Mtoto mmoja huuawa kila baada ya dakika kumi Gaza

Chanzo cha picha, EPA
Maafisa wa Israel wanasema watu wake wapatao 5400 wamejeruhiwa katika mzozo na Hamas. Kwa upande mwingine, Wizara ya Afya ya Palestina inasema zaidi ya watu 25,400 wamejeruhiwa huko Gaza na Ukingo wa Magharibi na Mto Jordan.
Takribani watu 2260 wamepotea Gaza, ambapo 1270 ni watoto. Wengi wa watu hao wanaaminika kuzikwa chini ya vifusi vya majengo yaliyobomolewa na mashambulizi ya Israel.
Maafisa wa Israel wanadai takribani raia 242 wa Israel na wa kigeni wanashikiliwa mateka na Hamas, ambapo 30 kati yao ni watoto. Hamas inasema kuna mateka 57 wamefariki kutokana na mashambulizi ya Israel Gaza.
Hamas imewaachilia mateka wanne hadi kufika Oktoba 20. Walioachiliwa walikuwa ni raia, akiwemo mvulana wa miaka 17.
Jeshi la Israel lilisema lilimwokoa mmoja ya askari wake wa kike katika operesheni ya ardhini tarehe 29 Oktoba. Mwanajeshi huyo alikuwa chini ya udhibiti wa Hamas tangu Oktoba 7.
Kutokana na mzozo wa Israel na Hamas, zaidi ya nusu ya wakazi wa Gaza wamelazimika kuyahama makazi yao na kujihifadhi katika maeneo 'salama.'
Mtoto mmoja hufariki kila baada ya dakika 10

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Novemba 6, Wizara ya Afya ya Gaza ilisema zaidi ya watu elfu 10 wameuawa na mashambulizi ya Israel. Kuna zaidi ya watoto 4100 miongoni mwa waliouawa - ina maana kwa wastani mtoto mmoja anafariki kila baada ya dakika kumi huko Gaza.
Kuna watu milioni 2.2 wanaoishi katika Ukanda wa Gaza na zaidi ya nusu yao ni watoto. Oktoba 13, Israel ilitoa onyo kwa watu kuhama eneo la Gaza kaskazini na kwenda Kusini.
Mwezi mmoja baada ya shambulio la Hamas ndani ya Israel, inasemekana zaidi ya majengo laki mbili ya makazi huko Gaza yameharibiwa. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Palestina ya Gaza, hii ni karibu nusu ya idadi ya nyumba katika Ukanda wa Gaza.
Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa - hadi Novemba 5, takriban watu milioni 1.5 walikuwa wakimbizi wa ndani Gaza. Watu hawa wamejihifadhi katika shule, makanisa, hospitali, majengo ya umma au nyumba za familia wa karibu.
Watu wa Gaza hawawezi kuondoka katika eneo hilo kwa sababu kivuko cha Erez kinachounganisha Israel na Gaza kimefungwa na kivuko cha Rafah, cha kuingia Misri, kinafunguliwa kwa ajili tu ya uhamisho wa raia wa kigeni na baadhi ya watu waliojeruhiwa.
Mauaji ya wafanyakazi wa misaada

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wizara ya Afya ya Palestina inayoendeshwa na Hamas inasema hadi tarehe 5 Novemba, hospitali 16 kati ya 35 na vituo 51 vya matibabu kati ya 76 katika Ukanda wa Gaza vilikuwa havifai tena kutumika.
Kulingana na Wizara ya Afya ya Palestina, ambulensi 50 zimeharibiwa na ambulensi 31 kwa sasa hazifanyi kazi. Takaribani wafanyikazi wa afya 175 wameuwawa.
Chini ya sheria za kimataifa, wafanyakazi wa misaada na watu wanaohusika katika huduma za matibabu na vituo vya afya lazima walindwe kwa gharama zote.
Umoja wa Mataifa unasema takribani wafanyakazi 88 wanaofanya kazi katika shirika lake la misaada la Umoja wa Mataifa la Usaidizi na Kazi na wafanyakazi 18 wa ulinzi wa wameuawa katika mzozo huu.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (UNOCHA), hadi Novemba 5, waandishi wa habari 46 wameuawa katika mzozo wa Israel na Hamas.
Wakati usalama na kazi za waandishi wa habari vinapaswa kulindwa chini ya Mkataba wa Geneva wa 1949. Kwa mujibu wa shirika lisilo la kiserikali la 'Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari,' vita vya sasa vya Israel huko Gaza ndio vibaya zaidi kwa waandishi wa habari wanaoripoti mzozo huu kwa miongo mitatu iliyopita.
Shida ya maji

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Maisha ya Gaza yanazidi kuwa magumu kila siku. Wale ambao wako hai hadi sasa wanakabiliwa na uhaba wa chakula na ukosefu wa vituo vya afya.
Shirika la Afya Ulimwenguni linasema kufikia Oktoba 15 - familia na watoto wanaoishi Gaza walilazimika kuishi kwa lita tatu tu kwa kila mtu kwa siku.
Lita hizo ndizo huzitumia kwa kunywa, kupika na kufanya usafi. Ingawa inaelezwa mtu anahitaji angalau lita 15 za maji kwa siku.
Kiasi kidogo sana cha maji kimepelekwa Gaza kupitia kivuko cha Rafah katika siku za hivi karibuni. Miundombinu ya usambazaji maji imeharibiwa kwa kiasi kikubwa.
Tarehe 5 Novemba, shirika la Umoja wa Mataifa UNOCHA lilisema katika ripoti yake - matumizi ya maji Gaza yamepungua kwa asilimia 92 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya kuanza vita.
Vituo 65 vya kusukuma maji taka vilivyokuwa vikifanya kazi havifanyi tena kazi.
Oktoba 31, Shirika la Afya Ulimwenguni lilionya kuna uwezekano wa watu wengi kuhama makazi yao Gaza, msongamano wa watu unaweza kuongezeka katika baadhi ya maeneo, miundombinu ya maji na ya huduma za afya yatazidiwa.















