Ligi Kuu England: 'Ubingwa ni wetu' - anasema nahodha wa Man City

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Nahodha wa Manchester City, Kyle Walker anasema ubingwa wa Ligi Kuu ya England ni wao, huku timu yake ikitarajia kushinda taji la tano mfululizo, jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa.

City ilikuwa klabu ya kwanza kushinda taji mara minne mfululizo katika ligi kuu ya Uingereza msimu uliopita na wataanza kutetea taji hilo siku ya Jumapili watakaposafiri kukutana na Chelsea.

Akizungumza na BBC Radio 5 Live, beki wa pembeni wa Uingereza Walker anasema: "Sisemi ni kujisifu, lakini tumeshashinda sasa mara nne mfululizo - hili ni kombe letu. Ninaweza kukwambia, unapotazama kwenye mkono wako na una beji ya dhahabu ambayo hakuna mtu mwingine yuko nayo, unapata hisia nzuri."

Chini ya meneja Pep Guardiola, City imekuwa mashine ya kushinda bila huruma. Walker anasema: "Kuchukua ubingwa mara nne mfululizo, huku tukiwa tumechukua makombe matatu katika msimu mmoja, ni mafanikio makubwa. Na kwenda tena na kushinda Kombe la Super Cup na Kombe la Dunia la Klabu.

"Sasa, kipi kitukwamishe kushinda mara tano mfululizo? Kwa nini tusifanya kitu ambacho sidhani kama kitafanyika tena? Hiyo ndiyo motisha tunayopaswa kuwa nayo kama wachezaji, na mimi kama nahodha."

Walker anakiri kuwa klabu hiyo inataka "mafanikio ya papo hapo - na hilo ndilo tunalopaswa kulitekeleza".

"Nadhani kama huna njaa ya ushindi, Guardiola hawezi kuwa nawe kwenye klabu. Ushindi ni sehemu kubwa ya vinasaba vyake."

"Angalia timu alizoondoka na kuzisimamia, wachezaji aliofanya nao kazi. Haoni aibu kukwambia usipofanya vizuri, haogopi kukuambia."

Pia unaweza kusoma

Kuhusu Euro 2024

d

Chanzo cha picha, MARTIN MEISSNER / AP

Maelezo ya picha, Muingereza Jude Bellingham akishangilia baada ya kufunga bao katika mechi ya Kundi C kati ya Serbia na England kwenye michuano ya Euro 2024 mjini Gelsenkirchen, Ujerumani, Juni 16, 2024.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya kupata ushindi dhidi ya Serbia katika mechi yao ya kwanza ya Kundi C kwenye michuano ya Euro, England ilikosolewa vikali kwa ushindi huo wa 1-0 na kufuatiwa na sare dhidi ya Denmark na Slovenia.

Akizungumza kwenye kipindi cha You'll Never Beat Kyle, Walker, beki huyo amefichua kuwa kikosi hicho kilijadili ukosoaji wa vyombo vya habari walipokuwa Ujerumani.

"Nitakuwa nasema uwongo ikiwa nitasema hatukuzungumzi jambo hilo," anasema. "Sisi sote ni wanadamu na kila mtu anataka kupendwa - haswa kwa kazi ambayo tunaifanya kwa shauku na upendo mwingi."

The Three Lions baadaye iliiondoa Slovakia katika hatua ya 16 bora, na kushinda 2-1. Walikuwa nyuma kwa bao 1-0 kwa timu iliyoorodheshwa ya 44 hadi dakika ya 95, wakati Jude Bellingham alipofunga na kupeleka mchezo katika muda wa nyongeza, ambapo nahodha Harry Kane alifunga bao la pili la kichwa.

Walker, ambaye pia alikuwa sehemu ya kikosi cha England kilichotolewa kwa aibu na Iceland katika hatua ya 16 bora kwenye michuano ya Euro 2016, alikiri kuwa alidhani historia inaweza kujirudia kabla ya bao la Bellingham.

"Unawaza tu, 'hivi kweli inatokea tena?'," anasema.

Uamuzi wa kocha wa England

sdc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Aliyekuwa kocha wa England, Gareth Southgate

Habari moja kuu ilikuwa ni uamuzi wa Gareth Southgate kutomjumuisha mshambuliaji wa Manchester City, Jack Grealish katika kikosi chake cha wachezaji 26 wa England. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye amecheza mechi 36 na England, anasema "aliumia moyoni" kuachwa.

Mchezaji mwenzake wa klabu hiyo Walker anasema, "alishtushwa sana na uamuzi wa Southgate, akisema kuwa Grealish "huleta kitu tofauti" kwa wachezaji wengine waliosafiri kwenda Ujerumani.

Aliongeza kwa kusema "sio juu yangu lakin kuamua ni nani awe kwenye kikosi."

Uchaguzi wa timu ya Southgate pia ulichunguzwa katika muda wote wa mashindano, huku baadhi ya wachambuzi na mashabiki wakitaka Cole Palmer, Ollie Watkins na Anthony Gordon waanze katika mechi au waingizwe uwanjani mapema walivyokuwa kama wachezaji wa akiba.

Walker anasema wachezaji "wanaelewa kuwa meneja ana uamuzi mgumu sana wa kufanya" na akaongeza kusema "sio mara zote wachezaji wa mwanzo ndio huleta mafanikio."

Watkins alifunga bao la ushindi katika dakika ya 90 katika nusu fainali dhidi ya Uholanzi baada ya kuingizwa kama mchezaji wa akiba. Palmer wa Chelsea, kwa upande wake, aliisawazishia England dhidi ya Uhispania katika mchezo wa fainali baada ya kuingizwa kipindi cha pili.

Southgate alijiuzulu mwisho wa michuano hiyo na Lee Carsley ameteuliwa kuwa meneja wa muda.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla