kumsikia mtoto akizungumza mbele ya wakubwa zake lakini mambo yanaonekana kubadilika. Karne hii, wanapewa fursa sawa za kujieleza na hilo pengine limeondoa uoga ulioshuhudiwa hapo awali wa kuzungumza mbele ya wakuu.
Kwa mtazamo wa jinsi ukuaji wa kizazi cha Gen Z kinavyokwenda, wataheshimu wakubwa wao, sio kulingana na cheti au mamlaka yao bali kulingana na uwezo wao, ujasiri na ustadi wa kusikiliza.
Lakini tofauti na vizazi vilivyotangulia, Gen Z hakina subra. Wanapofikwa kooni na jambo fulani, hawana tena mswalie Mtume, wala kujali huyu anayezungumza naye ni nani.
Hiyo ilijitokeza wakati wa kikao cha Rais William Ruto na vijana cha X- Space. Mmoja wa vijana aliyepata fursa ya kuzungumza kwenye kikao hicho alikuwa Marvin Mabonga, mhitimu wa chuo kikuu asiye na kazi.
Mabonga alimweleza rais bila kupepesa jicho kuwa Baraza lake la Mawaziri limeundwa na alichodai kuwa Mawaziri wazembe wasiofahamu kazi walizopewa.
"Katika baraza lako la mawaziri, tuna makatibu wengi wasio na uwezo," Mabonga alimwambia Rais Ruto.
Pengine huenda ikawa, uwazi na ukakamavu aliopata Marvin Mabonga wakati akizungumza na Rais umezaa matunda.
Rais William Ruto amelivunja baraza lake la mawaziri na kuziacha nafasi mbili pekee - ya Kiongozi wa mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi na afisi ya naibu wa rais Rigathi Gachagua.
''Mara moja nitashiriki katika mashauriano ya kina katika sekta mbalimbali na miundo ya kisiasa, kwa lengo la kuunda serikali pana ambayo itanisaidia katika kuongeza kasi na kuharakisha yanayohitajika…'', rais alisema katika hotuba yake kwa taifa.
Upande wa pili, miongoni mwa changamoto wanazopitia katika jamii kama ile ya Mabonga, Gen Z, imekuwa ikikabiliana na ukosefu wa mapato, jambo ambalo limesababisha kuongezeka kwa dhiki kwa familia.
Mtandao, rafiki wa dhati wa Gen Z

Chanzo cha picha, BBC/MERCY JUMA
Kutokana na kukua katika enzi ya kiteknolojia, kizazi cha Gen Z, kimezoea kupokea habari nyingi ambazo wanahitaji ndani ya muda mchache kwa utumiaji mkubwa wa intaneti.
Kwa mfano, wanapotafuta mambo mtandaoni, wanakutana na maelfu ya tovuti ambazo wanaweza kuchagua, kujifanyia utafiti wa kina na kujua jinsi ulimwengu unavyokwenda tena kwa haraka mno.
Chimbuko la teknolojia iliyopo ikiwa ni mapinduzi ya wavuti yaliyotokea katika miaka ya 1990 kulifanya kumiliki simu ikawa jambo la kawaida kwa idadi kubwa ya Gen Z na kufanya iwe vigumu kwa vijana kuishi bila simu ya mkononi.
Lakini, sio tu kila wakati kinatumia simu kwa sababu ya uvumbuzi au uchambuzi, inasemekana mara nyingi pia hutumia simu kuepuka matatizo ya kiakili na kihisia yanayowakabili nje ya ulimwengi wa kimtandao.
Kwa upande mwingine, wazazi wa Gen Z wana wasiwasi kuhusu watoto wao kutumia mtandao kupita kiasi kwani ni rahisi sana kufikia picha na taarifa zisizofaa.
Pia, mara nyingi huwa hawajui wanazungumza na nani mtandaoni au ikiwa mtu wa upande mwingine ni wa kweli. Hivyo basi, wanakuwa katika hatari ya kulaghaiwa mitandaoni.
Gen Z wanataka kuchukuliwa namna gani?

Chanzo cha picha, Reuters
Kufikia hatua hii, ni jambo lisiloweza kupingika kwamba, Gen Z wanajieleza kuwa watu wanaofikiria, wenye huruma, waaminifu, wenye nia ya kudhamiria, walioazimia, na wanaowajibika. Lakini upande mwingine wa shilingi, wakianza kutokuwa na imani nawe inakuwa vigumu kukuamini tena.
Wakati vijana wakiendelea kuandamana kushinikiza matakwa yao, Rais William Ruto alisalimu amri na kusema hatotia saini Mswada wa Fedha wa mwaka 2024 kuwa sheria.
Ruto pia alitangaza hatua mbalimbali za kupunguza mgao wa fedha za matumizi katika Ofisi ya Rais na idara nyingine za serikali ikiwemo bunge.
Lakini hata baada ya Rais William Ruto kusema hayo, bado walionekana kujitokeza tena barabarani na kuibua maswali ya ni namna gani unaweza kuishi na Gen Z na kuelewana lugha moja.
"Haya mambo, tumeyasoma, tunayajua, tumeona madhara yake na tunapozungumza na wazazi, tunataka wajue tumekua wenye uelewa na ikiwa hatueleweki, watusaidie badala ya kutupuuza," Muia amesema.
Muia anaongeza kuwa kizazi cha Gen Z kinaona ni kama "hatueleweki na jamii.
"Tunaona wanatupaka mafuta kwa mgongo wa chupa, ama wanasema watatenda au wametenda na hawatatenda. Kwa mtazamo wa kizazi hiki ni kwamba mara nyingi, unapokuwa na tatizo unakata shina badala ya kutafuta mizizi ili kukabiliana nayo kabisa."
Gen Z, wameonyesha wazi kuchoshwa kujitokeza kwa watu wale wale na ahadi zile zile zisizotimizwa.
Wakati Bwana Ruto akitangaza kuvunjwa kwa baraza lake la mawaziri, alisema atachukua muda kufanya majadiliano ya kuunda baraza jipya litakalohusika na uendeshaji wa serikali.
Ni wazi kuwa mwamko wa Gen Z, umepelekea mabadiliko si haba kwa serikali ya Kenya.
Na labda namna ya kushughulikia mambo kwa njia tofauti kuanzia kwenye jamii hadi ngazi ya juu, inaweza kuwa hatua yenye kuleta matumaini kwao.
Ni vyema ijulikane pia, Gen Z inapenda sana mageuzi ya wazo kutoka mwanzo hadi mwisho wake. Na kuamini kuwa wao ndio wakombozi wa kizazi kilichotangulia, cha leo, na kijacho.
Imehaririwa na kuchapishwa na Seif Abdalla








