Ligi Kuu England: Wafahamu wachezaji wapya wa kuwatazama msimu huu

ds

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ni vijana gani wanaweza kucheza katika timu kubwa katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Uingereza
Muda wa kusoma: Dakika 5

Msimu wa Ligi Kuu ya Uingereza unakaribia kuanza.

Sote tunawajua nyota maarufu ambao watakuwa katika vichwa vingi vya habari katika msimu mpya - lakini ni wachezaji gani wachanga ambao tunapaswa kuwaangalia?

Waandishi wa soka wa BBC Sport wanachagua baadhi ya vijana wanaotarajiwa kuwa maarufu katika msimu utakaoanza Agosti 16, 2024.

Pia unaweza kusoma

Trey Nyoni (Liverpool)

Mtangazaji wa BBC Sport Nizaar Kinsella anasema: Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 17 amemvutia meneja mpya Arne Slot wakati wa maandalizi ya msimu mpya.

Alifanya vyema katika mechi ya kirafiki dhidi ya Real Betis, ambayo ilimfanya apewe sifa na meneja ambaye huwa anasita kufanya hivyo. Nyoni alijiunga na Liverpool kutoka Leicester msimu uliopita wa joto.

Josh Acheampong (Chelsea)

Mtangazaji wa BBC Sport Nizaar Kinsella anasema: Beki huyo mwenye umri wa miaka 18 alicheza mechi yake ya kwanza na Chelsea msimu uliopita dhidi ya Tottenham na alikuwa mmoja wa vijana wawili waliokuwa ziarani nchini Marekani kutoka katika akademi ya timu hiyo.

Ni mchezaji bora ambaye anaweza kucheza beki wa kati au kulia.

Mikey Moore (Tottenham)

Mtangazaji wa BBC Sport Nizaar Kinsella anasema: Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 16 amekuwa akifunga mabao chini ya kocha Ange Postecoglou katika mechi za kabla ya msimu mpya.

Kinda huyo mwenye kipawa cha hali ya juu alifanya vyema katika timu ya vijana chini ya miaka 21 msimu uliopita. Ni mchanga sana kwenda nje kwa mkopo kwa hivyo atabaki na kujichanganya wa timu ya kwanza.

Ethan Nwaneri (Arsenal)

Mtangazaji wa BBC Sport Alex Howell anasema: Kumekuwa na matarajio mengi kuhusu Nwaneri tangu alipokuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Ligi Kuu ya Uingereza, alipoanza kuichezea Arsenal akiwa na umri wa miaka 15 katika msimu wa 2022-23.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 17 alicheza mechi moja pekee msimu uliopita kwenye Ligi Kuu dhidi ya West Ham lakini matumaini bado yapo kwa kiungo huyo.

Nwaneri alianza mechi ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya dhidi ya Manchester United nchini Marekani na kutoa pasi ya goli kwa Gabriel Jesus wakati Arsenal waliposhinda mechi hiyo.

Iwapo Nwaneri ataendelea kufanya zaidi ya alivyofanya hadi sasa, kuna uwezekano wa kupata dakika nyingi zaidi za kucheza msimu huu.

Adam Wharton (Crystal Palace)

Mtangazaji wa BBC Sport Alex Howell anasema: Inashangaza kwamba Adam Wharton alicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu mwezi Februari mwaka huu.

Uchezaji wake wa kuvutia katika muda mfupi ulimfanya acheze kwa mara ya kwanza England na kujumuishwa kwenye kikosi kilichofika fainali ya Euro 2024.

Vyanzo vya Crystal Palace vinaamini kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 ndiye usajili wao bora zaidi kutoka ligi ndogo.

Jesurun Rak-Sakyi (Crystal Palace)

Alex Howell wa BBC Sport anasema: Rak-Sakyi alikwenda kwa mkopo Charlton katika Ligi ya Kwanza msimu wa 2022-23 na alishinda tuzo yao ya mchezaji bora wa mwaka baada ya kufunga mabao 15 na kutoa pasi nne za goli.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 aliumia msimu uliopita na alicheza mechi nane pekee katika mashindano yote akiwa na The Eagles. Hata hivyo, amefanya vyema katika mechi za kujiandaa na msimu mpya.

Chido Obi-Martin (Man Utd)

Simon Stone wa BBC Sport anasema: Arsenal [ambapo Obi-Martin alicheza kwa miaka miwili iliyopita] wanaamini walitoa ofa ya haki kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 16, ambaye amewakilisha Uingereza na Denmark katika ngazi ya vijana. Lakini ameamua kujiunga na Manchester United.

Obi-Martin amejidhihirisha kuwa hatari katika safu ya vijana - alifunga mabao 10 katika mchezo mmoja dhidi ya Liverpool Under-16 alipokuwa na umri wa miaka 15.

Itakuwa vyema kuona jinsi atakavyo imarika na kama atapata nafasi katika Kombe la EFL na Ligi ya Vijana ya UEFA. Ikiwa atafanya vizuri huko, tunaweza kumuona kwenye benchi la kikosi cha kwanza cha United.

Nico O'Reilly (Manchester City)

Simon Stone wa BBC Sport anasema: O'Reilly mwenye umri wa miaka 19 alifanya vyema dhidi ya Barcelona huko Florida. Ingawa baadhi ya nyota wakubwa bado hawajarejea mazoezini baada ya michuano ya Euro na Copa America, lakini kiwango cha O'Reilly ni kizuri.

Kiungo huyo wa kati, anajua kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza haiwezekani kwa sasa kutokana na uwepo wa Rodri. Lakini anaweza kupata nafasi kutokea benchi, haswa baada ya kucheza vizuri katika ushindi wa Ngao ya Jamii dhidi ya Man Utd.

Eric da Silva Moreira (Nottingham)

Nottingham Forest ilimleta winga Moreira kutoka St Pauli msimu huu wa joto kwa chini ya pauni milioni 2.

Mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani chini ya miaka 17, alicheza mechi yake ya kwanza ya kulipwa msimu uliopita lakini aliisaidia St Pauli kupanda daraja Bundesliga kwa mara ya kwanza baada ya miaka 13.

Moreira, ambaye pia anaweza kucheza beki wa kulia, aliisaidia Ujerumani kushinda Ubingwa wa Ulaya chini ya miaka 17 na Kombe la Dunia mwaka jana.

Pedro Lima (Wolves)

Wolves walimleta Lima mwenye umri wa miaka 18 kwa Molineux kwa pauni milioni 8.5 kutoka Sport Recife mwezi Julai, ikiripotiwa kuwa walimpokonya kutoka mikononi mwa Chelsea, na ameonyesha kiwango kizuri katika maandalizi ya msimu mpya.

Kadi nyekundu ya Nelson Semedo katika kichapo cha siku ya mwisho kwa Liverpool msimu uliopita, kilimpa Lima fursa ya kujidhihirisha kama beki wa kulia, huku Semedo akifungiwa mechi tatu za mwanzo.

Mchezaji wa kimataifa wa Ureno, Semedo bado ana uwezo wa kurejea katika nafasi yake, lakini Lima anatarajiwa kuacha alama msimu huu.

Harrison Armstrong (Everton)

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 amefanya vyema katika chuo cha michezo cha Everton na kupata kandarasi yake ya kwanza ya kulipwa mwezi Julai, na kusaini mkataba wa miaka mitatu.

Kiungo huyo aliingia katika kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 21 msimu uliopita na amepewa nafasi ya kushiriki katika kikosi cha kwanza wakati wa maandalizi ya msimu mpya.

Pia unaweza kusoma

Paul Melly ni mjumbe mwelekezi wa Mpango wa Afrika Chatham House huko London.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla