Yote unayostahili kujua kuhusu Ligi Kuu ya England msimu huu

Wachezaji wa Manchester City wakisherehekea ushindi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Manchester City ndio klabu ya kwanza ya England kushinda mataji manne mfululizo ya ligi kuu
    • Author, Emlyn Begley
    • Nafasi, Mwandishi BBC Sport
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Ligi ya Premia inaanza wikendi hii, huku Manchester City ikipigiwa upatu kuendeleza ubabe wao katika soka ya England nayo Ipswich ikirejea katika ligi hiyo baada ya misimu 22.

Manchester United watakuwa wenyeji wa Fulham Ijumaa, katika mechi zitakazochezwa kwa siku nne.

Ipswich inawakaribisha Liverpool Jumamosi kabla ya Manchester City kuivaa Chelsea Jumapili katika mechi mbili zilizovutia macho zaidi wikendi ya ufunguzi.

Arsenal watakuwa na matumaini kwamba hatimaye wataishinda Manchester City na kutwaa ubingwa, huku Manchester United wakipania kujinasua baada ya msimu wao mbaya zaidi tangu 1990.

Kutakuwa na marekebisho katika kuunawa mpira kwa mikono, VAR na muda wa majeruhi, miongoni mwa mengine.

BBC Michezo inaangazia ni nini kipya na tutarajie nini katika michuano ya Ligi Kuu 2024-25.

Nini kipya? Mabadiliko ya VAR, kuzuia na mpira wa mikono

Ujumbe wa VAR kwenye skrini kubwa wakati wa mechi ya Ligi Kuu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tarajia marudio na maelezo ya kina zaidi kwenye skrini kubwa kwenye michezo msimu huu, ili kuwashirikisha mashabiki wasiachwe nyuma

Mfumo wa VAR utaimarishwa zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.

"Uamuzi ni wa refa" kumaanisha kuwa VAR inapaswa kuingilia kati pale tu kuna ushahidi kwamba "mwamuzi uwanjani atakuwa amefanya makosa ya wazi".

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Vinginevyo, uamuzi wa awali utadumishwa. Hiyo itapunguza visa vya mchezo kusitishwa mara kwa mara ili kuangalia VAR.

Akaunti ya Kituo cha Mechi za Ligi Kuu kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii wa X itachapisha maelezo ya "kina" ya uamuzi wa VAR.

Inapanga kuonyesha marudio zaidi na kutoa maelezo ya kina ya uamuzi kwenye skrini kubwa uwanjani.

Muda wa kusimamishwa kwa mechi utapungua msimu huu - kwa sababu ya mabadiliko katika sherehe za ufungaji wa goli.

Muda ulikuwa umeongezwa kwa kila mpira unapoingia wavuni na kila mechi inapoendelea.

Sasa muda utaanza kuhesabiwa baada ya sekunde 30. Kwa hivyo mchezo wenye mabao sita utakuwa na dakika tatu zimepunguzwa kabla ya mechi kukamilika.

Mbali na VAR, wachezaji wanaoshambulia, wanaozuia au kuwazuia wachezaji wa timu pinzani wakati wa kupigwa kwa mkwaju wa adhabu wataadhibiwa .

Ben White alikuwa akivuma katika mitandao ya kijamii huku pakiwa na hofu kwamba hatua zake katika kona zinaweza kuzifanya timu pinzani kuwa na mikwaju mingi ya adhabu

Sheria ya kunawa mpira kwa mkono italegezwa kidogo. Wachezaji wa Ligi Kuu ya England wamefahamishwa kwamba hawatalazimika kusogea huku mikono yao ikiwa pembeni au nyuma ya migongo yao.

Mahali mikono yao itakapokuwa wakati wanaruka itaamuliwa na jinsi viungo vingine vya mwili itakavyosogezwa.

"Tunahisia kwamba tunatoa adhabu nyingi za kunawa mpira kwa mikono na hivi ni vitendo ambavyo ni vya kawaida kabisa na vinavyokubalika," alisema Webb.

"Mwongozo kwa maafisa msimu huu uko wazi. Utaona penati chache zinazotokana na mpira wa kuunawa na mikono."

Wakati huo huo, visa vya kugusa mpira kwa mikono bila kukusudia ambavyo vimechangia kuongezeka kwa adhabu vitapunguzwa.

Wakati wa penalti mpira lazima uwe juu au uwe katikati ya eneo la penati, badala ya wakati wowote papo hapo.

Mpira wa Nike Flight

Chanzo cha picha, Getty Images

Uvamizi wa wachezaji kwenye kisanduku cha lango wakati penati inapigwa utaadhibiwa pale hatua hiyo itakuwa na athari.

Hilo linamaanisha iwapo mchezaji wa timu pinzani anagongana ama kumgusa anayepiga mpira au kuzuia bao au fursa ya mpira unaorejea.

Iwapo ni mchezaji mwenza wa anayepiga penalti, hatia itakubalika iwapo watamuathiri au kumvuruga mlinda lango, kufunga bao au kuunda fursa.

Wasaidizi{ wavulana na wasichana} nje ya uwanja wataruhusiwa kumpatia kipa mpira ili kuanza upya mchezo, badala ya kipa kulazimika kuuchukua. Mfumo wa mipira mingi - kuokota mpira nje ya kona - utabaki kwa wasaidizi walio nje.

Mabadiliko mengine madogo - Wachezaji watano wa ziada wanaweza kupasha misuli moto wakati mmoja kando ya uwanja kwani mbeleni walikuwa watatu.

Kutakuwa na mpira mpya msimu huu, Nike Flight, ambao "umeundwa kwa teknolojia ya kipekee, itakayowezesha hewa kuingia kwa urahisi".

Wakufunzi na wachezaji wapya

Enzo Maresca

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kocha wa Chelsea Enzo Maresca hajawahi kucheza wala kuwa mkufunzi wa Ligi ya Premia - ingawa alikuwa msaidizi wa Pep Guardiola katika klabu ya Manchester City.

Robo ya wakufunzi katika Ligi ya Premia watakuwa wakiongoza klabu za Ligi Kuu ya England kwa mara ya kwanza wikendi hii wakati wa mechi ya ufunguzi.

Makocha hao ni pamoja na Arne Slot wa Liverpool, Enzo Maresca wa Chelsea, Russell Martin wa Southampton, Kieran McKenna wa Ipswich na Fabian Hurzeler wa Brighton.

Slot na Hurzeler wametoka Feyenoord na St Pauli mtawalia, huku Martin, McKenna na Maresca - ingawa wakati huo wakiwa Leicester City - wote walipanda daraja kutoka Ubingwa msimu uliopita.

Kuna wachezaji wengi wapya pia.

Manchester United ilimsajili mlinzi wa Lille Leny Yoro kwa pauni milioni 52 lakini atakosa kuanza msimu huu baada ya kuvunjika mguu, mbali na mshambuliaji wa Bologna Joshua Zirkzee na walinzi wa Bayern Munich Matthijs de Ligt na Noussair Mazraoui kwa ada inayokaribia £60m.

Mabingwa Manchester City wamemsajili winga wa Brazil Savinho kutoka klabu dada Troyes kwa £30.8m, wakati Arsenal wamemsajili beki wa Bologna Riccardo Calafiori, ambaye alionyesha umahiri wa Italia kwenye Euro 2024, kwa hadi £42m.

Brighton ilimsajili winga wa Gambia Yankuba Minteh kutoka Newcastle United kwa pauni milioni 30 na viungo wawili wa kati kwa pauni milioni 25, Mats Wieffer kutoka Feyenoord na Brajan Gruda kutoka Mainz.

Minteh ni mgeni kwenye Ligi ya Premia kwa sababu alijiunga na Feyenoord, akicheza pamoja na Wieffer, kwa mkopo siku ambayo alijiunga na Magpies msimu uliopita.

Chelsea imesajili wachezaji wengi, akiwemo mshambuliaji wa Barcelona, ​​Marc Guiu na kipa Filip Jorgensen kutoka Villarreal kwa pauni milioni 20.7. Raia huyo wa Denmark atachuana na Robert Sanchez kuwania nafasi ya kwanza.

Kiungo wa kati Archie Gray pia ni mgeni kwenye Ligi ya Premia baada ya kujiunga na Tottenham Hotspur kutoka Leeds United kwa takriban £30m.

West Ham inayonolewa na Julen Lopetegui ililipa pauni milioni 27 kumsajili mshambuliaji wa Ujerumani Niclas Fullkrug.

Ipswich hatimaye yajiunga na EPL

Kieran McKenna akiinua mikono juu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kocha Kieran McKenna alikaribia kuhama Ipswich Town majira ya kiangazi

Klabu tatu kati ya mbili zilizopanda daraja zinafahamika katika Ligi Kuu ya England- mabingwa Leicester City na Southampton wakirejea mara baada ya kushuka daraja 2022-23.

Lakini Ipswich Town waliwashangaza wengi walipomaliza wa pili na kurejea kwenye ligi kuu baada ya kuwa nje kwa misimu 22.

Watakuwa na wachezaji wachache sana kwenye kikosi chao walio na uzoefu wa Ligi Kuu, wakiwa na kocha McKenna.

Wachezaji watatu waliofunga mabao mawili msimu uliopita - Conor Chaplin, Nathan Broadhead na Omari Hutchinson - wamecheza mechi mbili za Ligi Kuu.

Ipswich imemsajili Hutchinson, ambaye alijiunga nao kwa mkopo kutoka Chelsea msimu uliopita na mshambuliaji wa Manchester City Liam Delap kwa ada ambayo inaweza kufikia £20m.

Beki wa Hull Jacob Greaves, Ben Johnson wa West Ham na kipa wa Burnley Arijanet Muric ni miongoni mwa wachezaji wengine waliosajiliwa majira ya kiangazi.

Leicester wamewasajili wakufunzi wapya mara tatu tangu wamtimue Brendan Rodgers Aprili 2023. Dean Smith aliondoka baada ya klabu hiyo kushushwa daraja. Maresca aliwasaidia Foxes kupanda daraja ndani ya msimu mmoja lakini akaamua kuhamia Chelsea, huku kocha wa zamani wa Nottingham Forest Steve Cooper akichukua nafasi yake.

Jamie Vardy, ambaye sasa ana umri wa miaka 37, alikuwa mfungaji wao bora msimu uliopita akiwa na mabao 20.

Mchezaji bora wa msimu Kiernan Dewsbury-Hall, aliyeuzwa ili kutimiza sheria za kifedha, amejiunga na Maresca huko Stamford Bridge kwa kima cha pauni milioni 30.

Wanaweza kupunguziwa alama kwa kuvunja Kanuni za Faida na Uendelevu (PSR) mara ya mwisho walipokuwa kwenye Ligi Kuu.

Martin aliirejesha Southampton kwenye Ligi ya Premia kupitia mchujo, baada ya kuandikisha rekodi ya kutofungwa mechi 25 kuanzia Septemba hadi Februari.

Adam Armstrong alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa Saints msimu uliopta baada ya kufunga mabao 24.

Che Adams, mchezaji wao pekee aliyefunga zaidi ya mabao tisa, ameondoka kwenda Torino na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji wa Chile Ben Brereton Diaz, aliyesajiliwa kutoka Villarreal.

Watatu waliopandishwa daraja ndio waliopendekezwa kurejea chini moja kwa moja, wakifuatiwa kwa karibu na Nottingham Forest, Everton na Wolves.

Kuna klabu inaweza kuizuia Man City kushinda taji mara ya tano mfululizo?

Manchester City ndio klabu ya kwanza ya England kushinda mataji manne mfululizo ya ligi kuu - je wanaweza kunyakua taji hilo tena kwa mara ya tano?

Arsenal wanatarajia kuwa wapinzani wao wakuu wa taji - tena msimu huu.

Chini ya Mikel Arteta, The Gunners wamemaliza wa pili katika misimu miwili iliyopita. Msimu uliopita walijitahidi kusalia kileleni mwa jedwali hadi siku ya mwisho, wakimaliza kwa pointi mbili nyuma ya City.

Liverpool - timu nyingine ambayo imepania kushinda taji katika misimu saba iliyopita - inaanza msimu bila Jurgen Klopp kwa mara ya kwanza tangu 2015-16.

Slot, ambaye ameshinda ligi ya Uholanzi akiwa na Feyenoord, anajiunga na soka la England kwa mara ya kwanza.

Manchester United watakuwa na matumaini ya msimu mzuri zaidi baada ya Sir Jim Ratcliffe kuchukua uongozi wa klabu hiyo. Amefanya mabadiliko mengi nje ya uwanja, lakini ameamua kusalia na mkufunzi Erik ten Hag, wakati Mholanzi huyo alitarajiwa kuondolewa.

Hakuna anayejua hatma ya Chelsea baada ya klabu hiyo kubadilisha kocha na kuwasajili wachezaji kadhaa wapya.

Tottenham wanawania kuimarika katika nafasi ya tano msimu uliopita wakiwa chini uongozi wa Ange Postecoglou, huku Aston Villa wanatazamia kuimarisha nafasi ya nne bora wakicheza ligi ya nyumbani na kushiriki Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Seif Abdalla